BAKI NA YESU HATA BAADA YA KUJIBIWA HITAJI LAKO.

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
Bwana YESU atukuzwe ndugu yangu..
Karibu tujifunze Neno muhimu sana la MUNGU wa mbinguni..
Kuna watu Walipomjua MUNGU Hawakumtukuza Kama Ndiye MUNGU, Yeye MUNGU Amewaacha Ili Wapotelee Kwenye Uzushi Wao walioufuata baada ya kumwacha YESU Mwokozi.


Warumi 1:21-22 '' kwa sababu, walipomjua MUNGU hawakumtukuza kama ndiye MUNGU wala kumshukuru; bali walipotea katika uzushi wao, na mioyo yao yenye ujinga ikatiwa giza.Wakijinena kuwa wenye hekima walipumbazika; ''

Watu hao Walimpokea Bwana YESU Wakati Wa Matatizo, Yeye Akawaponya Lakini Baada Ya Kuwa Wazima Kwa Muda Wamerudi Tena Duniani. Wanajua Kabisa Kwamba Hakuna Uzima Kwingine Nje KRISTO Lakini Wameshupaza Shingo zao.

Matendo 4:12 '' Wala hakuna wokovu katika mwingine awaye yote, kwa maana hapana jina jingine chini ya mbingu walilopewa wanadamu litupasalo sisi kuokolewa kwalo.''


Wanajua kabisa kwamba ni hakika ya milele kwamba hakuna kuokolewa kwingine nje na Bwana YESU.

Kuna watu baada ya kupitia vifungo vingi vya kipepo hatimaye walikutana na Neno la KRISTO lililo hai na wakaombewa na kupona kisha wakakiri mbele ya Kanisa na Mkutano kwamba sasa kwa YESU wamefika na hawataondoka kamwe, lakini baada ya muda watu wao walimwacha YESU na kisha kugeuka maadui wa Kanisa kwa kuwasema vibaya watumishi wa MUNGU waliowaombea wakapona.

Yoshua 24:15 '' Nanyi kama mkiona ni vibaya kumtumikia BWANA, chagueni hivi leo mtakayemtumikia; kwamba ni miungu ile ambayo baba zenu waliitumikia ng'ambo ya Mto, au kwamba ni miungu ya wale Waamori ambao mnakaa katika nchi yao; lakini mimi na nyumba yangu tutamtumikia BWANA.''


Ndugu ukiona ni vibaya kumtumikia Bwana YESU unaweza ukamwacha na kuirudia miungu uliyokuwa unaitumikia kabla hujamjua YESU, Lakini katika miungu hiyo hakuna Wokovu na katika miungu hiyo kunaweza kukawa jehanamu yako hivyo ni heru kumrudia Bwana YESU haraka sana.
Muujiza uliotendewa baada ya kuokoka usiwe ndio sababu ya kumwacha YESU.
Kuna Mtu aliookoka na baada ya kuokoka akawa mwimbaji na mwanamaombi mzuri, hakukosa kanisani kabisa na hakukosa mkesha hata mmoja wa maombi. Kumbe lengo lake ni kupata Mchumba tu, baada ya kujibiwa ombi lake la Mchumba akafunga ndoa na kutokomea kusikojulikana. Hana haja na YESU tena na hana muda wa kumtukuza MUNGU.
Mtu kama huyo anajua kabisa kwamba bila YESU KRISTO hakuna uzima wa milele, lakini ameshupaza singi. Ukitaka mkosane na mtu kama huyo basi Mwambie habari za kwenda kanisani kumwabudu MUNGU.


Warumi 6:23 ''Kwa maana mshahara wa dhambi ni mauti; bali karama ya Mungu ni uzima wa milele katika KRISTO YESU Bwana wetu.''


Ni heri kurudi kwa Bwana YESU na kutubu na kusonga mbele na wokovu.
Ndugu, Kumbuka ulipokuwa unalia sana na hakuna msaada.
Kumbuka ulipokuwa unakabwa na majinamizi na ulipokuwa unateswa na wachawi kila mara, kumbuka walipokuwa wanakutisha kwamba watakuua, kumbuka walipokuwa wanakaribia kukumaliza kabisa lakini Neema ya MUNGU ikakugusa na ukakimbilia maombezi na Bwana YESU akakuhurumia na kukuponya, kisha ukaapa mbele ya Watu wa MUNGU wengi kwamba umeokoka hakika na hautarudi nyuma tena.

Ndugu, umepatwa na nini tena?
Umeridhika kuwa hivyo?
MUNGU amekubariki kazi kwa muda mfupi tu baada ya maombezi.
Wewe kwa akili zako ulijaribu kila mara kupata kazi lakini hukufanikiwa kwa sababu ya vifungo vya mganga na mchawi. Umesoma lakini waajiri hawana mpango na wewe, mbele yao wewe unanuka na jambo hilo limekusumbua miaka mingi. Lakini ulipopata tu akili ya kukimbilia maombezi na ukaombewa na MUNGU BABA akakupa kazi.
Umekuwa mwaminifu kwa kanisa miezi kadhaa tu lakini baada ya hapo wala huna haja na kanisa tena.
Ndugu wewe kwanini umekuwa hivyo?
Ndugu, geuka kabla ya hatari yako.


1 Yohana 1:9 ''Tukiziungama dhambi zetu, Yeye ni mwaminifu na wa haki hata atuondolee dhambi zetu, na kutusafisha na udhalimu wote.''


Kuna ndugu wameacha ibada kwa sababu tu ya kufundishwa kutoa fungu la kumi.
Mtu kama huyo alipokuwa hajapata kazi alikuwa anatoa fungu la kumi kwa uaminifu wote.
Baada ya MUNGU kujibu hitaji lake la kupata kazi, ndugu yule sasa anapokea zaidi ya milioni moja kwa mwezi, amenunua gari na watu wa kanisani anawaona kuwa masikini tu. Sasa amechagua marafiki wapya wazinzi na wapenda mambo ya dunia. Amekuwa ni mtu wa starehe tu sasa na huko kwenye starehe anaweza kutumia hata laki mbili kwa siku. Huyo alikimbia kanisa kwa sababu aliambiwa ame anamtolea MUNGU fungu la kumi, akaona ni mzigo na kuliacha kanisa na hataki tena habari za kusali.
Ndugu huyo anajua kabisa kwamba bila YESU hakuna uzima wa milele lakini ameshupaza shingo yake.
Ndugu. kumbuka na hii 


Mithali 29:1 ''Aonywaye mara nyingi akishupaza shingo, Atavunjika ghafula, wala hapati dawa.''


Ndugu mmoja ambaye alikuwa amerogwa na ndugu zake na kuteseka muda mrefu sana na mapepo, hatimaye alipata Neema ya kumkimbilia Bwana YESU. Ndugu yule baada ya kuokoka alifunguliwa vifungo vyote na wakati wa maombezi waliomroga walipata mapigo kule kule na wakamuomba msamaha. Yule ndugu baada ya kuokoka ROHO MTAKATIFU akampa karama za kuhubiri na kuimba na hakika alikuwa baraka kwa kanisa lote.
MUNGU akambariki gari na nyumba nzuri na biashara nzuri sana. Baada ya kubarikiwa akaanza kuwa na kiburi kwa Mchungaji, hakutaka kusaidiwa kwa lolote na hakutaka kumsikiliza Mchungaji wake aliyemwombea sana na kufunga mara kadhaa kwa ajili yake.
Baadae yule ndugu aliondoka Kanisani akisema ''Siwezi kusali kanisa la maskini'' akaondoka.
Hiyo ni nini?
Ni hatari hakika kumkimbia Bwana YESU baada ya muujiza wako.


''Lakini zikimbie tamaa za ujanani; ukafuate haki, na imani, na upendo, na amani, pamoja na wale wamwitao Bwana(YESU) kwa moyo safi.- 2 Timotheo 2:22''


Najua kuna watu pia wanasoma ujumbe huu na hawajamwacha Bwana YESU.
Ndugu najua kabisa unaenda kubarikiwa lakini baraka hiyo isikufanye uote kiburi, baraka hiyo isikufanye udharau Mchungaji na viongozi wa Kanisa lako, Baraka hiyo isikufanye uwe mtu wa Michanganyo, baraka hiyo usikubali ikakuomndoa kwa Bwana YESU.


Wakolosai 2:6-15 '' Basi kama mlivyompokea KRISTO YESU, Bwana, enendeni vivyo hivyo katika yeye; wenye shina na wenye kujengwa katika yeye; mmefanywa imara kwa imani, kama mlivyofundishwa; mkizidi kutoa shukrani. Angalieni mtu asiwafanye mateka kwa elimu yake ya bure na madanganyo matupu, kwa jinsi ya mapokeo ya wanadamu, kwa jinsi ya mafundisho ya awali ya ulimwengu, wala si kwa jinsi ya KRISTO. Maana katika yeye unakaa utimilifu wote wa MUNGU, kwa jinsi ya kimwili. Na ninyi mmetimilika katika yeye aliye kichwa cha enzi yote na mamlaka. Katika yeye mmetahiriwa kwa tohara isiyofanyika kwa mikono, kwa kuuvua mwili wa nyama, kwa tohara ya KRISTO. Mkazikwa pamoja naye katika ubatizo; na katika huo mkafufuliwa pamoja naye, kwa kuziamini nguvu za MUNGU aliyemfufua katika wafu.
Na ninyi mlipokuwa mmekufa kwa sababu ya makosa yenu na kutokutahiriwa kwa mwili wenu, aliwafanya hai pamoja naye, akiisha kutusamehe makosa yote; akiisha kuifuta ile hati iliyoandikwa ya kutushitaki kwa hukumu zake, iliyokuwa na uadui kwetu; akaiondoa isiwepo tena, akaigongomea msalabani; akiisha kuzivua enzi na mamlaka, na kuzifanya kuwa mkogo kwa ujasiri, akizishangilia katika msalaba huo. ''


Ndugu yangu mpendwa sana nakuomba baraka yeyote isikufanye umwache Bwana YESU.
Baraka yeyote isikufanye uache Wokovu wa Bwana YESU.
Kupata kazi, kufunga ndoa, kufaulu masomo, kupandisha cheo, kuwa na biashara nzuri,Kupata nafasi za kwenda nje ya nchi au baraka ya aina yeyote hakikisha haikuondoa katika Wokovu wa Bwana YESU.


''Afichaye dhambi zake hatafanikiwa; Bali yeye aziungamaye na kuziacha atapata rehema.- Mithali 28:13''


MUNGU akubariki na pia Ukipenda kunisapoti kwa sadaka yako ya hiari katika huduma yangu karibu sana na pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane nitakujulisha jinsi ya kukipata.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo  ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa BWANA YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
0714252292.
0786719090
mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu

Comments