MAONO NILIYOYAONA.

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
Bwana YESU atukuzwe ndugu yangu.
Leo nimeona maono na nakushirikisha maono hayo maana ni ujumbe kwako na kwangu pia.

Nimeona kwenye maono mteule mmoja wa MUNGU ambaye ni kijana mdogo tu akimaliza safari yake ya duniani(Akifariki)
Kijana huyo simjui na wala sijawahi kumuona ila alikuwa anaishi kijijini sana ila alikuwa ameokoka na mwaminifu kwa MUNGU.
Baada ya kuondoka Duniani akipelekwa mbinguni na Malaika wa MUNGU nikaona wakati anaingia mbinguni kwa furaha akitaka kuwaambia wateule wa KRISTO wote duniani ujumbe fulani lakini alijaribu na sauti yake haikufika duniani. Malaika wa MUNGU akaniambia mimi kwamba mteule huyo alikuwa anamwambia kila mteule wa MUNGU aliyeokolewa na Bwana YESU kwamba '' Hakikisha unakuwa Mwaminifu, Mtakatifu na Mkamilifu''
Malaika akaniambia niandike ujumbe huo kwenye Daftari yangu ya masomo ili niwaambie wote ambao MUNGU atanipa kuwafikia, nikaandika.


Asubuhi hii Neno hilo nimelitafakari sana na Kabla sijaenda Kanisani nikaona nikujulishe ndugu wewe uliyeokoka na uanataka uzima wa milele.
Neno ni hilo tu kwamba ''HAKIKISHA UNAKUWA MWAMINIFU, MTAKATIFU NA MKAMILIFU''
Narudia tena labda hukuelewa vyema au ulisoma ukiwa na mawazo au ulikuwa kwenye kelele, Ni kwamba ''Hakikisha unakuwa MWAMINIFU, MTAKATIFU na MKAMILIFU''


Baada ya hapo nimeangalia Biblia angalau maandiko matatu matatu kila kipengele ili uone Mwanga juu ya kuwa Mwaminifu, Mtakatifu na Mkamilifu.

Maandiko haya matatu yakusaidie ndugu yangu na hata mimi yanisaidie.

Maandiko kuhusu uaminifu.

1. =Ufunuo 17:14 ''Hawa watafanya vita na Mwana-Kondoo, na Mwana Kondoo atawashinda, kwa maana Yeye ni Bwana wa Mabwana, na Mfalme wa Wafalme, na hao walio pamoja naye ndio walioitwa, na wateule, na waaminifu.''

2.= 2 Timotheo 2:2 '' Na mambo yale uliyoyasikia kwangu mbele ya mashahidi wengi, hayo uwakabidhi watu waaminifu watakaofaa kuwafundisha na wengine.''

2. =Ufunuo 2:10 ''Usiogope mambo yatakayokupata; tazama, huyo Ibilisi atawatupa baadhi yenu gerezani ili mjaribiwe, nanyi mtakuwa na dhiki siku kumi. Uwe mwaminifu hata kufa, nami nitakupa taji ya uzima. 

Maandiko kuhusu utakatifu.

1. =1 Petro 1:15 '' bali kama yeye aliyewaita alivyo mtakatifu, ninyi nanyi iweni watakatifu katika mwenendo wenu wote;
16 kwa maana imeandikwa, Mtakuwa watakatifu kwa kuwa mimi ni mtakatifu.''


2. =1 Thesalonike 4:3-5 ''Maana haya ndiyo mapenzi ya MUNGU, kutakaswa kwenu, mwepukane na uasherati; kila mmoja wenu ajue kuuweza mwili wake katika utakatifu na heshima; si katika hali ya tamaa mbaya, kama Mataifa wasiomjua MUNGU.''

3. =Mathayo 5:8 ''Heri Wenye Moyo Safi; Maana Hao Watamwona MUNGU". 

Maandiko kuhusu ukamilifu.

1. =Mithali 113 '' Ukamilifu wao wenye haki utawaongoza Bali ukaidi wao wenye fitina utawaangamiza.''

2 . =Zaburi 37:18 ''BWANA anazijua siku za wakamilifu, Na urithi wao utakuwa wa milele. ''

3. =Waebrania 9:27-28 '' Na kama vile watu wanavyowekewa kufa mara moja, na baada ya kufa hukumu; kadhalika KRISTO naye, akiisha kutolewa sadaka mara moja azichukue dhambi za watu wengi; atatokea mara ya pili, pasipo dhambi, kwa hao wamtazamiao kwa wokovu. ''

Ndugu yangu hayo ni baadhi tu ya maandiko maana yapo maandiko mengi sana sana yanayokutaka kuwa mwaminifu, mtakatifu na mkamilifu.
Ujumbe nimeufikisha sehemu husika na nakuomba share kwa marafiki zako au wasambazie ndugu zako uwapendao.
MUNGU akubariki sana na hakikisha unakuwa Mwaminifu, Mtakatifu na Mkamilifu.

 

Comments