TOKA KATIKA ENEO AMBALO MAWAKALA WA SHETANI WAMEKUWEKA KATIKA ULIMWENGU WA ROHO.

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
Bwana YESU atukuzwe ndugu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.
Kuna watu wamewekwa kichawi katika maeneo fulani kwenye ulimwengu wa roho kwa sababu bado wao wako katika ufalme wa giza.
Watu ambao wanateswa na nguvu za giza, vifungo na laana ni kwa sababu wamekubali kuwekwa katika maeneo mabaya kwenye ulimwengu wa roho.
Katika ulimwengu wa roho adui amekuweka sehemu gani?
Ndugu, toka huko Leo walikokuweka mawakala wa shetani, toka kwa jina la YESU KRISTO mfalme wa uzima.

Watu wengi hawajui kama kuna kuhamishwa kutoka ufalme wa giza na kuwekwa katika ufalme wa nuru.
Kabla mtu hajaokoka alikuwa katika ufalme wa giza, Mtu huyo anapookolewa na Bwana YESU huhamishwa na kuwekwa katika ufalme wa MUNGU ambao pia huitwa ufalme wa nuru.

Wakolosai 1:13 ''Naye alituokoa katika nguvu za giza, akatuhamisha na kutuingiza katika ufalme wa Mwana wa pendo lake;''

MUNGU Baba ndiye hutuhamisha kutoka utawala wa giza na kutuweka katika Ufalme wa Mwana wa Pendo lake yaani ufalme wa Bwana YESU.
Ndugu ukiokoka hakikisha unahamishwa ili usihusike tena na ufalme wa giza.
Hakikisha haihamishwi roho yako tu bali na mwili wako wote na nafsi yako yote na mali zako zote na kila baraka yako hakikisha inahamishwa.
Tunahamishwa kwa maombi hivyo inatupasa sana kuwa waombaji.
Mkristo asiye na maombi huyo anaweza kujikuta bado hajahama kutoka utawala wa giza na kwa jinsi hiyo shetani atakuwa anamuonea.
Kumbuka  jambo hili ya kwamba kazi ya Bwana YESU ni kukuokoa na kazi ya kukombolewa ni juhudi yako wewe kwa YESU.
Inabidi kwa maombi yako uhakikishe shetani anaachia vitu vyako vyote ambavyo anaendelea kuvishikilia.
Kazi ya Bwana YESU ni kuharibu na kufuta nguvu zote za giza katika maisha yako hivyo omba na atakushindia. 

1 Yohana 3:8 ''atendaye dhambi ni wa Ibilisi; kwa kuwa Ibilisi hutenda dhambi tangu mwanzo. Kwa kusudi hili Mwana wa MUNGU alidhihirishwa, ili azivunje kazi za Ibilisi.''

Kumbe kwa kusudi hili Bwana YESU alidhihilishwa ili azivunje kazi zote za shetani katika maisha yako.
Leo Kwa jina la YESU KRISTO Mwambie shetani aiachie baraka yako.
Mwambie shetani aiachie ndoa yako na familia yako.
Waambie mawakala wa shetani waachie kibali chako.
Waambie waachie kibali chako cha kuoa/ kuolewa na waambie waachie kibali chako cha kufanikiwa kwako na kazi yako.
Kila kibali chako waambie wakiachie.
Kama walivyoachia roho yako hata ukaokolewa na Bwana YESU basi waambie waachie pia na vitu vyako vyote.
Mwambie shetani na wachawi wake waiachie elimu yako na vyeti vyako.
Mwambie shetani aiachie bishara yako na N.k.
Kuhamishwa na kukombolewa kunahitaji juhudi yako wewe kwa MUNGU.

Yohana 14:2-3 ''Nyumbani mwa BABA yangu mna makao mengi; kama sivyo, ningaliwaambia; maana naenda kuwaandalia mahali. Basi mimi nikienda na kuwaandalia mahali, nitakuja tena niwakaribishe kwangu; ili nilipo mimi, nanyi mwepo.''
 
YESU anakuandalia makao ya uzima wa milele, hivyo usikubali sasa kuwa katika eneo ambalo shetani amekuweka sasa katika maisha yako ya duniani.
Usikubali kuwa katika eneo sasa ambalo machawi wamekuweka kwenye ulimwengu wa roho.
Usikubali kuwa katika eneo ambalo wamekuweka waganga wa kienyeji.
Kumbuka kazi ya shetani na mawakala zake ni uharibifu tu hivyo usikubali kuwa katika eneo la uharibifu.

Kuna watu wamewekwa sasa kipepo katika eneo linaloitwa kukataliwa.
Kuna ambao wako katika eneo la kupuuzwa, kudharauliwa.
Kuna ambao wako leo katika eneo la kukosa kibali.
Kuna ambao wako leo katika eneo la madeni na kuonewa.
Ndugu leo hama katika maeneo hayo kwa jina la YESU KRISTO aliye hai.
Wachawi na waganga wanaweza kukuweka sasa katika eneo ambalo utagongwa na gari na kufa, eneo hilo la kipepo kwenye ulimwengu wa roho lifute kwa damu ya YESU KRISTO.
Kama wamekuweka kwenye eneo la kuumwaumwa tu toka Leo kwa jina la YESU KRISTO.
Kama wamekuweka katika eneo la wanaokataliwa, toka Leo kwa jina la YESU KRISTO.
Kama wamekuweka kwenye eneo la umasikini na kuonewa tu, toka Leo kwa jina la YESU KRISTO Mfalme wa uzima.
Ndugu nakuomba tafakari ninasemayo ili uombe.
Wewe wamekuweka katika eneo gani kwenye ulimwengu wa roho?


Toka huko kwa jina la YESU KRISTO na sasa kaa katika eneo ambalo MUNGU wamekuweka, kaa katika eneo la utakatifu na haki na maombi.
Kaa katika Wokovu wa KRISTO.
Kaa ndani ya YESU KRISTO.

Bwana YESU anasema tukae ndani yake  '' Kaeni ndani yangu, nami ndani yenu. Kama vile tawi lisivyoweza kuzaa peke yake, lisipokaa ndani ya mzabibu; kadhalika nanyi, msipokaa ndani yangu.-Yohana 15:4'

Kuna maeneo mengi mno unaweza ukakuta mawakala wa shetani wamekuweka sasa kwenye ulimwengu wa roho, wewe toka huko kwa damu ya YESU KRISTO na kwa jina la YESU KRISTO
Ushindi upo sehemu moja tu yaani ndani ya JEHOVAH MUNGU aliye hai.
Ndani ya JEHOVAH kuna jina la YESU KRISTO, damu ya YESU KRISTO na nguvu za ROHO MTAKATIFU.
Usikubali katika maisha yako kukaa katika eneo ambalo wamekuweka mawakala wa shetani.

Kuna watu hudhani kwamba akiongozwa sala ya toba tu basi amehama na vitu vyake vyote vimehama. Ndugu naomba nikuambie ukweli ya kwamba ukiongozwa sala ya toba hakika jina lako linaandikwa katika kitabu cha uzima mbinguni na tangu wakati huo wewe unakuwa mtakatifu kwa MUNGU kama hutarudi dhambini.
Lakini kuombolewa katika vitu vilivyokufunga inahitaji maombi zaidi na sio sala ya toba tu, ndio maana kuna watu huongozwa sala ya toba na watumishi na kisha watumishi wanawaombea na unashangaa nguvu za giza zinawaacha na vifungo vinakatika. Baada ya hapo inahitaji juhudi ya mtu huyo kwa MUNGU na maombi ya kudumu ndipo atastawi kiroho na atajua hata katika maeneo gani mengine anatakiwa kuombea ili yakombolewe.
Ndio maana nikasema mwanzo kwamba kazi ya Bwana YESU ni kukuokoa lakini kukombolewa ni juhudi yako kwa Bwana YESU.
Unaweza ukaokoka roho hakika lakini biashara yako ikawa bado haijakombolewa hivyo ni maombi na kujua kanuni ya MUNGU ndio vinahitajika ili kuikomboa biashara hiyo.

Kazi ya kuomba ni ya kila mteule wa MUNGU aliyeokolewa hivyo hata wewe unatakiwa sana kuwa muombaji ili kukomboa mambo mengine ambayo adui aliyakamata au kuyafunga.
Kumbuka watu wengi huwa tunaokoka kipindi tukiwa wakubwa na shetani anakuwa alishatuwahi siku nyingi kipindi ukiwa kwake.
Unaweza ukaokoka leo lakini shetani kabla ya wewe kupata neema alishakuweka katika chumba cha saba cha gereza ya kiroho hivyo ni juhudi yako kwa YESU kwa njia ya maombi na utakatifu kutoka katika vyumba hivyo vya kipepo ili uwe huru kabisa.
Ndugu inakupasa sana kuwa muombaji na husika zaidi na utakatifu pia.
Mambo manne(4) ambayo mtu akiokoka anatakiwa kuyashika ni siku zote ni .
1.  Kuishi maisha matakatifu.
2.  Kujifunza na kulitafakari Neno la MUNGU
3.  Kuishi maisha ya maombi.
4. Kumtumikia Bwana YESU.
Katika maombi ni muhimu pia kujua kwamba kuna maombi sahihi na maombi yasiyo sahihi.

Yakobo 4:3 "Hata mwaomba, wala hampati kwa sababu mwaomba vibaya, ili mvitumie kwa tamaa zenu."

 Kumbe kuna kuomba vizuri na kuomba vibaya.
Kumbe kuna maombi sahihi na maombi yasiyo sahihi.

Ngoja nikuambie maombi sahihi.

1.  Maombi sahihi ni maombi kwa MUNGU yanayoambatana na utakatifu.
Waebrania 12:14 ''Tafuteni kwa bidii kuwa na amani na watu wote, na huo utakatifu, ambao hapana mtu atakayemwona Bwana asipokuwa nao;''
Hakuna atakayemuona MUNGU asipokuwa na utakatifu.
Utamuona MUNGU baada ya maombi yako, utamuona MUNGU baada ya MUNGU kukutendea muujiza lakini ili umuone MUNGU ni lazima kwanza uombe ndipo umuone lakini pia maombi yako yaambatane na utakatifu.

2. Maombi sahihi ni maombi kwa MUNGU kupitia jina la YESU KRISTO.
Yohana 14:13-14 '' Nanyi mkiomba lo lote kwa jina langu, hilo nitalifanya, ili BABA atukuzwe ndani ya Mwana. Mkiniomba neno lo lote kwa jina langu, nitalifanya.'' 

3. Maombi sahihi ni maombi ya Imani katika jina la YESU KRISTO.
Waebrania 11:6 '' Lakini pasipo imani haiwezekani kumpendeza; kwa maana mtu amwendeaye MUNGU lazima aamini kwamba yeye yuko, na kwamba huwapa thawabu wale wamtafutao.'' 

4. Maombi sahihi ni maombi katika ROHO MTAKATIFU.
Yuda 1:20-21 ''Bali ninyi, wapenzi, mkijijenga juu ya imani yenu iliyo takatifu sana, na KUOMBA katika ROHO MTAKATIFU, jilindeni katika upendo wa MUNGU, huku mkingojea rehema ya Bwana wetu YESU KRISTO, hata mpate uzima wa milele.'

5. Maombi sahihi ni maombi sawa sawa na mapenzi ya MUNGU.
1 Yohana 5:14 ''Na huu ndio ujasiri tulionao kwake, ya kuwa, tukiomba kitu sawasawa na mapenzi yake,atusikia.''
Kuomba sawasawa na mapenzi ya MUNGU maana yake ni kuomba sawasawa na matakwa ya MUNGU.
Kumbe katika kila maombi yako ni vyema kwanza kutafuta matakwa ya MUNGU juu ya hayo unayoyaombea.

Kwa njia hiyo tunagundua kwamba kuna makundi mengi ya maombi yakiwemo:
1. Maombi sawasawa na mapenzi ya MUNGU.
2. Maombi sawasawa na mapenzi ya muombaji.
3. Maombi sawasawa na mapenzi ya muombaji ila ndani yake kuna mapenzi sawasawa na kusudi la MUNGU.
Lakini muhimu kujua ni kwamba tukiomba sawasawa na mapenzi yake MUNGU yeye hutusikia na kutujibu.
Tujajifunza nini?
Kumbe katika baadhi ya maombi unayoomba ndani yake kuna mapenzi ya MUNGU hivyo kabla hujaomba taka/tafuta kwanza kujua nini mapenzi ya MUNGU kwa hayo unayotaka kuombea.

Mfano kijana anaweza kuomba apewe mke kumbe mapenzi ya MUNGU sio tu kumleta huyo mke Bali kwanza huyo anayetaka kupewa mke anatakiwa labda afunguliwe kwanza yeye ili aweze kuhimili ndoa.
Lakini ninachojua Mimi ni kwamba ROHO MTAKATIFU akikuongoza kuomba hakika hapo moja kwa moja unakuwa unaomba sawasawa na mapenzi ya MUNGU.
Kumbuka ROHO MTAKATIFU hutuombea Biblia ndivyo inavyosema lakini maombi hayo ya ROHO MTAKATIFU ni kupitia vivywa vyetu na hutuombea kupitia maombi yetu kwa kutuelekeza kuliendea hitaji sahihi.

Tukumbuke na hii kwamba tukiomba tu sawasawa na mapenzi yetu au tamaa zetu kupokea ni ngumu.
Ndugu hakikisha unatoka katika utawala wa shetani.
Njia nyingine ya kutoka ni kuzingatia kanuni za MUNGU zinazoagizwa na Neno la MUNGU katika Biblia.

MUNGU akubariki na pia Ukipenda kunisapoti kwa sadaka yako ya hiari katika huduma yangu karibu sana na pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane nitakujulisha jinsi ya kukipata.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa BWANA YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
+255714252292.
mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu

Comments