FANYIA KAZI WAZO LA MUNGU

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU

Bwana YESU atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.
Neno ''Wazo" ni mpango,pendekezo au picha inayoingia moyoni mwa mtu kama ramani ya kufanya jambo fulani na kufanikiwa.
Wewe huwa unafanyia kazi wazo la nani?
Kuna makundi manne(4) ya mawazo yanayoweza kuingia moyoni mwako.
1. Wazo kutoka kwa MUNGU.
Yeremia 29:11-13 '' Maana nayajua MAWAZO ninayowawazia ninyi, asema BWANA, ni mawazo ya amani wala si ya mabaya, kuwapa ninyi tumaini siku zenu za mwisho. Nanyi mtaniita, mtakwenda na kuniomba, nami nitawasikiliza. Nanyi mtanitafuta na kuniona, mtakaponitafuta kwa moyo wenu wote.''
 Wazo kutoka kwa MUNGU ndilo  ndilo wazo pekee lilikamilika na linalokuwazia mema ya kukusaidia.
 
2. Wazo kutoka kwa shetani.

2 Kor 4:4 ''ambao ndani yao mungu wa dunia hii amepofusha fikira zao wasioamini, isiwazukie nuru ya injili ya utukufu wake KRISTO aliye sura yake MUNGU.''
Hakuna wazo zuri hata moja kwako linalotoka kwa shetani.
Shetani anaweza kumletea mtu wazo ambalo mtu huyo akilifanyia kazi linaweza kumpofua fikra zake hata asimpendeze MUNGU.

3. Wazo kutoka kwa mtu likiwa baya.

 Zaburi 41:7 '' Wote wanaonichukia wananinong'ona, Wananiwazia mabaya.''
 Watu unaoongea nao, kuonana nao, kufanya kazi nao mara nyingine unaweza ukafanyia kazi mawazo yao lakini yakawa ni mawazo ya kukuletea madhara makubwa.
Watu wengi sana hawamchi MUNGU na ndio maana watu hao wamejaa mawazo mabaya, ukifanyia kazi ni kwa uangamivu wako.
Mtu anaweza kukushauri ili ufanyie kazi wazo lake, lakini kwa sababu mtu huyo anakuchukia na kukuwazia mabaya basi atafanya kila mbinu uingie katika mtego wake mbaya.
 
4. Wazi kutoka kwa mtu likiwa ni wazo zuri.
 Mithali 21:5 ''Mawazo ya wenye bidii huuelekea utajiri tu; Bali kila mwenye pupa huuelekea uhitaji.''

 Wazo zuri kutoka kwa wanadamu linawahusu tu watu wanaokuwazia mema.
Hawa wanaweza kuwa ni watumishi wa MUNGU wenye hofu ya MUNGU, wazazi au ndugu wenye Hofu ya MUNGU, Mke au Mume anayemcha MUNGU na hata marafiki lakini tu wawe wana hofu ya MUNGU.
Kwa sababu ni wanadamu basi tambua kwamba wakati mwingine wanadamu hubadilika hivyo usiwawekee sana tumaini kama wako mbali na Utauwa yaani ucha MUNGU.
 Mika 7:5-7 '' Msimwamini rafiki, msimwekee kiongozi tumaini; ilinde milango ya midomo ya kinywa chako ili mkeo alalaye kifuani mwako asijue habari.  Kwa maana mwana humwaibisha babaye, na binti huondoka ashindane na mamaye; na mwanamke aliyeolewa hushindana na mavyaaye; adui za mtu ni watu wa nyumbani mwake mwenyewe. Lakini mimi, nitamtazamia BWANA; nitamngojea MUNGU wa wokovu wangu; MUNGU wangu atanisikia.   ''
Kuna mawazo mema ambayo ni mawazo kutoka kwa MUNGU Na mengine kutoka kwa watu, Lakini ni heri wazo la mwanadamu hata kama ni mwema, lipime wazo hilo ndani ya Neno la MUNGU.
1 Yohana 4:1 ''Wapenzi, msiiamini kila roho, bali zijaribuni hizo roho, kwamba zimetokana na MUNGU; kwa sababu manabii wa uongo wengi wametokea duniani.''
Ninatambua kabisa kila jambo huanza na wazo ndani ya moyo ndipo utende jambo hilo lililotokana na wazi.
Wengi sana wamefanyia kazi wazo la kipepo na ndio maana wamepishana na mbingu.
Hata kuna dini chanzo chake ni wazo la kishetani ndio maana wako kinyume na injili ya YESU KRISTO.
Wazo lina nguvu sana na ndilo hupelekea maamuzi ya vitendo kwa mhusika lakini ni lazima sana upime wazo lako au unaloambiwa maana hata kuna watu wamefanyia kazi wazo la majini ndio maana wanateswa na vifungo vya giza kila leo.
Kama ndani yako liko wazi la ki MUNGU hakika wazo hilo la ki MUNGU lifanyie kazi, wazo la ki MUNGU huletwa na ROHO MTAKATIFU na kusimamiwa na yeye kwa Neno la MUNGU.
Waefeso 3:20 '' Basi atukuzwe yeye awezaye kufanya mambo ya ajabu mno kuliko yote tuyaombayo au tuyawazayo, kwa kadiri ya nguvu itendayo kazi ndani yetu;''
 
Kuna mawazo mabaya ambayo ni kutoka kwa shetani na mengine kutoka kwa watu, uwe makini sana na mawazo mabaya.

Mwanzo 6:5 ''BWANA akaona ya kuwa maovu ya mwanadamu ni makubwa duniani na kwamba kila kusudi analowaza moyoni mwake ni baya tu sikuzote.''
Kuna watu wamefanyia kazi wazo la kishetani na wakajikuta wameenda kwa waganga wa kienyeji, badala ya kupungua vifungo vya giza ndio vimeongezeka sana vifungo hivyo na hali imekuwa mbaya kuliko mwanzo.
Kuna watu walipoonekana wana sauti nzuri ya kuimba basi walishauriwa na watu wawe waimbaji wa nyimbo za kidunia na jambo hilo likawafanya kuwa mbali na MUNGU Muumba wao.
Ndugu hakiki kwa Neno la MUNGU hilo wazo unalopewa na watu.
Dada mmoja alinipigia simu siku moja akiniambia kwamba yeye ni mwanafunzi wa chuo kikuu na amekuwa kwenye mahusiano ya kimapenzi kisha amepata mimba, lakini yule mwanaume amemwacha na kuvunja uhusiano. Yule dada akasema kwamba kwao wazazi wake wamemsomesha kwa tabu sana na wameuza ng'ombe wote ili asome, hivyo kwa sababu ya mimba sasa anataka kuitoa na marafiki zake wote chuoni wamemwambia aitoe tu maana hakuna jinsi. Alipotaka kuitoa alijikuta kwa bahati amefungua facebook muda mfupi kabla hajaenda kuitoa hiyo mimba. Alipoingia facebook alikutana na somo langu likikemea utoaji mimba. Alijikuta analia sana na kuamua anitafute akidhani kwamba labda mimi kwa sababu ya hali yake na hali ya wazazi wake kijijini basi nitamwambia kwamba atoe tu kisha atubu. Alipiga simu na kunieleza, wakati ananielezea yaliyomsibu mimi nilikua naona kwenye ulimwengu wa roho kwamba mtoto atakayezaliwa ndiye atamsaidia huyo dada uzeeni kipindi ambacho anaowategemea hawatakuwa na msaada kwake. Nilimwambia maneno magumu sana sana yule Dada na kumuongoza sala ya toba kwa sababu ya uasherati na mawazo mabaya ya kuua mtoto asiye na hatia, na akajikuta anaapa kwamba hatatoa mimba ile, ni kweli hakutoa na alipotaka kujifungua alinijulisha nimuombee, baada ya kujifungua alinitumia picha ya mtoto wake na hata sasa anaendelea vyema yeye na mtoto wake. Neema ya MUNGU dada baada ya kuzaa alikaa mwaka akaja kuendelea na masomo na kumaliza salama.
 Kijana au binti kama huna msingi imara wa kiroho utaliabisha kanisa la MUNGU kila Mara.
Msingi mkuu wa kiroho ni kulitii Neno la MUNGU hivyo ni wajibu wako sasa kulitii Neno la MUNGU siku zote ili usiwe aibu kwa kundi la MUNGU.

Ukiona mtu anamwacha YESU kwa ajili ya mambo ya kidunia ujue kwamba huyo ndugu hakuwa na msingi imara wa Neno la MUNGU.
Ukiona kijana anadanganywa danganywa kwa vizawadi na chipsi mayai ili ausaliti wokovu ujue kijana huyo hakuna na msingi imara katika Neno la KRISTO.

Ndugu hakikisha huwi mtu wa kuliabisha kanisa la MUNGU Bali liletee heshima kanisa kwa wewe kumcha MUNGU na kumtii katika njia zako zote.

Ndugu, Mawazo kutoka kwa watu au kwa mtu Binafsi yapo katika kundi la mema na kundi la mabaya , uwe makini sana

1 Wafalme 8:18 '' Lakini BWANA akamwambia Daudi baba yangu, Kwa kuwa ilikuwa moyoni mwako kujenga nyumba kwa jina langu, ulifanya vema kuwaza hivi moyoni mwako.''
 
Muhimu kujua kuhusu Mawazo.
1. Upo hapo kwa sababu ya ulivyowaza.
2. Usiridhike na hali yako ya sasa ambayo imetokana na kuwaza kwako.
3. Tafuta wazo la MUNGU kwenye Biblia ili utembee katika hilo.
4. Yapime kwa Neno la MUNGU mawazo yote yanayokujia.


Mimi sijui ndugu yangu wewe huwa unafanyia kazi wazo la nani.
Mimi nakushauri fanyia kazi wazo la MUNGU.
Wazo la MUNGU ni Neno la MUNGU.
Wazo la MUNGU analo ROHO MTAKATIFU, Msikilize yeye na kumtii ndipo utakuwa umefanyia kazi wazo la MUNGU.
Fanyia kazi pia mawazo ya watu mema lakini uyachunguze mawazo hayo kwa kuyapima katika Neno la MUNGU ili yasiwe mawazo yanayokupeleka katika dhambi na yanayokupeleka katika vifungo vya kipepo.
Unahitaji kuwa na muda wa kuomba juu ya mawazo maana ni muhimu sana.

Zaburi 94:11 ''BWANA anajua mawazo ya mwanadamu, Ya kuwa ni ubatili.''
Katika maombi yako leo.
1. Futa mawazo mabaya wanayokuwazia kwa hila watu wabaya au mawakala wa shetani.
Zaburi 10:2 ''
Kwa kiburi chake asiye haki mnyonge anafuatiwa kwa ukali; Na wanaswe kwa hila zizo hizo walizoziwaza.''
Wao ndio wanaswe na hila wanazoziwaza.


2. Futa mawazo mabaya uliyojiwazia wewe na kujipangia wewe
Mwanzo 6:5 ''
BWANA akaona ya kuwa maovu ya mwanadamu ni makubwa duniani na kwamba kila kusudi analowaza moyoni mwake ni baya tu sikuzote.''
 
3. Ombea kuwaza mema
Isaya 32:8 ''
Bali mwungwana huwaza mambo ya kiungwana, naye hushika sana mambo ya kiungwana. ''
 
4. Ombea wazo la MUNGU litimie juu ya maisha yako.
Nahumu 1:9 ''
Mnawaza nini juu ya BWANA? Yeye atakomesha kabisa; mateso hayatainuka mara ya pili. ''
 
5. Omba MUNGU akupe kuwaza yaliyo yake.
 Zaburi 19:13-14 ''
Umzuie mtumishi wako asitende mambo ya kiburi, Yasinitawale mimi. Ndipo nitakapokuwa kamili, Nami nitakuwa safi, sina kosa lililo kubwa. Maneno ya kinywa changu, Na mawazo ya moyo wangu, Yapate kibali mbele zako, Ee BWANA, Mwamba wangu, na mwokozi wangu. ''

Natamani niseme mengi mno lakini naamini mwenye kuelewa ameelewa.
MUNGU akubariki kwa kujifunza somo hili muhimu pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane nitakujulisha jinsi ya kukipata.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa BWANA YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
0714252292.
0786719090
mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu

Comments