SABABU 5 ZILIZOMFANYA IBRAHIMU KUBARIKIWA SANA NA MUNGU.

Na Mwl Peter Mabula 
Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi 




Bwana YESU KRISTO Mwokozi atukuzwe.
Karibu Tujifunze Neno la MUNGU.

➡️Kwanini Ibrahimu alibarikiwa na MUNGU?

◼️Kuna sababu za Ibrahimu kubarikiwa na MUNGU.

◼️Biblia inatoa majibu matano yafuatayo.

Mwanzo 26:5 " Kwa sababu Ibrahimu alisikia sauti yangu, akayahifadhi maagizo yangu, na amri zangu, na hukumu zangu, na sheria zangu."

1. Aliisikia sauti ya MUNGU na kuitii.

◼️Sauti ya MUNGU ni kusudi la MUNGU.

◼️Maandiko mengi yanaonyesha kwamba Ibrahimu alikuwa Mtu wa kuisikia Sauti ya MUNGU aliposema naye na alipoisikia Sauti ya MUNGU aliitii.

Mfano ni huu

Mwanzo 17:1 "Abramu alipokuwa mtu wa miaka tisini na kenda, BWANA akamtokea Abramu, akamwambia, Mimi ni MUNGU Mwenyezi, uende mbele yangu, ukawe mkamilifu."

◼️Ibrahimu alipoisikia Sauti ya MUNGU iliyomtaka kwenda kwa ukamilifu alitii na kuzingatia.

◼️Ukiona umeanza kuisikia Sauti ya ROHO MTAKATIFU ukaitii ujue huo ndio Mwanzo wa Mafanikio Yako makubwa .

◼️ Ibrahimu alipoisikia Sauti ya MUNGU akaitii ndio ukawa Mwanzo wa kufanikiwa kwake, MUNGU anasema na sisi kupitia ROHO MTAKATIFU hivyo ukiitii Sauti ya ROHO MTAKATIFU umemtii MUNGU na huo ndio Mwanzo wako wa kupata Mafanikio makubwa sana katika Maeneo mengi.

2. Alitunza maagizo ya MUNGU.

◼️Kama Kuna Mtu alikuwa mwepesi kutunza maagizo ya MUNGU basi mmojawapo ni Ibrahimu.

➡️Ibrahimu aliloambiwa kuondoka kwa wazazi wake aliondoka bila maswali, aliloambiwa abadili Jina yeye na Mke wake alianza kujiita Ibrahimu pale pale, hata alipokuwa mzee wa miaka 99 akasikia Sauti ya MUNGU ikimtaka yeye na Wanaume wote wa familia yake watahiriwe Ibrahimu akakubali kutahiriwa akiwa mzee wa miaka 99, hakuna kitu Ibrahimu alipishana na MUNGU hivyo MUNGU akajiridhisha kwamba Ibrahimu ataweza hata kuwafundisha na Watoto wake kutunza maagizo ya MUNGU hivyo MUNGU akampa hao Watoto na kumbariki pia.

Mwanzo 18:19 "Kwa maana nimemjua ya kwamba atawaamuru wanawe, na nyumba yake baada yake waishike njia ya BWANA, wafanye haki na hukumu, ili kwamba BWANA naye akamtimizie Ibrahimu ahadi zake."

3. Alitunza Amri za MUNGU.

◼️Kuna mambo ya MUNGU ni Amri, Ibrahimu alitunza Amri za MUNGU zote.
Mfano wa Amri za MUNGU ni kutokuabudu miungu, Ibrahimu hakuwahi kuabudu miungu Bali alimwabudu MUNGU wa Mbinguni Pekee na kumjengea madhabahu zaidi ya mara Moja.

Mwanzo 12:7-8 " BWANA akamtokea Abramu, akasema, Uzao wako nitawapa nchi hii. Naye huko akamjengea madhabahu BWANA aliyemtokea. Kisha akaondoka huko akaenda mpaka mlima ulio upande wa mashariki wa Betheli, akaipiga hema yake; alikuwa na Betheli upande wa magharibi, na Ai upande wa mashariki, akamjengea BWANA madhabahu huko, akaliitia jina la BWANA.

◼️Ibrahimu hata alipopewa Amri ya kumtoa Sadaka Mtoto wake wa Pekee alifuata Amri ya MUNGU na jambo hilo likamuongezea baraka maradufu ingawa hata Mtoto hakufa.

Mwanzo 22:15-17 " Malaika wa BWANA akamwita Ibrahimu mara ya pili kutoka mbinguni akasema, Nimeapa kwa nafsi yangu asema BWANA, kwa kuwa umetenda neno hili, wala hukunizuilia mwanao, mwanao wa pekee, katika kubariki nitakubariki, na katika kuzidisha nitauzidisha uzao wako kama nyota za mbinguni, na kama mchanga ulioko pwani; na uzao wako utamiliki mlango wa adui zao;"

4. Alitunza hukumu za MUNGU.

◼️Hukumu za MUNGU ni uamuzi wa MUNGU.

Ibrahimu alifuata maamuzi ya MUNGU na alihakikisha walio chini yake wanafuata uamuzi wa MUNGU.

➡️Mfano hai ni pale MUNGU alimwambia Ibrahimu juu ya Hukumu anayoipeleka Sodoma na Gomora, Ibrahimu hakupinga Hukumu ya MUNGU ingawa alitamani sana ndugu yake aliyeko Sodoma apone mawazo yake yalikuwa sawa na mawazo ya MUNGU maana MUNGU alikuwa amekusudia kumponya Lutu ambaye ni mwenye haki.

Hata kesho yake Ibrahimu alirudi pale pale MUNGU aliposema naye ili aone Hukumu ya MUNGU ambayo hakuipinga.

Mwanzo 19:27-28 " Ibrahimu akatoka asubuhi kwenda mahali aliposimama mbele za BWANA, naye akatazama upande wa Sodoma na Gomora na nchi yote ya hilo Bonde, akaona, na tazama, moshi wa nchi ukapanda, kama moshi wa tanuru."

◼️Je ni uamuzi gani wa MUNGU umeuheshimu?

➡️Mfano MUNGU amekuambia ufute urafiki na fulani unayemhusudu sana, Je utafuata Uamuzi/Hukumu ya MUNGU ?

➡️Mfano una Mchumba lakini MUNGU anakuambia sio Mtu sahihi kwako, Je utamuacha kwa kufuata uamuzi wa MUNGU huku unampenda sana Mtu huyo?

◼️Kushika Hukumu za MUNGU ni muhimu sana kama unahitaji Mafanikio makubwa ya ki MUNGU.

5. Alitii sheria za MUNGU.

◼️Sheria  za MUNGU ni Neno la MUNGU.

◼️Je unalitii Neno la MUNGU?

➡️Unaweza ukajiuliza maswali kwamba kipindi hiki Cha Ibrahimu hakukuwa na Torati wala amri kumi za MUNGU lakini Ibrahimu alimcha MUNGU kwa usahihi, Neno la MUNGU wakati huo lilikuwa ni kile ambacho MUNGU anasema.

◼️Ibrahimu alitii Sheria za MUNGU ambazo ni Neno la MUNGU.

◼️Kila Neno la MUNGU Ibrahimu alilitii.

➡️Leo tunalo Neno la MUNGU ambalo ni Mafundisho ya Ufunuo wa ROHO MTAKATIFU tunayofundishwa na Watumishi waaminifu wa Bwana YESU KRISTO, Je tunashika Neno hilo la MUNGU?

➡️Leo ROHO MTAKATIFU anawapa ujumbe wa Neno la MUNGU Watumishi wa KRISTO Kila mara Je tunafuata  Neno hilo?

➡️Unaweza ukaishi Maisha ya kulaumi tu na kulalamika na kumbe tatizo lako hutaki kuwa na akili kama za Ibrahimu za kufuata haya Mambo matano ya MUNGU.

➡️Unaweza ukawa unalalamika tu na kumbe ungefuata Neno la MUNGU la Ufunuo wa ROHO MTAKATIFU ungeanza Mwanzo mpya wa Mafanikio ya ajabu kwako.

◼️Maagizo ya MUNGU ni muhimu sana kwa wateule wa MUNGU waliookolewa kwa damu ya YESU KRISTO.

◼️Ndugu, ujumbe huu ni Ufunuo, Mimi na Wewe tuufuata ili tuone Mafanikio makubwa.

Waefeso 5:1-3 " Hivyo mfuateni MUNGU, kama watoto wanaopendwa; mkaenende katika upendo, kama KRISTO naye alivyowapenda ninyi tena akajitoa kwa ajili yetu, sadaka na dhabihu kwa MUNGU, kuwa harufu ya manukato. Lakini uasherati usitajwe kwenu kamwe, wala uchafu wo wote wa kutamani, kama iwastahilivyo watakatifu;"

Asante kwa kujifunza Neno la  siku ya leo, Kabla sijamaliza nakuomba Wewe ambaye hujaokoka au uliokoka ukarudi nyuma, nakusihi sana amua Leo kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi wako na Jina lako litaandikwa katika kitabu Cha uzima Mbinguni, katika maeneo Yako tafuta Kanisa safi la kiroho linalohubiri Wokovu wa KRISTO YESU nenda kamweleze Mchungaji atakuongoza Sala ya Toba utaokoka Kisha baada ya hapo fuata mafundisho ya Neno la MUNGU hapo Kanisani.
MUNGU wa Mbinguni akubariki sana.
By Mwl Peter Mabula 
Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi.
+255714252292 ( kwa Ushauri, maombezi,  pamoja na Whatsapp)
Ubarikiwe.

Comments