MAOMBI YA KUZUIA VITU VIBAYA ILI VISITOKEE.

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU
Bwana YESU atukuzwe ndugu yangu!
Karibu tujifunze Neno la MUNGU kisha tuombe maombi ya ushindi.
Leo tunaomba maombi ya kuzuia vitu vibaya vilivyokusudiwa vitokee. Kwa maombi unaweza kufuta mpango wa kipepo uliopangwa dhidi yako.
Kuomba maombi ya kuzuia vitu vibaya ni kama kuweka ukuta wa chuma katika ulimwengu wa roho kukuzunguka ili mishale ya kipepo itakaporushwa kwako basi haitaweza kuutoboa ukuta wa chuma uliouweka kwa njia ya maombi yako.
Katika taifa Jambo likizuiliwa na mahakama hakika hakuna anyeweza kuvunja zuio hilo, ndivyo ilivyo pia katika maombi, kuna vitu mtumishi wa MUNGU anaweza kuvizuia kwa njia ya maombi na asiweze adui kuvileta tena.
Watumishi wa MUNGU wa zama za Biblia  waliomba maombi ya kuzuia vitu vibaya  na ikawezekana maana ni watumishi wa MUNGU waliolisimamia kusudi la MUNGU.
Kuna vitu vya kipepo ni lazima uombe vizuiliwe ndipo utafanikiwa na kustawi.
Jambo la kwanza ni lazima utambue unachotakiwa kuzuia kwa njia ya maombi.
Baada ya hapo inakupasa uombe ili kuzuia kitu hicho kwenye ulimwengu wa roho na kitazuiliwa.
Mfano kunaweza kukawa na magonjwa ya mlipuko katika maeneo yako na kwa sababu unatambua kwamba MUNGU BABA anaweza yote, basi unaomba maombi katika jina la YESU KRISTO ili ugonjwa huo uzuiliwe kuenea zaidi na unauzuia kukupata wewe au familia yako.
Katika maombi kila jambo linawezekana.
Kuna mambo mengi sana mawakala wa shetani huyatuma ili kuwadhuru watu wa MUNGU au kuwaharibia. Unapoomba maombi ya kuzuia kitu hicho cha kishetani maana yake unaruhusu ulinzi wa MUNGU kwako ili kuzuia jambo hilo baya kukupata wewe.
Kumbuka sio kila magonjwa ni magonjwa tu, mengine ni magonjwa ya kichawi.
Sio kila kudharauliwa au kuonewa ni hali ya kawaida tu, mengine ni maroho kabisa ili maisha yako yote yawe ya kudharauliwa tu na kuonewa.
Sio kila kufeli mitihani ni hali ya kawaida, mengine ni mipango ya kichawi kabisa ili ufeli hata kama unasoma sana.
Sio kila umasikini ni kwa sababu ya uzembe wa mtu, mengine ni maroho kabisa ya kuzimu ili kumtesa mtu.
Sio kila vita na mafarakano katika ndoa au familia au ukoo au jamii ni jambo tu la kawaida, mengine huwa ni ajenda kabisa ya kuzimu ni kukutesa.
Ashukuriwe MUNGU wa mbinguni maana ukimtegemea kwa maombi katika jina la YESU KRISTO mabaya yaliyokusudiwa kwako yanaweza kuzuiliwa baada ya maombi yako.
Biblia naipenda maana inatoa uhakika kwa muombaji makini kwamba '' Mabaya hayatakupata wewe, Wala tauni haitaikaribia hema yako. Kwa kuwa atakuagizia malaika zake Wakulinde katika njia zako zote.-Zaburi 91:10-11''

 Biblia inasema mabaya hayatatupasa sisi wateule wa Bwana YESU waombaji, lakini ni hadi tuombe maombi ya kuzuia vitu vibaya.
Inaposemwa kwamba mabaya hayatakupata wewe maana yake baada ya kuomba kutakuwa na kizuizi katika ulimwengu wa roho ili kuzuia mabaya yote yaliyokusudiwa kwako na sasa hayatakupata.
Kumbuka kwamba kizuizi hicho hakitajileta bali kitakuja baada ya maombi yako ya kuzuia vitu hivyo vibaya vilivyopagwa.
Utakatifu pia  ni jambo kuu kabisa katika maisha ya mkristo yeyote hivyo hakikisha unaishi maisha matakatifu ya wokovu wa Bwana YESU siku zote.
Baada ya wewe kuomba basi MUNGU ataleta kizuizi hicho  na ndipo ''Mabaya hayatakupata wewe, Wala tauni haitaikaribia hema yako.''
 Biblia inasema kwamba ''tauni haitaikaribia hema yako''
 Tauni kibiblia ni magonjwa, ni magonjwa yote yanayotumwa na kuelekezwa kwako, ni magonjwa ya kichawi ili yakupate, lakini kwa maombi yako katika jina la YESU KRISTO hakika hakuna ugonjwa wa kichawi utakupata.

Maadui katika ulimwengu wa roho wapo wengi sana na Biblia inathibitisha.
Zaburi 37:12 ''Asiye haki hunuia mabaya juu ya mwenye haki, Na kumsagia meno yake.''
 Inawezekana kabisa kuna watu wanaokusaigia meno na kupanga mabaya dhidi yako, kwa maombi yako unaweza kufuta hicho walichokipanga.

 Jambo moja mimi Peter nimeshajifunza kwenye Biblia ni kwamba MUNGU husema sana na wanadamu kwa njia ya ndoto na maono.
MUNGU anaweza kusema kwa njia ya ndoto na watu waliookoka na hata watu walio wapagani tu.
Katika ndoto jambo la kujua ni kwamba wakati mwingine huwa unaonyeshwa vitu vibaya sio tu ujue na kuwasimulia watu, bali ni ili ujue mipango ya kipepo dhidi yako na kwa kujua hilo uombe kuzuia kitu hicho kibaya ulichokiona ili kisitokee.
Familia moja walilia sana siku moja baada ya mtoto wao wa kiume mdogo kufariki. Wiki moja kabla mtoto huyo alikuwa ameota kuna ng'e wanamuuma hadi anakufa. Alipowasimulia baba na mama yake kwamba ameota anaumwa na ng'e hadi kufa walimkemea. Kesho yake akaota tena na wao wakapuuza bila kuomba. Baada ya wiki yule mtoto akaugua ghafla na kufariki ndipo walipoaanza kusema kwamba wangejua wangeomba kuzuia uchawi huo wa ng'e hakika mtoto wao asingekufa.
Ndugu, Kuna mengine MUNGU hukufunulia ili tu uombe kuzuia jambo hilo.
Kumbuka ni MUNGU alisema '' Hata itakuwa, baada ya hayo, ya kwamba nitamimina roho yangu juu ya wote wenye mwili; na wana wenu, waume kwa wake, watatabiri, wazee wenu wataota ndoto, na vijana wenu wataona maono; tena juu ya watumishi wenu, wanaume kwa wanawake, katika siku zile, nitamimina roho yangu.-Yoeli 2:28-29''

Hivyo usidharau kila maono unayoonyesha na usidharau kila ndoto unayoonyeshwa, mengine huwa ni MUNGU kabisa kwa huruma zake anakujulisha ili uombe na mambo mabaya kwako yazuiliwe.
Maombi ya kuzuia vitu vibaya ni ya muhimu sana sana.
Eliya alizuia mvua kwa miaka mitatu na nusu kwa sababu ya uasi wa waisraeli. 
Yakobo 5:17-18 '' Eliya alikuwa mwanadamu mwenye tabia moja na sisi, akaomba kwa bidii mvua isinyeshe, na mvua haikunyesha juu ya nchi muda wa miaka mitatu na miezi sita. Akaomba tena, mbingu zikatoa mvua, nayo nchi ikazaa matunda yake.''

Wewe usizuie mvua ila zuia vitu vyote vya kishetani vinavyopangwa kuja kwako.
Eliya kwa maombi yake alizuia mvua, kama asingezuia hakika mvua ingeendelea kunyesha.
Wewe usizuie mvua lakini kila jambo la kichawi lililopangwa kukuhusu wewe unaweza kulizuia.
Ndugu weka ukuta wa moto kwa maombi yako ili kuwazuia mawakala wa shetani wanaotaka kuingilia ndoa yako au kazi yako au uzao wako au biashara yako au kitu chako chochote chema.
Kumbuka usipoomba hakika hawatazuiliwa kukuonea maana hujaweka kizuizi.

Usipoweka kizuizi cha kiroho dhidi ya wanaokupangia mabaya kipepo yatatokea yafuatayo;
1. Utadhurika.
Utadhulika kwa sababu hakuna kizuizi cha kuzuia mishale ya shetani katika maisha yako.

2. Utatakiwa kutumia nguvu nyingi sana wakati tatizo limetokea.
Jiulize hukuweka kizuizi dhidi ya wanaoroga kazi yako, kisha baadae ukagundua kuna mchawi anakuroga na ameshakuroga kwa sehemu kubwa, kisha ukaanza kuomba ili kumuondoa katika kazi yako. Wakati huo adui atakuwa ameshajiimalisha hivyo unaweza hata ukafunga na kuomba na kutumia nguvu nyingi ndipo ataondoka lakini ungekuwa umezuia mapema kwa maombi yako hakika hata kuingia tu katika kazi yako asingeweza.

3. Hata kama utalilishinda jambo hilo lakini linaweza kuacha makovu.
Mfano hukuzuia kazi yako kuvamiwa kipepo kisha ikavamia kabisa kwa sababu hakuna kizuizi, kisha kwa miezi miwili ukawa na mgogoro kazini kiasi kwamba mshahara wako kwa miezi miwili hukupewa na kisha kwa maombi yako baadae mshahara wako ukarejea na ukaendelea na kazi kama kawaida, huko kukosa mshahara kwa miezi miwili ndio kovu lenyewe.

4. Utakuwa mtu wa kuonewa tu kipepo.
Kama hakuna kitu kinachomzuia wakala wa shetani kuingia katika maeneo yako basi tarajia kuonewa tu kila mara na wachawi au wakuu wa giza maana hawazuiliwi na chochote kukufikia.
Maombi ni muhimu sana

5. Utapata hasara.
Kama utafilisika kwa sababu umerogwa basi hiyo ni hasara, hivyo muombe MUNGU ukizuia kila jambo baya lililopangwa katika ulimwengu wa roho kukuhusu.
Mathayo 7:7 '' Ombeni, nanyi mtapewa; tafuteni, nanyi mtaona; bisheni, nanyi mtafunguliwa;''

Leo zuia magonjwa yote yaliyotumwa kichawi ili yakupate, zuia kwa jina la YESU KRISTO na kwa damu ya YESU KRISTO.
Leo tengeneza ukuta wa chuma ili maadui zako wakituma mishale yao wakutane na ukuta. Wakati huo watatarajia wakuone unateseka lakini kwa sababu ya maombi yako MUNGU amezuia hivyo utasonga mbele huku wakiwa hawaelewi wafanyeje.
Zaburi 21:11-12 '' Madhali walinuia kukutenda mabaya, Waliwaza hila wasipate kuitimiza. Kwa maana utawafanya kukupa kisogo, Kwa upote wa uta wako ukiwaelekezea mishale.''

Leo weka kizuizi cha kiroho cha kuwazuia wabaya wako kuingilia maisha yako.
Kisha futa mazuio yao yote waliyoyaweka zamani ili kukuzuia wewe kupata baraka fulani.
Ni nani anataka akuzuie kichawi ili usiolewe au usioe?
Ni nani anataka ahakikishe hupati kazi hata kama una vyeti safi?
 Ni nani anakuzuia kichawi ili usizae?
Leo zuia afya yako kuvamiwa, zuia watoto wako kuwamiwa kipepo, Leo zuia mimba yako kutoka kichawi.
Zuia ndoa yako kuingiliwa kichwai na washirikina.
Uwe na imani katika maombi yako hakika waliokuzuia watazuiliwa wao sasa katika jina la YESU KRISTO.
Maombi yako ya leo yatatengeneza kizuizi cha kuwazuia majini au mapepo wasiguse baraka yako.
Mwite MUNGU aliyewazuia simba kumtafuta Danieli.
Danieli 6:19-22 ''Asubuhi mfalme akaondoka mapema, akaenda kwa haraka mpaka penye lile tundu la simba. Naye alipolikaribia lile tundu, akamlilia Danielii kwa sauti ya huzuni; mfalme akanena; akamwambia Danielii, Ee Danielii, mtumishi wa MUNGU aliye hai, je! MUNGU wako, unayemtumikia daima, aweza kukuponya na simba hawa? Ndipo Danielii akamwambia mfalme, Ee mfalme, uishi milele. MUNGU wangu amemtuma malaika wake, naye ameyafumba makanwa ya simba, nao hawakunidhuru; kwa kuwa mbele zake mimi nalionekana kuwa sina hatia; tena, mbele yako, Ee mfalme, sikukosa neno.   ''

 Hakika inawezekana kabisa katika jina la YESU KRISTO.
Mwite MUNGU awazuie wachawi kukuibia mali zako.
Mwite MUNGU awazuie mawakala wa shetani kutoa furaha katika ndoa yako.
Kazi ya kuwazuia mawakala wa shetani wanaokufuatilia ni kazi ya MUNGU lakini hadi wewe uombe kwa kutamka kuzuia vitu vya kishetani walivyopangwa kuja kwako.
Leo kwa maombi yako zuia wakuu wa giza wanaowinda kibali chako.
Zuia waganga wanaoroga kazi yako kwa msaada wa wafanyakazi wenzako wasiokupenda.

Zaburi 64:2 '' Utanificha mbali na shauri la siri la watenda mabaya, Mbali na ghasia ya watu wafanyao maovu;''

Inawezekana uko katika zuio la kichawi la kupata kazi au kuolewa au kuoa.
Inawezekana kabisa unazuiliwa na mizimu ya ukoo wenu.
Leo kwa damu ya YESU KRISTO na kwa jina la YESU KRISTO futa mazuio yote ya kipepo.
 Leo wazuie watu wabaya kukufunga kiroho ili usifanikiwe.
Omba na MUNGU hakika atakushindia.

Katika maombi ya leo licha ya kuombea hayo niliyokutajia lakini husika pia kuombea yafuatayo.
1. Zuia kila jambo baya  lililowekwa kipepo tangu zamani ili usifanikiwe katika maisha yako.

2. Yafungue majitra yako ya baraka zako yaliyokuwa yamefungwa kipepo.

3. Omba mabaya yaliyokuwa yamekusudiwa na wabaya wako yawapate wao na sio wewe.

Zaburi 71:12-13 '' Ee MUNGU, usiwe mbali nami; Ee Mungu wangu, fanya haraka kunisaidia. Waaibishwe, watoweshwe, adui za nafsi yangu. Wavikwe laumu na aibu wanaonitakia mabaya ''

 MUNGU akubariki sana sana na kama ukipenda kunisapoti katika huduma yangu kwa sadaka ya hiari ya kiwango chochote utakachopenda karibu na MUNGU akubariki sana, pia kitabu cha MAOMBI YA KINA kipo na wasiliana nami utakipata na ukifanyia kazi itakusaidia sana.
Hapa chini ni maombi ya kuzuia kila jambo la kipepo na kisha wewe kuweka kizuizi.
Maombi haya naomba yamsaidie mtu yule ambaye hajui kuomba ili katika kuomba kwa kutumia hayo basi atakumbuka mahitaji yake na kuyataja katika maombi yake.
Kwa waombaji wazoefu naamini baada tu ya kulisoma somo na kulielewa basi anajua aombee nini.



MAOMBI YA KUZUIA VITU VIBAYA ILI VISITOKEE.

Baba katika jina la YESU KRISTO ninakushukuru MUNGU wangu kwa kulinda hata siku ya leo.
Najikabidhi kwako muumba wangu na ninaomba ulinzi wako katika maisha yangu, kazi yangu, ndoa yangu na familia yangu yote.
Nakushukuru MUNGU wangu maana leo umenipa mamlaka na kibali ili nizuie kila kitu cha kishetani ambavyo mawakala wa shetani wanakipanga au walikipanga zamani kunihusu.
Katika jina la YESU KRISTO ninazuia kila ugonjwa ulioelekezwa kwangu kichawi, nauzuia kwa damu ya YESU KRISTO na kwa jina la YESU KRISTO. Sitaumwa na mangonjwa hayo ya kichawi na wala sitadhulika kwa lolote lililotumwa kwangu na wakuu wa giza.
Ninazuia kila mpango mbaya kuhusu maisha yangu au familia yangu.
Ninazuia kila ajali zilizopangwa, Ninazuia kila balaa na majanga vilivyokusudiwa vinipate, Ninazuia kwa damu ya YESU KRISTO na kwa jina la YESU KRISTO.
Ninazuia kila mpango ili nisifunge ndoa,  Ninazuia kwa damu ya YESU KRISTO na kwa jina la YESU KRISTO.
Ninazuia kila uchawi unaopangwa ili niabike, Ninazuia kwa damu ya YESU KRISTO na kwa jina la YESU KRISTO.
Ninazuia kila mapepo yanayotumwa kwangu ili kuharibu ufahamu wangu, Ninazuia kwa damu ya YESU KRISTO na kwa jina la YESU KRISTO.
Ninazuia kila mwanadamu anayepanga mabaya juu ya maisha yangu,
Ninazuia kila roho za wizi na utapeli, Ninazuia kwa damu ya YESU KRISTO na kwa jina la YESU KRISTO.
Kila jambo baya na kila aliyekusudia mabaya kwangu, Ninazuia kwa damu ya YESU KRISTO na kwa jina la YESU KRISTO.
Nafungua majira yangu ya baraka zangu yaliyokuwa yamefungwa kichawi.
Majira yangu ya kupata kazi na kufunga ndoa, Nayafungua majira hayo kwa damu ya YESU KRISTO na kwa jina la YESU KRISTO.
Majira yangu ya ushindi, Nayafungua majira hayo kwa damu ya YESU KRISTO na kwa jina la YESU KRISTO.
Majira yangu ya kufungua biashara nzuri, Nayafungua majira hayo kwa damu ya YESU KRISTO na kwa jina la YESU KRISTO.
Majira yangu ya kushinda uchaguzi, Nayafungua majira hayo kwa damu ya YESU KRISTO na kwa jina la YESU KRISTO.
Majira yangu ya kumiliki na kutawala katika ulimwengu wa roho,Nayafungua majira hayo kwa damu ya YESU KRISTO na kwa jina la YESU KRISTO.
Majira yangu ya kupokea uzao, Nayafungua majira hayo kwa damu ya YESU KRISTO na kwa jina la YESU KRISTO.
Kila majira yangu yaliyobeba baraka zangu,  Nayafungua majira hayo kwa damu ya YESU KRISTO na kwa jina la YESU KRISTO.
Kila yaliyokuwa yamekusudiwa yanipate sasa hayatanipata kwa jina la YESU KRISTO.
Kila madhara yaliyokuwa yamekudiwa yanipate au yapate familia yangu au ndoa yangu au kazi yangu, sasa hayatanipata kwa jina la YESU KRISTO.
Kila wakala wa shetani anayepanga mabaya kuja kwangu, sasa namrudishia yeye kwa jina la YESU KRISTO.
Neno la MUNGU linasema katika Zaburi 91:10 kwamba mabaya hayatanipata mimi na wala magonjwa hayatanipata. Hayo mabaya yawapate wachawi wote waliokuwa wameyatuma kwangu.
Neno la MUNGU linasema katika Zaburi 71:13 kwamba waabishwe na watoweshwe maadui zanfu wanaoniwazia mabaya.
Sasa mabaya waliyoyakusudia yanawapata wao kwa jina la YESU KRISTO.
Asante MUNGU Baba maana kwako uko ushindi na uzima.
Kuanzia sasa mimi sitadhulika na uchawi wala uganga.
Niko huru sasa kwa jina la YESU KRISTO.
Asante MUNGU wangu maana umenishindia.
Katika jina la YESU KRISTO nimeomba na kupokea ushindi mkuu sana.
Amen Amen.

 Asante kama umelielewa Neno la MUNGU ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa BWANA YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
0714252292.
mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu.

Comments