BAADHI YA VIFUNGO NA LAANA.

Na Mwl Peter Mabula 
Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi 



Bwana YESU KRISTO Mwokozi atukuzwe rafiki.
Karibu Tujifunze Neno la MUNGU.

◼️Kuna watu huteswa na laana na wengine vifungo mbalimbali vya kiroho.

Kumbu 11:26-29 " Angalieni, nawawekea mbele yenu hivi leo baraka na laana; baraka ni hapo mtakapoyasikiza maagizo ya BWANA, Mungu wenu, niwaagizayo leo; na laana ni hapo msiposikiza maagizo ya BWANA, Mungu wenu, mkikengeuka katika njia niwaagizayo leo, kwa kuandama miungu mingine msiyoijua."

◼️Ukisoma maandiko hapo juu unagundua kwamba Vyanzo vikuu  vya laana  ya Mtu ni 3.

1. Kutokusikiliza maelekezo ya MUNGU katika KRISTO YESU na kuyafuata.

◼️Laana hii inaweza kumpata hata Mtu wa Kanisani ila ameasi maelekezo ya MUNGU.

◼️Mtu asipofuata Utakatifu atakuwa anatenda maovu na baadhi ya maovu huleta laana kwa Mtu husika.
Mfano hai ni andiko hili ambalo linaonyesha wanaotenda maovu haya Wana laana.

2 Petro 2:14 "wenye macho yajaayo uzinzi, watu wasiokoma kutenda dhambi, wenye kuhadaa roho zisizo imara, wenye mioyo iliyozoezwa kutamani, wana wa laana;"

➡️Sasa Mfano mmojawapo kati ya mingi ni huu wa Mtu kukosea Kanisa fulani  la Wokovu wa KRISTO  akahama ili kuficha dhambi yake, Mfano Mtu amezini akaonywa na Viongozi wa Kanisa akahama na kuanza kuwasema vibaya kwa uzushi Watumishi waaminifu wa Bwana YESU KRISTO.

➡️Ndugu, usitoke Mahali Bila Kutengeneza Kama Umekosea kama unataka kuiepuka laana .

➡️Kuna Watu Akiharibu Kanisa Fulani Anahama Haraka Sana, Ni Mbaya Sana Hiyo. 
Rudi Ukatengeneze Ndipo Uhame Kwa Amani. 
Kumbuka Kwamba Unaweza Kuwakimbia Wanadamu Lakini Sio MUNGU. 
Narudia Tena Unaweza Ukawakimbia Wanadamu Lakini Sio MUNGU. 

MUNGU Wa Mbinguni Amenituma Nikuambie Kwamba Rudi Ukatengeneza Kule Ulikoharibu.

 Utakimbilia Makanisa Mangapi! Maana Kila Kanisa Unalohamia Unakosea Na Kuhama. 

Ewe Binti Na Mama Wa Uzinzi Nakuonya, Ewe Kijana Na Baba Wa Uzinifu Nakuonya. 
Ewe Mwizi Na Mchawi Nakuonya, Ewe Mchonganishi Na Msingiziaji Nakuonya, 
Ewe Tapeli Na Mgombanishi Nakuonya. 
Kuwasema Vibaya Wachungaji Ulikoharibu Ni Kuongeza Laana Katika Kikombe Chako Chenye Dhambi. 
Rudi Ukatubu, Ukaweke Wazi Dhambi Yako Na Utoke Kwa Amani.

2. Chanzo kingine Cha laana ni kukengeuka kuacha njia ya MUNGU katika KRISTO YESU.

◾Kukengeuka ni Nini?

➡️Kukengeuka ni kupita njia ya pembeni huku njia halisi unaijua na unaiona.

➡️Mfano Mtu anajua kabisa hakuna Uzima wa Milele nje na YESU KRISTO lakini yeye anaamua kumwacha YESU na kufuata miungu mingine, huko ni kukengeuka.

Ayubu 34:27 "Kwa sababu walikengeuka, wasimwandame yeye, Wasikubali kuzishika njia zake hata moja;"

➡️Mfano mmojawapo kati ya mingi sana  ya kukengeuka ni kutoa mimba.
Mtu anajua kabisa kutoa mimba ni dhambi lakini anaamua kutoa.

Mtu anayetoa mimba ni Mtu aliyekengeuka akaacha njia ya MUNGU.

➡️Laana yaweza kuja kwa kutoa mimba (abortion) yaani kuua kiumbe kabla hakijazaliwa na kwasababu hiyo mtu anakuwa na laana, na hii laana ya kutoa mimba inafuatilia kuanzia mwenye mimba, mtoa nauli ya kwenda kutoa mimba huku akijua, mshauri wa kutoa mimba hiyo, msindikizaji wa kwenda kutoa mimba maana anajua na daktari mtoaji mimba, wote wapo chini ya laana. 

Kama hujui Kuna laana humpata hata Mtu ambaye ana Mamlaka ya kukemea Uovu ila yeye akaacha kukemea hivyo Uovu huo unaendelea.
Mfano hai ni huu 

1 Samweli 3:13 "Kwa maana nimemwambia ya kwamba nitaihukumu nyumba yake milele, kwa ajili ya ule uovu alioujua; kwa kuwa wanawe walijiletea laana, wala yeye hakuwazuia."

◼️Kama unahusika katika kipengele chochote katika hivyo; Tubu na okoka kisha ishi sasa maisha mataktifu daima.

1 Petro 2:1 "Basi, wekeni mbali uovu wote na hila yote, na unafiki na husuda na masingizio yote."

 3. Kuiandama miungu mingine.

Kumwacha MUNGU katika KRISTO YESU na kuifuata miungu mingine hupelekea laana kwa mhusika.

Kumbu 8:19 "Lakini itakuwa, kama ukimsahau BWANA, Mungu wako, na kuiandama miungu mingine, na kuitumikia na kuiabudu, nawashuhudia leo ya kuwa mtaangamia bila shaka."

➡️ Kumwacha MUNGU katika KRISTO YESU ni ujinga mbaya zaidi ambao Mtu anaweza kuufanya.

Ukimwacha YESU huko unakoenda utafanya mabaya yatakayokutengenezea laana.

◼️Na siku zote laana ni mbaya sana.

Isaya 24:6 ''Ndiyo sababu laana imeila dunia hii, na hao wanaoikaa wameonekana kuwa na hatia, ndiyo sababu watu wanaoikaa dunia wameteketea, watu waliosalia wakawa wachache tu."

◼️Lakini pia zipo laana ambazo zinaweza kumpata Mtu kwa sababu ya kufanya asiyopaswa kuyafanya kwa watu Maalumu Mfano Wazazi, Watumishi wa MUNGU au watu ambao MUNGU aliwapa jukumu la kumsaidia Mtu huyo lakini anapofanikiwa anaanza kuwasema vibaya.
Laani hizi hutamkwa kwa Vinywa na vinamkamata Mtu, hizi zinaitwa laana Zenye sababu.

Kumbu 27:16 "Na alaaniwe amdharauye baba yake au mama yake. Na watu wote waseme, Amina."

➡️Kama vile kamba inavyoweza kumkamata kuku aliyefungwa kwayo hata asivuke eneo la urefu wa kamba ile, Ndivyo vile laana inavyoweza kumkamata Mtu hata asiweze kuvuka mpaka wa maneno ya laana aliotamkiwa.

◼️Dawa ya kupona laana zote  ni Moja tu.
Ni kuamua Kuokoka yaani kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi wako Kisha ukaanza kuishi maisha matakatifu katika yeye.

Yohana 8:36 "Basi Mwana akiwaweka huru, mtakuwa huru kweli kweli."

➡️Watu wengi huteseka na laana ingawa wanajua kabisa kwamba kama wakimkimbilia Bwana YESU kwa kuamua hakika atawafungua kutoka laana na kuwaweka huru.

◼️Wengi sana hupenda kuombewa tu huku wakiendelea na dhambi lakini taarifa muhimu sana ni hii Maombi bila utakatifu ni kazi isiyoleta faida.

Asante kwa kujifunza Neno la  siku ya leo, Kabla sijamaliza nakuomba Wewe ambaye hujaokoka au uliokoka ukarudi nyuma, nakusihi sana amua Leo kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi wako na Jina lako litaandikwa katika kitabu Cha uzima Mbinguni, katika maeneo Yako tafuta Kanisa safi la kiroho linalohubiri Wokovu wa KRISTO YESU nenda kamweleze Mchungaji atakuongoza Sala ya Toba utaokoka Kisha baada ya hapo fuata mafundisho ya Neno la MUNGU hapo Kanisani.
MUNGU wa Mbinguni akubariki sana.
By Mwl Peter Mabula 
Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi.
+255714252292 ( kwa Ushauri, maombezi,  pamoja na Whatsapp)
Ubarikiwe.

Comments