KAA KATIKA MUNGU ALIYE HAI NA UMWABUDU YEYE PEKE YAKE.

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU
Bwana YESU atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.
Katika jamii ya leo Kila mtu na muono wake.
Kuna watu husema hakuna kama mama.
Kuna watu husema hakuna kama baba.
Kuna watu husema hakuna kama baba wa taifa kwenye mataifa yao.
Kuna watu husema hakuna kama baba watakatifu wao.
Kuna wengine husema hakuna kama mitume wao, japo ni mitume wa uongo.
Kuna watu husema hakuna kama maaskofu wao.
Kuna wengine husema hakuna Kama mwanasoka Fulani.
Kuna watu husema hakuna kama kama mwanamziki Fulani.
Kuna wengine husema hakuna kama wao wenyewe.
  Biblia inasema hiviiiii.
Hakuna Kama JEHOVAH MUNGU muumbaji.

Zaburi 83:18 "Wajue ya kuwa Wewe, uitwaye jina lako YEHOVA, Ndiwe peke yako Uliye juu, juu ya nchi yote."

Ndani ya JEHOVAH kuna Mwokozi  YESU KRISTO.
Ndani ya JEHOVAH kuna ROHO MTAKATIFU aliye kiongozi  na Mwalimu wetu.
Kabla ya mwaka huu wa 2017  haujaanza yaani Wiki ya mwisho ya mwaka 2016 nilisikia sauti ikiniambia Neno hili la kweli la MUNGU  "Hapana hata mmoja aliye kama wewe, Ee BWANA; wewe ndiwe uliye mkuu, na jina lako ni kuu katika uweza.-
Yeremia 10:6"
Hakika ni kweli hakuna aliye kama MUNGU.
Watu wengi wanamjua MUNGU vyema lakini tatizo kubwa ni kukubali kurudishwa nyuma na mambo ya dunia.
Ndugu ngoja nikushauri mambo yafuatayo;
Kuwa kwenye wakati mgumu sio sababu ya kuacha kumwabudu MUNGU katika Roho na kweli.
Biblia inakutaka umwabudu MUNGU katika Roho na kweli.
Yohana 4:24 '' MUNGU ni ROHO, nao wamwabuduo yeye imewapasa kumwabudu katika roho na kweli.''

Kuwa kwenye mazingira magumu isiwe sababu ya kuacha kumwabudu MUNGU katika kweli yake.


Kuoa au kuolewa isiwe sababu ya kukufanya upunguze kumwabudu MUNGU Baba.


Kupata kazi nzuri isiwe kigezo cha kukufanya upunguze kumwabudu MUNGU Baba.


Kwenda safari ya mbali isiwe sababu ya kuacha kumwabudu MUNGU.


Kuwa gerezani au mahabusu isiwe sababu ya kuacha kumwabudu MUNGU.
Mazingira na nyakati tulizopo havitakiwi kutupunguzia sisi chochote katika kumwabudu MUNGU Muumba wetu.

MUNGU anataka tumwabudu.

Zaburi 29:2 '' Mpeni BWANA utukufu wa jina lake; Mwabuduni BWANA kwa uzuri wa utakatifu.''  

MUNGU Anataka tumwabudu katika roho na kweli.
Anataka ibada yetu ijae kweli na haki na utakatifu.
Maisha yetu yanatakiwa kuwa maisha mema, ya haki na matakatifu.
MUNGU anawatafuta waabudio halisi ambao humwabudu yeye katika Roho na kweli.


Yohana 4:23 '' Lakini saa inakuja, nayo sasa ipo, ambayo waabuduo halisi watamwabudu BABA(MUNGU) katika roho na kweli. Kwa maana BABA  awatafuta watu kama hao wamwabudu.''

Bwana YESU alipokuja alitangaza uhalisi wa kumwabudu MUNGU.
Kwa sababu Wokovu wa KRISTO ndio mwanzo wa kumwabudu MUNGU.
Mwanadamu akiwa nje na KRISTO hakika huyo anaabudu asichokijua.
Kuokoka ndio mwanzo wa kuabudu katika kweli.

Yohana 1:12-13 ''Bali wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa MUNGU, ndio wale waliaminio jina lake; waliozaliwa, si kwa damu, wala si kwa mapenzi ya mwili, wala si kwa mapenzi ya mtu, bali kwa MUNGU.''

MUNGU Baba anawatafuta waabuduo halisi ili wamwabudu.
Ni saa ya kumwabudu MUNGU Baba katika kweli.

Leo katika ibada nyingi kuna tatizo.
Watu wengi huenda kanisani, wanaimba na kucheza vizuri wakati wa ibada.
Ni vizuri lakini naomba niseme kwamba kuimba na kucheza hakuwezi kumjenga mtu huyo kiroho.
Neno la MUNGU ndilo linatakiwa liwe la kwanza na muhimu katika kumbariki mtu katika ibada aliyohudhuria.
Watu wengi ukiwauliza wamebarikiwa na nini katika ibada hutaja waimbaji au waliokuwa wanacheza.
Akili za watu wengi zimetekwa na kuimba na kucheza hata hawana habari na neno la MUNGU tena.
Leo katika makanisa mengi watu kikiisha tu kipindi cha kusifu na kuabudu huondoka kanisani.
Kwa wakristo wenye akili hakika neno la MUNGU ndilo lingepewa kipaumbele.
Nyimbo na kusifu kwa kucheza ni jambo jema sana na la muhimu sana lakini hivyo haviwezi kumjenga mtu kiroho. Neno la MUNGU ndilo muhimu kuliko yote na hilo pekee ndilo linaweza kumjenga mtu kiroho.
Huwezi ukawa mtakatifu kwa kuimba, Bali utakuwa mtakatifu kwa kulizingatia neno la MUNGU na kulitii.
Huwezi ukawa mtakatifu kwa kucheza step nzuri, Bali utakuwa mtakatifu kwa kulizingatia neno la KRISTO na kulitii.
Huwezi kuwa mtakatifu kwa sababu una sauti nzuri na nyororo ya kuimba, Bali utakuwa mtakatifu kwa kulizingatia neno la MUNGU na kulitii.
Ni neno la MUNGU tu ndio linalotakiwa kuzingatiwa na kupewa kipaombele na kila Mkristo.
Ndugu zangu, ni muhimu sana tukazingatia neno la MUNGU zaidi ya mengine yote.

1 Petro 2:2 ''Kama watoto wachanga waliozaliwa sasa yatamanini maziwa ya akili yasiyoghoshiwa(Neno la MUNGU), ili kwa hayo mpate kuukulia wokovu;''

Kila mwanadamu anayetaka kumwabudu MUNGU katika kweli yake basi inampasa ndugu huyo kumpokea YESU kama Mwokozi wake kwanza.
YESU ni Alfa na omega.
YESU ni mwanzo na mwisho.
Wahurumieni wanaong'ang'ania dini huku hawana YESU moyoni mwao.

Yoshua 4:23 ''  Basi sasa, iondoeni miungu migeni iliyo kati yenu, mkaielekeze mioyo yenu kwa BWANA, Mungu wa Israeli. ''

Waokoeni katika moto kwa kuwaleta kwenye wokovu wa YESU KRISTO.
Yuda 1:21-23 '' jilindeni katika upendo wa MUNGU, huku mkingojea rehema ya Bwana wetu YESU KRISTO, hata mpate uzima wa milele. Wahurumieni wengine walio na shaka, na wengine waokoeni kwa kuwanyakua katika moto; na wengine wahurumieni kwa hofu, mkilichukia hata vazi lililotiwa uchafu na mwili.''

Wasaidieni waliong'ang'ania dhehebu huku hawana wokovu ndani yao.
Wasaidieni wana dini wanaomwabudu shetani wakidhani ni MUNGU, wamejitenga na KRISTO kwa kufuata dini ya majini.

Watu wengi husema wanamheshimu MUNGU.
Lakini matendo yao hayaonyeshi kwamba wanamheshimu MUNGU.


Kumheshimu MUNGU kunahusisha haya yafuatayo.
1. Kumcha MUNGU na kumwabudu yeye peke yake.
 1 Samweli 12:24 '' Mcheni BWANA tu, mkamtumikie kwa kweli kwa mioyo yenu yote; maana, kumbukeni jinsi alivyowatendea mambo makuu. ''

2. Kutoa zaka na sadaka sahihi.
Mithali 3:9 "Mheshimu BWANA kwa mali yako, Na kwa malimbuko ya mazao yako yote."


3. Kwa kulitii Neno la MUNGU.
 Zaburi 119:11 '' ''Moyoni mwangu nimeliweka neno lako, Nisije nikakutenda dhambi.''

4. Kwa kumpokea YESU kama Mwokozi na kumtii.
 Yohana 3:16-18 '' Kwa maana jinsi hii MUNGU aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele. Maana MUNGU hakumtuma Mwana ulimwenguni ili auhukumu ulimwengu, bali ulimwengu uokolewe katika yeye. Amwaminiye yeye hahukumiwi; asiyeamini amekwisha kuhukumiwa; kwa sababu hakuliamini jina la Mwana pekee wa MUNGU.''
 
5. Kwa kutubu dhambi zote na kuziacha.
Isaya 55:6-7 ''Mtafuteni BWANA, maadamu anapatikana, Mwiteni, maadamu yu karibu; Mtu mbaya na aache njia yake, Na mtu asiye haki aache mawazo yake; Na amrudie BWANA, Naye atamrehemu; Na arejee kwa MUNGU wetu, Naye atamsamehe kabisa. ''

Je unamweshimu MUNGU?
Ndugu mweshimu MUNGU na timiza kusudi la kuokolewa kwako na Bwana YESU.


Kwa kuwa sasa uko kwa Bwana YESU Furaha yangu ni wewe ushinde kila hila ya Giza.
Neno hili likaongeze ushindi katika ushindi wako unaotokana na maombi yako.

Isaya 35:4 "Waambieni walio na moyo wa hofu, Jipeni moyo, msiogope; tazama, MUNGU wenu atakuja na kisasi, na malipo ya MUNGU; atakuja na kuwaokoa ninyi."
Jipe moyo maana MUNGU atakushindia.
Usiogope maana MUNGU atawapiga maadui zako.
MUNGU atakuokoa na kila hila.
MUNGU akubariki na pia Ukipenda kunisapoti kwa sadaka yako ya hiari katika huduma yangu karibu sana na pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane nitakujulisha jinsi ya kukipata.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa BWANA YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
0714252292.
0786719090
mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu

Comments