DINI INAWEZA KUDANGANYA LAKINI YESU HADANGANYI.

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.
DINI INAWEZA KUDANGANYA LAKINI YESU HADANGANYI.

Bwana YESU atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU aliye hai.
Kuna Dini Nyingi Tu Duniani Lakini Kama Wewe Umefuata Dini Hakika Dini Yako Haitakusaidia Siku Ya Mwisho Maana Dini Haiwezi Kumuokoa Mtu Hata Mmoja. 
Kuna Dini Ni Wanaabudu Sanamu, Kuna Dini Ni Taasisi Tu Za Majini, Kuna Dini Ni Miradi Tu Ya Majini(mashetani), Kuna Dini Ni Waabudu Shetani, Kuna Dini Ni Waabudu Wanyama, Kuna Dini Wanaabudu Watu, Kuna Dini Wanaabudu Mawe N.k. 

Kuna Aina Mbili Za Maana Ya Neno Dini. 
1.Dini Ni Mpango Wa Mwanadamu Kumwabudu MUNGU Wa Mbinguni Kwa Njia Takatifu Au Wengine Kumwabudu Vibaya. 

2. Dini Ni Mpango Wa Shetani Kumtumia Mwanadamu Ili Mwanadamu Huyo Amwabudu Shetani Na Kuikosa Mbingu. 

Kuifuata Dini Hakuna Msaada Kwa Mwanadamu. 
Kuifuata Njia Ya Uzima Ndio Kuufuata Uzima Wa Milele. 
Biblia Inadokeza Kuhusu Njia Ikisema Njia Ya Uzima Wa Milele Ni YESU KRISTO Pekee.
Yohana 14:6-7 ''YESU akamwambia, Mimi ndimi njia, na kweli, na uzima; mtu haji kwa Baba(MUNGU), ila kwa njia ya mimi. Kama mngalinijua mimi, mngalimjua na Baba(MUNGU); tangu sasa mnamjua, tena mmemwona.''

 Tena Biblia Inasema Kwamba Maamuzi Ya Njia Pekee Ya Watu Wote Kuifuata Ili Wafike Uzima Wa Milele Imetolewa Na Muumba Mbingu Na Dunia.
Yohana 3:16-21 '' Kwa maana jinsi hii MUNGU aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele. Maana MUNGU hakumtuma Mwana(YESU) ulimwenguni ili auhukumu ulimwengu, bali ulimwengu uokolewe katika yeye. Amwaminiye yeye hahukumiwi; asiyeamini amekwisha kuhukumiwa; kwa sababu hakuliamini jina la Mwana pekee wa MUNGU. Na hii ndiyo hukumu; ya kuwa nuru imekuja ulimwenguni, na watu wakapenda giza kuliko nuru; kwa maana matendo yao yalikuwa maovu. Maana kila mtu atendaye mabaya huichukia nuru, wala haji kwenye nuru, matendo yake yasije yakakemewa. Bali yeye aitendaye kweli huja kwenye nuru, ili matendo yake yaonekane wazi ya kuwa yametendwa katika MUNGU. ''
 Ndugu Yangu, Je Umefuata Njia Au Dini?.
Watu wengi sana na wa dini zote wanajua kabisa kwamba njia ya uzima wa milele ni YESU KRISTO tu.
Ni ajabu mtu anajua kabisa kwamba dunia nzima inasubiri ujio wa YESU KRISTO lakini watu hao hao wameshikilia dini na kumwacha YESU.
Kuna watu wameamua kabisa kujitengenezea akina yesu wao na ndio maana hawahubiri injili ya kweli ya Bwana YESU. Ukweli ni kwamba YESU KRISTO ni mmoja tu, ndivyo Biblia inavyofundisha.
Ukiona mwingine anajiita Yesu huyo ni Baryesu tu na sio YESU KRISTO.
Na Biblia iko wazi Kabisa kwamba akina Baryesu huwa ni wachawi, tena manabii wa uongo maana wanampinga Bwana YESU KRISTO.
Akina Bar-yesu ni watoto wa shetani na maadui ya haki.
Akina Baryesu ni wenye hila na uovu ndani yao.
Hulipotoa Neno la MUNGU kwa kuwazuilia watu Kuokolewa na Bwana YESU.
Maandiko haya yathibitisha vyema tabia za Bar-Yesu.

Matendo 13:6-12 "Walipokwisha kupita katikati ya kisiwa chote mpaka Pafo, wakaona mtu mmoja, mchawi, nabii wa uongo, Myahudi jina lake Bar-Yesu; mtu huyu alikuwa pamoja na liwali Sergio Paulo, mtu mwenye akili. Yeye liwali akawaita Barnaba na Sauli waje kwake, akataka kulisikia neno la MUNGU. Lakini Elima, yule mchawi (maana ndiyo tafsiri ya jina lake), akashindana nao, akitaka kumtia yule liwali moyo wa kuiacha ile imani. Lakini Sauli, ambaye ndiye Paulo, akijaa ROHO MTAKATIFU, akamkazia macho, akasema, Ewe mwenye kujaa hila na uovu wote, mwana wa Ibilisi, adui wa haki yote, huachi kuzipotoa njia za BWANA zilizonyoka? Basi, angalia, mkono wa BWANA u juu yako, nawe utakuwa kipofu, usilione jua kwa muda. Mara kiwi kikamwangukia na giza, akazunguka-zunguka na kumtafuta mtu wa kumshika mkono na kumwongoza. Ndipo yule liwali, alipoyaona yaliyotendeka, akaamini, akiyastaajabia mafundisho ya Bwana(YESU KRISTO)."
Akina baryesu ni wepesi sana kuhubiri watu waishike dini japokuwa dini hiyo wala sio ya MUNGU wa mbinguni.

Ndugu, usimfuate Bar-Yesu bali mfuate Mfalme wa uzima wa milele YESU KRISTO.
Ngoja nikupe ushuhuda mfupi ili uje kile ambacho akina baryesu wanakitaka.
Kuna Ndugu mmoja alikuwa ananipigia simu na kunipongeza sana kwa mahubiri yangu mtandaoni. Aliweka ukaribu na mimi na siku moja akasema ana maongezi maalum na mimi, akasema yuko tayari kuja kuniona ili tuongee. Sikupenda tuongee ana kwa ana bali kwa simu na ili kutakuwa na ziada basi atakuja kuniona. Yule ndugu aliniambia kwamba ''Wewe Peter ni mtumishi mzuri sana ila unapungukiwa jambo moja tu.'' Nikamwambia niambie ndugu yangu ili nitengeneze. Akasema ''ulichopungukiwa wewe kutokuabudu kanisa ninaloabudu mimi'' Nikamwambia labda niambie imeandikwa wapi kwamba hilo dhehebu tu ndio waenda mbinguni? Akasema kwamba Mwanzilishi wa Kanisa miaka 200 iliyopita alipewa wito wa kuhubiri hivyo atakayesali kanisa lingine huyo sio wa MUNGU. Akaendelea kusema kwamba watu wote wanaoutaka uzima wa milele ni lazima kwanza wamkiri huyo mwanzilishi kwamba ametumwa na MUNGU. Yule ndugu nilimwambia kwamba mimi nina ROHO wa MUNGU na nashuhudiwa kwamba huyo mwanzilishi wa dhehebu hilo ni wakala wa shetani. Yule ndugu akakata simu na nikafuta namba yake, na hakuwahi kunipigia tena. Baada ya siku kadhaa nikasoma ushuhuda wa dada mmoja ambaye alifanikiwa kupelekwa mbinguni na kuzimu na ameandika kwamba alipopelekwa kuzimu na Bwana YESU alimuona huyo mwanzilishi wa dhehebu hilo akijuta na kulia. 
Ndugu unahitaji kuwa makini sana na dini na uwe makini sana na dhehebu.

Wakolosai 2:8 '' Angalieni mtu asiwafanye mateka kwa elimu yake ya bure na madanganyo matupu, kwa jinsi ya mapokeo ya wanadamu, kwa jinsi ya mafundisho ya awali ya ulimwengu, wala si kwa jinsi ya KRISTO.''

Kuna watu wameharibiwa kabisa na mafundisho ya uongo ambayo wala sio mafundisho ya injili ya KRISTO iokoayo.
Ninachoweza kusema kwamba mafundisho hayo yana chanzo na siku zote ujinga Tegemezi Ni Matokeo Ya Malezi Tegemezi.
Ujinga Tegemezi Ni Kuabudu Sanamu Kwa Sababu Tu Umeamua Kulishika Neno La Mlezi Tegemezi, Huku Huna Habari Na Neno La MUNGU.
Ujinga Tegemezi Ni Kuishi Ukijua Kwamba Dhehebu Lenu Tu Ndio Waenda Mbinguni Kwa Sababu Ulifundishwa Na Mlezi Tegemezi, Lakini Biblia Inafundisha Kwamba Wokovu Wa KRISTO Na Utakatifu Ndivyo Humfanya Mtu Kuingia Uzima Wa Milele.
Ujinga Tegemezi Ni Kuibadili Biblia Baada Ya Mlezi Tegemezi Kupata Ufunuo Utokao Kwa Joka La Kuzimu.
Ujinga Tegemezi Ni Kudhani Kwamba Uzima Wa Milele Umo Kwenye Vyakula fulani tu maana vingine ni najisi.
Ujinga Tegemezi Ni Kukataa Kuokoka.
Je Wewe Ni Mjinga Tegemezi?.
Je Unayatii Maneno Ya Mlezi Tegemezi Na Kuliacha Neno La MUNGU?.
Masaa Yameenda Sana Ndugu Zangu.
Ni Wakati Wa Kutubu Na Kuliishi Neno La KRISTO Na Kuachana Na Uongo Wa Walezi Tegemezi.
Mteule Uwe Macho Maana Hizi Ni Siku Za Mwisho.

Waefeso 5:5-6 ''Maana neno hili mnalijua hakika, ya kwamba hakuna mwasherati wala mchafu wala mwenye tamaa, ndiye mwabudu sanamu, aliye na urithi katika ufalme wa KRISTO na MUNGU. Mtu asiwadanganye kwa maneno yasiyo na maana; kwa kuwa kwa sababu ya hayo hasira ya MUNGU huwajia wana wa uasi. ''

Je Unautaka Uzima Wa Milele?.

Warumi 10:9-10 '' Kwa sababu, ukimkiri YESU kwa kinywa chako ya kuwa ni Bwana, na kuamini moyoni mwako ya kuwa MUNGU alimfufua katika wafu, utaokoka. Kwa maana kwa moyo mtu huamini hata kupata haki, na kwa kinywa hukiri hata kupata wokovu.''

Kama Unautaka Uzima Wa Milele Uko Pekee Kwa BWANA YESU, Mpokee Leo Na Anza Kuishi Maisha Matakatifu.
Kama Uko Nje Na Wokovu Wa BWANA YESU Hakika Huko Unapoteza Muda Wako Bure Na Unajichosha Bure Bila Faida Hata Moja. Biblia inasema kwamba hakuna Wokovu nje na Bwana YESU, Matendo 4:12 ''Wala hakuna wokovu katika mwingine awaye yote, kwa maana hapana jina jingine chini ya mbingu walilopewa wanadamu litupasalo sisi kuokolewa kwalo. ''

Ndugu, Wapo watu hawalali usiku na mchana ili kazi ya MUNGU iende mbele.
Lakini wapo pia watu ambao wamelala usiku na mchana ili kazi ya MUNGU isiende mbele.
Lakini pia wapo ambao hawalali usiku na mchana ili tu kuivuruga kazi ya MUNGU ya injili ya KRISTO.
Wapo watu hutunga uongo ili tu injili ya KRISTO itukanwe.
Wapo ambao hata huwazushia watumishi wa MUNGU ili tu Kanisa litukanwe.

Ndugu Yangu katika kazi ya Bwana YESU nakuomba songa mbele haijalishi wazushi ni wengi.
Ndugu hubiri injili haijalishi mawakala wa shetani ni wengi kuliko kazi yenyewe.
Wewe una ROHO MTAKATIFU hivyo hubiri injili ya KRISTO wakati unaofaa na wakati usiofaa.
Mawakala wa shetani lazima wazibwe vinywa vyao vinavyoeneza uongo.
Tito 1:10-11 " Kwa maana kuna wengi wasiotii, wenye maneno yasiyo na maana, wadanganyaji, na hasa wale wa tohara, ambao yapasa wazibwe vinywa vyao. Hao wanapindua watu wa nyumba nzima, wakifundisha yasiyowapasa kwa ajili ya mapato ya aibu."

Usifuate tu dini maana dini inaweza ikakufanya ujione u mtakatifu wakati katika Viwango vya Biblia wewe sio mtakatifu maana umekataa kuokoka.

 MUNGU akubariki kwa kujifunza somo hili muhimu na pia Ukipenda kunisapoti kwa sadaka yako ya hiari katika huduma yangu karibu sana na pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane nitakujulisha jinsi ya kukipata.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa BWANA YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
+255714252292.
mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu.

Comments