MWANAMKE ANAYEKARIBIA KUOLEWA.

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
Bwana YESU atukuzwe ndugu zangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.
Nina Neno fupi kwa mabinti au wanawake wanaotegemea kufunga ndoa, hata hivyo Ujumbe huu utamfaa hata yeyote aliye ndani ya ndoa tayari.


Mithali 14:1“Kila mwanamke aliye na Hekima hujenga nyumba yake; Bali aliye mpumbavu hibomoa kwa mikono yake mwenyewe”

Maana yake inahitajika hekima kwa Mwanamke aliye katika ndoa au ambaye anatarajia kuwa katika ndoa.
Hekima maana yake elimu na elimu huleta akili.
Hekima ya wateule wa MUNGU ni neno la MUNGU hivyo katika kuepuka kuibomoa ndoa yako itakupasa ulitii neno la MUNGU na kulifuata.
Neno la MUNGU hukutaka kuomba na kuishi maisha matakatifu.
Ukifanya hayo unakuwa unaijenga ndoa yako.
Kuenenda kwa ROHO MTAKATIFU na kukataa marafiki wabaya(Zaburi 1:1-3) ni njia salama pia na kuijenga ndoa yako na sio kuibomoa.
Hiyo Zaburi 1:1-3 inasema " Heri mtu yule asiyekwenda Katika shauri la wasio haki; Wala hakusimama katika njia ya wakosaji; Wala hakuketi barazani pa wenye mizaha. Bali sheria ya BWANA ndiyo impendezayo, Na sheria yake huitafakari mchana na usiku. Naye atakuwa kama mti uliopandwa Kandokando ya vijito vya maji, Uzaao matunda yake kwa majira yake, Wala jani lake halinyauki; Na kila alitendalo litafanikiwa."


Kabla binti hajaingia katika ndoa anatakiwa ajue kwamba mambo yanayoweza kuibomoa ndoa yake ili ajiepuke nayo na anatakiwa ayafuate mambo ya Ki MUNGU yanayoweza kuijenga ndoa yake na kwa njia hiyo hiyo ndoa haitabomoka milele.
Biblia inasema juu ya mke mwema kwamba " Hufumbua kinywa chake kwa hekima, Na sheria ya wema I katika ulimi wake -31:26"
Mwanamke lazima autumie ulimi wake vizuri.
Wengi hujinenea mabaya na mabaya hayo yanawafunga wanashindwa kuingi katika ndoa au yanawafunga kuishi maisha ya furaha ya ndoa 


Mithali 6:2 " Basi umetegwa kwa maneno ya kinywa chako, Umekamatwa kwa maneno ya kinywa chako,"


Lakini pia ni muhimu kujua kwamba sio wanaume wote wanapenda wanawake waongeaji sana na mapepe.
Sio wanaume wote wanapenda wanawake waongo waongo na wanaowaganda wanaume hao kwa maneno mengi yasiyoisha hadi vichwa vinauma.
Ninachotaka kusema ni kwamba binti anayetarajiwa kuolewa au mama aliye katika ndoa inawapasa sana kutumia vyema ndimi zao katika maongezi.
Ndio maana Biblia imesema hapo juu kwamba mke mwema anatakiwa kuwa na sheria ya wema ulimini mwake.
Maneno ya mikato mikato, matusi na matumizi mabaya ya kinywa katika kuongea yanaweza kumfanya binti akosea mchumba au aachwe na mchumba bila sababu za msingi.
Kumbe chanzo ni matumizi mabaya ya kinywa chake katika kuongea


Mithali 19:14 '' Nyumba na mali ni urithi apatao
mtu kwa babaye; Bali mke mwenye busara, mtu
hupewa na BWANA.''


Kumbuka mwanamke ndio huchaguliwa kwanza na mwanaume hivyo kasoro kidogo tu kwa binti inaweza kuwafanya vijana waoaji wawe wanampita tu kama hawamuoni.

Mithali 31:10A '' Mke mwema, ni nani awezaye
kumwona? ''


Binti anatakiwa aonekane kimatendo ndipo itakuwa rahisi kuolewa na kuwa mke mwema wa mtu.
Kama huonekani itakusumbua kumpata mume sahihi.
Kuonekana sio kujionyesha Bali matendo yako, tabia zako na ucha MUNGU wako ndivyo vitaonekana kwako hata upate mume mwema wako
Binti lazima ahakikishe anaonekana ndio itakuwa rahisi kuwa mke mwema wa mtu
Kumbe ni lazima binti aonekane ndio maana andiko likasema "Mke mwema ni nani awezaye kumwona?"
Ni lazima huyo mke mwema aonekane ndio atapata nafasi ya kuolewa.
Wengi wasiomcha MUNGU huonekana kwa ukahaba wao na uasherati wao ndio maana kuolewa inakuwa vigumu pia.
Wengi hutumia mbinu mbadala za kishetani ili waolewe, lakini huolewa na baada ya muda matatizo yanakuwa makubwa sana kwa sababu shetani hajawahi kuwa rafiki wa kudumu kwa mwanadamu yeyote.
Binti anatakiwa sana awe mcha MUNGU aliyeokolewa na Bwana YESU na awe anamtii MUNGU na kumwabudu MUNGU BABA katika ROHO na kweli.

Jambo Jingine binti kujua ni hili.

Mwanzo 2:24 ''Kwa hiyo mwanamume
atamwacha baba yake na mama yake naye
ataambatana na mkewe, nao watakuwa mwili
mmoja.''


Binti lazima ajue kwamba atakapoolewa ataambatana na mumewe, ni muhimu ajiandae kwa hilo ili isimletee shida baadae.
Maisha ya ndoa yana mambo mengi hivyo maandalizi ya kiroho na kimwili yanahitajika.

Wasiojiandaa na hilo ndio hao kila wiki anaenda nyumbani na kuleta shida kwenye ndoa.
Wasiojiandaa ndio hao ambao hutoa siri za ndoa nje na mwisho hujikuta ameibomoa ndoa yake kwa mikono yake.
Kunahitajika maandalizi.

Usipofanya maandalizi basi ndugu zako ndio watakuwa wasemaje wa ndoa yako na waamuzi wa ndoa yako.

Mithali 18:22 ''Apataye mke apata kitu chema;
Naye ajipatia kibali kwa BWANA. ''


Apatae mke apata kitu chema na apatae mume mwema hakika naye ajipatia kitu chema hivyo ndoa lazima ithaminiwe na kulindwa.
Najua binti unaenda kufunga ndoa takatifu lakini jambo muhimu la mwisho ni kwamba ndoa bila YESU KRISTO ni hasara.
Unamhitaji YESU katika ndoa yako unayoenda kufunga.

Unahitaji utakatifu na maombi na kuyaishi matunda 9 ya ROHO MTAKATIFU.
Matunda tisa ya ROHO MTAKATIFU yakikaa ndani ya mtu, mtu huyo utu wake wa ndani umekamilika.

Wagalatia 5:22-23 " Lakini tunda la ROHO ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu, upole, kiasi; juu ya mambo kama hayo hakuna sheria.''


Hayo ndio matunda Tisa ya ROHO MTAKATIFU ambayo mteule akiwa nayo hakika mteule huyo utu wake wa ndani umekamilika.
Ndugu hakikisha utu wako wa ndani unakamilika kwa wewe kuwa na matunda 9 ya ROHO MTAKATIFU na kuyaishi.
Ukimuona mteule hana upendo, huyo utu wake wa ndani haujakamilika.
Ukiona mtu hana furaha, amani au uvumilivu ujue Kabisa utu wake wa ndani huyo ndugu una tatizo.
Ukimuona si Mtu mwema na wala hawezi kuwafadhili wengine na tena sio mwaminifu kwa MUNGU na kwa Kanisa, huyo ndugu hana tunda la ROHO MTAKATIFU na utu wake wa ndani haujakamilika.
Ukimuona mtu hana upole na kiasi katika maisha yake ya Wokovu huyo utu wake wa ndani haujakamilika.
Matunda 9 ya ROHO MTAKATIFU ni lazima yawe sehemu ya maisha yetu kama wateule wa MUNGU tuliozaliwa Mara ya pili.
Ukiwa huna ROHO MTAKATIFU tambua pia kwamba huwezi kuwa na karama za ROHO MTAKATIFU zikifanya kazi na huwezi kuwa na matunda Tisa ya ROHO MTAKATIFU ndani yako.
Kama kuna kitu muhimu sana kwa mwenda mbinguni basi ni kuongozwa na kuenenda katika ROHO MTAKATIFU.
Ukifanya kinyume na matunda 9 ya ROHO MTAKATIFU utu wako wa ndani utakuwa na matatizo makubwa sana.
Hakikisha unalinda utu wako wa ndani.
Ulinde utu wako wa ndani kwa kuyaishi matunda Tisa ya ROHO MTAKATIFU.
Tunza sana matunda Tisa ya ROHO MTAKATIFU.


MUNGU akubariki kwa kujifunza somo hili muhimu na pia Ukipenda kunisapoti kwa sadaka yako ya hiari katika huduma yangu karibu sana na pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane nitakujulisha jinsi ya kukipata.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa BWANA YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
0714252292.
0786719090
mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu.

Comments