MAOMBI YA KUBATILISHA MAAMUZI MABAYA YA KINYWA CHAKO ULIYOJITAMKIA ZAMANI.

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
Bwana YESU atukuzwe ndugu zangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU kisha tuombe maombi ya ushindi, Pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana sasa hivyo nakuomba tuwasiliane ili uweze kukipata kokote uliko Tanzania.
Leo tunaomba tukibatilisha maamuzi mabaya tuliyowahi kujitamkia wenyewe.
Mathayo 12:37 '' Kwa kuwa kwa maneno yako utahesabiwa haki, na kwa maneno yako utahukumiwa.''

Katika jamii kuna watu wamefungwa na wachawi, kuna watu wamefungwa na waganga, kuna watu wamefunga na wazazi wao au ndugu zao, Kuna watu wamefungwa kipepo na wafanyakazi wenzao, kuna watu wamefungwa na majini. Lakini cha ajabu kuna watu wamejifungwa wenyewe kwa maneno yao waliyojitamkia.
Biblia inasema kwa maneno yako unaweza ukahesabiwa haki na kwa maneno yako unaweza ukahukumiwa.
Watu wengi hawajui nguvu za wanayoyatamka.
Wengi hawajui kwamba shetani na majini hufanyia kazi maneno mabaya uliyojinenea na kuyathibitisha.
Kujinenea vibaya hufungua mlango wa shetani kukutesa.
Kuna watu walikuwa wanajinenea kwamba heri wafe tu kuliko kuishi na matokeo yake shetani alifanyia kazi maneno hayo baadae wakajiua na kujipeleka jehanamu.
Watu wengi wanaojiua hali hiyo haiji ghafla tu bali kwanza hujinenea kufa na kwa njia hiyo mapepo hupata nafasi ya kumwingilia mtu huyo na kupelekea kujiua kweli na kujipeleka jehanamu, maana Biblia inasema ''Usiue- Kutoka 20:13'' na hata ukijua mwenyewe maana yake umeua na hauwezi kwenda uzima wa milele hata kama ulifanya mema mengi kiasi gani.
Ndugu leo jina la YESU KRISTO lipo kukushindia, omba tu.
Leo Damu ya YESU KRISTO ipo kubatilisha maneno yote mabaya uliyojinenea.
Katika harakati za maisha inawezekana kabisa uliwahi kujinenea mabaya ambayo ndio yanakutesa sasa.
Biblia inasema kwa maneno yako unaweza kuhukumiwa na kwa maneno yako unaweza kuhesabiwa haki.
Maneno yako yanaweza kukuhukumu.
 Maneno yako yanaweza kukufunga.
Maneno yako yanaweza kukuamulia hatima yako.
Leo sio watu wote wamerogwa bali wengine wamejiroga wenyewe.
Kuna watu leo wanateswa na vifungo vilivyoumbwa kwa maneno ya vinywa vyao.
Mthali 6:2 '' Basi umetegwa kwa maneno ya kinywa chako, Umekamatwa kwa maneno ya kinywa chako,''

Kumbe maneno yako yanaweza kukutega hata ukaanguka kabisa.
Kumbe maneno yako yanaweza kukufunga, na usipojua kuomba maombi ya kufuta maneno yaliyokukamata hakika utabaki umefungwa.
 Mama au Baba unaweza kuunenea mabaya uzao wako kwa sababu ya hasira zako lakini maneno hayo shetani akayatumia kuwatesa watoto wako waliolaaniwa na wewe mzazi wao.
Maneno yana nguvu sana sana na shetani anaweza kuyatumia kukuharibia kabisa.
Katika Kitabu cha Waamuzi sura ya 11 utagundua Maneno ya kinywa yaliyo na nguvu sana.
Ukisoma Kuanzia mstari wa 30 hadi 32 Biblia inasema '' Naye Yeftha akamwekea BWANA nadhiri, akasema, Kwamba wewe utawatia wana wa Amoni mkononi mwangu kweli, ndipo itakuwa ya kwamba, kile kitakachotoka katika milango ya nyumba yangu kunilaki, hapo nitakaporudi na amani kutoka kwa hao wana wa Amoni, kitu hicho kitakuwa ni cha BWANA, nami nitakisongeza kiwe sadaka ya kuteketezwa. Basi Yeftha akavuka kuwaendea wana wa Amoni ili kupigana nao; naye BWANA akawaua mkononi mwake.''

Yeftha aliweka nadhiri kwa kinywa chake ambapo nadhiri hiyo ya maneno yake ilitakiwa aitimize. Hakuna aliyemwambia atamke maneno hayo na hakuna aliyemlazimisha.
Baada ya kuweka nadhiri yake kwa maneno yake hakika alishinda vita.
Wakati akirudi nyumbani ilikuwa kwamba kitu cha kwanza kumlaki atakitoa sadaka ya kuteketezwa.  Nadhani labda alidhani ataona ng'ombe kwanza au kondoo au kuku, Hakujua kwamba atakayekuwa wa kwanza kumlaki atakuwa ni binti yake ya pekee.
Nini kilifanyika ilibidi binti yule afe, majuto ya Yeftha naamini yalikuwa makubwa sana, maumivu yake nadhani yalimtesa maisha yake yote lakini alitakiwa kutimiza alichoahidi kwa kinywa chake.
Biblia inasema hivi katika hiyo Waamuzi 11  Kuanzia mstari wa 34 hadi 39 '' Kisha Yeftha akafika Mispa nyumbani kwake, na tazama, binti yake akamtokea kumlaki, na matari na machezo; naye alikuwa ni mwanawe pekee; hakuwa na mwingine, mwana wala binti, ila yeye. Ikawa alipomwona akayararua mavazi yake, akasema, Ole wangu! Mwanangu, umenitweza sana, nawe u mmoja miongoni mwa hao wanisumbuao; kwa kuwa mimi nimemfunulia BWANA kinywa changu, nami siwezi kurejea nyuma. Binti yake akamwambia, Baba yangu, wewe umemfunulia BWANA kinywa chako; basi unifanyie sawasawa na hayo yaliyotoka kinywani mwako; kwa kuwa yeye BWANA amekulipia kisasi juu ya adui zako, hao wana wa Amoni. Kisha akamwambia baba yake, Basi na nifanyiwe neno hili; niache peke yangu muda wa miezi miwili, ili nipate kwenenda milimani, na kuombolea uanawali wangu, mimi na wenzangu. Akamwambia, Haya, enda. Akampeleka mbali muda wa miezi miwili; naye akaenda zake, yeye na wenziwe, akauombolea uanawali wake huko milimani. Basi ikawa mwisho wa hiyo miezi miwili, akarudi kwa babaye, aliyemtenda sawasawa na ile nadhiri yake aliyokuwa ameiweka; naye alikuwa hajamjua mtu mume. Kisha ikawa desturi katika Israeli,''

 Yeftha alirarua mavazi akijuta kwanini alitamka maneno ya ahadi ile.
Maneno ya nguvu sana.
Kama umezoea kujisemea mabaya ndugu nakuomba acha mara moja na omba maombi ukifuta kila kifungo ambacho kimekukamata wewe kwa sababu ya maneno ya kinywa chako.
Nimewahi kuombea watu wengi na wengine katika hao wakati wakinisimulia wanavyoumwa nililazimika kuwakatisha kueleza maana kila akisema maneno kadhaa anasema ''Sidhani kama nitapona'', Mtu kama huyo anajidhani hatapona hakika asipopona sio kwa sababu maombezi hayajafanya kazi bali ametaka mwenyewe asipone.

Mithali 18:20-21 ''Tumbo la mtu litajazwa matunda ya kinywa chake; Atashiba mazao ya midomo yake. Mauti na uzima huwa katika uwezo wa ulimi; Na wao waupendao watakula matunda yake.''

Kuna watu walijitamkiwa ''Sijui kama nitapata Mwenzi aliyetulia'' hakika katika maisha yao hawakupata huyo mwenzi aliyetulia.
Kuna watu husema ''Sijui kama nitapata kazi'' na cha ajabu miaka imeenda mingi na kazi hawajapata.
Biblia hapo juu inasema kwamba mtu atashiba mazao ya kinywa chake. Kumbe kinywa kinalima na utavuna kwa maneno ya kinywa chako.
Kwenye maneno yako unayotamka tambua kwamba kuna uzima na mauti.
Mauti maana yake uharibifu.
Je unajinenea uzima au uharibifu?
Je watu wamewahi kukunenea uharibifu?
Je umewahi kujinenea uharibifu?
Kumbuka '' Sikilizeni, mfahamu; Sicho kiingiacho kinywani kimtiacho mtu unajisi; bali kitokacho kinywani ndicho kimtiacho mtu unajisi-Mathayo 15:11''
Kitokacho kinywani kinaweza kumtia mtu unajisi.
Najisi ni chafu hivyo maneno yako yanaweza kukufanya uwe mchafu au uwe umelaaniwa.
Kwenye Kitabu changu cha MAOMBI YA KINA yapo maombi mengi ya kumfungua mtu kutoka kwenye vilivyomfunga, hasa maneno ya watu.
Leo nahusika na maneno ya kujitamkia wewe mwenyewe.
Kuna watu zamani walikuwa wanajisemea ''Sijui kama nitapata mume/mke na watoto'' Leo wanahangaika kupta hivyo ambavyo walivikataa zamani kwa maneno yao.
Kijana unaweza kuwa uliwahi kumwambia binti kwamba ''Sitaoa mwingine yeyote ila ni wewe tu'' Baadae yule binti aliolewa na wengine na wewe umehaha kupata mchumba lakini miaka mitatu hujapata na unaowapata wanakukataa. Hujui tatizo ni nini kumbe ''umetegwa kwa maneno ya kinywa chako, Umekamatwa kwa maneno ya kinywa chako,-Mithali 6:2''

Binti inawezekana kabisa miaka imeenda na hujapata Mchumba sahihi. Wewe ndoto zako kila mara ni kuota tu unaolewa lakini anayekuoa ni mume wa mtu. Unadhani kwamba ndoto hiyo ni ndoto ya mbaya kumbe ni ndoto sahihi ya kukujulisha ni wapi umefungwa na ni nini kimekufunga.  Inawezekana kabisa kuna mtu alikutongoza ukamkataa lakini akakutamkia maneno kwamba hata uende wapi lakini mwisho utarudi kwake. Baadae yeye alioa na kuendelea na maisha yake na wala hakumbuki kama aliwahi kukufunga kwa maneno yake, unamuona mwanaume aliyeoa kwenye ndoto akifunga ndoa na wewe kumbe maana yake unatakiwa uombe maombi ya kufuta kile alichokufunga mwanaume. Huyo mwanaume ndiye anakuzuia usiolewe. Sio lazima mume wa mtu utakayemuona ndotoni ndio huyo huyo kakufunga, wakati mwingine huyo huwakilisha tu kwamba kuna  mwanaume aliye kwenye ndoa amekufunga. Kumbuka shetani kazi yake ni kukuonea hivyo usipojua kuomba katika jina la YESU KRISTO hakika unaweza kuteseka sana. MUNGU anakataza uasherati kwa kutusaidia sisi wanadamu lakini wengi hawajui. Leo unaweza kukuta binti amehaha kupata mchumba na hakufanikiwa na hajui amefungwa wapi, kumbe walipokuwa wanafanya uzinzi, kwa upendo feki walijiapia kwamba wataishi milele, baadae mambo yanabadilika na kijana anaoa kwingine na kumwacha binti amefungwa na maneno aliyoyatamka zamani kipindi cha uzinifu wake. Inawezekana kabisa wewe binti imekuwa ngumu kutulia na mchumba bila hata kujua tatizo ni nini.
Ndugu wengine wamefungwa kwa maneno ya vinywa vyao waliyojinenea zamani. Inawezekana kabisa ulijinenea kwamba wewe utakuwa na mtu fulani miaka yako yote, cha ajabu baada ya uasherati uliouruhusu shetani alipanda magugu na kupelekea mkaachana kabla ya ndoa, baadae mwenzako akaoa na wewe umebaki umefungwa na maneno ya kinywa chako hata leo maana hujawahi kuomba maombi ya kubatilisha maneno yako uliyoyatamka bila kujua au bila kutafakari kwa kina.

Yakobo 3:5-6 '' Vivyo hivyo ulimi nao ni kiungo kidogo, nao hujivuna majivuno makuu. Angalieni jinsi moto mdogo uwashavyo msitu mkubwa sana. Nao ulimi ni moto; ule ulimwengu wa uovu, ule ulimi, umewekwa katika viungo vyetu, nao ndio uutiao mwili wote unajisi, huuwasha moto mfulizo wa maumbile, nao huwashwa moto na jehanum.''

MANENO MABAYA UNAYOJITAMKIA YANAWEZA KULETA VITU HIVI KWAKO;

1.  Kukufunga ili usifanikiwe baadae.
2. Kukutega ili unaswe katika mabaya.
3. Kukukamata ili usiendelee mbele.
4. kukuhukumu.
 5. Kukulaani.
6. Kubomoa vitu vyako au fursa zako.
7. Kukuletea uharibifu mbalimbali kulingana na ulivyotamka.

Luka 6:45 ''Mtu mwema katika hazina njema ya moyo wake hutoa yaliyo mema, na mtu mwovu katika hazina mbovu ya moyo wake hutoa yaliyo maovu; kwa kuwa mtu, kinywa chake hunena yale yaujazayo moyo wake. ''

Kazi mojawapo ya shetani ni kukuletea hasira ili utamke mabaya kutokana na hasira yako.
 Biblia inakataza kutamka maneno ya ujinga maana yanaweza kukufunga.
Mhubiri 5;2 ''Usiseme maneno ya ujinga kwa kinywa chako, wala moyo wako usiwe na haraka kunena mbele za MUNGU; kwa maana, MUNGU yuko mbinguni, na wewe upo chini, Kwa hiyo maneno yako na yawe machache.''

Unaweza  kujilaani kwa maneno ya kinywa chako na laana hiyo ikakupata kweli.
Unaweza kulaani uzao wako kwa maneno ya kinywa chako.
Unaweza kujipeleka kwenye gereza la kiroho kwa maneno ya kinywa chako.
Unaweza ukakosa baadhi ya baraka zako kwa sababu tu ya maneno ya kinywa chako.
Maneno yatokayo moyoni yanaweza kumnajisi mtu, mawazo mabaya nayaweza kumnajisi mtu.
Ndugu leo omba maombi ya kufuta maneno mabaya uliyojinenea kwa kinywa chako haijalishi ni miaka mingi sana imepita, kama hukuyafuta maneno hayo hakika bado yapo na yanaweza kukufunga.
Nuhu alitamka laana zikawapata wajukuu na uzao hadi miaka mingi. Ashukuriwe MUNGU kwa kutuletea YESU KRISTO kutukomboa.
Ndugu yangu leo pambana na hata unaweza ukafunga ili kuombea mambo haya niliyoyataja leo.

Zaburi 34:13 '' Uuzuie ulimi wako na mabaya, Na midomo yako na kusema hila.'' 
 
 Kuna uponyaji hakika kwa watakaoomba maombi ya kufuta maneno mabaya waliyojinenea au kujilaani.
Wengine hata hawajui kama waliwahi kujinenea mabaya lakini kwa hasira za muda mfupi waliwahi kutamka vitu vingi vibaya na baada ya hasira kuisha hawakumbuki kama walijinenea mabaya.
MUNGU anakataza pombe maana wapo wailiowahi kulaani watoto wao, wake zao au kujilaani wao wenyewe kwa sababu tu ya dhambi ya pombe wakiwa wamelewa.
Ndugu zangu japokuwa maneno yako yamekufunga miaka mingi lakini ukimkimbilia Bwana YESU hakika utafunguliwa.
Wakati naandika somo hili nimeona mabinti kwenye ulimwengu wa roho kwa ufunuo wanalia kwa uchungu sana kwa sababu ya hali zao za sasa ambazo zilisababishwa na maneno ya kinywa.
Ni mara chache sana kuona ufunuo wa moja kwa moja huku naandika, mara nyingi huona ufunuo wakati nikiomba  kabla ya kufundisha
Ndugu yangu, kama hujaokoka nakuomba kimbilia kanisa liliko ukaokoke na omba maombi ya kufuta maneno mabaya uliyojinenea, pia ukiona nguvu yako ni ndogo na imani yako ni ndogo nakuomba shirikisha watumishi wa MUNGU katika maeneo yako, waeleze jinsi ujumbe ulivyo na waombe wakuombee wakifuta maneno mabaya uliyotamkiwa na uliyojitamkia wewe zamani.
Kwa maneno mabaya unayoyakumbuka nakuomba yafute kwa damu ya YESU KRISTO kwa kuyataja moja baada ya lingine, kama hukumbuki basi ombe ukitaja mengi na kama katika hayo yamo yanayohusika basi yatakuwa yamefutika.
MUNGU akubariki sana sana na kama ukipenda kunisapoti katika huduma yangu kwa sadaka ya hiari ya kiwango chochote utakachopenda karibu na MUNGU akubariki sana, pia kitabu kipo na wasiliana nami utakipata na ukifanyia kazi itakusaidia sana.
Hapa chini ni maombi ya kubatilisha maneno mabaya uliyojitamkia.
Maombi haya naomba yamsaidie mtu yule ambaye hajui kuomba ili katika kuomba kwa kutumia hayo basi atakumbuka mahitaji yake na kuyataja katika maombi yake.
Kwa waombaji wazoefu naamini baada tu ya kulisoma somo na kulielewa basi anajua aombee nini.
Lakini muhimu zingatia kuombea mambo haya.
1.Futa kumbukumbu mbaya za zamani na futa maneno mabaya uliyojitamkia zamani.
2. Funga ukurasa wa mabaya ya zamani kwa kufuta kila neno baya la zamani ulilotamka.
3. Batilisha mabaya yote uliyojinenea zamani kwa kujua au kwa kutokujua.

 
MAOMBI YA KUBADILISHA MAAMUZI MABAYA YA KINYWA CHAKO ULIYOJITAMKIA ZAMANI.

BABA katika jina la YESU KRISTO aliye hai.
Niko mbele zako MUNGU wangu nikiomba msamaha wako.
Naomba unisamehe MUNGU wangu dhambi zangu zote na maovu yangu yote.
Naomba unisamehe MUNGU wangu kwa maneno yangu mabaya na ambayo yamenifunga miaka mingi, nisamehe kwa hayo MUNGU wangu na naomba nifunguliwe sana kutoka vifungo vyote vilivyotokana na kinywa changu.
Neno lako linasema katika Zaburi 68 Mstari wa 20 kwamba njia za kutoka mautini zina JEHOVAH BWANA. Nimetambua hakika kwamba njia za kutoka kwenye uharibifu zina wewe MUNGU muumbaji wangu.
Katika jina la YESU KRISTO aliye hai.
Ninafuta maneno yote mabaya ambayo nimewahi kujinenea tangu utotoni mwangu, yanafuta kwa damu ya YESU KRISTO na kwa jina la YESU KRISTO.
Kila neno baya linalonifunga ambalo nilijitamkia zamani, leo nalifuta Neno hilo kwa damu ya YESU KRISTO na kwa jina la YESU KRISTO.
Kila maneno mabaya ambayo nililazimishwa kuyatamka, leo yanafuta maneno hayo yote kwa damu ya YESU KRISTO na kwa jina la YESU KRISTO.
Kila maneno mabaya ambayo uzao wa tumbo la mama yangu ulinenewa, leo yanafuta maneno hayo yote kwa damu ya YESU KRISTO na kwa jina la YESU KRISTO.
 Kila maneno mabaya ambayo niliahidi kwa watu niliokuwa na uhusiano nao ambayo yamenifunga, leo yanafuta maneno hayo yote kwa damu ya YESU KRISTO na kwa jina la YESU KRISTO.
Kila maneno mabaya ambayo nilimwahidi mtu na sasa yamenifunga, leo yanafuta maneno hayo yote kwa damu ya YESU KRISTO na kwa jina la YESU KRISTO. 
 Kila maneno mabaya ambayo nilimtamkia mtu na maneno hayo yamegeuka na kunifunga mimi, leo yanafuta maneno hayo yote kwa damu ya YESU KRISTO na kwa jina la YESU KRISTO.
 Nafuta kumbukumbu mbaya za zamani zote ambazo zimenifunga, Nafuta kwa damu ya YESU KRISTO na kwa jina la YESU KRISTO.
Nafuta kumbukumbu mbaya za kutukana na kujilaani, Nafuta kwa damu ya YESU KRISTO na kwa jina la YESU KRISTO.
Nafuta kumbukumbu mbaya za watu nilikuwa ninauhusiano nao na kuwaahidi mengi lakini tukaachana na ahadi hizi zimeendelea kunifunga, Nafuta kumbukumbu hizo kwa damu ya YESU KRISTO na kwa jina la YESU KRISTO.
 Kumbukumbu za kutoa mimba na kujisemea kwamba sitazaa tena na sasa niko kwenye ndoa na sina mtoto, Nafuta kumbukumbu hizo kwa damu ya YESU KRISTO na kwa jina la YESU KRISTO
 Kumbukumbu za kuachwa na mchumba kisha nikasema siwapendi wanaume wote au wanawake wote,  Nafuta kumbukumbu hizo kwa damu ya YESU KRISTO na kwa jina la YESU KRISTO
 Kumbukumbu za kufanya mabaya kisha kujilaani, Nafuta kumbukumbu hizo kwa damu ya YESU KRISTO na kwa jina la YESU KRISTO
Kumbukumbu za kudanganya watu kwa kijisemea maneno mengi ambayo yamenifunga, 
Nafuta kumbukumbu hizo kwa damu ya YESU KRISTO na kwa jina la YESU KRISTO
 Kila ukurasa wa mabaya ya zamani naufunga kwa damu ya YESU KRISTO na kwa jina la YESU KRISTO.
Ukurasa wa magonjwa yaliyopelekea kujinenea mabaya, Naufunga ukurasa huo kwa damu ya YESU KRISTO na kwa jina la YESU KRISTO.
Ukurasa wa dhambi ulionifanya nijinenea mabaya, Naufunga ukurasa huo kwa damu ya YESU KRISTO na kwa jina la YESU KRISTO.
 Ukurasa wa mateso na kunyanyaswa uliopelekea mimi kujilaani au kujinenea mabaya,  Naufunga ukurasa huo kwa damu ya YESU KRISTO na kwa jina la YESU KRISTO.
Ukarasa wa machukizo ulioambatana na maneno yangu mabaya, Naufunga ukurasa huo kwa damu ya YESU KRISTO na kwa jina la YESU KRISTO.
 Kwa damu ya YESU KRISTO nabatilisha maneno yote mabaya ambayo yamenifunga.
Kila chumba kwenye ulimwengu wa roho kilichotunza maneno mabaya ambayo nilijitamkia na yamenifunga, chumba hicho cha kiroho nakiharibu chote na maneno hayo yanafuta kwa damu ya YESU KRISTO na kwa jina la YESU KRISTO.
Kila neno baya nililolitamka usiku au mchana au jioni, Nabatilisha Neno hilo  kwa damu ya YESU KRISTO na kwa jina la YESU KRISTO.
Kila Neno nililojitamkia na neno hilo limenifunga katika ndoa, uchumba, uchumi, akili, uzao, kazi afya au nafsi  Nabatilisha Neno hilo  kwa damu ya YESU KRISTO na kwa jina la YESU KRISTO.
Nakushukuru MUNGU BABA maana umenishindia na hakuna Neno baya nililowahi kujitamkia na limenifunga.
Niko huru sana kwa jina la YESU KRISTO.
Damu ya YESU KRISTO imeniandika huru leo kutoka kwenye kila neno baya ambalo niliwahi kulinena kwa kinywa changu.
Katika jina la YESU KRISTO nimeomba na kushukuru.
Amen Amen Amen.
 Asante kama umelielewa Neno la MUNGU ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa BWANA YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
0714252292.
mabula1986@gmail.com
Umeshashare sana jumbe zisizo na maana leo
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu.

Comments