JE UNATAKA KUNENA KWA LUGHA?

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu yangu!
Karibu tujifunze Neno la MUNGU la uzima.
Kwa sababu unatamani kunena kwa lugha basi hakika MUNGU atakupa kunena kwa lugha.


Vyanzo vya mtu mpaka anene kwa lugha ni:

1. Kwanza ni kumjua Bwana YESU na Wokovu wake maana YESU KRISTO ndio chanzo cha ROHO MTAKATIFU kuja kwetu. Mtu asipompokea YESU hakika hawezi kumpokea ROHO MTAKATIFU.
Yohana 15:26 " Lakini ajapo huyo Msaidizi, nitakayewapelekea kutoka kwa BABA, huyo ROHO wa kweli atokaye kwa BABA, yeye atanishuhudia."

2. Ili mtu anene kwa lugha inampasa sana awe muombaji sana maana bila maombi hakuna kunena kwa lugha.
Yuda 1:20 "Bali ninyi, wapenzi, mkijijenga juu ya imani yenu iliyo takatifu sana, na kuomba katika ROHO MTAKATIFU,"

3. ROHO MTAKATIFU ni mtakatifu na hutufundisha sisi wateule wa MUNGU utakatifu, hivyo maisha matakatifu katika KRISTO ni mlango wa kupokea karama za ROHO MTAKATIFU, na kunena kwa lugha ni moja ya karama hizo japokuwa kunena kwa lugha lugha ni karama ambayo Bwana YESU alitupa wateule wote.
Marko 16:16-17 "Aaminiye na kubatizwa ataokoka; asiyeamini, atahukumiwa. Na ishara hizi zitafuatana na hao waaminio; kwa jina langu watatoa pepo; watasema kwa lugha mpya;"

4. Ili unene kwa lugha inakupasa ujifunze sana kuhusu ROHO MTAKATIFU na matunda yake na karama zake na kazi zake.
Wagalatia 5:22-23 ' Lakini tunda la Roho ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu, upole, kiasi; juu ya mambo kama hayo hakuna sheria."

Tamani kunena kwa lugha na uwe unahudhuria ibada Mara kwa Mara maana kila jambo na wakati wake. Kuna siku MUNGU anaweza akashusha nguvu zake katika ibada na waliopo wakapokea, asiyekuwepo hatapokea.

5. Ili unene kwa lugha inakupasa umwombe ROHO MTAKATIFU akujalie kunena.
Mathayo 7:7-8 " Ombeni, nanyi mtapewa; tafuteni, nanyi mtaona; bisheni, nanyi mtafunguliwa; kwa maana kila aombaye hupokea; naye atafutaye huona; naye abishaye atafunguliwa."

Kwa waliookoka kuna changamoto kwao kujua kama wana ROHO MTAKATIFU au hawana.
Unaweza ukadhani kwamba wewe huna ROHO MTAKATIFU kwa sababu tu huneni kwa lugha lakini ukweli ni kwamba kama umeokoka kwelikweli na hautumiki kipepo kwa vyovyote hakika ROHO MTAKATIFU unaye, maana ROHO MTAKATIFU tunampokea kwa Imani kwa kuombewa baada ya kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi wetu.
Mfano wa hilo la jinsi ya kumpokea ROHO MTAKATIFU ni huu.


Matendo 8:14-17 " Na mitume waliokuwako Yerusalemu, waliposikia ya kwamba Samaria imelikubali neno la MUNGU, wakawapelekea Petro na Yohana; ambao waliposhuka, wakawaombea wampokee ROHO MTAKATIFU; kwa maana bado hajawashukia hata mmoja wao, ila wamebatizwa tu kwa jina lake Bwana YESU. Ndipo wakaweka mikono yao juu yao, nao wakampokea ROHO MTAKATIFU."


Unapompokea Bwana YESU kama Mwokozi wako, ukatubu na kuacha uovu hakika ROHO MTAKATIFU anaingia ndani kwako ukiomba.
Tunampokea ROHO MTAKATIFU kwa maombi ya imani baada ya kujifunza Neno la MUNGU sahihi kumhusu ROHO MTAKATIFU

Ndugu yangu, Kama hujawahi kunena kwa lugha nakuomba kwa sasa nakuomba endelea kujifunza kuhusu ROHO MTAKATIFU kupitia masomo mbalimbali kumhusu na endelea kutamani kunena huku ukiomba maombi sana hasa maombi ya toba na utakaso na kumwitaji ROHO MTAKATIFU hakika baaada ya muda utaongozwa maombi ya ujazo wa ROHO MTAKATIFU na utanena. 

Mambo ya lazima ili ufikie kunena kwa lugha ni;
1. Utakatifu
2. Kiu ya kutaka kujazwa nguvu za ROHO MTAKATIFU
3. Kumwamini MUNGU.
4. Hamu na shauku ya kutaka kujazwa nguvu za ROHO MTAKATIFU
5. Kujiachilia katika neema ya YESU KRISTO.
6. Maombi ya kina
7. Utii 


Utajuaje kama unaomba katika ROHO MTAKATIFU?
=Utajua kama utanena kwa lugha katika ROHO MTAKATIFU.
Kunena kwa lugha ni ishara Kabisa kwamba una ROHO MTAKATIFU

=Jambo la pili utajua pale ambapo ROHO MTAKATIFU atakujulisha kitu cha kuombea.
Mfano Unaweza kuwa unaomba kuhusu ndoa yako lakini katikati ya maombi hayo ukasikia kwa sauti uombe juu ya wazazi wa mmeo maana kuna maagano ambayo yanamwathiri mmeo hadi yanaathiri ndoa yako, ukitii ushauri huo wa ROHO MTAKATIFU ambao unausikia ndani yako utakuwa unaomba katika ROHO MTAKATIFU. Inawezekana usisikie sauti lakini ukasikia msukumo tu, vyote kama vimetoka kwa ROHO MTAKATIFU hapo utaomba maombi katika ROHO MTAKATIFU.

Inawezekana usisikie sauti wala msukumo lakini kwa sababu ni Kanisani basi ukasikia mtumishi akisisitiza muombee jambo Fulani basi kama hilo limetoka kwa ROHO MTAKATIFU basi utakuwa unaomba katika ROHO MTAKATIFU.

Kumbuka kwa mjibu wa Biblia ni kwamba ROHO MTAKATIFU kazi yako mojawapo ni kutusaidia katika maombi hivyo ni lazima tu ukiwa Rohoni utasikia Ujumbe wa ROHO MTAKATIFU kukusaidia katika maombi ili kuombea hitaji halisi.
Zingatia somo hili na siku sio nyingi utanena kwa lugha.
Baada ya kunena kwa lugha hakikisha unakuwa na ushirika wa kudumu na ROHO MTAKATIFU, ukimtii na kukubali akusaidie katika yote.

MUNGU akubariki na pia Ukipenda kunisapoti kwa sadaka yako ya hiari katika huduma yangu karibu sana na pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane nitakujulisha jinsi ya kukipata.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa BWANA YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
0714252292.
0786719090
mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu.

Comments