NABII WA KWELI NA NABII WA UONGO

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU
Bwana YESU atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.
Ndugu mmoja aliniambia kwamba huduma ya kinabii haipo maana  ilikomea kwa Yohana mbatizaji maana waebrania inasema wakati huu MUNGU anazungumza nasi kupitia mwana sio manabii tena kama zamani.
Waebrania 1:1-4 ''MUNGU, ambaye alisema zamani na baba zetu katika manabii kwa sehemu nyingi na kwa njia nyingi, mwisho wa siku hizi amesema na sisi katika Mwana(YESU), aliyemweka kuwa mrithi wa yote, tena kwa yeye aliufanya ulimwengu. Yeye kwa kuwa ni mng'ao wa utukufu wake na chapa ya nafsi yake, akivichukua vyote kwa amri ya uweza wake, akiisha kufanya utakaso wa dhambi, aliketi mkono wa kuume wa Ukuu huko juu;  amefanyika bora kupita malaika, kwa kadiri jina alilolirithi lilivyo tukufu kuliko lao.'
Nilimjibu huyo ndugu na akanielewa.
Ndugu zangu, Huduma ya kinabii ipo na inatenda kazi kama huduma nyingine za ROHO MTAKATIFU.
Waefeso 4:11-15 '' Naye alitoa wengine kuwa mitume, na wengine kuwa manabii; na wengine kuwa wainjilisti na wengine kuwa wachungaji na waalimu; kwa kusudi la kuwakamilisha watakatifu, hata kazi ya huduma itendeke, hata mwili wa KRISTO ujengwe; hata na sisi sote tutakapoufikia umoja wa imani na kumfahamu sana Mwana wa MUNGU, hata kuwa mtu mkamilifu, hata kufika kwenye cheo cha kimo cha utimilifu wa KRISTO; ili tusiwe tena watoto wachanga, tukitupwa huku na huku, na kuchukuliwa na kila upepo wa elimu, kwa hila ya watu, kwa ujanja, tukizifuata njia za udanganyifu. Lakini tuishike kweli katika upendo na kukua hata tumfikie yeye katika yote, yeye aliye kichwa, KRISTO.''
Kwa sababu MUNGU ameteua watu ili wamtumikie kila mmoja kulingana na huduma yake, basi hiyo inatupa uhakika kwamba huduma zote tano zinafanya kazi.
Mitume wapo leo na wanatimiza huduma hiyo waliyopewa na ROHO MTAKATIFU.
Manabii wapo na wanatimiza huduma hiyo waliyopewa na ROHO MTAKATIFU.
Wainjilisti wapo na wanatimiza huduma hiyo waliyopewa na ROHO MTAKATIFU.
Wachungaji wapo na wanatimiza huduma hiyo waliyopewa na ROHO MTAKATIFU.
Walimu wapo na wanatimiza huduma hiyo waliyopewa na ROHO MTAKATIFU.
Shida ya Kanisa la leo ni kuoa huduma moja ni bora kuliko huduma nyingine wakati Biblia haifundishi hivyo.
Changamoto ya Kanisa la leo ni watu kujiita na kujipachika majina kwa lengo ambalo sio zuri.
Kuna makanisa leo Ukiwa mwinjilisti baadae unapandishwa cheo na kuwa Mchungaji, baadae Mchungaji anaweza akapanda cheo na kuwa Mtume, Mtume huyo akipanda cheo anakuwa Nabii na Nabii huyo akipanda cheo anakuwa Mtume na nabii, hayo yote wala sio kibiblia bali ni mipango ya wanadamu ili tu kujitofautisha na wengine.
Kwangu MUNGU ameweka huduma ya ualimu, haiwezekani eti baadae niwe mtume wakati ndani yangu nina huduma ya ualimu. Ualimu peke yake unatosha kufanya kazi ya MUNGU kuliko hata nabii wakati mwingine, inategemeana na mipaka ambayo MUNGU amekupa. Kuna watu katika huduma zao wamepewa taifa na wengine mataifa na wengine miji tu au maeneo fulani tu.
Kuna makundi matano ya mitazamo ya watu kuhusu huduma ya Kinabii.
1.  Kuna watu huamini kila mtu akiitwa nabii basi huyo ni nabii wa uongo anayezungumzwa katika Biblia.
2.  Kuna watu huamini Nabii ni mkuu kuliko Mtume, Mchungaji, Mwalimu na Mwinjilisti.
3.  Kuna watu wahaamini kama kwa sasa kuna nabii yeyote .
4.  Kuna watu katika madhehebu yao hawataki aweko nabii maana nabii ni jina kubwa mno kuliko yote.
5. Kuna watu hudhani kwamba Mtu akipewa karama ya unabii basi huyo anatafuta tu sifa na wengine wadharaulike.

Ndugu zangu naomba tujue kwamba mitazamo hiyo yote ni feki.
Kama hauamini kama manabii wapo basi hata wachungaji na wainjilisti hawapo, hata walimu hawapo na hata mitume hawapo; kwa sababu Biblia inazungumza kwamba huduma hizo zote zipo na zinafanya kazi.
Ingekuwa vyema zaidi kwa watu kutaka kumjua nabii wa kweli na nabii wa uongo maana waongo wengi sana wamejipenyeza katika Kanisa ili kudanganya watu wa MUNGU pia.
 1 Kor 12:4-11 ''Basi pana tofauti za karama; bali ROHO ni yeye yule.  Tena pana tofauti za huduma, na Bwana(YESU) ni yeye yule. Kisha pana tofauti za kutenda kazi, bali MUNGU ni yeye yule azitendaye kazi zote katika wote.  Lakini kila mmoja hupewa ufunuo wa ROHO kwa kufaidiana. Maana mtu mmoja kwa ROHO apewa neno la hekima; na mwingine neno la maarifa, apendavyo ROHO yeye yule; mwingine imani katika ROHO yeye yule; na mwingine karama za kuponya katika ROHO yule mmoja; na mwingine matendo ya miujiza; na mwingine unabii; na mwingine kupambanua roho; mwingine aina za lugha; na mwingine tafsiri za lugha; lakini kazi hizi zote huzitenda ROHO huyo mmoja, yeye yule, akimgawia kila mtu peke yake kama apendavyo yeye. ''

Tukirudi katika Swali la ndugu aliyesema kwamba anatambua tu kwamba MUNGU hasemi na sisi kwa kupitia manabii bali anazungumza na sisi kupitia Bwana YESU tu.
Hiyo waebrania inasema kwamba MUNGU zama hizi anazungumza na sisi kupitia YESU KRISTO pekee, maana yake kama yuko nabii au mtume kama ni wa MUNGU basi huyo lazima awe ameokolewa na Bwana YESU na awe anadumu katika Wokovu wa KRISTO huku akiishi maisha matakatifu.
MUNGU anazungumza nasi kupitia YESU lakini na YESU naye anaongea na sisi kupitia Neno lake na Neno hilo linafanya kazi kupitia huduma tano za ROHO MTAKATIFU, Na huduma hizo mojawapo ni huduma ya unabii.
 Ila ni muhimu kujua kwamba kuna tofauti kati ya nabii na huduma ya unabii. MUNGU anaweza akakupa unabii na bado wewe ukawa sio nabii. Waliotengwa kuwa manabii wapo ila na kanisa yaani mkristo aliyeokoka anaweza kupewa unabii lakini asiwe nabii maana hajatengwa na ROHO MTAKATIFU kwa ajili ya kuwa nabii ila kwa sababu anaye ROHO MTAKATIFU basi huyo ROHO MTAKATIFU ndiye huyo pia hutoa roho ya unabii na huduma ya unabii na ni huyo pia anayeweza kumteua mtumishi wake awe nabii. 
Nabii wa MUNGU lazima awe na ROHO MTAKATIFU na amtii ROHO MTAKATIFU na ROHO MTAKATIFU ndiye pia mwandishi wa Biblia hivyo unabii unapimwa kwa Neno la MUNGU, ukiona nabii anaenda kinyume na  injili ya KRISTO huyo sio nabii wa MUNGU. 
Kumbuka Neno hili '' Mkijua kwanza neno hili ya kwamba katika siku za mwisho watakuja na dhihaka zao watu wenye kudhihaki, wafuatao tamaa zao wenyewe,-2 petro 3:3''
Hizi ni zama za siku za mwisho na waongo wengi wapo hakika wakijaribu kudanganya watu wa MUNGU kwa mafundisho.
Kumbuka Bwana YESU alitusaidia akisema ''kwa matunda yake mti hutambulikana.-Mathayo 12:33c ''
Kama mtu hutambulikana kwa sababu ya kazi zake azifanyazo basi hakika ni rahisi tu kumjua nabii wa kweli au wa uongo.
Lakini tujue jambo hili kwamba;Sio kila anayeitwa nabii ni nabii wa uongo. Kibiblia Nabii wa uongo ni mtu yeyote anayefundisha kinyume na Neno la KRISTO yaani Biblia.
Kuwa nabii wa uongo hakumo katika jina la kuitwa nabii bali unabii wa uongo ni pale unapofundisha watu wamwache YESU KRISTO mwenye uzima wao wa milele.
Kwanza MUNGU hahitaji tu mtu ajiite nabii au mwalimu au mtume au mchungaji au mwinjilisti bali kazi ndio imtambulishe.
Kuna watu hujiita Mchungaji wakati hajawahi kuwa na kondoo hata mmoja.
Kuna watu wanajiita wainjilisti wakati hawajawahi hata siku moja kuipeleka injili kwa kuwahubiria watu ili waokoke.
Kuna watu wanajiita mitume wakati hawajawahi kupanda kanisa hata moja.
Kuna watu wanajiita walimu wa Neno la MUNGU lakini hufundisha tu ujasiliamali na sio Wokovu.
Kuna  watu hujiita nabii wakati hata Biblia hawasomo na hawaijui, ndio maana hutoa unabii kutoka kwenye mioyo yao na macho yao na sio kutoka kwa MUNGU.
2 Yohana 1:7 '' Kwa maana wadanganyifu wengi wametokea duniani, wasiokiri ya kuwa YESU KRISTO yuaja katika mwili. Huyo ndiye yule mdanganyifu na mpinga KRISTO.'
Kwa jinsi hiyo tunagundua kwamba kila anayefundisha uongo ni nabii wa uongo hata kama anaitwa mchungaji au mwinjilisti.
Kila aliyeanzisha dini kinyume na KRISTO YESU huyo ni nabii wa uongo na hayuko mbinguni kama hakutubu kwa Bwana YESU.
Kila aliteanzisha dini au dhehebu na hamkubali YESU KRISTO kama Mwokozi wake huyo ni nabii wa uongo na hayuko mbinguni kama hakutubu kwa Bwana YESU.
Nimewahi kuulizwa sana maswali kuhusu manabii wa uongo na waulizaji wote huwatuhumu watumishi wanaoitwa nabii wakidhani hao ndio manabii wa uongo walionenwa na Biblia.
Ukweli ni kwamba hata mchungaji anaweza akawa nabii wa uongo kama anafundisha watu kinyume na KRISTO YESU.
Hata Askofu au mtume au mwinjilisti au padri anaweza akawa nabii wa uongo kama tu anawatoa watu kwenye wokovu wa KRISTO kupitia mafundisho yake ya uongo.

Ajabu ni kwamba leo unakuta Mkristo wa uongo anamwita mwenzake nabii wa uongo.
Hebu ngoja nijisomee Obadia 1:15 inayosema hivi.
'' Kwa maana hiyo siku ya BWANA i karibu juu ya mataifa yote; kama ulivyotenda, ndivyo utakavyotendwa; malipo yako yatakurudia juu ya kichwa chako mwenyewe.''

 Penye ukweli, uongo hujitenga,Kwenye uongo, Ukweli haukai.
 Watu wengi wameshikilia andiko la siku za mwisho watatokea manabii wa uongo, wamesahau pia watatokea na waalimu wa uongo na wakristo wa uongo. Na tukipinga kuwa hakuna manabii tunalipinga neno la MUNGU, Agano la kale manabii waliokuwepo na Agano jipya manabii wapo pia. Na ndani ya huduma tano za kanisa ipo ya nabii, tofauti ya nabii wa agano la kale na jipya ni kuwa agano la kale manabii walikuwa wanaongoza watu na agano jipya nafasi ya nabii ni huduma.

 Mtu akiokoka ROHO MTAKATIFU anaingia ndani yake na kuanza kumuongoza lakini pia mtu hiyo akiwa chini ya wa watumishi wa YESU KRISTO  basi kwa Yale asiyoyajua atajifunza kwao na kuwauliza wao kiasi kwamba kuna kuna nabii wa uongo anataka kumuondoa kwa YESU basi hataweza. Kwa mtu mchanga kiroho Mimi naamini wiki 3 zinamtosha kukua kiroho hata manabii wa uongo wasiweze kumuondoa kwa YESU. Ndani ya wiki 3 hizo akiwa anahudhuria kila ibada na akawa anaomba na kufunga na kusoma Neno la MUNGU kila muda na kulitafakari hilo hakika atakuwa kiroho ghafla.
2 Petro 2:1-3 '' Lakini kuliondokea manabii wa uongo katika wale watu, kama vile kwenu kutakavyokuwako waalimu wa uongo, watakaoingiza kwa werevu uzushi wa kupoteza, wakimkana hata Bwana(YESU) aliyewanunua, wakijiletea uharibifu usiokawia.  Na wengi watafuata ufisadi wao; na kwa hao njia ya kweli itatukanwa.  Na katika kutamani watajipatia faida kwenu kwa maneno yaliyotungwa; ambao hukumu yao tangu zamani haikawii, wala uvunjifu wao hausinzii.''

 Aliye wa MUNGU huyanena yaliyo ya KRISTO anayeokoa bila kuyapotoa. Biblia inatushauri kuzipima roho kwa Neno maana sio zote kutoka kwa MUNGU
Mtu akiitwa nabii harafu hana huo unabii huyo anajidanganya mwenyewe. Kama anaongea vitu kutoka kwenye tamaa zake na mipango ya kichwa chake kisha akawaaminisha watu kwamba huo ni unabii huyo ni hasara kwake. Kama kuna mtu anadhani kuwa na nabii ni cheo hakika huyo naye ni pole yake.

1Yohana 4:1-6 ''Wapenzi, msiiamini kila roho, bali zijaribuni hizo roho, kwamba zimetokana na MUNGU; kwa sababu manabii wa uongo wengi wametokea duniani. Katika hili mwamjua ROHO wa MUNGU; kila roho ikiriyo kwamba YESU KRISTO amekuja katika mwili yatokana na MUNGU.  Na kila roho isiyomkiri YESU haitokani na MUNGU. Na hii ndiyo roho ya mpinga Kristo ambayo mmesikia kwamba yaja; na sasa imekwisha kuwako duniani. Ninyi, watoto wadogo, mwatokana na MUNGU nanyi mmewashinda, kwa sababu yeye aliye ndani yenu ni mkuu kuliko yeye aliye katika dunia.  Hao ni wa dunia; kwa hiyo wanena ya dunia na dunia huwasikia Sisi twatokana na MUNGU. Yeye amjuaye MUNGU atusikia; yeye asiyetokana na MUNGU hatusikii. Katika hili twamjua ROHO wa kweli, na roho ya upotevu.''
 MUNGU akubariki na pia Ukipenda kunisapoti kwa sadaka yako ya hiari katika huduma yangu karibu sana na pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane nitakujulisha jinsi ya kukipata.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa BWANA YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
0714252292.
0786719090
mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu.

Comments