MBONA UMEKUWA HIVYO NDUGU?

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.
Bwana YESU atukuzwe!
Karibu tujifunze Neno la MUNGU na hapa naongea na mtu moja kwa moja.
Mbona Umekuwa Hivyo Ndugu? 
Unaimba Kikristo Ila Kucheza Kipagani.
Unaomba Kikristo Ila Mavazi Ya Kipagani. 
Unaongea Kikristo Lakini Matendo Ya Kipagani. 
Unahubiri Kikristo Lakini Maombezi Hayaeleweki Maana Humtaji Tena KRISTO. 
 Mbona Umekuwa Hivyo Mpendwa? 
 Nimeambiwa Nikuonye Ndio Maana Nakuonya.
Unahitaji kutengeneza kwa Bwana YESU ndugu.
Ya kale yanatakiwa yapite na sio kuyarudia, ya kale ni machukizo ya kidunia na ni dhambi na mipango ya zamani kabla hujaokoka. Kwanini unataka kuyaleta katika katika kanisa la MUNGU mambo uliyokuwa unayafanya kipindi hujokoka?
Ulikuwa mlevi zamani, kwanini na sasa ukiwa umeokoka umekuwa mtu wa kunywa pombe?
Kwanini umekuwa mtu wa kufanya machukizo ya zamani?
Biblia inasema kwako uliyempokea Bwana YESU kwamba '' Kama watoto wa kutii msijifananishe na tamaa zenu za kwanza za ujinga wenu; bali kama yeye(YESU) aliyewaita alivyo mtakatifu, ninyi nanyi iweni watakatifu katika mwenendo wenu wote;-1 Petro 1:14-15''

 Kuna Watu Sasa Wanatamani Kurudi Katika Kaburi La Dhambi. Watu Hawa Walifanikiwa Kufufuliwa Kutoka Kaburi La Dhambi Siku Walipookoka, Lakini Sasa Baadhi Yao Wameanza Kutamani Tena Kuzikwa Kwenye Kaburi La Dhambi. 
Ndugu, Nakusihi Sana Jitahidi Sana Usikubali Kurudi Kaburi La Dhambi Tena. 
2 Kor 4:2 ''lakini tumekataa mambo ya aibu yaliyositirika, wala hatuenendi kwa hila, wala kulichanganya neno la MUNGU na uongo; bali kwa kuidhihirisha iliyo kweli twajionyesha kuwa na haki, dhamiri za watu zikitushuhudia mbele za MUNGU.''
Endelea Mbele Na KRISTO Aliyekufufua Siku Ulipompokea. 

Ni muhimu kujua kwamba Mwanadamu akiondoka duniani huwa harudi.
Naomba ndugu ulijue hilo.
Ndugu uliyepata neema ya kusoma Ujumbe huu muda huu nakuomba tubu kwa Bwana YESU, mpokee kama Mwokozi wako, acha dhambi zote na anza kuishi maisha matakatifu, ili tu usiende jehanamu.

Ndugu yangu, sijaandika Ujumbe huu kwa sababu najua kuandika, Bali nimekuandikia ili utengeneze kwa Bwana YESU hata akupe uzima wa milele.
Ujumbe huu ni ufunuo binafsi kwako kutoka kwa ROHO MTAKATIFU ili tu utengeneze maisha yako na njia zako.
Usijiite umeokoka wakati wewe ni mtenda dhambi mkubwa.
Usijione una dini yako nzuri wakati hujaokoka.
Usijivunie dhehebu lako.
Ndugu nakuomba sana sana mpokee Bwana YESU, tubu na acha dhambi kuanzia Leo ndipo utahusika na uzima wa milele.

Kumbuka tunaokolewa kwa neema hivyo usiitumie Neema ya MUNGU vibaya na neema ya wewe kuandikwa jina lako kwenye kitabu cha uzima ni leo ndio maana unajifunza somo hili ili uokoke kwelikwli na kuwa mshirika mzuri wa kanisa.
Waefeso 2:8 '' Kwa maana mmeokolewa kwa neema, kwa njia ya imani; ambayo hiyo haikutokana na nafsi zenu, ni kipawa cha MUNGU; ''

 Ndugu,usikubali tena  kuwa mteja wa shetani katika maisha yako.
Shetani anauza pombe, anauza magonjwa na anauza madawa ya kulevya.
Ndugu nakuomba usikubali kuwa mteja wa shetani.
Shetani anauza rushwa na anauza hirizi.
Ndugu usikubali kuwa mteja wa shetani katika maisha yako.
Shetani anauza uongo na kiburi, shetani anauza umbea na usengenyaji.
Ndugu usikubali kuwa mteja wa shetani.
Shetani anauza kila dhambi unayoitamani, ndugu usikubali kuinunua hiyo dhambi.
Ndugu usikubali kununua chochote kwa shetani.

Kumbuka Bwana YESU anarudi kuchukua walio wake.
Walio wake ni wale waliompokea Kama Mwokozi wao.
Yohana 1:12 '' Bali wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu, ndio wale waliaminio jina lake;''
Kisha wanaishi maisha matakatifu ya Wokovu wake.
Zaburi 34:14 '' Uache mabaya ukatende mema, Utafute amani ukaifuatie.''
Mtu akiwa hajashika hayo mawili huyo sio wake KRISTO.
YESU haji kuchukua dhehebu wala dini anakuja kuchukua waliompokea kama Mwokozi wao kisha wanaishi maisha matakatifu.
YESU haji kuchukua walipewa tuzo maofisini kwao kwa sababu ya kufanya kazi za kidunia kwa juhudi, Bali YESU KRISTO anakuja kuchukua waliompokea kama Mwokozi kisha. Wanaishi maisha matakatifu ya Wokovu wake.
YESU haji kuchukua wachungaji, maaskofu, mitume na manabii Bali anakuja kuchukua waliompokea kama Mwokozi kisha wanaishi maisha matakatifu.
Madaraka, vyeo, Huduma au karama bila utakatifu ni hasara. Ndio maana Bwana YESU haji kuchukua wenye Huduma au vyeo Bali anakuja kuchukua watakatifu.

YESU haji kuchukua matajiri au masikini Bali anakuja kuchukua waliompokea na wanaishi maisha matakatifu ya Wokovu wake.
YESU haji kuchukua weupe au weusi au wafupi au warefu Bali anakuja kuchukua waliompokea Kama Mwokozi wao kisha wanaishi maisha matakatifu ya Wokovu wake.
Cha ajabu kila mtu duniani kutoka dini zote wanajua ni YESU KRISTO atakuja kuhukumu watu wote duniani, lakini wengi hawamhitaji YESU na wengine hawapendi hata kusikia jina YESU KRISTO likitajwa.
Ni rahisi kwamba siku hiyo Bwana YESU hatawachukua watu hao wanaomkataa.
Na Biblia iko wazi sana kwamba watakaoachwa wote kutoka dini zote na kutoka mataifa yote wataenda jehanamu

Mathayo 24:37-42 '' Kwa maana kama vile ilivyokuwa siku za Nuhu, ndivyo kutakavyokuwa kuja kwake Mwana wa Adamu.
 Kwa kuwa kama vile siku zile zilizokuwa kabla ya Gharika watu walivyokuwa wakila, na kunywa, wakioa na kuolewa, hata siku ile aliyoingia Nuhu katika safina, wasitambue, hata Gharika ikaja, ikawachukua wote, ndivyo kutakavyokuwa kuja kwake Mwana wa Adamu. Wakati ule watu wawili watakuwako kondeni; mmoja atwaliwa, mmoja aachwa; wanawake wawili watakuwa wakisaga; mmoja atwaliwa, mmoja aachwa.''

YESU haji kuchukua wanaomkataa kuwa Mwokozi wao.
Ndugu kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi wako ni Leo wala sio kesho.
Nakuomba wajulishe watu neno hili la MUNGU huku wewe mwenyewe ukiwa kielekezo safi cha kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi na hakikisha unaishi maisha matakatifu.
Alama za mtu aliyeasi Wokovu wa KRISTO.
1. Ana roho ya kiburi.
2. Anawaogopa watumishi wa MUNGU na kuwakimbia au kukataa mawasiliano nao.
3. Amejitenga mbali na Kanisa la MUNGU.
4. Haoni tatizo kuendelea na dhambi.
5. Hana tena hofu ya MUNGU.
6. Kujifanya anajua kila kitu hata wakati anasaidiwa kiroho.
7. Hana tena moyo wa toba.
8. Hahudhurii ibada au popote kwenye fundisho la Neno la MUNGU.
9. Amebakiza kusema tu uongo juu ya watumishi wa MUNGU na wana Kanisa wengine, kwa kuzusha uongo ili yeye muasi aonekane ni bora kuliko Kanisa.
10. Amekauka kiroho.
- Hana maombi tena.
- Hana hamu ya kusoma Neno la MUNGU wala kulitafakari.
- Ameacha kumtolea MUNGU zaka na sadaka.

Ndugu unayesoma Ujumbe huu hakikisha hauko miongoni mwao waliomwasi MUNGU na kuondoka katika Wokovu wa Bwana YESU.
Kumbuka hii.
Wagalatia 5:19-21 " Basi matendo ya mwili ni dhahiri, ndiyo haya, uasherati, uchafu, ufisadi, ibada ya sanamu, uchawi, uadui, ugomvi, wivu, hasira, fitina, faraka, uzushi, husuda, ulevi, ulafi, na mambo yanayofanana na hayo, katika hayo nawaambia mapema, kama nilivyokwisha kuwaambia, ya kwamba watu watendao mambo ya jinsi hiyo hawataurithi ufalme wa MUNGU."


Umepoteza vitu vingapi ambavyo MUNGU alikupa?
Ulipewa huduma katika KRISTO ila sasa umeipoteza maana hutumiki tena.
Ulipewa karama na ROHO MTAKATIFU lakini sasa umeipoteza karama yako kwa sababu ya kukubali kuzongwa na dunia.
Umekataa wito wa injili, umekataa Wokovu na kwa jinsi hiyo umemkataa MUNGU.
Ndugu unahitaji kuwa makini sana katika alichokupa MUNGU ili utende katika Injili.

MUNGU amekupa YESU KRISTO ili uokoke.
MUNGU amekupa huduma,karama na vipawa katika Kanisa lake ili utanyie kazi.
MUNGU amekupa Neno lake Biblia ili uishi maisha matakatifu na ili ujue mpango wa MUNGU wa uzima.

Ndugu hakikisha;
1. Unaishi maisha matakatifu katika Wokovu wa Bwana YESU.
2. Hakikisha unamtumikia MUNGU.
3. Hakikisha unaacha dhambi zote.
4. Hakikisha unaongozwa na Neno la KRISTO.

Usiache ibada na usiache maombi.
Usikengeuke na kugeuka mpagani.
Walioacha ibada na kuacha Wokovu ndio hao hao ambayo kazi yao kubwa ni kuutukana Wokovu.
Watu hao wameungana na wapinga Kristo ili kuhakikisha kila mtu anakuwa kwa shetani kama walivyo wao kwa shetani. Ewe ndugu wa namna hiyo nakuomba usimcheke mtu anayetafuta ufalme wa MUNGU.
Huyo anatafuta hatima njema ya maisha yake.
Huyo anaweka mazingira ya mawakala wa shetani kumuogopa na kumkimbia siku zote.
Huyo anaitengeneza kesho yake kwa YESU kwenye uzima wa milele.
Huyo anachagua uzima wa milele na sio jehanamu ya moto.
Usimcheke Bali hakikisha na wewe unakuwa kama yeye kwa kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi wako na kuanza kuishi maisha matakatifu.
Huyo amelichagua fungu jema ambalo asiporudi nyuma hakika hakuna atakayemuondolea fungu lake mema la uzima wa milele.
Usimcheke huyo ndugu.
Usione kwamba anapoteza muda wake kwa kwenda kanisani kila Mara.
Usimuone hana ajili kwa sababu anaenda kwenye maombi na mikesha .
Usimuone ana kihelehele kwa sababu kila siku ameshika Biblia.
Usimuone mshamba kwa sababu anashuhudia injili na kila siku anasema Bwana YESU asifiwe.
Ndugu usimcheke huyo ndugu, huyo ni heri hakika.
Ni heri uungane naye na uwe kama yeye.

Mathayo 5:3-12 "Heri walio maskini wa roho; Maana ufalme wa mbinguni ni wao. Heri wenye huzuni; Maana hao watafarijika. Heri wenye upole; Maana hao watairithi nchi.
Heri wenye njaa na kiu ya haki; Maana hao watashibishwa.
Heri wenye rehema; Maana hao watapata rehema.
Heri wenye moyo safi; Maana hao watamwona MUNGU. Heri wapatanishi; Maana hao wataitwa wana wa MUNGU. Heri wenye kuudhiwa kwa ajili ya haki; Maana ufalme wa mbinguni ni wao.
Heri ninyi watakapowashutumu na kuwaudhi na kuwanenea kila neno baya kwa uongo, kwa ajili yangu. Furahini, na kushangilia; kwa kuwa thawabu yenu ni kubwa mbinguni; kwa maana ndivyo walivyowaudhi manabii waliokuwa kabla yenu."


Ndugu usikubali moyo wako ukudanganye hata umwache Mwokozi  YESU KRISTO.
Moyo wako unaweza ukakudanganya.
Moyo wako unaweza kutamani vitu ambavyo ni uharibifu ukivipata.
Moyo wako unaweza ukakushawishi kufanya mambo ambayo ni machukizo kwa MUNGU.
Ndugu unahitaji sana kuutiisha Moyo wako ili uendane na utakatifu.
Utiishe moyo wako kwa kuliweka kwa wingi sana moyoni Neno la MUNGU.
Tiisha Moyo wako kwa Neno la MUNGU.
Yeremia 17:9 "Moyo huwa mdanganyifu kuliko vitu vyote, una ugonjwa wa kufisha; nani awezaye kuujua?"

Ndugu unahitaji kuwa makini sana na moyo wako ili moyo huo usikupeleke pabaya.
Ndio maana Biblia inakujulisha kwamba unahitaji sana kuulinda moyo wako kuliko yote uyalindayo.
Mithali 4:23 "Linda moyo wako kuliko yote uyalindayo; Maana ndiko zitokako chemchemi za uzima."

Moyo wako unaweza kukushawishi ili umwache YESU, huko ni kujiangamiza.
Moyo wako unaweza ukakushawishi kuacha Ibada kanisani, huko ni kujipoteza.
Ndugu hakikisha unakuwa makini na moyo wako na usiuruhusu moyo wako ukufanye uwe mtenda dhambi.
Usikubali hata siku moja moyo wako utumiwe na shetani.
Ndugu pigana vita vya kiroho ukizuia shetani kuweka mawazo yake moyoni mwako.
2 Wakorintho 10:3-5 " Maana ingawa tunaenenda katika mwili, hatufanyi vita kwa jinsi ya mwili; (maana silaha za vita vyetu si za mwili, bali zina uwezo katika MUNGU hata kuangusha ngome;) tukiangusha mawazo na kila kitu kilichoinuka, kijiinuacho juu ya elimu ya MUNGU; na tukiteka nyara kila fikira ipate kumtii KRISTO;"

 
MUNGU akubariki kwa kujifunza somo hili muhimu pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane nitakujulisha jinsi ya kukipata.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa BWANA YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
0714252292.
0786719090
mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu.

Comments