MAOMBI YA KUIFUTA RATIBA YA KISHETANI ULIYOTENGENEZEWA WEWE.

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.
Bwana YESU atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze kisha tuombe maombi ya ushindi mkuu.
Matatizo mengi waliyonayo baadhi ya watu huanza kabla hawajazaliwa.
Yaani kabla hajazaliwa shetani alishamfunga na kumcholea ramani ya kipepo yenye kalenda ya kipepo ili apite katika maisha yake yote.

Matendo 3:2 ''Na mtu mmoja aliyekuwa kiwete toka tumboni mwa mamaye alichukuliwa na watu, ambaye walimweka kila siku katika mlango wa hekalu uitwao Mzuri, ili aombe sadaka kwa watu waingiao ndani ya hekalu.'' 
Huu ni mfano hai juu ya mtu kuwa amepangiwa kuishi katika hali fulani mbaya katika maisha yake.
Biblia inasema '' alikuwa kiwete tangu tumboni mwa mamaye''
Sio viwete wote ni mpango wa MUNGU wawe viwete na sio viweto wote wamerogwa ili wawe viwete, lakini waliofanywa viwete na wachawi wapo na ni wengi tu.
Kiwete maana yake ni mtu aliyelemaa miguu yote miwili, hawezi kutembea.
Huyo ndugu katika andiko aliombewa kwa Jina la YESU KRISTO na kupona na akarudi katika hali ya uumbaji wa MUNGU.
Hata leo wapo watu wengi tu hutengenezewa na kuamuliwa kipepo jinsi wanavyotakiwa kuishi.
Wapo watu leo ni waganga wa kienyeji kwa sababu tangu walipozaliwa walikulia katika mazingira ya kiganga tu na hadi na wao wakawa waganga, ni mbaya sana.
Mawakala wa shetani wanaweza kukupangia kabisa maisha ya kuishi yaliyo na maumivu ndani yake, majanga na balaa nyingi ndani yake.
Leo jiondoe katika ratiba ya kipepo waliyoitengeneza wachawi ili wewe uiishi.
Wapo watu wala hawakuzaliwa na matatizo lakini kwa hila za watu wabaya wamejikuta katika matatizo makubwa.
Binti mmoja siku moja alikuwa ananisimulia kwa njia ya simu jambo la ajabu sana. Wazazi wake walikosana na jirani mmoja na yule jirani akasema atawakomesha. Hata wiki haikupita yule dada siku moja anatoka shuleni, alipofika nyumbani tu alidondoka na kupalalaizi na kwa miaka zaidi ya saba hawezi kutembea wala hata kujigeuza tu hawezi. anajisaidia hapo hapo alipo na kwa muda wote huo chakula hadi alishwe. Yaani anahudumiwa kama mtoto mchanga asiyeweza lolote wakati alikuwa mzima na hakuwahi kuwa na tatizo lolote. Yule jirani baada ya kuikomesha familia ile akama na mji, ni hatari sana kama huna YESU.
Zaburi 69:1-4 '' Ee MUNGU, uniokoe, Maana maji yamefika mpaka nafsini mwangu. Ninazama katika matope mengi, Pasipowezekana kusimama. Nimefika penye maji ya vilindi, Mkondo wa maji unanigharikisha. Nimechoka kwa kulia kwangu, Koo yangu imekauka. Macho yangu yamedhoofu Kwa kumngoja MUNGU wangu. Wanaonichukia bure ni wengi Kuliko nywele za kichwa changu. Watakao kunikatilia mbali wamekuwa hodari, Adui zangu kwa sababu isiyo kweli. Hata mimi nalilipishwa kwa nguvu Vitu nisivyovichukua.''

Kuna watu wana roho kama wanyama, kuna watu ni mawakala wa shetani na hao hawaoni tatizo kumzuri mtu.
Siku za karibuni niliona kwenye maono kuna mwanamke mmoja alikuwa katika mahusiano ya kimapenzi na mwanaume fulani. Baadae wakaachana na kila mmoja akaendelea na maisha yake. Aliyeumia katika kuachana kwao ni Mwanamume hivyo kwa sababu alikuwa na picha za mpenzi wake huyo wa zamani basi alichukua picha ya yule mwanamke na kuipeleka kwa mganga wa kienyeji ili kumfunga yule mwanamke asiolewe na hata ikitokea akaolewa basi asizae.
Niliona picha ile ya yule Binti akiwa ameishika mganga huku akiitamkia maneno ya laana na vifungo.

Ndugu zangu, Wapo watu wengi wanateswa na vifungo vya aina nyingi sana.
Kama wachawi wamekupangia ratiba kwamba hutaolewa/hutaoa wewe leo ifute ratiba hiyo kwa jina la YESU KRISTO.
Kama wakuu wa giza wamekupangia ratiba kwamba wewe hautazaa au hautapata kazi hata ufanyeje, leo kata rufaa mbinguni kwa maombi ya kufuta ratiba ya kipepo waliyokucholea.
Kama kuna mtu amekuendea kwa mganga ili ndoa yako ivunjike au ili ufukuzwe kazi, leo kataa kwa jina la YESU KRISTO na simama imara ukiharibu ratiba yao ya kipepo.
Unahitaji kuwa muombaji sana na hakikisha unaharibu kila maagano ya kipepo na kila madhabahu za kipepo zilizokufunga.
Watu wanaweza wakakufunga hata kwa kutumia tu picha mlizopiga zamani.

Unaweza ukaishi na watu na unaweza ukamwamini mtu aliye rafiki yako sana na kumbe huyo ni wakala wa shetani ili kukuharibia.
Unahitaji sana kuwa na urafiki na wateule wa KRISTO wanaoiishi kweli ya MUNGU.
Kumbuka adui yako anaweza kabisa wakati mwingine akawa ni yule wa karibu yako au uliywahi kuishi naye.
Mathayo 10:36 '' na adui za mtu ni wale wa nyumbani mwake.''
Ndugu hakikisha unaharibu kila mpango wa kishetani kukuhusu.

Kama kuna mtu alikuendea kwa waganga hakikisha unamkimbilia Bwana YESU ili ukae salama.
Kwenye maombi hayo hakikisha kwa jina la YESU KRISTO unamshambulia kuanzia mganga, aliyeenda kwa mganga na kisha kiharibu kifungo hicho walichokufunga.
Lakini pia utakatifu katika Wokovu wa KRISTO ni jambo la muhimu sana kwako ili shetani asikufunge tena.
Wakati mwingine omba maombi magumu kwa ajili ya wachawi waliokuonea kwa miaka mingi na wanajidai.
Usiombe tu kwamba washindwe bali omba maombi yanayofuta uchawi wao.
Musa aliomba maadui zake wafe, tena wafe kifo ambacho sio cha kawaida, na MUNGU alitenda sawasawa na maombi ya Musa mtumishi wake.
Hesabu 16:28-35 '' Musa akasema, Kwa jambo hili mtajua ya kwamba BWANA amenituma, ili nifanye kazi hizi zote; kwa kuwa mimi sikuzifanya kwa akili zangu mwenyewe. Kama watu hawa wakifa kifo cha sikuzote, kama watu wote wafavyo, au kama wakipatilizwa kwa mapatilizo ya watu wote; hapo basi BWANA hakunituma mimi. Lakini BWANA akiumba kitu kipya, na hiyo nchi ikifunua kinywa chake na kuwameza, pamoja na wote walio nao, nao washukia shimoni wali hai; ndipo mtatambua ya kwamba watu hawa wamemdharau BWANA. Basi ilikuwa, hapo alipokwisha kusema maneno haya yote, nchi iliyokuwa chini yao ikapasuka; nchi ikafunua kinywa chake, na kuwameza, na watu wa nyumba zao na wote walioshikamana na Kora, na vyombo vyao vyote. Basi wao, na wote waliokuwa nao, wakashukia shimoni wali hai; nayo nchi ikawafunika wakaangamia kutoka mle mkutanoni. Nao Israeli wote waliokuwa kando-kando yao wakakimbia kwa ajili ya kilio chao; kwa kuwa walisema, Nchi isije kutumeza na sisi. Kisha moto ukatoka kwa BWANA, ukawateketeza hao watu mia mbili hamsini waliofukiza uvumba.''


Watu wengi huwahurumia wachawi wanaowatesa.
Ndugu, nakuomba wakizidi sana omba maombi magumu, usiende kimwili na wala usifanye vita ya kimwili bali vita ya kiroho.
Ukienda kimwili watakuua bali Nenda kiroho kwa maombi hakika mamlaka ya KRISTO iliyo ndani yako itawaangamiza maadui hao.
Ukiwaruhusu wachawi na waganga waendelee kukufunga kiroho na kukuroga hakika utateseka sana.
Ndugu, Wakati mwingine omba maombi magumu na sio kusema tu washindwe.
Biblia inasema kwamba MUNGU hawahitaji wachawi bali atawahukumu.
Mlakai 3:5 ''Nami nitawakaribieni ili kuhukumu; nami nitakuwa shahidi mwepesi juu ya wachawi, na juu ya wazinzi, na juu yao waapao kwa uongo; na juu yao wamwoneao mwenye kuajiriwa, kwa ajili ya mshahara wake, wamwoneao mjane na yatima, na kumpotosha mgeni asipate haki yake, wala hawaniogopi mimi, asema BWANA wa majeshi. ''


Kama uliomba maombi wakapunguza tu kukutesa lakini baadae waliendelea kukutesa sasa omba maombi magumu na MUNGU naweza kuwaondoa kabisa kwenye maisha yako.
Omba ndugu na sio vinginevyo.

Kutoka 14:13-14 '' Musa akawaambia watu, Msiogope, simameni tu, mkauone wokovu wa BWANA atakaowafanyia leo; kwa maana hao Wamisri mliowaona leo hamtawaona tena milele. BWANA atawapigania ninyi, nanyi mtanyamaza kimya.''

Omba na utashinda ndugu.
Lakini pia kumbuka kuishi maisha matakatifu maana maisha ya dhambi ni mlango wa maadui hao kukutesa, nakuomba usiwaruhusu wapate nafasi katika maisha yako.
Katika maombi zingatia haya.
1. Likatae kwanza jambo baya ambalo linakusibu ndipo umwambie MUNGU akuondoleee.
Mwambie MUNGU aliondoe jambo hilo baada ya wewe kulikataa ndipo litaondoka.
Kama unataka ugonjwa upone kwanza ukatae wewe ndipo umwambie MUNGU akuondolee.
Kama unateswa na maroho Fulani ya kipepo, yakatae kwanza wewe hayo ndipo umwambie MUNGU akuondolee.
Kuna watu huomba sana MUNGU awaondolee mabalaa Fulani maishani mwao lakini katika hali halisi mioyo yao wala haijakubali kuyakataa hayo japokuwa kwenye maombi kila siku huomba MUNGU awaondolee.
Ni ngumu mno kufunguliwa katika kitu ambacho wewe hutaki kufunguliwa.


2. Maombi ya muda mrefu yakakufanya uwe na hadhi katika ulimwengu wa roho, yaombe hayo itakusadia.

3. ROHO MTAKATIFU hawezi kuongea ndani yako kama wewe sio mtu wa maombi.

4. Maombi ya muda mrefu yanafunga vivywa vya wachawi.
Yaombe hayo siku zote ili wachawi wasipate hata dakika moja ya kukufanyia uchawi wao.


Yoshua 23:10 "Mtu mmoja miongoni mwenu atafukuza watu elfu; maana BWANA, Mungu wenu, ndiye anayewapigania, kama alivyowaambia."

Kumbe wewe una mamlaka ya kuwafukuzwa wachawi 1000 wanaofatilia maisha yako.
Kumbe mapepo wabaya wote wanaweza kukukimbia wewe kwa muda mfupi sana maana Bwana YESU amekupa mamalaka kuu.
Hebu Leo fukuza kila adui yako kwa maombi.

Wakati mwingine shetani anaweza kushindwa kabisa kukuzuia kupata baraka fulani maishani mwako lakini anaweza kukuchelewesha, hivyo futa ratiba ya kipepo ya kukuchelewesha kupata baraka yako.
Nani na wa wapi amekupangia ratiba ya kipepo ili utembee kwenye ratiba hiyo?
Kama wamekupangia ajali leo kataa, kama wamekupangia kufilisika leo kataa kwa jina la YESU KRISTO.
Kataa leo kwa damu ya YESU KRISTO.
Haiwezekani kila tatizo liwe lako, haiwezekani kila mara kuumwa ni wewe tu, haiwezekani ndoa yako tu ndio haina amani, leo futa ratiba ya kipepo waliyokupangia kipepo.
Kumbuka MUNGU huifuta mipango ya wabaya wako kama ukiamua Kumuomba Yeye Muumba wako.
Ayubu 5:12 '' Yeye(MUNGU) huyatangua mashauri ya wadanganyifu, Mikono yao isipate kuyatimiza makusudi yao.'


Natamani niseme mengi mno lakini naamini mwenye kuelewa ameelewa.
MUNGU akubariki kwa kujifunza somo hili muhimu pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane na nitakujulisha jinsi ya kukipata
na  Naamini kitakusaidia sana.
Hapa chini ni  MAOMBI YA KUIFUTA RATIBA YA KISHETANI ULIYOTENGENEZEWA  WEWE.
Maombi haya naomba yamsaidie mtu yule ambaye hajui kuomba ili katika kuomba kwa kutumia hayo basi atakumbuka mahitaji yake na kuyataja katika maombi yake.
Kwa waombaji wazoefu naamini baada tu ya kulisoma somo na kulielewa basi anajua aombee nini maana alikuwa anaandika points za kuombea.

 

MAOMBI YA KUIFUTA RATIBA YA KISHETANI ULIYOTENGENEZEWA  WEWE.

 BABA yetu wa mbinguni, MUNGU Muumbaji wangu ninakuabudu na  ninaungana na malaika mbinguni kukuabudu maana peke yako JEHOVAH unastahili.
Nakushukuru kwa uzima ulionipa na ninakushukuru kwa nafasi hii uliyonipa ili niombe mbele zako BWANA wa majeshi.
Naomba msamaha katika jambo lolote ambalo nimekosea mbele zako MUNGU wangu, naomba damu ya Agano ya YESU KRISTO Mwokozi wangu initakase na kunifutia mashtaka yote kwenye ulimwengu wa roho kunihusu mimi. Naomba damu ya Bwana YESU KRISTO iyafute maagano ya kipepo yote yaliyowekwa na mawakala wa shetani ili yanikamate mimi, sasa kwa jina la YESU KRISTO maagano hayo ya giza yanafutika.
ratiba ya kishetani ambayo iliandaliwa kwa ajili yangu kipindi sijazaliwa ninaifuta ratiba hiyo kwa damu ya YESU KRISTO na kwa jina la YESU KRISTO.
Kama mizimu walinichagua mimi ili kufanya kazi yao, leo nawaharibu hao mizimu na kuwaangamiza kwa jina la YESU KRISTO.
Ratiba yao ya kipepo naifuta kwa damu ya YESU KRISTO aliye hai.
Kila ratiba ya kichawi ya kunifanya niwe mtu wa kuchanganyikiwa na kushindwa kuamua vyema, ratiba hiyo ya kipepo naifuta sasa kwa damu ya YESU KRISTO na kwa jina la YESU KRISTO.
Ratiba ya kuumwa kila mara,  ratiba hiyo ya kipepo naifuta sasa kwa damu ya YESU KRISTO na kwa jina la YESU KRISTO.
Ratiba ya kufukuzwa kazini kila nikipata kazi, ratiba hiyo ya kipepo naifuta sasa kwa damu ya YESU KRISTO na kwa jina la YESU KRISTO.
Ratiba ya kutokupata mchumba sahihi ili nifunge ndoa takatifu, ratiba hiyo ya kipepo naifuta sasa kwa damu ya YESU KRISTO na kwa jina la YESU KRISTO.
Ratiba ya kufiwa na ndugu kila mwaka, ratiba hiyo ya kipepo naifuta sasa kwa damu ya YESU KRISTO na kwa jina la YESU KRISTO.
Ratiba ya kuuonewa na majini kila siku nikiwa nimelala, ratiba hiyo ya kipepo naifuta sasa kwa damu ya YESU KRISTO na kwa jina la YESU KRISTO.
Ratiba ya kufilisika, atiba hiyo ya kipepo naifuta sasa kwa damu ya YESU KRISTO na kwa jina la YESU KRISTO.
Ratiba ya kuteswa na roho za hofu na woga, ratiba hiyo ya kipepo naifuta sasa kwa damu ya YESU KRISTO na kwa jina la YESU KRISTO.
Kila ratiba ya kishetani leo naifuta kwa jina la YESU KRISTO.
Sasa kila mwakala wa shetani aliyenipangia kuumwa, naamuru kwa jina la YESU KRISTO aumwe yeye. 
Kila aliyenipangia kupata ajali mwaka huu, ajali hiyo impate yeye kwa jina la YESU KRISTO.
Kila aliyenipangia ratiba ya kufukuzwa kazi mwaka huu, naamuru kwa mamlaka ya jina la YESU KTISTO afukuzwe kazi yeye tena kwa aibu kubwa.
kila wakala wa shetani aliyenipangia ratiba yake naamurru kwa mamlaka ya jina la YESU KRISTO mabaya na yampate yeye na sio mimi.
Naomba sasa damu ya YESU KRISTO inizingire pande zote.
Naomba ROHO MTAKATIFU wa MUNGU kwa neema yako naomba unijulishe na kunionyesha kila mipango ya kipepo na unifundishe ili nisitembee katika ratiba ya giza bali nitembee katika Neno la MUNGU la uzima.
Nakushuru MUNGU Baba maana kwa neema yako leo kila ratiba waliyonipangia watumishi wa shetani imefutika na haitanipata kamwe.
Ninakushuru MUNGU Baba maana Neema ya Bwana wangu YESU KRISTO itanifunika siku zote.
Katika jina la YESU KRISTO nimeomba na kushukuru.
Amen Amen Amen.

Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa BWANA YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
0714252292.
0786719090
mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu.

Comments