MAOMBI YA KUVUNJA NIRA ZA KICHAWI ZILIZOKUFUNGA.

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.

 Bwana YESU atukuzwe ndugu yangu.
Ni siku nyingine ambayo MUNGU ametupa tuiishi na kumtukuza.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU na kisha tuombe maombi ya ushindi.
Kuna watu wengi wanaenda kufunguliwa na Neno hili na sasa nira za kipepo/kichawi zitavunjika na wao kuwa huru.
Ziko nira nyingi za shetani tutaziona na mojawapo ni nguvu za giza yaani mapepo au majini.
Mapepo ni nira za shetani hivyo hakikisha huishi na mapepo ndani yako.
Kuna watu wana mapepo ya kiburi, ndio maana wanapishana na kusidi la MUNGU kila leo.
Kuna watu wana mapepo ya hasira ndio maana hutenda ubaya na majina yao hayamo katika kitabu cha uzima kwa sababu hawajawasamehe watu waliowakosea.
Kuna watu wana mapepo ya kukataliwa, ndio maana unaweza ukakuta ameachana na wachumba hata zaidi ya watano tena anaachana nao kipindi akikaribia tu kufunga ndoa.
Kuna watu wana mapepo ya utisho wa kipepo, ndio maana kila mtu anawaogopa hata bila kujua anawaogopea nini. Mtu wa aina hiyo kama ni mwanamke basi  wanaume waoaji humuona kama mwanaume mwenzao tu na sio mwanamke kama ilivyo jinsia yake. Mtu kama huyo kama ni mwanamume basi mabinti anaowachumbia humuona kama mwanamke mwenzao tu hivyo humukataa na hata kumsema vibaya.
Kuna watu wana mapepo ya balaa,ajali  na majanga, kila baya likitokea na yeye yumo.
Ndugu hakikisha leo unavunja nira za kipepo zote na hakikisha uko huru kwa jina la YESU KRISTO.
Tafuta maombezi na jinunge na kanisa la kiroho waombaji itakusaidia.
Katika jamii kwa ujumla nira ni kipande cha mti kilicho na kamba anachofungwa nacho ng'ombe au farasi anapolima au anapokokota tela  ili aweze kuongoza vizuri.
Bila nira ng'ombe hawezi kufanya kazi hiyo kwa ufanisi.
Kiroho nira ni kitu anachofungwa nacho mtu ili aendelee kumtumikia huyo aliyemfunga nira.

Isaya 14:24-25 '' BWANA wa majeshi ameapa, akisema, Hakika yangu kama vile vilivyoazimia, ndivyo itakavyokuwa; na kama nilivyokusudia, ndivyo itakavyotokea; kwamba nitamvunja huyo Mwashuri vipande vipande katika nchi yangu, na juu ya mlima wangu nitamkanyaga chini ya miguu yangu; ndipo NIRA YAKE ILIYO JUU YAO ITAKAPOONDOKA, na mzigo wake utatoka mabegani mwao '

Mwashuri lilikuwa taifa lililokuwa kinyume na wateule wa MUNGU Israeli. Ashuru kama taifa aliwatesa Israeli na kiroho Israeli alikuwa amefungwa nira ya kuteswa na Ashuru na Ashuru alikuwa amemwekea Mzigo Israeli yaani alikuwa mtumwa wake.
Kupitia unabii MUNGU anatangaza kwamba wakati umefika wa Nira ya Ashuru kuondoka na mzigo wa mateso ambao Mwashuri alikuwa amembembesha Israeli unaondoka katika shingo ya Isareli.
Hata leo wako watu wamefungwa nira na shetani ili waendelee kuteseka, dawa sio kulia bali kuomba kwa mamlaka ya jina la YESU KRISTO ili nira zote za kipepo zikuachie.
Shetani kuna watu amewafunga nira yake, kuna watu amewafunga nira za aina nyingi tu ambapo kuna matatizo huwapata lakini wao hawajui kama tatizo ni nira ya kipepo waliyofungwa nayo.
 Watu wengi walioenda kwa waganga wa kienyeji waliambulia kufungwa nira moja na majini na ni wengi sana wanaoteswa na majini/mapepo ni baada tu ya kwenda kwa waganga wa kienyeji.
Kuna matukio ya kiukoo unaweza kushiriki kumbe ndani yake kuna nira ya kipepo inayokufunga kipepo.
Wachawi wanaweza wakakufunga nira ya kuteseka.
Kuna watu magonjwa kwao ni jambo la kudumu, akipona malaria anaugua typhod, akipona hiyo anaugua UTI, akipona hiyo kifua mara uvimbe, mara kisukari, mara BP, Mara miguu inawaka moto n.k. Mtu kama huyo ni nira ya magonjwa kafungwa nayo kichawi hivyo ni muhimu kuvunja nira za kipepo zote  kwa maombi katika jina la YESU KRISTO.
Kuna watu wamefungwa nira za kuonewa tu kipepo.
Kuna watu wamefungwa nira za kunyanyasika tu.
Ndugu ukivunja nira ya kipepo utakuwa huru.
Kuna watu kuolewa au kuoa imekuwa tatizo kwa sababu ya mahusiano ya zamani yaliyotengeneza nira za kipepo.
Kuna watu huapiana na kuingia maagano kabisa kwamba hawataachana lakini baadae kwa sababu ya dhambi hujikuta wameachana lakini nira ya kipepo hiyo ni lazima ivunjwe.
Nahumu 1:13 '' Na sasa nitakuvunjia nira yake, nami nitakupasulia mafungo yako. '

MUNGU anasema anaivunja nira hiyo ya kipepo lakini ni hadi wewe uombe maombi.
Nira ya kipepo lazima ivunjike kwa jina la YESU KRISTO.
Vifungo vya kipepo lazima vipasuke na kufutika kwa jina la YESU KRISTO.
Dhambi inaweza ikatengeneza nira za kipepo maana shetani amefunguliwa mlango.
Mwanaume msaliti wa ndoa yake anaweza akajikuta amesahau hata familia yake na mshahara wote ukitoka anapeleka kwa hawara yake huku watoto wake wamefukuzwa shule kwa sababu ya ada na huku familia yake hawana chakula. Nini kilifanyika yule hawara alienda kwa mganga na kufungwa nira ya kichawi na mume huyo wa mtu mwingine hivyo ufahamu wa mwanaume yule umeisahau familia yake na sasa wanateseka huku hawajui tatizo ni nini. Mama ambaye uko katika ndoa na mume wako amefungwa nira ya kipepo na mwanamke mwingine hakikisha unaomba maombi ya kuivunja nira hiyo na achilia mapigo ya MUNGU juu ya mwanamke huyo ili asirudie tena kuingilia ndoa yako.
Katika maombi wakati mwingine MUNGU anataka tuvunje nira za giza kwa watu wa MUNGU ili wawe huru.
Isaya 58:6 ''Je! Saumu niliyoichagua, siyo ya namna hii? Kufungua vifungo vya uovu, kuzilegeza kamba za nira, kuwaacha huru walioonewa, na kwamba mvunje kila nira? ''

 Ndugu unateswa na nira gani?
Wapo watu walijiunga na dini za kishetani, wako watu waliingia mikataba ya kishetani. Kuna wakati wanatamani wamrudie Bwana YESU lakini shetani anawatisha kwamba atawaua. Watu hao kwa sababu ya nira hiyo ya kipepo wameendelea kumtumikia shetani kwa lazima. Ndugu kama ni wewe nakuomba kimbilia maombezi na Bwana YESU atakufungua na nira hiyo ya mikataba ya kishetani itaondoka katika maisha yako.
Kuna familia au koo zimefungwa nira ya umasikini, kiasi kwamba katika ukoo mzima kila anayejaribu kwa juhudi nyingi kufanikiwa kiuchumi anakwama au anafilisika. Ni kama kuna kitu kimemshikilia na hakijui kitu hicho, ndugu kama ni wewe vunja nira ya umasikini ya ukoo iliyokukamata  wewe.
Kuna watu ni walevi ukoo mzima, kuna watu ni wachawi ukoo mzima, kuna watu ni wazinzi ukoo mzima. Katika koo hizo ni wachache tu wanaosalimika na ni baada ya kumkimbilia Bwana YESU ili awaponye. Ndugu hakikisha leo unajitenga mbali na kila nira ya kipepo uliyofungwa nayo.
Unaweza ukashangaa mshahara wako ukitoka tu unapitiliza kwenye matatizo ambayo huja wakati tu umepokea mshahara. Ndugu vunja nira ya kipepo kwenye kipato chako au biashara yako.
Kama uko mbali na Wokovu hakikisha unaokoka maana kuna nira zitaondoka kwako kwa sababu tu umeingia katika ufalme wa MUNGU kwa kumpokea Bwana YESU kama Mwokozi wako na kisha unaishi maisha matakatifu katika yeye Mwokozi.
Isaya 10:27 ''Tena itakuwa katika siku hiyo mzigo wake utaondoka begani mwako, na nira yake shingoni mwako, nayo nira itaharibiwa, kwa sababu ya kutiwa mafuta.''

 Kuna watu hawafungi ndoa kwa sababu tu bado wamekamatwa na nira kichawi.
Nira njema ni moja tu na hiyo Biblia inatuagiza tufungwe nira hiyo tu na nira hiyo ni laini na wala haimtesi mtu bali inamsaidia Mwanadamu.
Bwana YESU anaizungumzia Nira hiyo akisema  '' Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha. Jitieni nira yangu, mjifunze kwangu; kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo; nanyi mtapata raha nafsini mwenu; kwa maana nira yangu ni laini, na mzigo wangu ni mwepesi.-Mathayo 11:28-30 ''

 Nira hii ni kumpokea YESU kama Mwokozi na mzigo wa nira hiyo ni utakatifu, Biblia inasema nira hiyo ni laini kabisa kiasi kwamba kila mwanadamu anaweza. Mzigo wa nira hiyo ni mwepesi kabisa kiasi kwamba kila mtu duniani anaweza akiamua.
Ulifungwa sana nira na wachawi sasa nakuomba mkimbilie Bwana YESU ili nira zako ziondoke maana nira ya Bwana YESU itafuta nira za kipepo zote kwa maombi.
MUNGU ameweka nira ya ndoa ili waiofungwa nira hiyo wawe mwili mmoja na wamtumikie MUNGU Baba katika maisha yao yote.
Mwanzo 2:24 ''Kwa hiyo mwanamume atamwacha baba yake na mama yake naye ataambatana na mkewe, nao watakuwa mwili mmoja.''
Lakini kuna baadhi ya watu badala ya kuwa katika nira ya ndoa takatifu wao wamefungwa nira ya ndoa na majini kiasi kwamba hata kupata Mchumba sahihi imeshindikana maana jini anawafukuza wachumba, na kama yuko katika ndoa anaweza kujikuta uzao hakuna na ndoa ina vita kila siku.
Kuna mtu kila siku huja jini na wanaingiliana ndotoni, hiyo nira ya kichawi hakikisha unaivunja.
Kuna watu wamefungwa nira moja na waume za watu, hiyo ni nira ya kishetani na hakikisha ndugu unaivunja nira hiyo.
Kuna watu wamefungwa nira za dhambi, nira hiyo ivunje ndugu kwa maombi na kuliruhusu Neno la MUNGU likutengeneze.
mimi sijui wewe umefungwa na nira gani ya kipepo lakini leo vunja nira zote za kipepo, kwa jina la YESU KRISTO.
Kuna watu bila kunywa pombe hawezi kuishi vyema, hiyo ni nira ya kishetani inayotakiwa kuvunjwa mara moja.
 Inawezekana kabisa wewe hujafungwa nira yeyote ya kipepo lakini unateseka kwa sababu wako wanaokuhusu wao wamefungwa nira za kipepo.
Kama baba hajafungwa nira ya kipepo lakini mama amefungwa nira hiyo basi mateso yanaweza kumpata baba hata kama yeye hajafungwa nira hiyo.
Ni muhimu sana kuwaombea watu wengine wanaokuhusu ili nira za giza ziwaache.
Kuna watu waliacha kazi ya MUNGU kwa sababu tu ya nira za dhambi.
Kuna watu waliacha kumcha MUNGU baada tu ya kufungwa nira moja na wasiomwamini YESU KRISTO kama Mwokozi.
Inawezekana kabisa wewe umefungwa nira na wasioamini katika Wokovu wa Bwana YESU ndio maana sasa unavaa kikahaba  hata kama unaenda kanisani.
Inawezekana unakaa katika familia ya watu waongo waongo na sasa na wewe umeanza kuwa muongo muongo na umesahau kwamba uongo ni dhambi.
Ndugu hakikisha unaivunja nira na wasio amini katika wokovu wa Bwana YESU maana ukifungwa nira moja na wao utajikuta unatumia muda wako mwingi katika mambo mabaya.
Sio kwamba uwatenge kabisa watu hao wasio amini bali usikubali kushirikiana nao katika mambo ambayo hayaendani na Wokovu wa Bwana YESU.
Nilichojifunza mimi Peter katika maisha yangu ya Wokovu ni kwamba kadri unavyong'ang'ania kwa YESU ndivyo wanaomtumikia shetani wanakukimbia.
Mimi nilipookoka mwaka 2008 nilikuwa na marafiki wengi sana na karibia wote walikuwa sio wakristo. Nilipookoka walinicheka. Baadae walisema wananipa mwezi mmoja nitakuwa nimemwacha YESU, mwezi ukapita mimi naendelea na YESU. Mwezi ulipoishi walitoa tena miezi mitatu nitakuwa nimerejea kwenye dhambi, Miezi hiyo mitatu ikaishi mimi ndio naongezeka kiroho kabisaaa. Baadae walikubali hakika kwamba mimi sio kama wao tena na kwa njia hiyo nilijikuta sina marafiki tena maana nikitokea tu wanasema Mchungaji kafika hivyo hawaongei tena mambo mabaya mbele yangu. Baadae nilipata marafiki wapya kanisani na hadi sasa miaka 9 naendelea mbele na Mwokozi wangu YESU KRISTO.
Ndugu usifungwe nira moja na wasioamini katika Wokovu.
2 Kor 6:14 '' Msifungiwe nira pamoja na wasioamini, kwa jinsi isivyo sawasawa; kwa maana pana urafiki gani kati ya haki na uasi? Tena pana shirika gani kati ya nuru na giza? ''

 Kufungwa nira moja na wasioamini katika Wokovu wa YESU KRISTO ni pamoja na kushirikiana nao katika maovu.
Inatupasa sana kujitenga nao katika maovu yao.
Kama unavuta sigara na wewe unasema umeokoka, je utawezaje kuwaambia wavuta sigara wenzako kwamba na wao waokoke wakati hawaoni mabadiliko kwako kama kweli umeokoka?
Kama tulikuwa tunalewa nao zamani sasa baada ya kuokoka sisi hatunywi pombe tena.
Lakini pia lazima utambue kwamba kutoka kundi la wasioamini kuna wachawi, waganga, na washirikina wengi tu. Ukikaa vibaya wanaweza kukufunga nira za kipepo ili usimtaje YESU wako mbele yao.
Nguvu zao za  ni nira za shetani hivyo hakikisha huishi kwa kuteswa na nguvu za giza  ndani yako.

MUNGU akubariki kwa kujifunza somo hili muhimu na  kama ukipenda kunisapoti katika huduma yangu kwa sadaka ya hiari ya kiwango chochote utakachopenda karibu na MUNGU akubariki sana, pia kitabu cha MAOMBI YA KINA kipo na wasiliana nami utakipata na ukifanyia kazi itakusaidia sana.
Hapa chini ni maombi ya Kuvunja nira za kichawi zilizokufunga zote.
Maombi haya naomba yamsaidie mtu yule ambaye hajui kuomba ili katika kuomba kwa kutumia hayo basi atakumbuka mahitaji yake na kuyataja katika maombi yake.
Kwa waombaji wazoefu naamini baada tu ya kulisoma somo na kulielewa basi anajua aombee nini.


 MAOMBI YA KUVUNJA NIRA ZA KICHAWI ZILIZOKUFUNGA.

 Ee MUNGU Baba umenichunguza kupitia Neno lako na kunijua vyema, unajua njia zangu zote na unajua kuketi kwangu na kuondoka kwangu.
Niko mbele zako Muumba wangu katika jina la YESU KRISTO nikiomba unisamehe na kunitakasa dhambi zangu zote. Nipe kuishi maisha matakatifu katika wewe muumba wangu.
Niko Mbele zako BWANA nikiomba uponyaji wa roho yangu, nafsi yangu na mwili wangu.
Chochote kile cha kishetani kilichonifunga na kunikamata kichawi na kunitesa, leo kwa mamlaka ya jina la YESU KRISTO ninavunja nira hiyo ya giza.
Kila nira ya giza iliyounganishwa na jina langu kichawi, naivunja nira hiyo kwa damu ya YESU KRISTO na kwa jina la YESU KRISTO.
Kila nira ya kichawi iniliyonifunga katika kipato changu, kazi yangu au biashara yangu, naivunja nira hiyo kwa damu ya YESU KRISTO na kwa jina la YESU KRISTO.
Kila nira ya mganga wa kienyeji niliyoenda mimi mwenyewe au walienda watu wengine kwa ajili yangu ili ninase, naivunja nira hiyo kwa damu ya YESU KRISTO na kwa jina la YESU KRISTO.
Nira za magonjwa zote ziniachie leo kwa jina la YESU KRISTO.
naivunja nira hizo kwa damu ya YESU KRISTO na kwa jina la YESU KRISTO.
 Watoto wangu waliofungwa na nira ya shetani, naivunja nira hiyo kwa damu ya YESU KRISTO na kwa jina la YESU KRISTO.
Wazazi wangu waliofungwa na nira ya shetani,naivunja nira hiyo kwa damu ya YESU KRISTO na kwa jina la YESU KRISTO.
Ndugu zangu waliofungwa na nira ya shetani,
naivunja nira hiyo kwa damu ya YESU KRISTO na kwa jina la YESU KRISTO.
Mchumba wangu aliyefungwa na nira ya shetani, naivunja nira hiyo kwa damu ya YESU KRISTO na kwa jina la YESU KRISTO.
Mke/Mume wangu namfungua nira ya kichawi, naivunja nira hiyo kwa damu ya YESU KRISTO na kwa jina la YESU KRISTO.
Nira ya kishetani iliyokama uchumi wangu hata hauendelei,naivunja nira hiyo kwa damu ya YESU KRISTO na kwa jina la YESU KRISTO.
Mganga au mchawi anayenizuia kujenga nyumba, hiyo nira yake ivunjike leo kwa jina la YESU KRISTO,
naivunja nira hiyo kwa damu ya YESU KRISTO na kwa jina la YESU KRISTO.
 Kila nira ya kukosa kazi iliyonifunga, Leo naivunja hiyo nira kwa damu ya YESU KRISTO na kwa jina la YESU KRISTO.
Nira ya uzinzi na uasherati, naivunja nira hiyo kwa damu ya YESU KRISTO na kwa jina la YESU KRISTO.
Nira ya uongo wa wizi,naivunja nira hiyo kwa damu ya YESU KRISTO na kwa jina la YESU KRISTO.
Nira ya kiburi cha kipepo,naivunja nira hiyo kwa damu ya YESU KRISTO na kwa jina la YESU KRISTO.
Nira ya kumilikiwa kipepo,naivunja nira hiyo kwa damu ya YESU KRISTO na kwa jina la YESU KRISTO.
Kila mtu anayenihusu aliyekamatwa na nira za giza leo namfungua kwa damu ya YESU KRISTO na kwa jina la YESU KRISTO.
Waliofungwa nira na pombe, nazivunja nira hizo kwa damu ya YESU KRISTO na kwa jina la YESU KRISTO.
Waliofungwa nira na uzinzi na uasherati,nazivunja nira hizo kwa damu ya YESU KRISTO na kwa jina la YESU KRISTO.
Waliofungwa nira za kuwategemea wanadamu na sio MUNGU, nazivunja nira hizo kwa damu ya YESU KRISTO na kwa jina la YESU KRISTO.
Kuanzia leo hakuna nira ya kichawi itanikamata.
Waliolichukua jina langu na kulipeleka kwa waganga na wachawi ili nisipate kazi, ili nifukuwe kazi na ili nisifunge ndoa, Nira hizo zote nazifuta kwa damu ya YESU KRISTO na waliokusudia hayo yawapate wao kama walivyonuipangia mimi.
Niko huru sasa katika jina la YESU KRISTO kama Neno la MUNGU linavyosema katika Yohana 8:36 ''Basi Mwana akiwaweka huru, mtakuwa huru kweli kweli.''
Katika jina la YESU KRISTO nimeomba na kupokea ushindi.
Amen Amen Amen.


 Asante kama umelielewa Neno la MUNGU ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa BWANA YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
0714252292.

0786719090
mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu.

Comments