UKITAKA KUSHINDA MJUE KWANZA ADUI YAKO.

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.

 Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu yangu.
Natamani kila muombaji ajifunze somo hili lote.
Karibu tujifunze  Neno la MUNGU.
Naamini wewe ni Mteule wa KRISTO na ni mwanamaombi mzuri tu.
Unapambana kiroho na maadui wengu na hao utawashinda kwa maombi yako katika jina la YESU KRISTO.
Katika maombi yako ya kupambana vita ya kiroho na maadui kwenye ulimwengu wa roho ni muhimu sana ukiwajua maadui hao ili ujue jinsi ya kuomba na kuwashinda kirahisi.
Mjue adui yako ni nani.
Mjue adui yako yuko wapi na mjue huyo adui anafanya nini ili kukuharibia wewe.
Biblia kwa kukusaidia inakujulisha juu ya maadui zako katika ulimwengu wa roho.
Waefeso 6:11-13 ''Vaeni silaha zote za MUNGU, mpate kuweza kuzipinga hila za Shetani. Kwa maana kushindana kwetu sisi si juu ya damu na nyama; bali ni juu ya falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili, juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho. Kwa sababu hiyo twaeni silaha zote za MUNGU, mpate kuweza kushindana siku ya uovu, na mkiisha kuyatimiza yote, kusimama.''
 Maadui zako ni falme zote za shetani. Ukiwa unapambana na falme ya giza ujue ni vita inayohusika wengi sana wanaotumika kipepo.
Falme ya giza inaweza ikawatumia hata watu wengi sana na ukashangaa sana.  Unaweza ukashangaa watu wote wanakuwa kinyume chako, unaweza ukashangaa uliowategemea wawe upande wako, wote wanakuwa kinyume chako.
Wanadamu wanaweza wakatumia na falme ya giza ili kuwa kinyume chako, wewe unaweza ukawa unapambana na wanadamu kumbe falme ya kishetani ndio inawatumia kukuharibia, pambana na falme ndipo vita vitakoma.
Kupigana na falme ya kishetani ni vita kubwa lakini Mteule wa KRISTO unayejitambua na unayeijua haki yako katika MUNGU Baba hakika utashinda falme hizo kirahisi sana.
Falme za kipepo zina mamlaka lakini wewe Mteule wa KRISTO uliyeokoka, MUNGU amekuweka juu ya kila falme na mamlaka za kipepo.
Yeremia 1:10 ''angalia, nimekuweka leo juu ya mataifa na juu ya falme, ili kung'oa, na kubomoa, na kuharibu, na kuangamiza; ili kujenga na kupanda.'' 
 
Maadui hao wakati mwingine hutumia wanadamu kukuharibia au kukudhuru.
Wewe unaweza ukawa unapambana na mwanadamu tu kumbe huyo ameibeba madhabahu ya kichawi inayomtumia yeye ili kukudhoofisha wewe.
Ukipambana na mtu huyo ujue unaweza ukamshinda lakini madhabahu ya giza bado ikawa ipo na inaweza ikatafuta mtu mwingine na vita na wewe ikaendelea maana hujaiharibu madhabahu hiyo ya kipepo.
Wana wa Israeli wakati wanapambana na maadui zako MUNGU aliwaagiza wana wa Israeli kubomoa madhabahu za kipepo hizo maana ndizo zinafanya kazi kubwa kuwadhoofisha watu wa MUNGU.
Kumb 7:5 ''Lakini watendeni hivi; zivunjeni madhabahu zao zibomosheni nguzo zao, yakateni maashera yao, ziteketezeni kwa moto sanamu zao za kuchonga.''

 Sijui kama unafahamu kwamba wewe Mteule wa KRISTO ndio unayeweza ukapanga kiwapate nini adui zako katika ulimwengu wa roho ili wasikusumbue tena.
Mteule mmoja alipanga hivi siku moja juu ya adui zake ''Waaibishwe, watoweshwe, adui za nafsi yangu. Wavikwe laumu na aibu wanaonitakia mabaya. Nami nitatumaini daima, Nitazidi kuongeza sifa zake(MUNGU) zote.-Zaburi 71:13-14''
 
Wewe ndio unaweza ukapanga kiwapate nini adui zako.
Adui zako hawana nguvu hata moja kama wewe una YESU KRISTO, YESU alikuja ili tu kuziharibu nguvu za giza zinazokusumbua.
1 Yohana 3:8b ''Kwa kusudi hili Mwana wa MUNGU alidhihirishwa, ili azivunje kazi za Ibilisi.''
 Ukijua kwamba YESU alikuja ili tu azivunje na kuzifuta kazi za shetani zinazokutesa basi utaomba na kushinda.
Naomba Neno hili liongeze imani ndani yako kwamba Hao mawakala wa shetani wanaokutisha, ukiamua kumkimbia Bwana YESU wataharibika na kuanza kukuogopa wewe kama ukoma.
Adu mwingine ni mamlaka za kipepo.
Shetani ameweka mamlaka zake na madhabahu zake katika maeneo mengi, katika Eneo hilo unaweza ukajikuta unapambana na mamlaka ya kipepo.
Mamlaka ya kipepo inaweza wakati mwingine ikatumia wanadamu ili kukudhuru au kukuharibia. 
Mamlaka ya kishetani ni pamoja na dini zote wanaompinga Bwana YESU na Wokovu wake.
Mamlaka za kishetani ni pamoja na dini za kishetani zote, hizo siku zote ziko kinyume na Wokovu wa YESU KRISTO.
Kuna watu wanakimbia miji  fulani  kwa sababu katika eneo hilo biashara haiendi. Ndugu uliye na YESU KRISTO hakikisha unaomba maombi kwa MUNGU aliye hai ili badala ya wewe kuikimbia mamalaka ya kishetani basi mamlaka hiyo ikukimbie wewe, inawezekana kwa jina la YESU KRISTO.
Adui zako hawana nguvu hata moja kama wewe una jina la YESU KRISTO
Adui zako hawana nguvu hata moja mbele yako kama una ROHO MTAKATIFU.
Jambo muhimu kujua ni kwamba wajue adui zako ili ujue unawakabili vipi na uwafanyeje.
Kuna adui wanaitwa wakuu wa giza.
Hao ni pamoja na waganga wa kienyeji, wachawi, wanajimu na nyota zao za majini, mizimu na kila madhabahu ya kishetani.
Hao ni makuhani wa shetani ili kuwaharibia watu wa MUNGU.
Inawezekana sana wanakutisha lakini nakujulisha kwamba hao hawana nguvu hata moja mbele yako wewe uliye na YESU.
MUNGU amekupa mamlaka ya kuwaponda kwa fimbo ya chumba na wakakukimbia wewe.
Mabaya yaliyokusudiwa katika ulimwengu wa roho wa giza hayatakupata wewe Mteule wa MUNGU.
Zaburi 91:10 ''Mabaya hayatakupata wewe, Wala tauni haitaikaribia hema yako.''

 Maadui wengine ni majeshi ya pepo wabaya.
Hao ni pamoja na majini wote na kabila zao zote.
Siku moja mimi Peter nilikuwa Zanzibar eneo linaitwa Darajani. Nilikuwa natembea Mchana jua likiwa kali sana, Ghafla mbele yangu nikakutana na dada mmoja aliyevaa hijabu na kufunika mwili mzima. Yule dada akaniambia kwamba nimsaidie Tsh 1,000 maana mepungukiwa nauli ya kwenda shamba(shamba ni miji midogo ya mbali na mji mkwa). Nilipomtazama machoni hakuwa na ujasiri wa kunitazama na macho yake yalikuwa yako kama ya paka na yanayoweza kugeuka geuka kama macho ya kuku, muda ule ule nilihisi mvutano wa ajabu kama ya mimi na yeye yaani ni kama upepo unavuta na mwili ulisisimka. Kwa sababu ilikuwa ni katikati ya watu wengi sikuogopa maana ilikuwa ni sokoni. Ghafla yule dada akaniambia basi niache tu kumpa ile pesa na akageuka nyuma na kuanza kuondoka, alipotembea kama hatua tano nikatazama mihuu yake na kuona ana kwato kama za ng'ombe na ghafla akapotea yaani akafutika huku namtazama. Niliowaangalia watu wote na kuona kila mtu anaendelea na shughuli zake, hakuna aliyemuona na hata alipokuwa anaongea na mimi nadhani hakuna aliyemuona. Ndugu hao ni maadui katika ulimwengu wa roho, inakupasa kupambana kwa jina la YESU KRISTO ili uwashinde.
Kila roho inayotumwa kuzimu ili ikushambulie hao ni maadui zako na unaweza ukawapiga kwa kipigo ambacho hawatatoka tena kuzimu kuja kukuchezea.
Hao usiwaogope maana hata bosi wao ambaye ni shetani hutukimbia sisi wateule wa KRISTO.
Kama shetani anatukimbia je watoto wake sio zaidi sana kutukimbia sisi?
Yakobo 4:7 '' Basi mtiini MUNGU. Mpingeni Shetani, naye atawakimbia.''
 Ndugu, wewe ndio unaweza ukaamua adui yako kimpate nini.
Jambo muhimu mjue adui yako na sasa pambana kwa jina la YESU KRISTO.
Unaweza ukasumbuliwa sana na magonjwa lakini adui yako ni jini uliyerushiwa, akajigeuza kuwa ugonjwa ndani yako ili uwe unapona kwa muda tu kisha unaumwa tena.
Jini huyo anaweza hata akavifanya vifaa vya hospitali vizionyeshe ugonjwa unaoumwa, ndio maana kuna watu wanaumwa sana sana lakini akienda hospitali madaktari hawaoni ugonjwa, huo ni ugonjwa wa kichawi na huo damu ya YESU KRISTO pekee inaweza kuuondoa ndani yako na ukawa huru, ndugu mkimbilie YESU KRISTO leo.
Kwanini huponi?
Ni kwa sababu katika maombi wewe huwa unapambana na ugonjwa lakini hujawahi kupambana na mleta huo ugonjwa. Ndugu mjue adui yako maana unayo mamlaka kuu sana kama utaamua kuitumia mamlaka hiyo ya jina la YESU KRISTO Mwokozi.
Luka 10:19 ''Tazama, nimewapa amri ya kukanyaga nyoka na nge, na nguvu zote za yule adui, wala hakuna kitu kitakachowadhuru.''

 Ndugu inawezekana kabisa wewe kila siku unapambana na adui wanadamu, hao hutumika kishetani dhidi yako.
Ngoja nikupe maarifa kidogo kuhusu adui wa namna hiyo.

ILI UMSHINDE ADUI MWANADAMU ANAYETUMIKA KIPEPO DHIDI YAKO.

1. Omba maombi ya vita katika jina la YESU KRISTO ukiharibu kazi zake za kipepo.

Mathayo 7:7 '' Ombeni, nanyi mtapewa; tafuteni, nanyi mtaona; bisheni, nanyi mtafunguliwa;''.
Kuna nguvu kubwa sana katika maombi ya Mteule wa KRISTO anayeomba katika jina la YESU KRISTO.
Yohana 14:13 ''Nanyi mkiomba lo lote kwa jina langu, hilo nitalifanya, ili Baba atukuzwe ndani ya Mwana.''

2. Usimpe siri zako.

Isaya 54:15 ''Tazama, yamkini watakusanyana; lakini si kwa shauri langu. Watu wo wote watakaokusanyana juu yako wataanguka kwa ajili yako.''
Ukisikia kuna kukusanyana yaani kukaa kikao ili kukujadili ujue wanafahamu vitu fulani kuhusu wewe, wanafahamu siri zako ndio maana wanakaa kikao kukujadili.
Ahadi ya MUNGU ni kwamba wataanguka hao maadui mbele yako, lakini hakikisha unakuwa muombaji na unayeishi maisha matakatifu.

3. Yajue mazingira ya yeye kukushambulia.

1 Yohana 4:4 ''Ninyi, watoto wadogo, mwatokana na Mungu nanyi mmewashinda, kwa sababu yeye aliye ndani yenu ni mkuu kuliko yeye aliye katika dunia.''
ROHO MTAKATIFU ndiye hukufanya umshinde shetani na mawakala zake wote kwa sababu yuko ndani yako na hukujulisha kila jambo la siri katika ulimwengu wa roho.
ROHO MTAKATIFUU atakujulisha kuhusu maadui zako na nini cha kufanya hivyo utayajua mazingira ya adui zako kukushambulia na kwa njia hiyo utakaa vizuri ili kuwaharibu na kuharibi mipango yao.

4. Mjue adui huyo na anaoshirikiana nao kukushambulia.

 Yeremia 18:18 '' Hapo ndipo waliposema, Njoni na tufanye mashauri juu ya Yeremia; maana sheria haitampotea kuhani, wala shauri halitampotea mwenye hekima, wala neno halitampotea nabii. Njoni, na tumpige kwa ndimi zetu, wala tusiyaangalie maneno yake yo yote. ''
Huu ni mfano hai wa watu wabaya wanaokaa kikao kupanga mipango ya kumdhuru Mteule wa MUNGU.
Watu wa aina hii wanaweza wakapanga hata mipango mibaya kukuhusu wewe ndugu, pambana kiroho utashinda.
Ukiwajua hao maadui na hao wanaowasaidia unaweza ukaomba hivi  ''Waaibike, wafedheheke pamoja, Wanaoitafuta nafsi yangu waiangamize. Warudishwe nyuma, watahayarishwe, Wapendezwao na shari yangu. Wakae hali ya ukiwa, na iwe aibu yao, Wanaoniambia, Ewe! Ewe!
Zaburi 40:14-15 ''

5. Usimruhusu akushambulie.

Zaburi  2:9 ''Utawaponda kwa fimbo ya chuma, Na kuwavunja kama chombo cha mfinyanzi.''
Biblia inaposema utawaponda kwa fimbo ya chumba maana yake ni wewe muombaji utawaponda.
Unapowaponda/Kuwaharibu maadui zako maana yake huwapi nafasi ya kukushambulia wewe.
Unapompiga adui, tendo hilo maana yake humruhusu akushambulie.

6. Haribu nguvu zake.

Mathayo 16:19 '' Nami nitakupa wewe funguo za ufalme wa mbinguni; na lo lote utakalolifunga duniani, litakuwa limefungwa mbinguni; na lo lote utakalolifungua duniani, litakuwa limefunguliwa mbinguni.''

Wewe uliyeokolewa na Bwana YESU unayo mamlaka kuu sana, itumie mamlaka hiyo kuwaharibu maadui zako katika ulimwengu wa roho.

 7. Hakikisha uko sahihi mbele za MUNGU siku zote.

Mithali 18:10 '' Jina la BWANA ni ngome imara; Mwenye haki huikimbilia, akawa salama.''
Jina la MUNGU wetu ni ngome imara sana na mwenye haki anaweza akakimbilia na kuwa salama.
Haijaribu maadui zake ni wengi kiasi gani, akikimbilia kwa YESU hakika anakuwa salama.
Muhimu awe tu mwenye haki mbele za MUNGU.
Mwenye haki ni mtu aliyeokoka na anaishi maisha matakatifu ya haki mbele za MUNGU.
Itafute hiyo haki ya MUNGU ili ukikimbilia ushinde maadui zako wote.

Natamani niseme mengi mno lakini naamini mwenye kuelewa ameelewa.
MUNGU akubariki kwa kujifunza somo hili muhimu pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane nitakujulisha jinsi ya kukipata.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa BWANA YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
0714252292.
0786719090
mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu.

Comments