USILICHANGANYE NENO LA MUNGU NA UONGO.

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU

Bwana YESU atukuzwe ndugu popote uliko.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.
 Biblia inasema  katika 2 Wakorintho 4:2 " lakini tumekataa mambo ya aibu yaliyositirika, wala hatuenendi kwa hila, wala kulichanganya neno la MUNGU na uongo; bali kwa kuidhihirisha iliyo kweli twajionyesha kuwa na haki, dhamiri za watu zikitushuhudia mbele za MUNGU. "
Hilo ni agizo la MUNGU kwa watumishi wake wote.
Ni agizo la MUNGU kwa kila aliyeokolewa na Bwana YESU.
 Ni wajibu wa Kanisa kukataa kulichanganya Neno la MUNGU na uongo.
Kuna baadhi ya watu hulichanganya Neno la MUNGU na uongo.
Hata kuna misemo mingi leo huwa inasemwa hadi na watumishi wa MUNGU na kuliaminisha kanisa kwamba hayo ni maandiko kumbe sio maandiko.
Kuna watu leo huhubiri kwamba ''MUNGU anasema jisaidie nami nitakusaidia'' Hakuna andiko la kivyo katika Biblia.
Huo ni mfano mmoja kati ya mingi ambayo baadhi ya watu kwa kuelewa au kwa kutokuelewa hufundisha watu kwamba ni Biblia inasema.
Wakati mwingine uovu wa mtumishi unaweza kutengeneza sumu kwa Kanisa maana atakuwa anafundisha uongo.
Ni ngumu sana mzinzi kuhubiri habari za toba na kuacha uzinzi.
MUNGU hataki Neno lake lichanganywe na uongo.
Hata hekima ya kibinadamu ni lazima tutambue kwamba hiyo hekima sio Neno la MUNGU.
Kumbuka hii sana 1 Wakorintho 1:19 "Kwa kuwa imeandikwa, Nitaiharibu hekima yao wenye hekima, Na akili zao wenye akili nitazikataa."

Ndugu yangu uliyempokea YESU KRISTO kama Mwokozi wako nakuomba usikubali kulichanganya Neno la MUNGU na uongo au ubatili wako.

Usilichanganye neno la MUNGU na uongo.
Usilichanganye neno la MUNGU na tamaa zako.
Usilichanganye neno la MUNGU na mila za kwenu.
Usilichanganye neno la MUNGU na elimu yako ya kidunia.
Usilichanganye neno la MUNGU na ushabiki wako wa kisiasa.
Usilichanganye neno la MUNGU na ubaguzi wako.
Usilichanganye neno la MUNGU na unafiki wako.
Usilichanganye neno la MUNGU na matakwa yako.
Usilichanganye neno la MUNGU na hisia zako.
Usilichanganye neno la MUNGU na utashi wako.
Usilichanganye neno la MUNGU na tabia zako.


Mtumishi wa MUNGU ni lazima ukatae mambo ya hila ya kulichanganya neno la MUNGU na uongo.

Akili yako inayochanganga neno la MUNGU na ubatili MUNGU
ataikataa akili hiyo, na akiikataa akili yako hiyo mbaya kwenye Neno basi hakika atakuwa amekutaa na wewe. Na ukikataliwa na MUNGU, usipotubu ni hatari sana kwako.
Jifunze kupitia maandiko haya uone jinsi wale waliomkataa MUNGU na yeye aliwakataa na kuwaacha.
Warumi 1:28-32 " Na kama walivyokataa kuwa na MUNGU katika fahamu zao, MUNGU aliwaacha wafuate akili zao zisizofaa, wayafanye yasiyowapasa. Wamejawa na udhalimu wa kila namna, uovu na tamaa na ubaya; wamejawa na husuda, na uuaji, na fitina, na hadaa; watu wa nia mbaya, wenye kusengenya, wenye kusingizia, wenye kumchukia MUNGU, wenye jeuri, wenye kutakabari, wenye majivuno, wenye kutunga mabaya, wasiowatii wazazi wao, wasio na ufahamu, wenye kuvunja maagano, wasiopenda jamaa zao, wasio na rehema; ambao wakijua sana hukumu ya haki ya MUNGU, ya kwamba wayatendao hayo wamestahili mauti, wanatenda hayo, wala si hivyo tu, bali wanakubaliana nao wayatendao."


Ndugu Usilichanganye neno la MUNGU na dhambi zako.
Usilichanganye neno la MUNGU na uoga wako wa kuogopa kuhubiri injili.

Ndugu usiyaache yakupasayo katika Injili kwa kufuata tamaa zako.
Bwana YESU anasema '' Yeye anikataaye mimi, asiyeyakubali maneno yangu, anaye amhukumuye; neno hilo nililolinena ndilo litakalomhukumu siku ya mwisho.-Yohana 12:48''


Kwanini uyaangamize maisha yako kwa tamaa za muda mfupi?
Kwanini unajitenga na uzima wa milele kwa sababu ya uovu wa muda mfupi?
Kwanini unataka kumwacha YESU kwa sababu ya tamaa zako?
Kwanini unajiunganisha na kuzimu kwa kuwafuata waganga na wachawi?
Ndugu, usikubali kuwa rafiki wa kuzimu, tena usikubali kuwa rafiki wa majuto.
Neno la MUNGU limekamilika na wala halihitaji nyongeza za shetani wala nyongeza za wanadamu.

Hutakiwi kuliongeza Neno la MUNGU wala kulipunguza, Biblia inaonya ikisema '' Namshuhudia kila mtu ayasikiaye maneno ya unabii wa kitabu hiki, Mtu ye yote akiyaongeza, MUNGU atamwongezea hayo mapigo yaliyoandikwa katika kitabu hiki. Na mtu ye yote akiondoa lo lote katika maneno ya unabii wa kitabu hiki, MUNGU atamwondolea sehemu yake katika ule mti wa uzima, na katika ule mji mtakatifu, ambao habari zake zimeandikwa katika kitabu hiki.-Ufunuo 22:18-19'

Ni heri sana kumtumikia MUNGU lakini heri hiyo ni katika kumtumikia MUNGU katika kweli yake.
Ni vyema sana katika muda wako wa kuishi duniani ukamtumikia Bwana YESU kwa kuihubiri injili yake iokoayo lakini ni lazima kutumika katika kweli na utakatifu.
Utakumbukwa kwa lipi katika wakati wako wa uhai duniani?
Ndugu, ubebe vyema wakati wa MUNGU aliokupa.
Usiutumie wakati wako kwa shetani au kwenye anasa za dunia.

Ona mfano huu wa watu wa MUNGU walioona ni heri kumtumikia MUNGU kuliko kutumikia dunia.

Waebrania 11:24-27 " Kwa imani Musa alipokuwa mtu mzima, akakataa kuitwa mwana wa binti Farao; akaona ni afadhali kupata mateso pamoja na watu wa MUNGU kuliko kujifurahisha katika dhambi kwa kitambo; akihesabu ya kuwa kushutumiwa kwake KRISTO ni utajiri mkuu kuliko hazina za Misri; kwa kuwa aliyatazamia hayo malipo."

Unajifunza nini juu ya Musa Kama Mtumishi wa MUNGU?
 
1. Kwa Imani Musa akagoma kuitwa mtoto wa mwabudu shetani.
Wewe je umejitenga na machukizo na matambiko ya familia?


2. Musa aliona heri mateso akiwa na wateule wa MUNGU, kuliko furaha ya muda ya dhambi akiwa na waabudu shetani.

Wewe je umekataa lini uzinzi na uasherati wa muda ili upate heshima kwa MUNGU?
Je umemkataa huyo tapeli anayetaka kukutendesha dhambi za muda tu ili ukose uzima wa milele.
Je ulipotukanwa kidogo kwa sababu ya Kuokoka kwako, uliamua kumwacha YESU aliyekuokoa?
Biblia inasema ni heri kupata mateso na taabu ukiwa mteule wa KRISTO na ukiwa na wateule wa KRISTO kuliko kujifurahisha katika dhambi na maovu ya kitambo tu kisha ukamkosa MUNGU milele.


3. Kushutumiwa kwa ajili ya YESU KRISTO ni bora kuliko hazina zote za misri.

Misri kibiblia ni kwa shetani.
Je ni Mara ngapi umeona bora kulitii Neno la MUNGU kuliko kwenda kwa waganga wa kienyeji?
Ni Mara ngapi umeamua bora kuachana na huyo hawara ili uitwe Mtoto wa MUNGU kuliko kuendelea na hawara ili ubaki kuwa mtoto wa shetani?
Je unasubiri nini kuokoka na kuacha dhambi zako zote?
Ni lini uliona bora kuacha kuimba nyimbo za kidunia na kuanza kuimba nyimbo za injili ya YESU KRISTO iokoayo?
Ni lini binti umewakataa wanaume wenye pesa na Mali ili tu umpendeze KRISTO anayekuandalia uzima wa milele?
Ni lini umeona bora kuwa masikini ila mtakatifu kuliko kuwa tajiri ila mwenda jehanamu kwa sababu ya Mali za wizi, uchawi, uganga na ufreemasoni?
Ni lini umeona bora kulala Nyumba ya chumba kimoja ila ni halali kuliko kuiba pesa ili ujenge Nyumba ya vyumba kumi ila kwa pesa za wizi?
Ni lini kijana umeona bora kuachana na shugamami kwa kumtii MUNGU kuliko kuendelea na uovu na ukose mbingu?
Ni lini mwanamke wewe umeona heri kuachana na mume wa mtu ili umtii MUNGU kuliko kuendelea na mume wa mtu kisha uende ziwa la moto milele?
Ni lini mwanaume wewe umeachana na mke wa mtu na vibinti kwa kumtii MUNGU kuliko kuendelea na dhambi zako hizo kisha uende jehanamu?
Ni lini Dada umeona bora kuacha kujiuza na kuacha ukahaba kwa kumtii MUNGU, kuliko kuendelea na kujiuza ili uende jehanamu?
Ni lini ndugu utaamua kuacha uongo ili tu uanze kumpendeza MUNGU?
Ni lini ndugu utaanza kuitwa mcha MUNGU na sio mdhambi.
Ndugu Yangu unayehusika katika dhambi yeyote na umesoma Ujumbe huu naomba ujue kwamba YESU ana haja na wewe Leo kabla hujachelewa. Ameniambia nikuambie hayo niliyokuambia.
Nakuomba usiwe na udhuru wowote Bali tubu na okoka kwa upya kwa kumkabidhi Bwana YESU maisha yako.
Maisha matakatifu ya Wokovu MUNGU aliyaumba ili Mimi na wewe tuyaishi.
Ukiishi maisha yasiyo matakatifu hakika unaishi maisha yaliyoumbwa na shetani ili uyaishi kisha ukose uzima wa milele.
Natamani kila mtu ajue kwamba Ujumbe huu umekuja kwa kusudi la MUNGU na KRISTO anahitaji kumsaidia mtu mnyenyekevu mmoja atakayetubu toba ya kweli kisha kuanza kumtii MUNGU na Neno lake.

Kumbuka Dunia itapita na mambo yake yote.
Falsafa Ya Dunia Hii Mwisho Wake Ni Mauti. Hata Kama Mtu Angejijengea Jina Kiasi Gani Duniani Lakini Mwisho Wake Ni Mauti. Hata Kama Mtu Angeitumikia Jamii Sana Na Watu Wote Kumshangilia Mwisho Wake Bado Unabaki Kuwa Ni Kifo. Hakuna Wa Kudumu Duniani. Hata Akina Adamu Walioishi Miaka Zaidi Ya 900 Bado Hawakuwa Wa Kudumu Duniani.

Waebrania 4:12 ''Maana Neno la MUNGU li hai, tena lina nguvu, tena lina ukali kuliko upanga uwao wote ukatao kuwili, tena lachoma hata kuzigawanya nafsi na roho, na viungo na mafuta yaliyomo ndani yake; tena li jepesi kuyatambua mawazo na makusudi ya moyo.''

Neno la MUNGU Leo limeyatambua yaliyoko moyoni mwako hivyo litii utaitwa heri na litumie kwa halali utaitwa heri sana.
Heri kuokoka Leo uwe mtakatifu kuliko kuendelea na maovu uwe mwenda jehanamu.
Mbinguni kuna Vitabu viwili.
Kimoja ni cha uzima na cha Pili ni kitabu che hukumu.
Wewe jina lako liko katika kitabu gani?
Ndugu, YESU KRISTO anaokoa, ukimpokea Leo na kulitii Neno lake UNAOKOKA.


Siku moja kwenye ndoto nilijulishwa mambo mawili.
1. Niliambiwa neno hili "Uzinzi ni mlango unaoweza kuonekana mzuri kwa wanadamu lakini mlango huo ni mlango uliofunguliwa ili kuwapeleka wanadamu jehanamu"
Ndugu zangu wote, ni muhimu sana kuifunga kwa vitendo na maombi milango ya uzinzi yote iliyofunguliwa kwako. Baada ya kuifunga milango hiyo ya uzinzi unatakiwa kuwa makini sana na kukataa ushawishi wowote unaokupeleka kwenye dhambi ya uzinzi. badilisha safari, badala ya kwenda jehanamu amua Leo kwenda mbinguni kwa kutubu na kuokoka na kuanza kuishi maisha matakatifu.

2. Baada ya julisho hilo nikaambiwa neno hili "Mtu aliyeokoka anatakiwa akue kiroho na kufikie eneo la A point of no return"
Yaani afikie eneo ambalo hakuna jinsi anaweza kurudi kwa shetani.
Hakuna jinsi ya kumrudisha nyuma.
Haiwezekani kumtengenisha na YESU KRISTO Mwokozi wake.
Baada ya neno hilo la kuifikia a point of no return nilitabasamu kwenye ndoto hadi nilipoamka na kuanza kuomba.
Ndugu zangu huwa siwezi kujulisha kila ninachoota lakini Leo nimepata msukumo wa kukushirikisha.
Fanyia kazi pale unapohusika ndani ya jumbe hizo.
1 Yohana 2:15-18 ''
Msiipende dunia, wala mambo yaliyomo katika dunia. Mtu akiipenda dunia, kumpenda Baba(MUNGU) hakumo ndani yake. Maana kila kilichomo duniani, yaani, tamaa ya mwili, na tamaa ya macho, na kiburi cha uzima, havitokani na Baba(MUNGU), bali vyatokana na dunia. Na dunia inapita, pamoja na tamaa zake, bali yeye afanyaye mapenzi ya MUNGU adumu hata milele. Watoto, ni wakati wa mwisho; na kama vile mlivyosikia kwamba mpinga Kristo yuaja, hata sasa wapinga Kristo wengi wamekwisha kuwapo. Kwa sababu hiyo twajua ya kuwa ni wakati wa mwisho.''

 MUNGU akubariki na pia Ukipenda kunisapoti kwa sadaka katika huduma yangu karibu sana na pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane nitakujulisha jinsi ya kukipata.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa BWANA YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
0714252292.
0786719090
mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu.

Comments