MAKUNDI YA WATU WANAOKUJA MAISHANI MWAKO.

 
Peter na Scholar   Mabula.
Watenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
MAKUNDI YA WATU WANAOKUJA MAISHANI MWAKO.


Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu yangu!
Karibu sana tujifunze Neno la MUNGU kisha tuombe maombi ya ushindi mkuu.
Leo ninao ujumbe ambao ROHO wa MUNGU amenipa.
Karibu tujifunze na kuongezeka maarifa ya kiroho.
Katika maisha ya kila mtu yeyote kuna watu ambao hutokea katika maisha yake. Kuna watu walitokea zamani na kuna watu watatokea baadae. Hakuna mtu ambaye tangu kuzaliwa hadi uzee wake ameishi peke yake tu, lazima kuna watu amewahi kuishi nao au ataishi nao. Watu hao wanaweza kuwa ni wazazi, walezi, washauri, marafiki, majirani, wanakikundi, wanajamii n.k.
Kila mmoja wetu najua kabisa umewahi kuishi au kufika mahali fulani fulani na ulikutana na watu fulani fulani.
Ngoja nianze na mfano wangu mwenyewe ili unielewe.
Mimi Binafsi  Nilizaliwa Mwanza  kisha baada ya Baba yangu kufariki nikaenda kuishi kwa Bibi Wilaya ya Chato kwa sasa, baadae ikabidi nikaishi kwa Shangazi yangu Biharamulo ambako ndiko nilisoma kuanzia darasa la kwanza hadi kidato cha nne. Baada ya hapo niliishi Mwanza, Kisha nikaishi Kigoma, kisha nikaishi Pwani, kisha nikaishi Iringa, Kisha Nikaishi Zanzibar(Unguja na Pemba)  na sasa Dar es salaam.
Katika maeneo hayo yote ambao niliishi nilikutana na watu wa aina tofauti tofauti na watu hao ndio wanatengeneza makundi ya watu waliokuja maishani mwangu. Hata wewe kuna makundi ya watu kadhaa wengi tu walitokea katika maisha yako katika maeneo tofauti uliyokaa. Kuna watu walitokea utotoni mwako, kuna watu walitokea shuleni ulikosoma, kuna watu walitokea chuoni na kila sehemu uliyokaa n.k.
Nilipopewa ujumbe huu hisia zangu zilienda mbali sana na ni moja ya masomo yangu ya kipekee sana, kuna wakati nilihisi maumivu na kuna wakati nilihisi furaha lakini mwisho nilimshukuru MUNGU Baba kwa uzima wake kwangu, Nilimshukuru Bwana YESU kwa kuniokoa na nilimshukuru ROHO MTAKATIFU kwa kuniongoza na kunifundisha.
Inawezekana kabisa kuna aina nyingi Kibiblia za makundi ya watu ambao wanaweza wakatokea katika maisha ya mtu.
Katika umri wako huo naamini kabisa umewahi kuishi na watu wengi na wa tabia mbalimbali na tamaduni mbalimbali.
Jifunze kitu katika ujumbe huu na utapata kitu cha kuombea ili kujiondoa katika vifungo na vikwazo vilivyosababishwa na watu waliokuja katika maisha yako.
Inawezekana kabisa kuna kundi la watu hujawahi kuishi nao lakini Neno la MUNGU la leo ninakujulisha ili hata kama utaishi nao baadae basi ujue nini cha kufanya.
 
Makundi manne(4) ya watu wanaokuja maishani mwako ni;

 1. WATU AMBAO NI BARAKA KWAKO.

Watu hawa hukuonyesha wewe kufanikiwa kiroho.
Watu hawa hukuthamini na kukutendea mema.
Watu hawa wanalibeba kusudi la MUNGU kwa ajili yako.
Watu hawa ni baraka kwako katika mambo mengi, hebu tuone zaidi katika maandiko.
Mwanzo 30:27-28 '' Labani akamwambia, Iwapo nimeona fadhili machoni pako, kaa, maana nimetambua ya kwamba BWANA amenibariki kwa ajili yako. Akasema, Sema mshahara wako utakao, nami nitatoa.''
 Labani alikuwa na maisha yake lakini baadae Yakobo akaja kuishi kwa Labani. Yakobo alikuwa baraka katika maisha ya Labani maana Labani mwenyewe alitambua kabisa kwamba MUNGU amembariki kwa sababu Yakobo yuko pale. Kwanini abarikiwe kwa sababu Yakobo yuko pale? Ni kwa sababu Yakobo alikuwa baraka kwa Labani. Yakobo alipotaka kuondoka Labani alitaka kumzuia kwa kutaka kumuongezea Mshahara maana Labani alitambua kabisa kwamba Yakobo ni Baraka kwake. 
Wako watu ni baraka kwako. 
Ndugu mmoja msomi alihangaika sana kupata kazi lakini siku moja alikutana na mtu ambaye ni baraka kwake. Yule msomi kijana alikwenda ibadani siku moja na katika ibadani ile ikajulikana kwamba alikuwa amehangaika sana kupata kazi lakini hakupata. Mama mmoja aliyeonekana wa kawaida sana alimfuta na kumwambia kwamba amtafute maana atapata kazi. Yule kijana alidharau maana hakujua kama kupitia mama yule angepata kazi na kufanikiwa. Baadae alienda kama kujaribu tu na alipofika kazini kwa Yule mama, yule mama alipiga simu na kisha akamwambia yule kijana aende ofisi fulani kubwa sana kuanza kazi. Yule kijana alijikuta amepata kazi Wizarani kwa kupitia yule mama. Ndugu kuna watu ni baraka katika maisha yako.
Watu ambao ni baraka kwako watakuombea, watakuthamini na kukufundisha Neno la MUNGU.
Watu ambao ni baraka kwako hawatakubagua, hawatakuwazia mabaya, hawatakupangia mabaya na watakupenda jinsi ulivyo.
Watu ambao ni baraka kwako hawataangalia udhaifu wako na hata hawataujali kama huo udhaifu upo.
Mfano mmoja wapo wa watu ambao ni baraka kwako ni Watumishi wa MUNGU. Watumishi  ni watu ambao ni baraka kwako maana wanakujulisha yaliyo ya KRISTO.
Kuna watu wamesimama kiroho kwa sababu tu waliishi na watu ambao ni baraka.
Watu waliombeba YESU ndani yao hao hakika ni baraka kwako.
Mwanzo 39:5 '' Ikawa tokea wakati alipomweka awe msimamizi juu ya nyumba yake, na vyote vilivyomo, BWANA akabariki nyumba ya yule Mmisri kwa ajili ya Yusufu. Mbaraka wa BWANA ukawa juu ya vyote alivyokuwa navyo katika nyumba, na katika shamba.'
Ndugu hakika kuna watu ambao ni baraka katika maisha yako. 
Huyu Potifa alikuwa na maisha yake lakini kuja kwa Yusufu katika nyumba ya Potifa kulileta baraka. Potifa alipomteua Yusufu kusimamia nyumba yake hakika ndipo baraka ya MUNGU ikawa juu ya familia ile.
Kwa nini baraka ya MUNGU iwe wakati ule? Ni kwa sababu Yusufu alikuwa ni baraka.
Kuna watu katika maisha yako ni baraka kwako. Inawezekana unawadharau kwa sababu hujui kama wamelibeba kusudi la MUNGU juu yako.
Kuna watu kila siku wanaokuombea, hao ni baraka kwako.
Kuna watu kila mara hufunga na kuomba kwa ajili yako, hao ni baraka kwako.
Kuna watu wako tayari kukusomesha bila malipo wala hila, hao ni baraka kwako.
Kuna watu ukiishi nao utashangaa utakavyostawi, kwa sababu hao ni baraka kwako.
Kuna watu wanaweza kukusaidia hata kipindi ambacho kila mtu anakuchukia.
Kuna watu wako tayari kukusaidia ili utoke katika magumu uliyonayo, hao ni baraka kwako.
Kitendo cha Yakobo kutokea katika maisha ya Labani tayari baraka za MUNGU zikaingia kwa Labani.
Kitendo cha Yusufu kuingia katika maisha ya Potifa tayari na baraka za MUNGU zikaingia katika maisha ya Potifa.
Baraka za MUNGU ziko za aina tano.
Kuna baraka za uzao, Kuna baraka za afya, kuna baraka za uchumi, kuna baraka za ndoa, na kuna baraka za kutamalaki.
Mteule wa KRISTO mmoja katika ukoo wenu au familia yenu anaweza kufanyika baraka kwetu maana anawaombea na kukataa mipango ya shetani kwenu.
Ndugu, Kuna watu ni baraka sana katika maisha yako.
Muhimu kwenye maombi yako kuhusu watu ambao ni baraka kwako .
a. Omba MUNGU akukutanishe na watu hao.
b. Omba MUNGU wakae kwenye nafasi zako za kiMUNGU kwa ajili yako.
c. Omba MUNGU kwamba walitimize kusudi la MUNGU kwa ajili yako.
 
2. WATU AMBAO NI DARASA KWAKO.

Watu ambao ni darasa kwako huja katika maisha yako kutoa somo kwako.
Watu hao wanaweza kuwa ni watu wema au watu wabaya. Watu hao wanaweza kutoa darasa zuri kwako au darasa baya kwako, yote ni madarasa kwako ila maamuzi ya kufuata unayo wewe mwenyewe, mimi nakushauri fuata watu ambao ni darasa jema kwako.
Mithali 16:4 '' BWANA amefanya kila kitu kwa kusudi lake; Naam, hata wabaya kwa siku ya ubaya.'

Kuna watu unaweza ukaishi nao lakini ni watu wakali sana kwako na wanaoonea hovyo, hao ni darasa kwako ili ukiingia katika maisha yako mwenyewe ukumbuke kwamba hutakiwi kufuata wao.
Binti mmoja baada ya kufiwa na mama yake na kisha baba yake kumkataa alienda kuishi kwa ndugu ambao walikuwa wanamtesa sana na kumbagua. Baadae aliingia katika ndoa yake na alianza kuishi na watu na kuwatendea mema maana alikumbuka vile ambavyo yeye aliteswa na akajifunza kwamba yeye hawezi kufanya ubaya huo.
Lakini pia kuna watu ni wakali sana lakini wanakusaidia sana, hao ni darasa kwako pia.
Kuna familia watoto wote wamesoma kwa sababu baba yao alikuwa mkali akitaka sana kila mtoto asome sana, mzazi huyo ni darasa.
Watu ambao ni darasa kwako huja katika maisha yako kutoa somo kwako.
Kuna watu wanakuja maishani mwako ili kutoa darasa la maisha kwako, Kuna watu ambao wanakuja maishani mwako ili kutoa darasa la kiroho kwako.
Ni lazima ujifunze kwao katika maisha yao ya kiroho.
Jifunze kwao walimalizaje safari yao duniani?
 Waebrania 13:7-8 '' Wakumbukeni wale waliokuwa wakiwaongoza, waliowaambia neno la MUNGU; tena, kwa kuuchunguza sana mwisho wa mwenendo wao, iigeni imani yao. YESU KRISTO ni yeye yule, jana na leo na hata milele.''
 Watu ambao ni darasa kwako wako katika makundi mengi sana ila wote ni darasa kwako.
Kuna mtu anaweza kuwa katika maisha magumu sana au anaumwa sana kwa muda mrefu lakini kila ukimtembelea ana furaha na anamkiri YESU bila kuyumba, huyo ni darasa kwako maana ikitokea umepitia magumu basi ujue kwamba wapo waliopitia magumu kuliko wewe lakini waliendelea mbele vyema kabisa na Wokovu.
Biblia inaonyesha jambo kwenye maandiko hapo juu kwamba uwakumbuke waliokuongoza kumjua KRISTO na ujifunze kwao huku ukikumbuka walimalizaje safari yao(Kuna mtu analia huku anasoma ujumbe huu).
Jifunze waliweka kipaombele katika nini?
Biblia imewazungumza watu wema hao kwamba iga imani yao kwa Bwana YESU.
Ndugu katika maisha yako najua kabisa kuna watu ambao watatokea katika maisha yako kama darasa kwako, hakikisha tu unafanyia kazi darasa la mema na sio darasa la mabaya.
Wako watu pia ni darasa kwako kwa maana uliona jinsi walivyookoka lakini baadae wakaanguka. Je walipungukiwa nini kiroho hata wakaanguka? Hao ni darasa kwako kwamba ujitahidi usipite katika tabia zao ambazo zilisababisha wakaanguka.
Kuna watu pia ni darasa baya kwako maana wamekufundisha uzinzi au  ulevi au uvutaji sigara na bangi au wamekufundisha jambo lolote baya ambao linakutesa sasa.
Wako watu ni makahaba kwa sababu walikubali kufuata darasa la mafundisho mabaya, kwa sababu waliishi na watu ambao ni walimu wabaya sana katika maisha yao.
Inawezekana kabisa umeishi na watu wengi ambao ni darasa kwako, lakini nakuomba fanyia kazi darasa la mema na sio mabaya.
Inawezekana kabisa katika familia yenu kulikuwa na mambo yanaochukiza sana, kwa sasa uko katika ndoa yako inakupasa usiyafuate yale ya familia yako maana ulijifunza kuwa sio mambo mazuri.
Mimi Peter Binafsi kuna jambo ambalo niliapa katika maisha yangu kwamba siwezi kulifanya hata kabla sijaokolewa na Bwana YESU. Jambo hilo ni kuoa wake zaidi ya mmoja. Niliwahi kuona baba wa familia akiuawa na mke wake kwa sababu tu yule baba amepunguza upendo kwake na kumpenda zaidi mke mwenza. Nimewahi kuona wanandoa wakipigana na kuumizana kwa sababu tu baba wa familia alimpenda zaidi mke mkubwa kuliko mke mdogo. Baada ya kujifunza hayo mimi niliapa ya kwamba katika maisha yangu nitaoa mke mmoja tu na nitampenda na kumthamini sana, hayo niliyawaza baada ya kuona madhara ya kuoa mke zaidi ya mmoja.
Ndugu kuna watu ni darasa kwako, hakikisha tu unafanyia kazi darasa la mema na sio mabaya.
Mabaya yajue na uyakatae katika maisha yako.
Kuna mtu anaweza akapitia magumu sana na majaribu ya kila aina, huyo ni darasa kwako kwamba hata ukipitia magumu uvumilie.
Kuna watu huamka usiku kuomba, hao ni darasa kwako.
Kuna watu akikosa ibada kanisani anatamani hata kulia, hao ni darasa kwako.
Kuna watu kila siku wanasoma Biblia, hao ni darasa kwako.
Kuna watu wengi sana umeishi nao au utaishi nao, hao ni darasa katika maisha yako.
Iga yaliyo mema yao na sio mabaya.
Biblia inasema  '' BWANA amefanya kila kitu kwa kusudi lake; Naam, hata wabaya kwa siku ya ubaya.-Mithali 16:4 ''

 3. WATU WALIOBEBA VIFUNGO KWAKO.

Hili linaweza kuwa ni kundi la watu waliotokea katika maisha yao au watatokea baadae katika maisha yako.
Watu hawa ni kundi baya kwako hivyo kama hawajatokea katika maisha yako unahitaji kuwa makini sana nao na kujihadhari sana nao.
Kama wameshatokea na kukufanya uingie katika vifungo vya kipepo unahitaji kuomba maombi ya kufuta vifungo vya kishetani katika maisha yako.
1 Wafalme 16:29-31 '' Ahabu mwana wa Omri alianza kutawala juu ya Israeli katika mwaka wa thelathini na nane wa Asa mfalme wa Yuda; akatawala Ahabu mwana wa Omri juu ya Israeli katika Samaria miaka ishirini na miwili. Ahabu mwana wa Omri akafanya yaliyo mabaya machoni pa BWANA kuliko wote waliomtangulia. Ikawa, kama ingalikuwa neno dogo tu kuyaendea makosa ya Yeroboamu mwana wa Nebati, akamwoa Yezebeli binti Ethbaali, mfalme wa Wasidoni, akaenda akamtumikia Baali, akamsujudia. ''
 Yezebeli alipoingia tu katika maisha ya Ahabu alimfanya Ahabu kuwa Mfalme muovu kuliko wafalme wote waliomtangulia kutawala katika Isareli.
Yezebeli alikuwa amebeba vifungo vya giza kwa Ahabu na Waisraeli.
Kipindi hiki pia ndio kipindi ambacho Eliya alikuwa anamtumikia MUNGU na ikafika kipindi kwa sababu ya Yezebeli mwabudu shetani basi Eliya Nabii alidhani kabisa kwamba Katika taifa zima la Israeli anayemwabudu MUNGU wa mbinguni amebaki peke yake, kumbe kulikuwa na wengine 450 wamejificha kwa sababu ya kumuogopa Yezebeli. Lakini bebu tujiulize kwanini ifike kipindi katika taifa zima watu wanaomcha MUNGU wawe 451 tu?
Yezebeli  mwabudu shetani alikuwa ametokea katika maisha ya Waisareli na huyo alikuwa amebeba vifungo vya giza kwao. Alipoolewa tu na Mfalme kwanza alitengeneza sanamu ya kuabudiwa ikulu kisha akafanya mbinu zake kuwafanya watu wote katika taifa wamwabudu shetani na sio MUNGU wa mbinguni.
Kuna watu wamebeba vifungo kwako.
Watu waliobeba vifungo kwako ni watu ambao ulipoishi nao walikuingiza katika mikataba ya shetani ambayo inawezekana kabisa inakutesa sasa.
Kuna watu ulipoishi nao tu walikupeleka kwa waganga wa kienyeji na ukajikuta umeingiza vifungo vya kishetani ambavyo inawezekana hadi leo vinakutesa(Kuna mtu analia wakati akisoma ujumbe huu)
Yezebeli alipotokea tu katika maisha ya Waisraeli basi majanga ndipo yalipoanza.
Watu waliobeba vifungo kwako ni watu waliokufundisha uzinzi(Usile ndugu, tubu)
Watu waliobeba vifungo kwako ni watu waliokufundisha uongo, , wizi, utapeli, ujambazi na kila aina ya dhambi.
Kundi hili ni kundi hatari sana na inawezekana umewahi kuishi na watu wa aina hii au utaishi nao baadae, ndugu uwe makini sana.
Unaweza ukaenda kuishi sehemu na ukajikuta unachanjwa chale kwa sababu tu utamaduni wa familia hiyo ni kuchanjwa chale kila baada ya miaka kadhaa.
Watu wengi sana wako katika maagano ya giza na vifungo vya kipepo kwa sababu waliishi na watu waliobeba vifungo vya giza.

4. WATU AMBAO MIOYO YAO IMEAMBATANA NA MOYO WAKO.

Watu hawa wako katika makundi mawili.
Kuna watu ambao moyo wako umeambatana na mioyo yao kwa mema tu lakini pia kuna watu ambao mioyo yao imeambatana na moyo wako kipepo, hapa uwe makini sana.
1 Samweli 18:1 ''Ikawa Daudi alipokwisha kusema na Sauli, roho ya Yonathani, ikaambatana na roho ya Daudi, Yonathani akampenda kama roho yake mwenyewe. ''
Daudi alijikuta moyo wake unaambatana na moyo wa Jonathan mtoto wa Sauli.
Hata wewe moyo wako unaweza ukaambatana na mtu fulani kwa sababu tu ametokea katika maisha yako, umeishi naye au mlikaa sehemu moja pamoja.
Watu ambao moyo wako unaambatana na mioyo yao kwa mema hakika hao huiona thamani yako.
1 Samweli 19:1-2 '' Kisha Sauli akasema na mwanawe Yonathani, tena na watumishi wake wote, kwamba wamwue Daudi. Lakini huyo Yonathani, mwana wake Sauli, alikuwa akipendezwa sana na Daudi. Basi Yonathani akamwambia Daudi, akasema, Sauli, baba yangu, anatafuta kukuua; basi, nakusihi, ujiangalie sana asubuhi, ukae mahali pa siri na kujificha;''
Tumeona mwanzo kwamba moyo wa daudi na moyo wa Jonathan viliambatana  na matokeo yake tunayaona katika maandiko maana Jonathan alimwepusha kifo Daudi kwa sababu mioyo yao iliambatana.
Kuna watu kabisa moyo wake unaweza ukaambatana nao kwa mwema kabisa.
Mtu ambaye moyo wake umeambatana na moyo wako anaweza kukuepusha na mabaya yaliyokusudiwa kwako.
Kuna watu wanaweza wakakuonea kinyaa lakini huyo ambaye moyo wako na wake vimeambana hakika hatakuonea kinyaa.
Lakini pia ni muhimu tukajua kwamba kuna watu mioyo yao imeambatanishwa kipepo na watu wengine, hii ni hatari sana na ina madhara makubwa.
Ndio maana Biblia inasema '' Linda moyo wako kuliko yote uyalindayo; Maana ndiko zitokako chemchemi za uzima.-Mithali 4:23''
Kuna ndoa nyingi ziko katika migogoro mikubwa sana kwa sababu tu baba wa familia moyo wake umeambatana kipepo na hawara. Hawara huyo alimwendea kwa mganga na mioyo yao ikaambatana kipepo. Baba yule hakumbuki tena familia yake wala watoto wake wala mke wake. Mama unaweza ukaomba sana na kulia sana lakini usipoifuta connection ya kipepo kati ya moyo wa mume wako na moyo wa hawara hakika mumeo ataendelea kutelekeza familia.
Kikawaida mume na mke wanatakiwa mioyo yao iambatane wao tu maana huo ndio mpango wa MUNGU. Ukiona moyo wa  mke wako au mume wako umeambatana na moyo wa  mtu mwingine wa jinsia tofauti tambua kabisa hapo kuna hila za shetani. Futa hiyo connection ya kipepo iliyoambatanisha moyo wa mwenzi wako na watu wengine.
Hata mumeo inawezekana kabisa hawezi kufanya jambo hadi amuulize shangazi, anaweza akafanya mambo mengi bila kukushirikisha ila mjomba au baba mdogo ndio anajua. Kuna connection zingine ni za kipepo baina ya moyo wa mtu na mtu.
Binti inawezekana kabisa moyo wa mchumba wako ambaye unampenda sana na mliahidiana mtafunga ndoa lakini kuna binti mwingine kamwendea kwa mganga mchumba wako au amefanya mbinu zingine na kuubadilia moyo wa mchumba wako na sasa hakutaki wewe kwa sababu anampenda mwingine ambaye mioyo yao imeambatana kipepo.
 Ndugu usipoomba maombi ya kuutenga mbali moyo wa mwenzi wako na mioyo na watu wabaya hakika unaweza kujikuta unateseka sana.
Mifano ipo mingi mno lakini naomba ulijue hiyo maana watu hao ni watu ambao wanaweza wakatokea maisha mwako.
Wakati mwingine ndugu jiulize maswali na kujijibu mwenyewe kwa usahihi.
Je huyo ambaye moyo wako umeambatana na moyo wako je hakuna hila za shetani?
Je huyo unayempenda sana na hauwezi kupitisha siku bila kumjulia hali hakuna hila za shetani?
Kwanini nasema haya?
Ni kwa sababu kuna hadi watumishi wa shetani ambao mioyo yao imeambatanisha kipepo na maelfu ya watu kiasi kwamba watu wanawafuata hata bila kujua wanawafuata kwa ajili ya nini.
Kuna mpaka wachungaji wa kishetani na wanafundisha uongo hata waumini wao wanajua, lakini hao waumini huwezi kuwaeleza kuhusu watumishi wao hao, Kumbe mioyo ya waumini hao imeambatanishwa kishetani na watumishi hao, ndugu unahitaji kuwa makini sana na leo omba maombi ukiutenga moyo wako na kila connection ya giza iliyokuambatanisha moyo wako na watu wabaya.
Kuna wanamziki wanaimb nyimbo za shetani kabisa na hata ndani ya nyimbo wanaweza kusema kabisa kwamba wao ni waabudu shetani, lakini wamekamata mioyo ya maelfu ya watu.
Ndugu unahitaji sana sana kuomba maombi ya kuutenga moyo wako na kila connection ya kishetani iliyouambatanisha moyo wako na wanaotumika kishetani.
Hao ni watu wanaokuja maishani wako hivyo unahitaji kuwa mtu wa maombi sana katika jina la YESU KRISTO ili kuvunja connection hiyo ya giza.
Uwe makini sana na watu wanaokuja maishani mwako maana wengine ni mawakala wa shetani ili kukuondoa kwa YESU KRISTO Mwokozi.

UFANYE NINI JUU YA WATU WANAOKUJA MAISHANI MWAKO?

a. Waliokuja maishani mwako na wanatumika kipepo fanya yafuatayo kimaombi.

1. Vunja connection kati yako aliyeambatana moyo kipepo na wewe.

2. Futa connection ya kipepo waliyoambatanishwa kipepo mioyo wapedwa wako

 3. Haribu vifungo vya kipepo vilivyosababishwa na moyo wako kuambatana kipepo na mtu anayetumika kipepo.

b. Waliokuja maishani mwako walio wema.

 1. Omba MUNGU akukutanishe na waliobeba kusudi  la MUNGU kwa ajili yako.

2.Omba MUNGU akupe kuwajua waliobeba  kusudi la MUNGU kwa ajili yako.

3. Omba MUNGU kwamba waliobeba kusudi lake kwa ajili yako wakae kwenye nafasi zao.

4. Omba MUNGU kwamba Kanisa litembee  kwenye kusudi la MUNGU.

5. Mshukuru MUNGU kwa kukushindia.

Maombi hapa chini naomba yamsaidie muombaji Mchanga ili ajue kuomba akiliendea hitaji lake halisi katika maisha yake. Kwa waombaji wazoefu naamini ulikuwa unaandika kila point ya kuiombea kwenye maisha yako tangu mwanzo wa somo.

 MAOMBI JUU YA WATU WALIOKUJA MAISHANI MWAKO.

 JEHOVAH MUNGU wa upendo utukuzwe.
Ninakushukuru muumba wangu kwa neema hii ya ajabu ya kusimama kuomba mbele zako.
Nakushukuru kwa Neno lako la leo na najua ulikuwa unayamulika maisha yangu ili nijitambue.
Ni mara nyingi MUNGU umesema na mimi kwa ndoto, maono na mazingira ili nijue ni wapi nilifungwa kipepo, Baba MUNGU naomba sasa kwa Neema yako leo unipe kutoka katika vifungo hivyo.
Katika jina la YESU KRISTO Mwokozi aliye hai sasa ninavunja kila connection ya kipepo kati ya moyo wangu na moyo wa mtu mwingine yeyote.
 Kila connection iliyotengenezwa kishetani ili moyo wangu uambatane na wakala wa shetani, ninaivunja na kuifuta connection hiyo ya giza kwa damu ya YESU KRISTO na kwa jina la YESU KRISTO.
Kila mtu ambaye aliniendea kuzimu, kwa waganga au wachawi ili moyo wangu uambatane na moyo wake, Leo kwa damu ya YESU KRISTO na katika jina la YESU KRISTO naivunja na kuifuta hiyo connectin ya kishetani. 
 Kila mtu anayenihusu ambaye moyo wake umeambatana kishetani na moyo wa mtu mwingine, hilo ambatano nalifuta kwa damu ya YESU KRISTO na kwa jina la YESU KRISTO.
Mchumba wangu/Mke wangu/Mume wangu kama moyo wake umeambatana kishetani na mtu mwingine yeyote, hiyo connection naifuta kwa damu ya YESU KRISTO na kwa jina la YESU KRISTO.
Baba yangu au mama yangu au ndugu zangu kama wameambatanishwa mioyo kipepo na watu wabaya, hilo ambatano la kishetani naivunja na kulifuta kwa damu ya YESU KRISTO na kwa jina la YESU KRISTO.
Kila mtu anayenihusu ambaye moyo wake umeambana kipepo na mtu mwingine ninalifuta hilo ambatano la giza, nalifuta kwa damu ya YESU KRISTO na kwa jina la YESU KRISTO.
Kila kifungo cha kipepo ambacho kinanitesa kwa sababu ya watu wabaya waliokuja maishani mwangu, sasa nakiharibu kifungo hicho kwa damu ya YESU KRISTO na kwa jina la YESU KRISTO.
Kila kifungo cha dhambi na kifungo cha uovu nakifuta kwa damu ya YESU KRISTO na kwa jina la YESU KRISTO.
Kila laana na maagano ya kipepo niliyonayo yaliyosababishwa na watu wabaya ambao niliishi nao, nafuta laana hizo na maagano hayo kwa damu ya YESU KRISTO na kwa jina la YESU KRISTO.
MUNGU Baba sasa naomba unikutanisha na watu wako wema waliobeka kusudi lako kwa ajili yangu.
Nikutanishe na watu ambao ni baraka kwangu wanaoliishi kusudi lako BABA wa mbinguni.
Nipe BWANA kuwajua waliobeba kusudi lako kwa ajili yangu na wafanye kukaa katika nafasi zao kwa ajili yangu.
Naomba pia MUNGU wangu kwa ajili ya kanisa lako kukaa katika kusudi lako. Watu wa kanisani pia ni watu ambao wako katika maisha yangu hivyo ninaomba MUNGU Baba kwamba watu wa kanisa wakae kwenye nafasi yao ya kusudi lako  katika injili ya KRISTO YESU.
Nakushukuru MUNGU Baba maana leo umenishindia.
Naamini sasa mimi ni mshindi katika jina la YESU KRISTO.
Asante BABA wa mbinguni maana sasa napokea ushindi.
Katika jina la YESU KRISTO naomba na kushukuru.
Amen Amen.

MUNGU akubariki kwa kujifunza somo hili muhimu pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane nitakujulisha jinsi ya kukipata.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa BWANA YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
0714252292.
0786719090
mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu.

Comments