MTEULE FANIKIWA KIMWILI KAMA UNAVYOFANIKIWA KIROHO.

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.

Bwana YESU atukuzwe ndugu zangu.
Karibuni sana tujifunze Neno la MUNGU.
3 Yohana 1-5 ''Mzee, kwa Gayo mpenzi, nimpendaye katika kweli.  Mpenzi naomba ufanikiwe katika mambo yote na kuwa na afya yako, kama vile roho yako ifanikiwavyo.  Maana nalifurahi mno walipokuja ndugu na kuishuhudia kweli yako, kama uendavyo katika kweli.  Sina furaha iliyo kuu kuliko hii, kusikia ya kwamba watoto wangu wanakwenda katika kweli. Mpenzi, kazi ile ni ya uaminifu uwatendeayo hao ndugu na hao wageni nao, '' 
Gayo ni mfano hai kwa kanisa juu ya kufanikiwa katika mambo yote kama vile roho zetu zinavyofanikiwa.
Mtume Paulo lazima kuna mafanikio ya upande mmoja aliyaona kwa  Gayo ndiyo maana akamwambia kwamba ''Mpenzi naomba ufanikiwe katika mambo yote na kuwa na afya yako, kama vile roho yako ifanikiwavyo''
Sio watu wote wamefanikiwa katika mambo yote.
Kuna wateule wamefanikiwa sana kiroho lakini sio kiuchumi.
Kuna wateule wamefanikiwa sana kihuduma lakini sio kuyashinda magonjwa.
Kuna wateule wamefanikiwa sana kiakili na hekima lakini sio katika kipato.
Je ni kusudi la MUNGU tuwe hivyo?
Jibu ni hapana maana MUNGU anataka tufanikiwe katika mambo yote kama vile roho zetu zifanikiwavyo. 
Wateule wa MUNGU wengi wamefanikiwa sana rohoni  lakini sio mwilini.
Watu wa ulimwengu wengi wamefanikiwa sana mwilini lakini sio rohoni.
Ninaposema rohoni maana yake kwenye mambo ya kiroho na ninaposema mwilini maana yake ni katika udhihilisho wa kile cha kiMUNGU ulichofanikiwa rohoni sasa ukione  na kukipata katika mwili.
Najua kuna wateule wengi tu wamefanikiwa katika mambo yote kama vile roho zao zinavyofanikiwa, lakini na wateule waliofanikiwa rohoni tu na sio mwilini nao wapo, hivyo tunahitaji kujifunza somo hili.
 
Kwa kuonyesha utofauti wa kufanikiwa kiroho au kimwili, Mfano ni huu, Ni rahisi kukuta tajiri maarufu anakabwa kila siku na majinamizi/Mashetani, hata halali usiku vizuri, hana amani japokuwa ana pesa nyingi sana, huyo kafanikiwa kimwili lakini sio rohoni.
Ikitokea mganga maarufu mfano Babu wa Loliondo anatibu ni rahisi sana kukuta matajiri zaidi wengi maana hao wamefanikiwa mwilini lakini sio rohoni.
Ikikitokea wakala wa shetani anatangaza kwamba ana uwezo wa kusafisha nyota, ni rahisi sana kuwapata waliofanikiwa kimwili wako huko.
Lakini sasa lipo kundi la watu pia waliofanikiwa kiroho lakini kimwili bado hawajafanikiwa, Baadhi ya hawa ni Wanakanisa.
Ni rahisi sana sana kumkuta Mchungaji amefanikiwa sana rohoni maana wachawi wanamuogopa, hakuna jini wa kumkaribia na wala hakuna mchawi anamsogolea lakini ajabu ni kwamba amefanikiwa rohoni tu lakini katika mambo ya kimwili hajafanikiwa maana ana madeni mengi na kushinda njaa kwa sababu chakula hakipo ni jambo la kawaida. Je huo ni mpango wa MUNGU?
Hapana, hakika sio mpango wa MUNGU.
Kusudi la MUNGU na maono ya MUNGU ni kwamba wateule wa KRISTO wote tufanikiwe kiroho na kimwili pia.
Inawezekana tu kuna pahali tunakosea kufuata kanuni za MUNGU za baraka.
Inawezekana tu hatujui kuyaunganisha mafanikio ya rohoni na ya mwilini.
Inawezekana tu hatujasimama kwa usahihi katika kusudi la MUNGU.
Inawezekana tu tumekalia kuwategemea wanadamu watuwezeshe wakati mwezeshaji wetu ni MUNGU.
Labda wengine wako kwenye majaribu ili wakivuka wabarikiwe, inanipa mtihani sana mimi maana natamani mimi na wewe mtumishi mwenzangu tufanikiwe katika mambo yote kama tunavyofanikiwa rohoni.
Inawezekana kabisa rohoni kila siku tunaangusha ngome za giza lakini kwanini mafanikio hayo ya rohoni yasiwe pia katika mambo ya mwili yaani tuangushe ngome za umasikini na magonjwa?
Ninaposema kufanikiwa mwilini sina maana ya kuwa matajiri wa mali  tu na pesa lakini nina maana ya kufanikiwa katika mambo yote kama roho zetu zinavyofanikiwa.

Luka 10:19 '' Tazama, nimewapa amri ya kukanyaga nyoka na nge, na nguvu zote za yule adui, wala hakuna kitu kitakachowadhuru.''
 Bwana YESU ametupa mamlaka ya Kukanyaga nyoka na ng'e yaani mamlaka ya kuzizimisha kila kazi za mawakala wa shetani, tuna mamlaka ya kumwingilia shetani wakati akifanya ubaya na ubaya huo ukasimishwa ili usifanye kazi, ndio maana ya kukanyaga nyoka na ng'e. Yaani wakuu wa giza wamerusha mishale yao ya magonjwa lakini kwa maombi sisi wakati mishale hiyo ikiwachoma watu tunaikataza na kuiondoa kwa watu, hiyo ni mamlaka kubwa sana.
Wewe Mteule wa KRISTO kwa imani unaweza ukauona wema wa MUNGU katika nchi ya walio hai.
Zaburi 27:13 '' Naamini ya kuwa nitauona wema wa BWANA Katika nchi ya walio hai.''
Wema wa MUNGU ni pamoja na kufanikiwa katika mambo yote kama vile roho yako inavyofanikiwa.
Mpango wa MUNGU kwa wateule wake ni kwamba tufanikiwe katika mambo yote kama roho zetu zinavyofanikiwa.
Sio kwenye ndoto tunamiliki nyumba na lakini kwenye mwili hatuna chumba hata kimoja.
Sio kwamba kwenye ndoto na maono tunaona tuna pesa lakini kwenye uhalisia hatuna hata pesa ya mboga.
Ndugu yangu, MUNGU atusaidie tufanikiwe katika mambo yote kama roho zetu zinavyofanikiwa.
Ulimwengu wa roho wa nuru una ufunguo wa Mteule wa KRISTO kufanikiwa katika mambo yote.
 Mathayo 16:19 '' Nami nitakupa wewe funguo za ufalme wa mbinguni; na lo lote utakalolifunga duniani, litakuwa limefungwa mbinguni; na lo lote utakalolifungua duniani, litakuwa limefunguliwa mbinguni.''

Inawezekana labda hutaki utajiri lakini naamini unatamani angalau siku zote uwe na pesa ya chakula ya kutosha familia yako.
Haiwezekanai mteule uwe na store ya madawa nyumbani kwako kwa sababu tu unajua muda wowote utaumwa au watoto wako au unaokaa nao wataumwa, aliyefanikiwa rohoni hatakiwi kuwa hivyo.
Inawezekana kabisa kila ukipokea mshahara huwa unatenga pesa fulani kila mwezi kwa ajili ya kuwapelekea hospitali familia yako kama wakiumwa, aliyefanikiwa rohoni hatakiwi kuwa na bajeti ya magonjwa.
Mpango wa MUNGU kwetu ni kwamba tufanikiwe katika mambo yote.

Kwa jinsi gani mteule wa MUNGU afanikiwe katika mambo yote kama vile roho yake ifanikiwavyo?

1. Awe mwaminifu kwa MUNGU katika utoaji wa zaka na sadaka.

Malaki 3:8-11 '' Je! Mwanadamu atamwibia MUNGU? Lakini ninyi mnaniibia mimi. Lakini ninyi mwasema, Tumekuibia kwa namna gani? Mmeniibia zaka na dhabihu. Ninyi mmelaaniwa kwa laana; maana mnaniibia mimi, naam, taifa hili lote. Leteni zaka kamili ghalani, ili kiwemo chakula katika nyumba yangu, mkanijaribu kwa njia hiyo, asema BWANA wa majeshi; mjue kama sitawafungulia madirisha ya mbinguni, na kuwamwagieni baraka, hata isiwepo nafasi ya kutosha, au la. Nami kwa ajili yenu nitamkemea yeye alaye, wala hataharibu mazao ya ardhi yenu; wala mzabibu wenu hautapukutisha matunda yake kabla ya wakati wake katika mashamba, asema BWANA wa majeshi.''

Unapoamua kufanyika Mteule wa MUNGU kupitia Wokovu wa YESU KRISTO hakika unakuwa umeingia katika Ufalme wa MUNGU, na jambo muhimu ukiingia katika ufalme wa MUNGU ni kufuata kanuni za Ki MUNGU za kufanikiwa katika kija jambo.

2. Kumcha MUNGU  kunakotengeneza maarifa ya ki MUNGU yanayoleta kufanikiwa katika mambo yote.

Mithali 1:7 '' Kumcha BWANA ni chanzo cha maarifa, Bali wapumbavu hudharau hekima na adabu.''

3. Omba ROHO MTAKATIFU akukutanishe na Neno lililotumwa na MUNGU ili likuponye na kukuondoa katika maangamizo yeyote ya shetani, yakiwemo maangamizo ya kiuchumi.

Zaburi 107:20 ''Hulituma neno lake, huwaponya, Huwatoa katika maangamizo yao.''

 4. Kuyajua kiroho kila majira na nyakati unazopitia ili ujue ufanyeje ili kufanikiwa na uombeje kwa MUNGU ili kufanikiwa.

Mhubiri 3:1 '' Kwa kila jambo kuna majira yake, Na wakati kwa kila kusudi chini ya mbingu.''

Majira na nyakati unaweza ukayajua kwa kuona kwa macho au kwa kufunuliwa na ROHO MTAKATIFU kupitia maombi yako.
Unaweza ukapata msukumo wa kufungua Biashara fulani kumbe hapo unajulishwa kwamba hayo ni majira ya kufanya hivyo na utafanikiwa.
Unaweza ukaona kwenye ndoto kwamba unapata pesa nyingi kumbe maana ya ndoto hiyo ni kwamba kuna fursa za kiuchumi kwako wakati huo hivyo fanyia kazi.
Nimeshawahi kuandaa somo la KUOMBEA MAJIRA NA NYAKATI unaweza ukali-search huku ukiandika mbele ya somo jina langu na utaliona somo hilo ili ujue zaidi kuhusu majira na nyakati.
Ndugu yangu  katika KRISTO YESU Mwokozi naomba MUNGU akupe kufanikiwa katika mambo yote kama vile roho yako inavyofanikiwa.
 Nisamehe sana kama kuna pahali ndani ya ujumbe huu nimekukwaza, najisikia kusema Neno hilo.

MUNGU akubariki kwa kujifunza somo hili muhimu pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane nitakujulisha jinsi ya kukipata.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa BWANA YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
0714252292.
0786719090
mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu.


Comments