MADHARA MATANO(5) YA KUTOKA NJE YA NDOA.

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
Bwana YESU atukuzwe ndugu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.
Leo nazungumzia jambo ambalo limekuwa tatizo katika jamii na limewaangamiza wengi wakakosa mbingu.

Mithali 14:12  ''Iko njia ionekanayo kuwa sawa machoni pa mtu, Lakini mwisho wake ni njia za mauti.''

 Kuna watu Kufanya dhambi ya uzinzi  wakati mwingine wao huona kama ni faida lakini hiyo ni njia ya mauti.
Kutoa nje ya ndoa ni njia ya mauti.
Njia ya mauti maana yake ni njia ya uharibifu na uharibifu huo unaweza kumtokea mhusika asipotubu  na kuacha.
Kwanini nasema hivyo?
Ni kwa sababu Maamuzi mabaya ya mtu hutengeneza kuharibikiwa kwa mtu huyo baadae.
 Unaweza ukaamua maamuzi ya kuisaliti ndoa yako lakini maamuzi hayo yakazaa kifo au kilema baada ya wewe kufumaniwa.
Unaweza ukaanzisha maamuzi hayo maamuzi hayo yakazaa jehanamu.
Biblia inaonye ikisema ''Uache mabaya ukatende mema, Utafute amani ukaifuatie.-Zaburi 34:14''

Kila mwanadamu anapaswa kuwa na maamuzi mazuri na sio maamuzi mabaya.
Maamuzi mazuri ya mtu hutengeneza ushindi wake baadae.
Maamuzi mazuri ya kwanza ni kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi.
Maamuzi mazuri ya pili ni kuishi maisha matakatifu ya Wokovu wa KRISTO.
Maamuzi mazuri ya tatu ni kuenenda kwa ROHO MTAKATIFU ukiwa ndani ya KRISTO.
Maamuzi mazuri ya nne ni kusoma Biblia na kulitii Neno la MUNGU.
Ni vyema sana kufanya maamuzi mazuri.

Watu wengi badala ya kufanya maamuzi mazuri wao hufanya maamuzi mabaya.
Maamuzi mabaya ya kwanza ni kuabudu shetani.
Maamuzi mabaya ya pili ni kutenda dhambi ikiwemo na dhambi ninayoizungumzia leo ya kutoka nje ya ndoa.
Maamuzi mabaya ya tatu ni kwenda kwa waganga wa kienyeji.
Maamuzi mabaya ya nne ni kuwa mpinga Kristo.
Ndugu, maamuzi mabaya kutengeneza kuharibikiwa sana.
Nakushauri amua maamuzi mazuri.

 Usikubali kuendelea na uzinzi na usaliti maana ni hatari kwako.
Usishupaze shingo na wala usiwe na kiburi kwa kujiona salama tu wakati uzinzi huo utakuangamiza usipotubu na kuacha.
Kumbuka Biblia inasema ''Kila mwenye moyo wa kiburi ni chukizo kwa BWANA; Hakika, hatakosa adhabu.-Mthali 16:5''

Uzinzi ni njia lakini ni njia ya mauti na ni njia ya uharibifu.
Uzinzi ni dhambi ya ngono anayofanya mtu aliye kwenye ndoa, yaani akitoka nje ya ndoa yake.
Uasherati ni dhambi ya ngono anayoifanya Mtu ambaye hajaingia katika ndoa.
Ndugu usikubali kuwa mzinzi na usikubali kuwa mwasherati.
Kumbuka waasherati na wazinzi makazi yao ni jehanamu wasipotubu sasa.

1 Wakorintho 6:9-10 " Au hamjui ya kuwa wadhalimu hawataurithi ufalme wa MUNGU? Msidanganyike; waasherati hawataurithi ufalme wa MUNGU, wala waabudu sanamu, wala wazinzi, wala wafiraji, wala walawiti, wala wevi, wala watamanio, wala walevi, wala watukanaji, wala wanyang'anyi."

Madhara ya kutoka nje ya ndoa wala sio matano tu ila ni mengi sana. Kwa leo nakuletea haya matano ili ikusaidie kutengeneza kwa Mwokozi YESU .
 
                  Madhara  ya kutoka nje ya ndoa.

1. Ni dhambi na dhambi huzaa mauti yaani kutengwa na MUNGU.

 Yakobo 1:14-16 '' Lakini kila mmoja hujaribiwa na tamaa yake mwenyewe huku akivutwa na kudanganywa. Halafu ile tamaa ikiisha kuchukua mimba huzaa dhambi, na ile dhambi ikiisha kukomaa huzaa mauti. Ndugu zangu wapenzi, msidanganyike.''
Ndugu, kama tamaa ndio imekudanganya basi tambua kwamba tamaa hiyo mbaya ya kuisaliti ndoa yako itazaa mtoto anayeitwa dhambi na dhambi mwisho itazaa mauti.
Mauti ni uharibifu unaoweza kuupata lakini usipopata neema ya kutubu na kuacha utapata uharibifu mkubwa zaidi uitwao jehanamu.
Ufunuo 20:11-15 ''Kisha nikaona kiti cha enzi, kikubwa, cheupe, na yeye aketiye juu yake; ambaye nchi na mbingu zikakimbia uso wake, na mahali pao hapakuonekana. Nikawaona wafu, wakubwa kwa wadogo, wamesimama mbele ya hicho kiti cha enzi; na vitabu vikafunguliwa; na kitabu kingine kikafunguliwa, ambacho ni cha uzima; na hao wafu wakahukumiwa katika mambo hayo yaliyoandikwa katika vile vitabu, sawasawa na matendo yao. Bahari ikawatoa wafu waliokuwamo ndani yake; na Mauti na Kuzimu zikawatoa wafu waliokuwamo ndani yake. Wakahukumiwa kila mtu kwa kadiri ya matendo yake. Mauti na Kuzimu zikatupwa katika lile ziwa la moto. Hii ndiyo mauti ya pili, yaani, hilo ziwa la moto. Na iwapo mtu ye yote hakuonekana ameandikwa katika kitabu cha uzima, alitupwa katika lile ziwa la moto ''

2. Kuingia agano la kishetani.

 Warumi 6:16,18 '' Au hamjui ya kuwa yeye aliyeungwa na kahaba ni mwili mmoja naye? Maana asema, Wale wawili watakuwa mwili mmoja. Ikimbieni zinaa. Kila dhambi aitendayo mwanadamu ni nje ya mwili wake; ila yeye afanyaye zinaa hutenda dhambi juu ya mwili wake mwenyewe.''
Biblia inasema jambo muhimu kwamba ni heri kuikimbia zinaa. uzinzi ni zinaa na tukio hilo ni kuingia agano la kipepo.
Unapoisaliti ndoa yako maana yake unaingia agano la kishetani.
Kumbuka una agano takatifu la ndoa na mkeo au mumeo hivyo unapotoka nje ya ndoa maana yake unaingia agani jingine na huyo mzinzi mwenzako na agano hilo ni la kishetani.
 Agano la kishetani lina madhara yake makubwa sana na mengi, siku moja nitafafanua kuhusu kipengele hicho tu lakini kwa ufupi yajua haya machache sana.
=Kuna watu katika baadhi ya koo tabia chafu za wazazi hata watoto wanajikuta wanaziendeleza kwa sababu ya agano la kishetani la wazazi.
=Unaweza kuangamia wewe na kisha kwa ujinga wako huo wa kuingia agano la kishetani na watoto wako ukawaangamiza  na  hadi wajukuu. Labda wao wampokee YESU na kufunguliwa kutoka mikataka ya kipepo ya wazazi ndipo hawatahusika na maagano yako.
=Kumbuka pia agano la kipepo ni la kipepo tu.
Unaweza ukatembea na huyo mzinzi na kisha akakufunga ufahamu kipepo hadi ukavunja ndoa yako sahihi na kwa njia hiyo ukabaki mzinzi maisha yako yote, kisha jehanamu.
Biblia kwa usahihi kabisa inakushauri baba na mama uliye mwanandoa kwamba usikubali kutoka njea ya Ndoa yao.
Ukishaolewa na mtu akikutongoza muone huyo kama kahaba tu.
Ukishaoa na mwanamke mwingine anakufuatilia ili akupate kimapenzi, huyo muone tu kama kahaba anayejiuza.
Biblai inakushauri
Mithali 6:25-29 '' Usiutamani uzuri wake moyoni mwako; Wala usikubali akunase kwa kope za macho yake. Maana kwa malaya mtu hutiwa katika hali ya kuhitaji kipande cha mkate; Na kahaba humwinda mtu anase nafsi yake iliyo ya thamani Je! Mtu aweza kuua moto kifuani pake, Na nguo zake zisiteketezwe? Je! Mtu aweza kukanyaga makaa ya moto, Na nyayo zake zisiungue? Ndivyo alivyo aingiaye kwa mke wa jirani yake; Kila mtu amgusaye huyo atakuwa na hatia.''

3. Ni kuonyesha huna akili hata moja maana Biblia inasema aziniye hana akili kabisa.

Mithali 6:32-33 ''Mtu aziniye na mwanamke hana akili kabisa; Afanya jambo litakalomwangamiza nafsi yake. Atapata jeraha na kuvunjiwa heshima; Wala fedheha yake haitafutika. ''
 Naipenda Biblia maana ndio msema ukweli wa mwisho.
Biblia inasema anayezini hana akili kabisa.
Hana akili kabisa maana yake hana akili zote yaani hana akili hata moja.
Ukweli ni kwamba  kama mzinzi angejua kwamba adhabu ya wazinzi wasiotubu na kuacha dhambi hiyo adhabu yao ni jehanamu ya moto hakika hakika asingekubali kuwa mzinzi maana kwa asili hakuna mwanadamu anayetaka kwenda jehanamu, lakini kukosa akili kunaweza kumfanya mtu akaenda huko.
Akili sahihi tunaipata katika Neno la MUNGU ambalo ndio mwongozo wa MUNGU kwetu kwamba tusikubali kufanya dhambi  zote ikiwemo uzinzi.
Uzinzi ndio usaliti wa ndoa maana uzinzi hufanywa na mtu aliye katika ndoa akitoka nje ya ndoa yake.
Kama ndugu huyo atazini na mtu ambaye hayuko katika ndoa yeye atabaki kuwa mzinzi na huyo wa pili ataendelea kuwa mwasherati, na tendo wanalolifanya linatwa dhambi ya uzinifu, ni hatari sana.
Ndugu unahitaji kuwa na akili  na akili njema ni hii ya Neno la MUNGU ''Ndoa na iheshimiwe na watu wote, na malazi yawe safi; kwa maana waasherati na wazinzi Mungu atawahukumia adhabu-Waebrania 13:4''
MUNGU anataka uiheshimu ndoa yako mama na MUNGU anataka uiheshimu ndoa yako baba maana ukitoka nje umezini yaani umekuwa mzinzi, na Biblia iko wazi sana kwamba wazinzi watakuhumiwa na MUNGU.
Na hukumu hiyo ni hii  ''Basi matendo ya mwili ni dhahiri, ndiyo haya, uasherati, uchafu, ufisadi, ibada ya sanamu, uchawi, uadui, ugomvi, wivu, hasira, fitina, faraka, uzushi, husuda, ulevi, ulafi, na mambo yanayofanana na hayo, katika hayo nawaambia mapema, kama nilivyokwisha kuwaambia, ya kwamba watu watendao mambo ya jinsi hiyo hawataurithi ufalme wa Mungu.-Wagalatia 5:19-21''

4. Magonjwa ya zinaa.

Madhara haya  yapo na ni wengi naamini umewaona wameathirika na ukimwi na magonjwa mengine ya zinaa.
Wengi wanaacha watoto wao katika umri mdogo kwa sababu ya ukimwi.
Wengi wanaacha wapendwa wao kwa sababu ya uzinzi walioufanya. 
Jiulize ndugu, unaamua kuwa msaliti wa ndoa yako na unakufa kwa ukimwi huku ukiwaacha wanao wakiwa na umri wa miaka 3 na ndugu wanagawana mali zako bila hata kuwajali watoto wako maana wewe haupo. Unaleta mateso makubwa kwa watoto wako kwa sababu ya starehe ya muda mfupi tu iitwayo uzinzi.
Ndugu, haipasi kuwa hivyo.
Unaweza kufanya uzinzi kwa kutumia kondomu lakini Biblia inasema kwamba kazi ya shetani ni kuiba, kuharibu na kuchinja(Yohana 10:10A ''Mwivi haji ila aibe na kuchinja na kuharibu;''
Kwa njia hiyo naomba utambue kwamba shetani aliyekushawishi uisaliti ndoa yako ndiye huyo huyo atakushawishi uache kutumia kondomu na ndio huyo huyo atakuangamiza maana huna ulinzi wa MUNGU kwa sababu ya uasi wako kwa MUNGU.
Unaweza ukatumia kondomu kwa muda lakini ipo siku utaacha na shetani ameshakutegea gonjwa na hapo unaweza kuiangamiza hatima yako.
Andiko tuliloanza nalo katika somo hili linasema
Mithali 14:12  ''Iko njia ionekanayo kuwa sawa machoni pa mtu, Lakini mwisho wake ni njia za mauti.''
 Mauti maana yake uharibifu na uharibifu huo unaweza kuwa magonjwa uliyoyapata baada ya dhambi ya uzinzi.

5. Kumtumikia shetani.

Kumtumikia shetani ni pamoja na kufanya yale ambayo shetani anayapenda.
Uzinzi au usaliti wa ndoa ni moja ya vitu shetani anapenda hivyo unavyofanya dhambi hiyo unakuwa unamtumikia shetani.
Kumbuka sasa kwamba wanaomtumikia shetani sehemu yao wakifa sio mbinguni bali kuzimu aliko shetani
Zaburi 9:17 '' Wadhalimu watarejea kuzimu, Naam, mataifa yote wanaomsahau MUNGU.''
 
Madhara mengine unaweza ukapoteza Mali zako bure, huku familia yako ikilala na njaa.
Nini nataka nikushauri ndugu?
 Mpende Mkeo/Mumeo kwa sababu MUNGU ametaka umpende.
Usimpende kwa sababu ya unene maana wakati mwingine anaweza kukonda.
Usimpende kwa sababu ni mrefu, maana wakati mwingine anaweza kuja kuwa mfupi baada ya ajali.
Usimpende kwa sababu ana uso mzuri Sana, wakati mwingine anaweza kuwa na uso mzuri lakini hazai.
Unatakiwa umpende Mumeo/Mkeo kwa sababu huyo ni wako wa pekee. 

 MUNGU akubariki na pia Ukipenda kunisapoti kwa sadaka yako ya hiari katika huduma yangu karibu sana na pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane nitakujulisha jinsi ya kukipata.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa BWANA YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
0714252292.
0786719090
mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu.

Comments