ITUMIE TALANTA YAKO ULIYOPEWA NA MUNGU.

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU

Bwana YESU atukuzwe ndugu yangu!
Karibu tujifunze Neno la MUNGU la uzima.
Talanta ni nini?
Talanta ni zawadi unayopewa na MUNGU  ili ilete faida kwa MUNGU.
Talanta ni mali ya MUNGU inayowekwa kwa watu wake.
 

Talanta ni fedha ya mtaji inayohitajika kuzalishwa ili kuongezeka.
Kibiblia talanta ni karama au Huduma unayotakiwa kuifanyia kazi ili kumletea faida MUNGU.
Talanta ni Huduma aliyoweka MUNGU ndani yako kwa lengo la kumzalia matunda.
Mathayo 25:14-18 " Maana ni mfano wa mtu atakaye kusafiri, aliwaita watumwa wake, akaweka kwao mali zake. Akampa mmoja talanta tano, na mmoja talanta mbili, na mmoja talanta moja; kila mtu kwa kadiri ya uwezo wake; akasafiri. Mara yule aliyepokea talanta tano akaenda, akafanya biashara nazo, akachuma faida talanta nyingine tano. Vile vile na yule mwenye mbili, yeye naye akachuma nyingine mbili faida. Lakini yule aliyepokea moja alikwenda akafukua chini, akaificha fedha ya bwana wake."

 
Ufalme wa MUNGU unakuhitaji ushughulike na unakuhitaji kuzitumia karama zako alizokupa ROHO MTAKATIFU baada ya wewe kuokoka.
Nguvu uliyonayo mteule ni talanta ambayo unatakiwa uitumie kuwaleta watu kwa YESU KRISTO.

1 Kor 2:14 '' Nimewaandikia ninyi, akina baba, kwa sababu mmemjua yeye aliye tangu mwanzo. Nimewaandikia ninyi, vijana, kwa sababu mna nguvu, na neno la MUNGU linakaa ndani yenu, nanyi mmemshinda yule mwovu.'' 
Kijana una nguvu sana, je unazitumia nguvu hizo katika nini?
Je unaitumiaje talanta yako?
Mali zako au fedha zako ni talanta unayotakiwa kuitumia kuipeleka injili ya KRISTO mbele. 
1 Kor 16:1-2 ''Kwa habari ya ile changizo kwa ajili ya watakatifu, kama vile nilivyoamuru makanisa ya Galatia, nanyi fanyeni vivyo.  Siku ya kwanza ya juma kila mtu kwenu na aweke akiba kwake, kwa kadiri ya kufanikiwa kwake; ili kwamba michango isifanyike hapo nitakapokuja; ''
Mali zako au pesa zako kama talanta unazitumiaje?
Je unaitumiaje talanta yako?
Bwana YESU anasema  '' Siwaiti tena watumwa; kwa maana mtumwa hajui atendalo bwana wake; lakini ninyi nimewaita rafiki; kwa kuwa yote niliyoyasikia kwa Baba yangu nimewaarifu.
 Si ninyi mlionichagua mimi, bali ni mimi niliyewachagua ninyi; nami nikawaweka mwende mkazae matunda; na matunda yenu yapate kukaa; ili kwamba lo lote mmwombalo Baba(MUNGU) kwa jina langu awapeni. Haya nawaamuru ninyi, mpate kupendana. Iwapo ulimwengu ukiwachukia, mwajua ya kuwa umenichukia mimi kabla ya kuwachukia ninyi. Kama mngekuwa wa ulimwengu, ulimwengu ungewapenda walio wake; lakini kwa kuwa ninyi si wa ulimwengu, bali mimi naliwachagua katika ulimwengu, kwa sababu hiyo ulimwengu huwachukia. -
Yohana 15:15-19 ''
Karama na Huduma uliyopewa na ROHO MTAKATIFU ni talanta unayotakiwa kuitumia vyema ili kumzalia KRISTO matunda.
Wewe una Mali za MUNGU na hizo Mali MUNGU anataka faida itakayotokana na kuzalisha kwako kutoka katika Mali hiyo aliyokupa MUNGU.
Mali za MUNGU kwako ni karama, vipawa,Huduma, utumishi,muda,fedha na vyote alivyokubariki.
Ndugu hakikisha unamletea MUNGU faida inayotokana na uhai aliokupa, kutoka katika talanta ambayo MUNGU amekupa.

Mathayo 25:15-18,28-29 '' Akampa mmoja talanta tano, na mmoja talanta mbili, na mmoja talanta moja; kila mtu kwa kadiri ya uwezo wake; akasafiri. Mara yule aliyepokea talanta tano akaenda, akafanya biashara nazo, akachuma faida talanta nyingine tano. Vile vile na yule mwenye mbili, yeye naye akachuma nyingine mbili faida. Lakini yule aliyepokea moja alikwenda akafukua chini, akaificha fedha ya bwana wake. Basi, mnyang'anyeni talanta hiyo, mpeni yule aliye nazo talanta kumi. Kwa maana kila mwenye kitu atapewa, na kuongezewa tele; lakini asiye na kitu, hata kile alicho nacho atanyang'anywa. ''

Sababu zinazoweza kumfanya mtu asiitumie talanta yake aliyopewa na MUNGU.

1. Kutokumwamini MUNGU na watumishi wake aliowatuma kwako.
2 Nyakati 20:20 ''
...................  mwaminini BWANA, Mungu wenu, ndivyo mtakavyothibitika; waaminini manabii wake, ndivyo mtakavyofanikiwa.''
Usipomwamini MUNGU ni dhambi.
Usipomwamini MUNGU ni vigumu kumtumikia hata umzalie matunda.


2. Hofu
Mathayo 25:15,18, 25 ''
Akampa mmoja talanta tano, na mmoja talanta mbili, na mmoja talanta moja; kila mtu kwa kadiri ya uwezo wake; akasafiri. Lakini yule aliyepokea moja alikwenda akafukua chini, akaificha fedha ya bwana wake. basi nikaogopa, nikaenda nikaificha talanta yako katika ardhi; tazama, unayo iliyo yako.''
Huu ni mfano halisi kwa watu wengi wenye talanta, maana huogopa kuzitumia talanta zao ili zilete faida.
Hofu ilimfanya asiitumie talanta yake aliyopewa .
Una hofu ya nini katika kutumia talanta yako aliyokupa Bwana YESU?
Ukitaka uifanyie kazi talanta yako kataa hofu.


3. Shughuli za kidunia.
Marko 4:18-19 ''
Na hawa ndio wale wapandwao penye miiba; ni watu walisikiao lile neno, na shughuli za dunia, na udanganyifu wa mali, na tamaa za mambo mengine zikiingia, hulisonga lile neno, likawa halizai.''
Talanta ya MUNGU kwako huambatana na Neno la MUNGU.
Mambo ya kidunia ukiyapa nafasi sana moyoni mwako yataliondoa Neno la MUNGU ndani yako na kukufanya usifanyie kazi talanta yako.
Udanganyifu wa Mali ni mambo ya kidunia.
Tamaa za mambo yeyote yanayokuondoa kwa YESU ni sumu Kali ya kuharibu utendaji kazi wa talanta yako hata izae matunda.


4. Uchanga wa kiroho
1 Kor 13:11 ''
Nilipokuwa mtoto mchanga, nalisema kama mtoto mchanga, nalifahamu kama mtoto mchanga, nalifikiri kama mtoto mchanga; tokea hapo nilipokuwa mtu mzima, nimeyabatilisha mambo ya kitoto.''
 
Uchanga wa kiroho unaweza kukufanya usimtumikie MUNGU katika talanta aliyokupa.
Inakupasa kufanya juhudi ili ukue kiroho.
Juhudi za kukufanya ukue kiroho ni maombi, kusoma Neno la MUNGU na kulitafakari na kukataa mazoelea mabaya na kukataa dhambi.


5. Uoga
Mathayo 10:28 ''
Msiwaogope wauuao mwili, wasiweze kuiua na roho; afadhali mwogopeni yule awezaye kuangamiza mwili na roho pia katika jehanum. ''
Uoga hautakiwa kuwa katika kundi la wateule wa MUNGU.
Kataa woga na tafuta namna ya kuondoa uoga wako kwa Neno la MUNGU.


6. Upofu wa kiroho
2 Kor 4:4 ''
ambao ndani yao mungu wa dunia hii amepofusha fikira zao wasioamini, isiwazukie nuru ya injili ya utukufu wake KRISTO aliye sura yake MUNGU. ''
Kuna ni vipofu wa rohoni.
Hawa wanaweza kufanya hata yasiyowapasa kwa sababu tu ya upofu wao wa kiroho.
Vipofu wengine wa kiroho ni wale wanaotumia talanta zako kwa shetani na sio kwa MUNGU, mfano waimbaji wa nyimbo za kidunia.


7. Kutokujua wajibu wako mteule kwamba unatakiwa kuzaa matunda.
Yohana 15:4-5 ''
Kaeni ndani yangu, nami ndani yenu. Kama vile tawi lisivyoweza kuzaa peke yake, lisipokaa ndani ya mzabibu; kadhalika nanyi, msipokaa ndani yangu. Mimi ni mzabibu; ninyi ni matawi, akaaye ndani yangu nami ndani yake, huyo huzaa sana; maana pasipo mimi ninyi hamwezi kufanya neno lo lote. ''
Unahitaji kujitambua kama mteule wa KRISTO na tambua wajibu wako.
Ndugu, Unahitaji sana kumtumikia MUNGU.

1 Kor 15:58 '' Basi, ndugu zangu wapendwa, mwimarike, msitikisike, mkazidi sana kutenda kazi ya Bwana sikuzote, kwa kuwa mwajua ya kwamba taabu yenu siyo bure katika Bwana.''
 Natamani niseme mengi mno lakini naamini mwenye kuelewa ameelewa.
MUNGU akubariki kwa kujifunza somo hili muhimu pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane nitakujulisha jinsi ya kukipata.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.
0714252292.
0786719090
mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu

Comments