Najisikia rohoni kukubariki kwa ujumbe huu.

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.
Bwana YESU atukuzwe ndugu yangu mpendwa sana!
MUNGU akubariki sana rafiki yangu na hongera kwa ajili ya baraka za kuishi mwezi wa kumi.
Najisikia rohoni kukubariki kwa ujumbe huu.
Nakushukuru sana wewe ambaye umekuwa ukijifunza Neno la MUNGU mahali hapa.
Namshukuru MUNGU maana nilijiwekea utaratibu kwa kuandaa masomo 17 mazima kwa Mwezi na kwa mwaka huu nifundishe masomo 204. Kwa Miezi yote tangu January ni miezi miwili tu ambayo sikutimiza masomo 17 kwa mwezi ukiwemo na mwezi uliopita ambao hadi unafika mwisho nilikuwa sijamalizia somo moja, lakini pia kuna mwezi nilivuka masomo 4 zaidi.
Changamoto yangu ni muda wa kuandika lakini masomo ni mengi mno ajabu. Kuna masomo zaidi ya 90 ambayo nimeyaandaa nusu kwa sababu ya muda. Nilichojifunza ni kwamba ROHO MTAKATIFU anazo hazina nyingi kiasi kwamba hata ukipewa kuhubiri miaka 100 kila siku huwezi kuzimaliza. Ndio maana Biblia inasema wanahitajika zaidi watenda kazi katika shamba la Bwana YESU '' Akawaambia, Mavuno ni mengi, lakini watenda kazi ni wachache; basi mwombeni BWANA wa mavuno apeleke watenda kazi katika mavuno yake.Luka 10:2''
Shamba la MUNGU ni mioyo ya wanadamu inayopandwa Neno la MUNGU na mavuno ni watu wale wanaoamua kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi na kuanza kuishi maisha matakatifu yanayoagizwa na Biblia takatifu.
Ukisikia msukumo wa kumtumikia Bwana YESU nakushauri anza mara moja na utashangaa ROHO MTAKATIFU atakavyo kupa ujumbe kwa Kanisa lake.

Siku moja miezi kama mitatu imepita nikiwa natoka Kanisani nilipitia sehemu fulani kununua kitu fulani na kisha nikaondoka kumbe nimeisahau notebook yangu kubwa yenye masomo.
Nilipofika nyumbani nikataka nianze kuandika somo fulani lakini notebook niliikosa. Niliwaza mno nilikoiacha ni wapi. nilijikuta namwambia ROHO wa MUNGU anisaidie maana masomo yale hata siwezi kuyapata popote maana sijawahi kumsikia mtu akifundisha ili hata nimfuate anielekeze. Niliyapata masomo yale kama ufunuo na hakika ilinichanganya na nikaanza kumkumbusha MUNGU kwamba itakuwaje au atanipa ufunuo kwa mara ya pili juu ya masomo yale. Nikaamua kuanza kufutilia kila sehemu niliyopita maana sikujua nimeacha wapi. Lakini nilipokaribia tu pale kwenye watu wengi nilipoacha hiyo notebook yangu dada mmoja akaanza kuwaelekeza wenzake kwamba mwenye mambo haya ya muhimu ni huyu kaka anaekuja. Akanipa Notebook yangu na nikamshukuru sana. Nilikuta wamekaa kikao wakijadili na kukagua kwamba huo mzigo utakuwa wa nani?
Namshukuru MUNGU maana niliupata na hakuna kilichopungua.

Kwanini namshukuru MUNGU leo na nakushukuru na wewe?
Ni kwasababu MUNGU ndiye Alfa na Omega kwangu.
Na kwa sababu wewe ni mtu muhimu sana maana unajifunza ujumbe ambao MUNGU amenipa. Wengi sana hunitia moyo sana kwa sms na wengi sana hunibariki kwa kunijulisha juu ya masomo waliyosoma.
Nimekuwa namshangaa tu MUNGU maana Neno lake li hai siku zote. Ukimuuliza Mtu aliyebarikiwa na somo unashangaa anapokutajia somo ambalo ulifundisha 2013 na hata ukasau, yeye analisoma kama somo la leo na anamshukuru MUNGU kwa ajili yako.
Ndugu nakushuru sana na uliye muombaji endelea na maombi ili MUNGU atupe nafasi zaidi ya kujifunza.
Nilichomshangaa pia MUNGU ni jinsi MUNGU alivyotumia watu mbalimbali ambao hata hatujawahi kuonana, MUNGU amewatumia kwa mambo mengi na kwa ushauri na wengine ROHO wa MUNGU aliwasemesha kabisa kuhusu mimi katika kunisaidia na kunijulisha.
Niseme tu MUNGU akubariki sana na hakikisha unamtumikia Bwana YESU katika siku zote za maisha yako.

Nakutakia mwezi wa kuwaponda mawakala wa shetani kwa maombi yako ili wajue kwamba wewe sio wa hivi hivi.
Zaburi 2:9 '' Utawaponda kwa fimbo ya chuma, Na kuwavunja kama chombo cha mfinyanzi. ''

MUNGU akubariki sana sana.

Comments