MAOMBI YA KUHARIBU NYAVU ZA KICHAWI ULIZOTEGEWA KWA SIRI.

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.

 Bwana YESU KRISTO apewe sifa ndugu yangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU kisha tuombe maombi ya kuharibu nyavu za kichawi.
Naamini kabisa unajua nyavu ni nini.
Samaki huvuliwa kwa nyavu, najua kabisa samaki hawapendi kuvuliwa lakini nyavu huwafanya wanaswe hata kama hawataki.
Hata wawindaji hutumia nyavu kuwakamata baadhi ya wanyama.
Hata mawakala wa shetani hutumia nyavu zao za kipepo ili kuwanasa wateule wa MUNGU.
Unaweza ukaingia katika mahusiano ya uchumba kumbe ndani ya mahusiano hayo kuna nyavu za shetani ili upoteze uhusiano wako na MUNGU au upoteze mwelekeo wa maisha yako.
Biashara yako inaweza ikategewa nyavu za kichawi ili ufilisike.
Maisha yako yanaweza kutegewa nyavu za kichawi ili unase na kushindwa kusonga mbele.
Hawara wa mke wako au mume wako, huyo ni nyavu ya shetani ili kuua ndoa yako.
Wako  watu wanaweza kujipendekeza kwako kumbe wanakutegea nyavu za kipepo ili unase.
Mitahli 29:5 ''Mwenye kujipendekeza kwa jirani yake, Hutandika wavu ili kuitega miguu yake.''

Maisha yako yanaweza kuwindwa kipepo ili tu unaswe na kushindwa kufikia malengo yako.
Uchumi wako unaweza ukategewa nyavu za kichawi ili ubaki kuwa mtu wa kuteswa na madeni kila siku.
Watoto wako au ndoa yako  inaweza kutegewa nyavu za kipepo ili wewe uteseke. 
Pepo la uzinzi na usaliti ni nyavu ya shetani  ili kuleta uharibifu kwako, katika uchumba wako au katika ndoa yako.
Mtu kuwa na roho ya kiburi ni nyavu ya shetani hiyo.
Zaburi :140:5 ''Wenye kiburi wamenifichia mtego na kamba; Wametandika wavu kando ya njia; Wameniwekea matanzi.''

Magonjwa ya kurogwa ni nyavu za shetani ili udhurike na ukatishe ratiba zako nzuri za maisha.
Dhambi ni nyavu ya shetani ili mwanadamu asiende uzima wa milele.
Uongo ambao watu wanaokuhusu wanaambiwa kuhusu wewe ili wakuchukie, hizo ni nyavu za kipepo ili kukuharibia.
Husika na ufunuo wa leo na uombe na MUNGU ataharibu nyavu zote za kipepo.
 Ndugu yangu, unahisi umetegewa nyavu katika eneo gani la maisha yako?
Unahitaji kuomba na kushinda leo kwa jina la YESU KRISTO.
Kuna watu wametegewa nyavu katika afya zao ndio maana kila siku wanaweka bajeti ya madawa tu.
Kuna watu wametegewa nyavu katika uzao wao.
Kuna watu wametegewa nyavu za giza katika uchumi wao.
Kuna watu wametegewa nyavu za kipepo katika ndoa zao.
Kuna watu wametegewa nyavu za giza katika kumiliki na kutawala, ndio maana badala ya wao kumiliki na kutawala, mawakala wa shetani ndio humiliki na kutawala katika maeneo yao.
Kama umerogwa ujue hiyo ni nyavu ya shetani moja kwa moja kukutesa.
Leo kwa maombi yako hakikisha unaharibu kila nyavu ya mchawi na mchawi mwenyewe.
Leo sema omba hivi '' Uharibifu na umpate kwa ghafula, Na wavu aliouficha umnase yeye mwenyewe; Kwa uharibifu aanguke ndani yake.-Zaburi 35:8 ''
 
KAZI ZA HIZO NYAVU ZA KICHAWI NI NINI?

1. Kukuzuia kutoka ndani ya kifungo walichokufunga.
2. Kukuchelewesha kupata baraka zako.
3. Kukuondolewa uwezo wa kufanikiwa katika kumiliki baraka zako.
4. Kukufanya uwe Mtumwa wa shetani.
5. Kukuondolea furaha katika maisha yako.


Usikubali, hakikisha leo unaomba kwa jina la YESU KRISTO aliye hai na utashinda, usikubali wachawi wanaotumika kishetani waendelee kukuchimbia shimo kupitia nyavu zao za kipepo.
Yeremia 18:19-22 '' Niangalie, Ee BWANA, ukasikilize sauti ya wanaoshindana nami. Je! Mabaya yalipwe badala ya mema? Maana wameichimbia nafsi yangu shimo. Kumbuka jinsi nilivyosimama mbele zako, ili niseme mema kwa ajili yao, nikaigeuze ghadhabu yako isiwapate. Kwa sababu hiyo, uwatoe watoto wao waone njaa, uwatoe nguvu za upanga ziwapate; wake zao wafiwe na watoto wao, na kufiwa na waume zao; wanaume wao wauawe, na vijana wao wapigwe kwa upanga vitani. Kilio na kisikiwe kitokacho katika nyumba zao, hapo utakapoleta kikosi juu yao kwa ghafula; kwa maana wamenichimbia shimo waninase, nao wameifichia miguu yangu mitego. ''

Tunapozungumzia nyavu za kipepo ni muhimu pia tukajua kwamba zipo nyavu za giza pia ambazo wewe mwenyewe unaweza kujinasa kwa nyavu hizo kwa sababu humtii MUNGU na Neno lake Biblia.
Baadhi ya nyavu hizo za kichawi ambazo wewe mwenyewe unaweza kujifunga nazo ni hizi.

1. Kuingia mikataba au maagano ya kipepo kwa sababu ya tamaa zako.

Isaya 28:15 ''Kwa sababu mmesema, Tumefanya agano na mauti, tumepatana na kuzimu; pigo lifurikalo litakapopita, halitatufikia sisi; kwa maana tumefanya maneno ya uongo kuwa kimbilio letu, tumejificha chini ya maneno yasiyo kweli; '' 
Maagano yote ya kipepo na mikataba yote ya kipepo ni agano na mauti yaani agano na uharibifu.
Maagano hayo ni nyavu inayoweza kukufanya ulitumikie ganao la giza lilikufunga.

2. Kwenda kwa waganga wa kienyeji.

Walawi 19:28 ''Msichanje chale yo yote katika nyama ya miili yenu kwa ajili ya wafu, wala msiandike alama miilini mwenu; mimi ndimi BWANA.''
Kwenda kwa waganga  ni wavu mbaya sana ambao mtu anaweza kujifunga mwenewe.
Kwenda kwa waganga kutakuletea majini, mizimu na maagano yatakayokufanya ubaki umefungwa kwenye wavu wa kipepo.
Mapepo ni nyavu za shetani ili kukufanya ubaki mtumwa wa shetani. Kwa uzoefu wangu karibia watu wote niliowaombea mapepo yakatawatoka ni wale ambao wamewahi kwenda kwa waganga wa kienyeji, iwe walienda wenyewe au walipelekwa.

3. Dhambi.

 Isaya 5:20 ''Ole wao wasemao kwamba uovu ni wema, na kwamba wema ni uovu; watiao giza badala ya nuru, na nuru badala ya giza; watiao uchungu badala ya utamu, na utamu badala ya uchungu!  ''
Dhambi unayoifanya ni wavu mbaya kuliko zote unaoweza kukushikilia ili usimpendeze MUNGU na ili usiende uzima wa milele katika KRISTO YESU Mwokozi.

JINSI YA KUTOKA KATIKA NYAVU ZA KICHWAWI ULIZOTEGEWA.

1. Omba katika jina la YESU KRISTO ili kutoka ndani ya nyavu za giza ulizotegewa.

Zaburi 25:15 ''Macho yangu humwelekea BWANA daima, Naye atanitoa miguu yangu katika wavu.''

2. Haribu kwa maombi nyavu za kipepo ulizotegewa kwa siri ili zikunase.

Zaburi 141:8-10 ''Macho yangu yanakuelekea Wewe, MUNGU Bwana, Nimekukimbilia Wewe, usiniache nafsi yangu. Unilinde na mtego walionitegea, Na matanzi yao watendao maovu. Wabaya na waanguke katika nyavu zao wenyewe, Pindi mimi ninapopita salama.''

3.Omba ROHO

Zaburi  32:8 ''Nitakufundisha na kukuonyesha njia utakayoiendea; Nitakushauri, jicho langu likikutazama.''

 4. Omba Nyavu zao  zinawane wao na sio wewe.

Zaburi 57:6 '' Wameweka wavu ili kuninasa miguu; Nafsi yangu imeinama; Wamechimba shimo mbele yangu; Wametumbukia ndani yake!''

 Natamani niseme mengi mno lakini naamini mwenye kuelewa ameelewa.
MUNGU akubariki kwa kujifunza somo hili muhimu pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane na nitakujulisha jinsi ya kukipata
na  Naamini kitakusaidia sana.
Hapa chini ni MAOMBI YA KUHARIBU NYAVU ZA KICHAWI ULIZOTEGEWA KWA SIRI.
Maombi haya naomba yamsaidie mtu yule ambaye hajui kuomba ili katika kuomba kwa kutumia hayo basi atakumbuka mahitaji yake na kuyataja katika maombi yake.
Kwa waombaji wazoefu naamini baada tu ya kulisoma somo na kulielewa basi anajua aombee nini maana alikuwa anaandika points za kuombea.


  MAOMBI YA KUHARIBU NYAVU ZA KICHAWI ULIZOTEGEWA KWA SIRI.

 BABA MUNGU wa mbinguni, katika jina la YESU KRISTO Mwokozi aliye hai ninakushukuru kwa uzima ulionipa. Ninakushukuru kwa ajili ya somo hili na naamini sasa katika wewe naenda kushinda.
Kwanza ninaomba unisamehe dhambi zangu zote na maovu yangu yote niliyokosea mbele zako, ifundishe roho yangu kukutii wewe Muumba wangu. Ninatubu kwa ajili ya nyavu za kichawi ambazo ni mimi mwenyewe nilijifunga nyavu hizo, kwa sababu ya kuingia mikataba mibaya na kwa sababu ya kwenda kwa waganga wa kienyeji na kwa sababu ya kufanya dhambi zilizotengeneza nyavu za giza ili kunikamata. Ninatubu MUNGU Muumba wangu na naomba sasa niwe mtu anayeliishi Neno lako la Wokovu wako katika KRISTO YESU.
Nyavu yeyote inaniyotesa ambayo niliisababisha mimi ninatubu kwa ajili ya hiyo na naomba kwa Neema yako JEHOVAH MUNGU wangu nitoke katika kifungo hicho cha nyavu ya giza.
Niko mbele zako MUNGU wangu sasa nikiharibu nyavu za giza zote zilizowekwa na mawakala wa shetani katika maisha yangu.
Kila nyavu ya kipepo ya aina yeyote niliyotegewa ininase na ikaninasa, sasa kwa mamlaka ya Jina la YESU KRISTO ninaiharibu nyavu hiyo na ninatoka salama. Neno lako MUNGU BABA linasema  ''Macho yangu humwelekea BWANA daima, Naye atanitoa miguu yangu katika wavu.-Zaburi 25:15'' Hivyo ninaomba MUNGU wangu unitoe katika kila nyavu ya kichawi iliyonasa maisha yangu, ndoa yangu, uchumi wangu, biasahara yangu, uzao wangu, uchumba wangu au kazi yangu.

Natoka sasa katika nyavu ya kipepo katika jina la YESU KRISTO.
Ninaomba kwa neema yako MUNGU BABA malaika zako wafanye kazi yako kwangu kama Neno lako linavyosema katika Waebrania 1:14  Kwamba '' Je! Hao(Malaika) wote si roho watumikao, wakitumwa kuwahudumu wale watakaourithi wokovu?''  Ninaomba Malaika wako MUNGU wanihudumie na mimi kwa kuziharibu nyavu zote za kichawi ambazo maisha yangu yalitegewa.
Ninaharibu kila nyavu ya mganga wa kienyeji iliyotegwa ili kuninasa, ninaharibu nyavu hizo  kwa damu ya YESU KRISTO na kwa jina la YESU KRISTO aliye hai.
Ninaharibu kila nyavu ya mchawi aliyoyategemea maisha yangu, ninaharibu nyavu hizo  kwa damu ya YESU KRISTO na kwa jina la YESU KRISTO aliye hai.
Ninaharibu kila nyavu ya mwanadamu anayetumika kipepo ili kunidhuru, ninaharibu nyavu hizo  kwa damu ya YESU KRISTO na kwa jina la YESU KRISTO aliye hai.
Ninaharibi kila nyavu ya kipepo aliyonitegea mtu aliyenipenda, ninaharibu nyavu hizo  kwa damu ya YESU KRISTO na kwa jina la YESU KRISTO aliye hai.
Ninaharibu kila nyavu ya kichawi aliyoitega mkuu wa giza katika maisha yangu,  ninaharibu nyavu hizo  kwa damu ya YESU KRISTO na kwa jina la YESU KRISTO aliye hai.
Ninaharibu na kuangamiza kila kazi za kila mshirikina anayewinda maisha yangu, ninaharibu nyavu hizo  kwa damu ya YESU KRISTO na kwa jina la YESU KRISTO aliye hai.
 Sasa kila aniyenitegea nyavu ya kipepo katika maisha yangu, ndoa yangu, uazo wangu, uchumi wangu au kila kitu changu ninaamuru kwa mamlaka ya jina la YESU KRISTO hiyo nyavu imnase yeye sawasawa na Neno la MUNGU katika Zaburi 57:6  Kwamba '' Wameweka wavu ili kuninasa miguu; Nafsi yangu imeinama; Wamechimba shimo mbele yangu; Wametumbukia ndani yake!''
 Watumbukie sasa kwa wao wote walionitegea nyavu za giza.
Kila aliyenitegea nyavu ya kipepo hata kabla sijazaliwa, leo namharibu huyo kwa jina la YESU KRISTO na nyavu yake naichoma moto kwa jina la YESU KRISTO.
Niko huru sasa mbali na nyavu za giza, na hata nyavu wakiitega muda ujao bado kwa jina la YESU KRISTO nyavu hiyo itawanasa wao.
Walionitegea nyavu ili nisioe/ Nisiolewe sasa kwa jina la YESU KRISTO nyavu yao naichoma moto na kuitowesha, kwa sasa sitazuilika tena.
Wanaonizuia kufanikiwa katika kazi yangu au biashara yangu nawaharibu wao na nyavu zao katika jina la YESU KRISTO.
Niko huru sasa katika jina la YESU KRISTO.
Nakushukuru MUNGU BABA maana umenishindia.
Katika jina la YESU KRISRO nimeomba na kuamini na kupokea ushindi.
Amen Amen Amen.
 Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa BWANA YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
0714252292.
0786719090
mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu.

Comments