USIMUOGOPE MFALME WA ASHURU.

 
Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.


Bwana YESU atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.
MUNGU akupe Neema juu ya ujumbe huu, ukaone Neema ya kutokea
Ukaone nguvu ya MUNGU ikiambatana na wewe kupitia Neno lake.
Kumbuka Biblia inasema katika Zaburi 107:20 kwamba " Hulituma neno lake, huwaponya, Huwatoa katika maangamizo yao."

Kwa hiyo Neno la MUNGU ambalo MUNGU huwa analiachilia, analituma lije kwako wakati mwingine lina kazi nyingi.
Kazi mojawapo ya Neno hilo ni kuponya, kazi mojawapo ni kukuondoa kwenye maangamizo , kazi nyingine ni kukuimalisha, lina kazi nyingi Neno la MUNGU, ni zaidi ya kazi kumi Neno la MUNGU linaweza likafanya katika maisha yako.
Ujumbe wa Leo ni Neno limetumwa kwako ili kukuambia kwamba usimwogope Mfalme wa Ashuru.
Fungua nami katika Biblia kitabu cha 2 Nyakati 32:7-8 " Iweni hodari, na wa moyo mkuu, msiogope, wala msifadhaike kwa sababu ya mfalme wa Ashuru, wala kwa majeshi yote walio pamoja naye; kwa maana yupo mkuu pamoja nasi kuliko aliye pamoja naye; kwake upo mkono wa mwili; ila kwetu yupo BWANA, Mungu wetu, kutusaidia, na kutupigania mapigano yetu. Na watu wakayategemea maneno ya Hezekia, mfalme wa Yuda."


Ni wakati Mfalme Hezekia kama mteule wa MUNGU alikuwa katika wakati mgumu sana.
Mfalme wa Ashuru aitwaye Senakeribu alikuwa ameteka sehemu za ardhi ya Israeli. Mfalme huyo alianza kuwaletea vitisho Waisraeli ili wawe kinyume na mfalme wao na wakubali kuwa watumwa wa Mfalme wa Ashuru.
Hezekia ni mfano wa wateule wa MUNGU waliookolewa na Bwana YESU lakini walijikuta katika magumu Fulani kwa muda.
Lakini Neno la MUNGU likamjia kusema kwamba Msiogope kwa ajili ya mfalme wa Ashuru, maana yeye huyo ana mkono wa mwili lakini sisi tunaye mkuu kuliko yeye waliyenaye maadui zetu, hivyo tukiamua kumtegemea MUNGU yeye atatushindia.
Nini kilitokea baadae?
Ni kwamba Hezekia na Nabii Isaya walimuomba MUNGU na MUNGU akatuma Malaika ambapo Malaika wa MUNGU aliwaua wababe wa vita wote wa Ashuru.
Mfalme wa Ashuru kuona Makomandoo wake wote wamechinjwa na Malaika wa MUNGU alikimbia huyo Mfalme kurudi Ashuru, alipofika watu wake mwenyewe walimgeuka na kumuua.
Nini nataka tujifunze?
Watu hao Waisraeli walikuwa wamekata tamaa kama ambavyo wewe umekata tamaa katika vitu Fulani kwenye maisha yako. Inawezekana umechoka, inawezekana kuna watu wanakutisha, inawezekana kuna nguvu za Giza umepambana nazo sana bila mfanikio hadi umeanza kuhesabu gharama, ndugu nakuomba usihesabu gharama.
Inawezekana unahesabu dharama kwamba "Nimefunga Mara nyingi sana, nimehudhuria maombezi Mara nyingi mno bila kupona, nimefanya vitu vingi sana kwa YESU, nimetoa sadaka na zaka nyingi mno. Ndugu nakuomba usihesabu gharama.
Inawezekana umechoka na huoni pa kutokea hadi umekuwa mtu wa kutukana tu watumishi na kuwasema vibaya. Ndugu, hayo hayatakusaidia Bali mtegemee MUNGU yeye atakushindia.
Usiogope kwa sababu ya Mfalme wa Ashuru.
Inawezekana yuko mfalme wa Ashuru katika maisha yako.
Mfalme wa Ashuru ni adui yako anayetumika kipepo.
Inawezekana kuna Mfalme wa Ashuru kazini kwako, anatumika kishetani ili kuhakikisha unashushwa cheo, unaonewa, unadharaulika na kufukuzwa kazi.
Inawezekana kuna Mfalme wa Ashuru amekupandikizia vitu mbele ya watu ili wakuchukie, wakuone haufai na hustahili.
Inawezekana kuna jirani yako ni kama Mfalme wa Ashuru maana anajaribu kueneza uongo mwingi, anasema mambo mengi ya uzushi.
Wako mabinti wengine wanakataliwa na wachumba ni kwa sababu tu kuna mtu anatumika kipepo, anajaribu kusema maneno mabaya kwa kuwasingizia kwamba hawafai, hawastahili. Ni mambo ya uongo ili kuwaharibia mabinti hao, ni roho ya shetani iliyo ndani ya watu hao wabaya inayowapelekesha kutamka vile. Ndugu wa aina hii anaweza akafanya kila mbinu ili apate mchumba na kuolewa lakini imeshindikana kwa sababu mfalme wa Ashuru amesima kumsema vibaya.
Ndugu mtegemee MUNGU aliyeziumba mbingu na dunia na usimuogope Mfalme wa Ashuru maana YESU yeye anaweza kukushindia.
Aliye upande wako ni mkuu sana. Kama ukiamua kutembea kwenye kusudi la MUNGU yeye atatenda tu, katika jina la YESU KRISTO aliye hai.
Ndugu naomba nikuambie kwamba yako mambo mengi katika maisha ni mfano wa Mfalme wa Ashuru katika maisha ya mtu.
Inawezekana kuna mtu anajaribu kukutisha kwa njia nyingi, anajaribu kukuonea kwa njia nyingi. Ok inawezekana adui huyo ana pesa,ana madaraka na inawezekana anafahamiana na wakubwa wengi. Hivyo sio vigezo vya wewe umnyenyekee.
Kwa sababu umekataa kumnyenyekea amesema kwamba atakukomesha hadi utakapokubali kumnyenyekea yeye.
Ndugu naomba nikuambie ya kwamba mtegemee yeye aliyeziumba mbingu na dunia, mtegemee yeye MUNGU maana anaweza mambo yote. Mtegemee yeye ambaye ni Alfa na Omega.
Isaya 35:4 Biblia inasema " Waambieni walio na moyo wa hofu, Jipeni moyo, msiogope; tazama, MUNGU wenu atakuja na kisasi, na malipo ya MUNGU; atakuja na kuwaokoa ninyi."


Naomba nikuambie neno moja kuhusu maombi kwa kutumia Neno.
Tunajua, Neno la MUNGU ni upanga, Neno la MUNGU ni moto, Neno la MUNGU ni nyundo n.k.
Neno la MUNGU ni silaha Kali sana kimaombi.
Unapoomba ni muhimu ujue unalitumia Neno kama nini.
Kuna adui mwingine ukiwa unapambana naye kimaombi unatakiwa ulitumie Neno kama upanga.
Kuna adui mwingine kupambana naye unatakiwa ulitumie Neno kama moto, kuna adui mwingine unatakiwa ulitumie Neno kama nyundo. Tambua sasa ya kwamba kuna adui mwingine ili ushinde unahitaji nyundo na sio upanga.
Kuna adui mwingine ili umshinde unahitaji moto na sio nyundo.
Kuna adui mwingine ili umshinde unahitaji upanga na sio moto.
Ziko aina kama nne za sifa za Neno la MUNGU lakini katika maombi yako nakuomba omba kiufunuo, omba kinabii.
Kuomba kinabii sio kuwa nabii.
Kuomba kinabii ni kujitamkia mambo yajayo kwamba yatakuwa yako, hujayafikia bado lakini kwa imani unajua utayamiliki.
Mfano wa kuomba kinabii ni kusema ya kwamba "Mimi najua hao maadui zangu watashindwa kwa jina la YESU, Mimi nitasonga mbele. Japokuwa wamechimba mashimo lakini nitapita katikati yao na kuendelea mbele katika jina la YESU KRISTO."
Hapo unaomba kinabii maana unatamka kitu ambacho hakijafika ila kitafika kwa jina la YESU KRISTO.
Ndugu nakuomba usimuogope Mfalme wa Ashuru, usiwaogope watu wabaya wanaopanga mambo mabaya kwa ajili yako.
Wapo watu wanatishwa na kuonewa, wako watu wanasingiziwa na kuwekewa vitu vingi vya ajabu, wako watu wanawekewa masharti mengi ili yawashinde wafukuzwe.
Ndugu kama wewe unaye YESU songa mbele, Wewe kama unamwabudu JEHOVAH aliyeziumba mbingu na dunia nakuambia songa mbele, shetani na kazi zake zote zitanyamaza tu. Mipango ya kipepo yote itanyamaza tu.
Haijalishi kuna adui wa wapi, anafanya nini na ana nguvu gani, wewe tembea kwenye kusudi la MUNGU, wewe tembea katika kile ambacho MUNGU Baba anasema, wewe tembea katika Neno la MUNGU.
Maadui zako wanaweza wakapanga mambo mengi sana lakini MUNGU anaweza kuyabatilisha muda wowote kupitia maombi yako.
Ndio maana unatakiwa kuwa mtu wa maombi sana sana sana.
Ukisoma Ayubu 5:12 Biblia inasema
"Yeye huyatangua mashauri ya wadanganyifu, Mikono yao isipate kuyatimiza makusudi yao."


Yeye MUNGU hutangua mipango ya watu wabaya.
Wanakusudia mambo mabaya, inawezekana wamekucholea ramani ya kishetani ili utembee katika hiyo ramani.
Wamekucholea ratiba yao ili utembee katika hiyo ratiba. Inawezekana huu ni mwezi wa nane lakini mawakala wa shetani wameshakuchorea ramani ya mwakani, mwaka huu wanajua wamekuzuia katika mambo mengi na tayari wameshapanga utembee kwenye ramani yao ya vifungo na kutokufanikiwa.
Unapanga mipango yako mizuri kila mwaka lakini haifanikiwi kwa sababu yuko adui aliyekupangia ramani yake ili wewe uiishi hiyo ramani.
Oooh kuna watu husema kwamba "Vitu vyako usishirikishe watu, fanya siri maana ukitamka tu shetani anavinasa na kufanya kinyume chako"
Ndugu naomba ujue kwamba adui anafanya kinyume na mipango yako siku zote. Sasa ukitaka umuweze sio tu kwamba ajue au asijue Bali wewe songa mbele. Ikiwa MUNGU wa Israeli ndiye MUNGU wako basi songa mbele, omba kiufunuo.
Mwambie MUNGU nipe kujua kusudi, mwambie MUNGU nipe kutembea kwenye kusudi lako.
Tambua pia kwamba kuna mengine MUNGU huwa anakuonyesha na kukujulisha kwa maono au ndoto, wakati mwingine fanyia kazi kimaombi hicho unachokiona kwenye ulimwengu wa roho. Kama ni kazi za shetani ziharibu zote, kama elimu umejua nini ufanye na uishi vipi ili uliendee hitaji lako.
Ndugu nakuomba usimuogope Mfalme wa Ashuru.
Kama ni magonjwa ndio yamechukua nafasi ya mfalme wa Ashuru, wewe omba Leo na MUNGU Baba atakushindia.
Hakika najua MUNGU Baba atakushindia.

MUNGU akubariki kwa kujifunza somo hili muhimu pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane nitakujulisha jinsi ya kukipata.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa BWANA YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
0714252292.
mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu.

Comments