Je unataka kazi na wewe ni muombaji kwa MUNGU?

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
Bwana YESU atukuzwe ndugu yangu.
Je unataka kazi na wewe ni muombaji kwa MUNGU?
Omba katika jina la YESU KRISTO na kisha tafuta hiyo kazi utaipata. 

Lakini utakatifu ni lazima uwe pamoja na wewe.
Usiombe tu na kubaki nyumbani Bali omba kisha tafuta ndipo utamuona MUNGU akikufanikisha.


Kwenye maombi yako hayo ya kupata kazi fanya hivi:

1. Ombea kibali cha MUNGU cha kuipata hiyo kazi.

2. Imiliki hiyo kazi katika ulimwengu wa roho kwa maombi katika jina la YESU KRISTO.

3. Ombea neema ya MUNGU iwe pamoja na wewe katika kufanikiwa kuipata hiyo kazi.

4. Watiishe wahusika wote wanaohusika na hiyo interview.

5. Kataa vizuizi vya kipepo vya kukuzuia kupata hiyo kazi.

6. Omba MUNGU awe pamoja na wewe katika yote.

7. Jizingire kwa damu ya YESU na tiisha kila hila ya kukuzuia.

8. Mshukuru MUNGU kwa kukupa kazi mwahidi MUNGU kwamba utakuwa mwaminifu katika kumtolea zaka na sadaka.

Katika maombi hayo Tumia maandiko haya au na mengine zaidi kutoka kwenye Biblia utakayopenda kuyatumia.

Luka 1:37 " kwa kuwa hakuna neno lisilowezekana kwa MUNGU."
Kwa sababu hakuna jambo linaloshindikana kwa MUNGU basi omba kwa imani kwa MUNGU ili MUNGU afanye yale ambayo kwa akili za kibinadamu yameshindikana.
MUNGU afanye yale ambayo wewe kwa akili zako na elimu yako ulishindwa.
MUNGU afanye yale ambayo kwa juhudi yako ya kupata kazi hukufanikiwa, Mwite Bwana YESU akushindie na sasa utapata kazi nzuri uitkayo.

Yeremia 1:19 "Nao watapigana nawe; lakini hawatakushinda; maana mimi nipo pamoja nawe, asema BWANA, ili nikuokoe."

Unaweza ukakutana na upinzani kidogo kutoka kwa wachawi wanaopanga usipate kazi.
Inawezekana kuna mizimu ya  ukoo ambayo imekuwekea mipaka ili usifanikiwe katika kazi, pambana ukisambaratisha kila mizimu ya inayokuzuia kuipata hiyo kazi.
Inawezekana kuna ambao wanaitaka hiyo kazi unayoomba wewe na kwa jinsi hiyo wameenda waganga ili wewe uonekane mbaya na wao wapate kazi, hivyo pambana kwa jina la YESU KRISTO katika maombi.
 

Marko 9:23 "YESU akamwambia, Ukiweza! Yote yawezekana kwake aaminiye."

Imani ni uhakika wa mambo yajayo.
Mteule wa KRISTO akiamini kwa njia ya maombi katika jina la YESU KRISTO hakika atafanikiwa.
Usiombe kwa sababu tu unajua kuomba bali omba kwa imani na MUNGU atakufanikisha. 
 

Zaburi 50:14-15 "Mtolee MUNGU dhabihu za kushukuru; Mtimizie Aliye juu nadhiri zako. Ukaniite siku ya mateso; Nitakuokoa, na wewe utanitukuza."

Mwite MUNGU na hakika utashinda.
Mwite MUNGU na hakika utapata kazi hiyo uitakayo.
 Timiza nadhiri zako zote na utamtolea MUNGU shukrani pamoja na fungu la kumi  kila mshahara na sadaka.
 

Zaburi 68:20 "MUNGU kwetu sisi ni MUNGU wa kuokoa; Na njia za kutoka mautini zina YEHOVA Bwana."

Hapa ndio kiini kabisa cha mafanikio yako ya kupata hiyo kazi.
MUNGU kwako awe ni MUNGU wa kukuokoa kutoka wanaokupangia usipate kazi.
MUNGU kwako awe MUNGU wa kukupa kazi na kukubariki.
Njia za kutoka kwenye uharibifu na mikosi zina MUNGU tumia maombi kutoka katika njia hiyo za balaa na mikosi.
 
Mwanzo 39:21 " Lakini BWANA akawa PAMOJA NA Yusufu, AKAMFADHILI, AKAMPA KIBALI machoni pa mkuu wa gereza."

Mwambie MUNGU kwa njia ya maombi kwamba awe pamoja na wewe katika kupata kazi na katika kuishi katika kazi hiyo kwa mafanikio.
Mwambie MUNGU  akufadhili.
MUNGU akiwa mfadhili wako hakuna adui atakugusa ili kukuharibia usifanikiwe.
Mwambie MUNGU  akupe kibali cha kupata kazi na kibali na kuishi katika kazi hiyo na kibali cha kufanikiwa katika kazi hiyo.

Yeremia 32:27 "Tazama, mimi ni BWANA, Mungu wa wote wenye mwili; je! Kuna neno gumu lo lote nisiloliweza?"

Hakuna jambo hata moja la kumshinda MUNGU.
Ukilijua hilo mtegemee MUNGU na Muombe hakika atakufanikisha maana yeye BWANA anaweza yote.
 
Baada ya hapo nakutakia kazi njema maana utapata kazi hiyo utakayoiendea.
Zingatia tu maombi na utakatifu na kumtii MUNGU kwenye kazi yako.
Najua kuna watu kadhaa wengi waliokusudiwa na MUNGU watapata kazi, ndugu usisahau kunijulisha nami nimshukuru MUNGU kwa ufunuo huu na kumtukuza.


 MUNGU akubariki na pia Ukipenda kunisapoti kwa sadaka yako ya hiari katika huduma yangu karibu sana na pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane nitakujulisha jinsi ya kukipata.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa BWANA YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
0714252292.
0786719090
mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu.

 Ubarikiwe sana na nakutakia kazi njema utakayoipata.

Comments