MAMBO MATATU(3) YA KUOMBEA WAKATI UMECHOKA NA UKO KATIKA MAGUMU SANA.

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU
 Bwana YESU atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU muhimu sana.
Katika maisha yako ya Wokovu  wakati mwingine kuna kupitia magumu sana na wakati mwingine kuna kuchoka sana.
Kuchoka ninakokuzungumzia sio kule kuchoka kwa sababu umefanya kazi fulani bali nazungumzia kuchoka kwa kusubiri ushindi na kuchoka kwa sababu umekosa tumaini la ushindi kabisa, kuchoka kwa sababu una maumivu mabaya ya moyoni.
Sio watu wote hupitia kuchoka  sana na hupitia magumu lakini jifunze kitu hapa itakusaidia.
Wakati wa magumu na kuchoka ndio wakati pia shetani huutumia  kuwakamata watu wengi wanaokuwa katika magumu, kuna watu kwa sababu ya magumu walibaki wakitukana tu watumishi wa MUNGU na kupata laana na kulitukana kanisa la MUNGU kana kwamba hao wanahusika na tatizo lililowapata. Kuna watu humkufuru MUNGU kabisa na kuna watu hujilaani na kujinenea mabaya ambayo baadae yatawatesa sana(Mithali 6:2). Kuna watu wakati huu hutafuta msaada kwa waganga wa kienyeji na badala ya kupunguza tatizo wao huliongeza tatizo na vifungo vya kipepo juu.
Katika wakati mgumu unahitaji sana kujua ufunuo wa leo itakusaidia.
Katika dharuba na magumu ya aina yeyote hakikisha unaishi maisha matakatifu, hakikisha unamtumikia MUNGU na endelea kumwabudu katika Roho na kweli.
Inawezekana kabisa umetegemea kitu fulani hadi umechoka na hujakipata.
Inawezekana kabisa umeomba hadi umekata tamaa.
Inawezekana kabisa ufahamu wako umefika mwisho.
Mimi  Binafsi niliwahi kuumizwa sana na uchumba mwaka 2012 Mwanzoni. Niliumizwa ghafla na kujikuta nimemaliza siku 5 Bila kula na sijafunga, nimebaki nikisema tu ''MUNGU wangu nisamehe, MUNGU wangu nisaidie''. Wakati huo ulikuwa wakati mgumu sana. Kwa Neema ya MUNGU nilitoka katika magumu hayo na kupata ushindi wa ajabu sana.
Mama mmoja aliniambia amesubiri mtoto kwa miaka 10 katika ndoa yake, amekuwa ni mtu wa kudhihakiwa tu na amekuwa ni mtu wa kulia tu. Anasema mbele anaona giza, haoni pa kutokea.
Dada mmoja aliachwa na Mchumba wake wiki moja kabla wafunge ndoa na aliyemchukulia Mchumba wake ni rafiki yake, huo ni wakati mgumu sana.
Mama mmoja alifiwa na mume wake na akiwa katika magumu yaani kipindi cha msiba hata siku 3 hazijaisha ndugu wa mume walikaa kikao cha ukoo na kumwambia aende kwao yaani arudi kwa wazazi wake wakati amekaa katika ndoa zaidi ya miaka 20, wale ukoo walisema kwamba kwa mjibu wa kabila lao watoto watachukuliwa na ndugu wa mume wake. Na ndugu watagawana mali maana wao ndio watalea watoto wa ndugu yao aliyefariki. Yule mama akaacha nyumba nzuri na gari na mali nyingi walizozipata wakiwa na mumewe, huyu mama alikuwa katika maumivu aina mbili yenye uzito mkubwa sana.
Baba mmoja alipalalaizi kwa muda baada ya kumfuma mkewe akimsaliti kwa rafiki yake.
Mifano hii yote niliyokupa inawahusu watu waliookoka kama wewe na wanamcha MUNGU kama wewe, huo ni wakati mgumu sana.
Hata wewe inawezekana kabisa ulipitia wakati mgumu sana na wakati huo ulihitaji kujua ufunuo wa leo ili ikusaidie.
Kuna watu hata wanaweza wakaacha ibada au kuacha wokovu kwa sababu ya magumu ya muda mfupi tu, ni hatari sana maana wanaweza wakakosa uzima wa milele.
Ndugu yangu nisikilize itakusaidia. 
 Wakati umechoka kwa sababu ya maumivu ya moyoni mwako unahitaji MUNGU akutie nguvu, akusaidie na kukushika mkono.
Isaya 41:10 '' usiogope, kwa maana mimi ni pamoja nawe; usifadhaike, kwa maana mimi ni MUNGU wako; nitakutia nguvu, naam, nitakusaidia, naam, nitakushika kwa mkono wa kuume wa haki yangu.''

1. Omba MUNGU akutie nguvu.

Hili ndio kanuni ya kwanza ambayo utakiwa kuitumia ukiwa katika magumu sana na umekata tamaa.
Ahadi ya kwanza ya MUNGU kwako ni kwamba atakutia ndugu.
 Isaya 40:29-31 ''Huwapa nguvu wazimiao, humwongezea nguvu yeye asiyekuwa na uwezo. Hata vijana watazimia na kuchoka, na wanaume vijana wataanguka; bali wao wamngojeao BWANA watapata nguvu mpya; watapanda juu kwa mbawa kama tai; watapiga mbio, wala hawatachoka; watakwenda kwa miguu, wala hawatazimia.''

Kwa jinsi gani MUNGU atakutia nguvu?

A. MUNGU atalituma Neno lake ili kukusaidia.
Zaburi 107:20 '' Hulituma neno lake, huwaponya, Huwatoa katika maangamizo yao.''
 Neno la MUNGU lina nguvu za MUNGU kubwa sana na linaweza kumtia nguvu mtu wa MUNGU, Neno la MUNGU linaweza kukutoa katika mawazao mabaya yaliyokuzonga kwa sababu ya magumu unayopitia.
Siku moja nilikuwa katika wakati mgumu sana sana lakini ghafla ndani yangu wimbo fulani wa injili ulio Neno la MUNGU ukaanza kuimba ndani yangu, wimbo huo uliimba ndani yangu hadi na mimi nikaanza kuuimba na katika kulikiri Neno hilo la MUNGU lililohubiriwa kwa njia ya wimbo wa injili nilijikuta huzuni imeicha na hata tatizo nililokuwa nalo nikaliona la kawaida kabisa, MUNGU hulituma Neno.
Unaweza ukalipata Neno kwa ufunuo, ukasikia kwa sauti, ukalisoma kwenye Biblia, ukaelekezwa na ROHO MTAKATIFU andiko n.k lakini kwa sababu ni Neno la MUNGU hakika litakutia nguvu sana.
Mtu mmoja alikuwa kwenye wakati mgumu sana kwa sababu ya kuumwa sana na yuko katika hali ya mahututi, alikuwa amekata tamaa sana ya kupona lakini ghafla akasikia sauti ikisema ''Bali(YESU) alijeruhiwa kwa makosa yetu, Alichubuliwa kwa maovu yetu; Adhabu ya amani yetu ilikuwa juu yake, Na kwa kupigwa kwake sisi tumepona.-Isaya 53:5''
 Ghafla yule ndugu alihisi nguvu za ajabu kwa kukiri Neno hilo na baada ya muda aliamka na kupona hata wakamshangaa waliokuwa wanamuuguza, MUNGU hulituma Neno.
Unapoomba MUNGU akutie nguvu basi wakati mwingine MUNGU anaweza akalituma Neno na ukajaa nguvu za kushinda tatizo.
Unaweza ukaona kwa ndoto au kwa maono au kwa njia nyingine yeyote lakini ni Neno la MUNGU la kukutia nguvu.

B. Malaika wa MUNGU au ROHO MTAKATIFU  kukusemesha na kukuelekeza 
1 Wafalme 19:1-8 ''Basi, Ahabu akamwambia Yezebeli habari ya mambo yote aliyoyafanya Eliya, na jinsi alivyowaua manabii wote kwa upanga.  Ndipo Yezebeli akampelekea Eliya mjumbe, kusema, Miungu wanifanyie hivyo na kuzidi, nisipokufanya roho yako kesho, panapo wakati huu, kama roho ya mmojawapo wa hao.  Naye alipoona hayo, aliondoka, akaenda aihifadhi roho yake, akafika Beer-sheba, mji wa Yuda, akamwacha mtumishi wake huko.  Lakini yeye mwenyewe akaendelea katika jangwa mwendo wa siku moja, akaenda akaketi chini ya mretemu. Akajiombea roho yake afe, akasema, Yatosha; sasa, Ee BWANA, uiondoe roho yangu; kwa kuwa mimi si mwema kuliko baba zangu.  Naye akajinyosha akalala chini ya mretemu; na tazama, malaika akamgusa, akamwambia, Inuka, ule. Akatazama, kumbe! Pana mkate umeokwa juu ya makaa, na gudulia la maji, kichwani pake. Akala, akanywa, akajinyosha tena.  Malaika wa BWANA akamwendea mara ya pili, akamgusa, akasema, Inuka, ule; maana safari hii ni kubwa mno kwako.  Akainuka, akala, akanywa, akaenda katika nguvu za chakula hicho siku arobaini mchana na usiku hata akafika Horebu, mlima wa MUNGU.''
 Eliya Nabii alifikia kipindi kigumu sana.
Hebu jiulize wewe ndio Eliya na umejaa upako na kwa maombi yako MUNGU alifunga mvua miaka mitatu na nusu, baada ya miaka mitatu na nusu  mvua ikanyesha kwa maombi yako, umesababisha mawakala wa shetani wamekufa na umesababisha taifa kumrudia MUNGU wa kweli, Umemfufua mtoto wa mama wa Sarepta kwa maombi na sio hivyo tu bali umefanya miujiza mingi kwa maombi yako na upako wako ambao MUNGU amekujaalia. Unadhani umefaulu katika utumishi wako maana silaha za shetani zimeteketea katika taifa lakini ghafla unapata taarifa za kuuawa siku moja tu baada ya MUNGU kukuonekania. Ulikuwa ni wakati mgumu sana kwa Eliya hadi akaanza kuomba maombi ya MUNGU kumuondoa duniani. Eliya alijua kabisa hawezi kujiua kwa sababu kujiua ni kujipeleka jehanamu hivyo yeye aliomba maombi kwamba MUNGU amchukue maana alifikia kiwango cha mwisho kabisa cha kuvumilia magumu. Eliya alivumilia magumu kwa siku arobaini lakini mwisho akajiombea kuondoka duniani na akajinyoosha kabisa kwenye mtu akijua kwamba muda mfupi ujao atakufa, Lakini ghafla tena ghafla sana Malaika wa MUNGU anakuja na kumsemesha akisema ''Inuka, ule.'' Maana Malaika alimletea Eliya Chakula cha mbinguni. Kwa maumivu ya moyo wa Eliya akiogopa kuuawa na Yezebeli ilibiki Malaika arudi tena na kumwambia Eliya Kwamba '' Inuka, ule; maana safari hii ni kubwa mno kwako.  Akainuka, akala, akanywa, akaenda katika nguvu za chakula hicho siku arobaini mchana na usiku hata akafika Horebu, mlima wa MUNGU. ''.
Ndugu kuna wakati hakika Malaika wa MUNGU anaweza akatumwa na MUNGU ili kukusemesha na kwa njia hiyo unajaa nguvu za kusonga mbele.
ROHO MTAKATIFU ndio kabisa huwajulisha sana watumishi wake wanapokuwa katika magumu na yeye ndiye anayetusaidia.
ROHO MTAKATIFU kukusemesha wakati wa magumu yako hakika huo ni msaada tosha na lazima ujae nguvu za kusonga mbele.
Katika wakati wetu huu ROHO MTAKATIFU ni wa muhimu sana maana ndiye Mwangalizi wa roho zetu na msimamizi wa kanisa la KRISTO duniani hivyo yeye yupo kutusaidia na kutupa ushindi na tumaini kuu.
Warumi 8:14 '' Kwa kuwa wote wanaoongozwa na ROHO wa MUNGU, hao ndio wana wa MUNGU.'' 
 

C. MUNGU kuwatumia watumishi wake kukutia nguvu.

Isaya 35:3-4 '' Itieni nguvu mikono iliyo dhaifu, yafanyeni imara magoti yaliyolegea.  Waambieni walio na moyo wa hofu, Jipeni moyo, msiogope; tazama, MUNGU wenu atakuja na kisasi, na malipo ya Mungu; atakuja na kuwaokoa ninyi.''
 Mimi Binafsi MUNGU ameshanitumia mara nyingi katika kuwatia nguvu baadhi ya marafiki zangu, ngoja nikupe mfano jinsi ambavyo MUNGU anaweza kuwatumia watumishi wake kwa ajili ya kukutia nguvu wewe unapokuwa katika magumu.
Siku moja nilikuwa naongea na rafiki yangu mmoja kwa simu na kuombea kwa sababu alikuwa katika magumu sana sana lakini wakati nikiomba nikasikia sauti ikisema ''Akupelekee msaada toka patakatifu pake, Na kukutegemeza toka Sayuni. Azikumbuke sadaka zako zote, Na kuzitakabali dhabihu zako. Akujalie kwa kadiri ya haja ya moyo wako, Na kuyatimiza mashauri yako yote.-Zaburi 20:2-4''
 Nilimwambia Neno hilo  la MUNGU na kumwambia kwamba alisome na kumshukuru MUNGU kwa maombi, hakika alishinda jambo hilo baya lililokuwa limevamia maisha yake.
Mama mmoja wa kanisani siku moja alikuwa katika wakati mgumu sana kwa sababu mumewe hajaokoka na huwa anamtesa sana, alilia kwa muda mrefu na kujikuta akijiwazia mabaya, ghafla akaona ngoja aende kanisani, alipofika kanisani alimkuta Mchungaji na Mchungaji akamwambia maneno ya faraja ambapo hata Mchungaji hakujua kama mama huyo yuko katika magumu. Baada ya pale yule mama alijiona amepona kabisa katika jambo hilo na akashangaa hada kuja kushuhudia ibadani maana uchungu wote uliisha na akawa na amani baada ya kuongea na Mchungaji.
Kwanini mama huyo aliumia sana, ni kwa sababu alikuwa ametoka kuomba maombi ya kufunga na alijua kabisa sasa Mambo yanaenda kuwa safi katika ndoa yake lakini baada ya kufunga ndipo mambo yakazidi kuwa mabaya na vipigo juu, ilimuumiza na kumkatisha tamaa sana hadi Mtumishi wa MUNGU alipomtia nguvu kwa maneno ya Neno la MUNGU.

2. Unahitaji MUNGU akusaidie.

Baada ya MUNGU kukutia nguvu basi omba MUNGU akusaidie ili ushinde hayo magumu na utoke katika magumu hayo.
Zaburi 121:2 ''Msaada wangu u katika BWANA, Aliyezifanya mbingu na nchi. ''

MUNGU anaweza kuutuma msaada na ukashinda hakika.
Watu wengi wakati wa magumu hulalamika tu na kulaumu tu, hiyo haipunguzi tatizo kwa vyovyote, ni heri kuomba.
Ukiuhitaji msaada wa MUNGU kwa maombi hakika utaupata na utamtukuza MUNGU.
Isaya 25:9 '' Katika siku hiyo watasema, Tazama, huyu ndiye MUNGU wetu, Ndiye tuliyemngoja atusaidie; Huyu ndiye BWANA tuliyemngoja, Na tushangilie na kuufurahia wokovu wake. ''
 Kumbuka wakati umechoka epuka mambo haya.
1. Epuka lawama.
2. Epuka manung'uniko na kujihesabia haki.
3. Epuka kujilinganisha na watu na watu ambao hawapitii hali kama yako kwa wakati huu wa magumu yako.
Omba MUNGU akusaidie na kukutia nguvu.
Isaya 12:2 '' Tazama, Mungu ndiye wokovu wangu; Nitatumaini wala sitaogopa; Maana Bwana YEHOVA ni nguvu zangu na wimbo wangu; Naye amekuwa wokovu wangu. ''

 Usiwategemee wanadamu na wala usiweke tumaini  lolote kwao bali mtegemee MUNGU maana yeye atakusaidia na atakuinulia watu hata tofauti na unaowawazia ili kukusaidia.
Zaburi 20:1-2 '' BWANA akujibu siku ya dhiki, Jina la MUNGU wa Yakobo likuinue.  Akupelekee msaada toka patakatifu pake, Na kukutegemeza toka Sayuni.''

 3. Unahitaji MUNGU akushike mkono.

Isaya 41:10-13  '' usiogope, kwa maana mimi ni pamoja nawe; usifadhaike, kwa maana mimi ni MUNGU wako; nitakutia nguvu, naam, nitakusaidia, naam, nitakushika kwa mkono wa kuume wa haki yangu. Tazama, wote walioona hasira juu yako watatahayarika na kufadhaika; watu washindanao nawe watakuwa si kitu, na kuangamia. Utawatafuta wala hutawaona wale wapiganao nawe; watakuwa si kitu; watakuwa kama kitu kisichokuwa, wale waliofanya vita juu yako. Kwa maana mimi, BWANA, Mungu wako, nitakushika mkono wako wa kuume, nikikuambia, Usiogope; mimi nitakusaidia.''

Kuna mambo yanaweza kuletwa na shetani kipindi umechoka ili akumalize au akuondoe kabisa katika Wokovu wa KRISTO.
Ndugu, wakati umehoka na wakati wa dhoruba unahitaji kumwambia MUNGU akushike mkono.
Katika dharuba na magumu ya aina yeyote hakikisha unaishi maisha matakatifu, hakikisha unamtumikia MUNGU na endelea kumwabudu katika Roho na kweli.
Inawezekana kabisa umetegemea kitu fulani hadi umechoka na hujakipata.
Inawezekana kabisa umeomba hadi umekata tamaa.
Inawezekana kabisa ufahamu wako umefika mwisho.
Ndugu uhahitaji kuomba toba juu ya kilichosababisha tatizo.
Unahitaji kuomba MUNGU akutie nguvu akusaidie na kukushika mkono.
 Mitahli 3:5-8 '' Mtumaini BWANA kwa moyo wako wote, Wala usizitegemee akili zako mwenyewe;  Katika njia zako zote mkiri yeye, Naye atayanyosha mapito yako.  Usiwe mwenye hekima machoni pako; Mche BWANA, ukajiepushe na uovu. Itakuwa afya mwilini pako, Na mafuta mifupani mwako.''
 
 Natamani niseme mengi mno lakini naamini mwenye kuelewa ameelewa.
MUNGU akubariki kwa kujifunza somo hili muhimu pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane nitakujulisha jinsi ya kukipata.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa BWANA YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
0714252292.
0786719090
mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu

Comments

Mike Royce said…
Ubarikiwe Kwa mafunzo haya. Mungu wa mbinguni azidi kukuinua