MAOMBI KUBOMOA NA KUHARIBU MADHABAHU ZA UHARIBIFU.

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.

 Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU la msaada na maombi ili tushinde madhabahu za uharibifu.
Madhabahu ni nini?
Madhabahu ni mpaka kati ya ulimwengu wa roho na ulimwengu wa mwili.
Madhabahu ni daraja kati ya ulimwengu wa roho na ulimwengu wa mwili.
Kuna Ulimwengu wa roho wa nuru na kuna ulimwengu wa roho wa giza, madhabahu za uharibifu hutoka katika ulimwengu wa roho wa giza.
Kuna vitu huachiliwa kutoka ulimwengu wa roho  kuja ulimwengu wa mwili.
Madhabahu ni kitu cha muhimu sana katika ufalme wa nuru, na pia wanaotumika kipepo nao kwao madhabahu zao za kipepo ni za muhimu sana kwao, maana bila madhabahu hakifanyiki chochote kutoka ulimwengu wa roho kuja ulimwengu wa mwili.
Wateule wa KRISTO hutumia madhabahu ya MUNGU aliye hai na mawakala wa shetani nao hutumia madhabahu zao za kishetani.
Zingatia haya katika maombi ya kuharibu madhabahu  itakusaidia kuharibu madhabahu na kile ilichokibeba;
Ili madhabahu yeyote ya kipepo  ifanye kazi ni lazima kuwe na mambo haya matano.
1. mungu wa madhabahu.
2. Madhabahu yenyewe.
3. Kuhani wa madhabahu.
4. Nguvu ya madhabahu inayotengenezwa na sadaka(Kafara) za madhabahu.
5. Watenda kazi wa madhabahu.
Kwa ufunuo wa leo tunajifunza jinsi ya kuharibu madhabahu za uharibifu. Madhabahu za shetani hutengeneza uharibifu  na kuuleta kwa mtu waliyemkusudia.
Shetani ndiye mungu wa madhabahu za uharibifu.
2 Wfalme 21:1-3 ''Manase alikuwa na umri wa miaka kumi na miwili alipoanza kutawala;  ......... Akafanya yaliyo mabaya machoni pa BWANA, sawasawa na machukizo ya mataifa ......akamjengea Baali(shetani) madhabahu, akafanya Ashera kama alivyofanya Ahabu mfalme wa Israeli. Akajiinama mbele ya jeshi lote la mbinguni na kulitumikia.''
 Huu ni mfano mmojawapo unaoonyesha mwanadamu akimjengea shetani madhabahu, shetani ndiye mungu wa madhabahu za giza zote. Madhabahu yenyewe ya kipepo inaweza ikawekwa kwa mganga wa kienyeji, mchawi, mkuu wa giza, baharini, porini, kwenye miti mikubwa walioichagua, kwenye ardhi au popote watakapopachagua hao wanaotumika kishetani.
tumeshaiona madhabahu yenyewe na tumeshamuona mungu wa madhabahu hizo za kishetani.
Sasa niendelee.
Nguvu ya madhabahu au utendaji kazi wa madhabahu za uharibifu ni kafara zinazotolewa. Kafara huhusisha damu na damu huwa haifi hivyo inaweza kutunza maagano ya kumfunga mtu hata kwa miaka  zaidi ya 20, kama haijaitwa damu ya YESU KRISTO ili ifute nguvu hiyo ya kafara na maagano. Ndani ya kafara ndipo hutengeneza maagano ya kumfunga mtu na utendaji kazi wa madhabahu husika lazima utegemee kafara
 Ndio maana kwa mganga ni rahisi tu kuambiwa upeleke kuku au mbuzi au kondoo au utoe hela za kununulia mnyama, ili tu nguvu za madhabahu hiyo ya giza ifanye kazi kupitia maagano yanayotengenezwa na kafara husika.
Makuhani wa madhabahu ya giza ni waganga wa kienyeji, wakuu wa giza wote, wanajimu au wasoma nyota, wachawi wote, washirikina na kila mwanadamu anayetumia nguvu za giza.
Watenda kazi wa madhabahu za giza ni mizimu, majini na kila maroho yanatotumwa na shetani.
Hao wote yaani makuhani wa madhabahu na watenda kazi wa madhabahu wamefafanuliwa vizuri katika Waefeso 6:12 ''Kwa maana kushindana kwetu sisi si juu ya damu na nyama; bali ni juu ya falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili, juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho.''
Baada ya kuyajua hayo sasa naomba utambue kwamba vita yako na madhabahu za giza ili ushinde ni lazima ujue kubomoa na kuharibu madhabahu hizo kwa maombi katika jina la YESU KRISTO.
Madhabahu huwa zinaharibiwa na kubomolewa, hiyo ndio kanuni ya kibiblia, usiombe maombi ya kuihamisha madhabahu au kuifuta bali ibomoe na kuiharibu. Tangu zamani MUNGU anaagiza wateule wake kubomoa na kuzivunja madhabahu za shetani.
Kumb 7:5 '' Lakini watendeni hivi; zivunjeni madhabahu zao zibomosheni nguzo zao, yakateni maashera yao, ziteketezeni kwa moto sanamu zao za kuchonga.''

Ndugu inakupasa uitambue vita ya kiroho  unayopambana nayo ili ushinde.
Inawezekana wewe huwa unapambana kiroho na watenda kazi tu wa madhabahu za giza lakini hujawahi kupambana na kuhani wa madhabahu ile inayoleta uharibifu kwako, ndio maana hujawahi kuyashinda matatizo husika.
Inawezekana wewe unapambana na madhabahu za uharibifu lakini maagano yaliyo katika kafara ya madhabahu hujawahi kuyafuta kwa damu ya YESU KRISTO, ndio maana bado unateseka.
Kumbuka kwamba hata ukifanikiwa kuiharibu madhabahu ya giza na ikatoweka kabisa, bado unaweza ukaendelea kuteseka kama hujafuta kafara iliyofanya agano ili kukufunga.
Ndugu leo haribu na kubomoa madhabahu zote za giza zinazoshindana na wewe.
Ziko madhabahu nyingi sana za shetani na ukiijua kila madhabahu na kuomba katika jina la YESU KRISTO na damu ya YESU KRISTO maombi ya kuiharibu pamoja na ilichobeba hakika Utashinda.
 Katika maombi ya kuharibu madhabahu nakuomba husika na kila mhusika wa madhabahu husika kama nilivyokutajia pamoja na madhabahu yenyewe iharibu.
Najua kabisa huwezi kumuua shetani bali unaweza Biblia inakupa kibali cha kumpinga na amepewa amri ya lazima ya kukukimbia(Yakobo 4:7b ''Mpingeni Shetani, naye atawakimbia.''
Shetani huwezi kumuua maana Biblia inasema kwamba yeye atakuwepo hadi siku ile ambayo atatupwa katika ziwa la moto akiwa mzima mzima, tena shetani ndio atakuwa wa tatu kutupwa katika ziwa la moto baada ya nabii wa uongo na mnyama(Walio upande wa mpingaKristo wanaabudu mnyama huyu), baada ya hapo ndipo wanadamu waliomkataa YESU kama Mwokozi wao watafuata kuingia katika ziwa la moto baada ya nabii wa uongo, mnyama na shetani.
Ufunuo 20:10 ''Na yule Ibilisi, mwenye kuwadanganya, akatupwa katika ziwa la moto na kiberiti, alimo yule mnyama na yule nabii wa uongo. Nao watateswa mchana na usiku hata milele na milele. ''
Hivyo ukisikia mtu yeyote anasema amemuua shetani huo ni uongo wa mchana peupe.
 Hao wahusika wengine wa madhabahu ya kipepo unaweza sasa kuwafanya vile utakavyowafanya kulingana na ufunuo wa ROHO MTAKATIFU katika maombi yako, kumbuka hao ndio maadui zako(Waefeso 6:12)
Kumbuka tu kwamba hao makuhani wa madhabahu za giza, watenda kazi, kafara yao na madhabahu yenyewe umepewa mamlaka ya kuwafanya vile utawafanya.
Unaweza ukawachapa kwa fimbo ya chuma(Zaburi 2:9)
Unaweza ukawapiga na kuwadhuru(Yoshua 23:10
Unaweza kufunga kazi zao(Mathayo 16:19)
Unaweza kuwaadhibu kwa kuwatamkia uharibifu(Yeremia 51:20-22) n.k kulingana na utakavyopenda.
 Kwenye kuombea madhabahu za giza  hakikisha tu unabomoa, kuvunja na kuharibu, hayo ndio maombi ya kuiharibu madhabahu ya giza.
 Yeremia 1:10 '' angalia, nimekuweka leo juu ya mataifa na juu ya falme, ili kung'oa, na kubomoa, na kuharibu, na kuangamiza; ........... ''
 Unaweza kila ukiomba kazi hupati kazi hiyo au unapata na kukutana na upinzani mkubwa sana, kumbe kuna madhabahu za uharibifu zinafanya kazi kinyume na wewe.
Unaweza kila ukipata mchumba  unakutana na vita kali hadi uchumba unavunjika, kwa sababu ya madhabahu ya uharibifu iliyokufunga.
Inawezekana unachukiwa na kudharauliwa sana bila kosa lolote wala sababu ila tu madhabahu ya uharibifu inafanya kazi kwako na kukutesa kwa njia hiyo.
Ndugu usikubali madhabahu ya uharibifu ikasimama na kuendelea kukutesa, kataa leo kwa jina la YESU KRISTO kwa njia ya maombi ya kuharibu kila madhabahu za giza.
Ibomoe na kuiangusha chini madhabahu hiyo a giza, Gidioni aliambiwa na Malaika wa MUNGU kuhakikisha anaangusha madhabahu za giza zilizokuwa nyumbani kwao na kutoa sadaka nzuri ya ng'ombe mzuri.
Waamuzi 6:25'' Ikawa usiku uo huo BWANA akamwambia, Mtwae ng'ombe wa baba yako, yaani ng'ombe wa pili, wa miaka saba, ukaiangushe madhabahu ya Baali, aliyo nayo baba yako, ukaikate Ashera ile iliyo karibu nayo; ''
 Haribu madhabahu za uharibifu katika ndoa yako.
 Haribu madhabahu za uharibifu katika afya yako.
 Haribu madhabahu za uharibifu katika uchumba wako.
 Haribu madhabahu za uharibifu katika kazi yako.
 Haribu madhabahu za uharibifu katika maisha yako.
 Haribu madhabahu za uharibifu katika biashara yako.
 Haribu madhabahu za uharibifu katika masomo yako.
 Haribu madhabahu za uharibifu katika uzao wako
 Haribu madhabahu za uharibifu katika kila kitu chako na katika kila baraka yako.

KAZI ZA MADHABAHU ZA UHARIBIFU.

1. Ni kutuma watenda kazi wa kipepo(Majini, mizimu n.k) ili kukutesa(Waefeso 6:12)

2. Kutunza maagano ya kipepo uliyonenewa kwa njia ya damu ya kafara(Isaya 28:15, Zaburi 106:37-38)

3. Kufanya kila njia ili wewe usifanikiwe katika jambo lolote kwenye maisha yako(Kutoka 7:22, Kutoka 8:7,18)

4. Kukufanya usimiliki na kutawala katika ulimwengu wa roho na mwili(2 Thesalonike 2:7)

 JINSI YA KUFUTA MADHABAHU YA UHARIBIFU NA ILICHOBEBA.

Hiki ndio kitu muhimu zaidi  katika kuzingatia kwenye maombi yako kuhusu kuziondosha maishani mwako madhabahu za giza.
 
1.  Tubu kwa ajili ya madhara yaliyokupata kutokana na madhabahu za giza, madhara uliyosababisha wewe mwenyewe kwa uzembe wa maombi, kutokulitii Neno la MUNGU, Kutokumtii ROHO MTAKATIFU N.k
Matendo 3:19 ''Tubuni basi, mrejee, ili dhambi zenu zifutwe, zipate kuja nyakati za kuburudishwa kwa kuwako kwake BWANA; ''

2. Mtii MUNGU, huku ukimpinga shetani ambaye ndiye mungu wa madhabahu ya uharibifu.
Yakobo 4:7 ''Basi mtiini MUNGU. Mpingeni Shetani, naye atawakimbia.   ''

 3. Omba maombi ya vita katika jina la YESU KRISTO huku ukiitumia damu ya YESU KRISTO kuharibu na kuifuta nguvu(kafara ya maagano) ya madhabahabu ya uharibifu
Ufunuo 12:11 ''Nao wakamshinda kwa damu ya Mwana-Kondoo, na kwa neno la ushuhuda wao; ambao hawakupenda maisha yao hata kufa. ''

 4. Haribu watenda kazi wa madhabahu za uharibifu
Waefeso 6:12 ''Kwa maana kushindana kwetu sisi si juu ya damu na nyama; bali ni juu ya falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili, juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho.''


 5. Haribu, vunja na kubomoa madhabahu yenyewe ya uharibifu.
Yeremia 1:10 '' angalia, nimekuweka leo juu ya mataifa na juu ya falme, ili kung'oa, na kubomoa, na kuharibu, na kuangamiza; ........... ''

6. Kama umewahi kushirikiana na makuhani wa madhabahu za giza(Waganga, wachawi, wanajimu na wakuu wa giza) Futa connection ya kipepo kati ya wewe na wao na madhabahu zao, haribu vitu walivyokupa na jitenge na kila kazi yao.
Mathayo 16:19 ''Nami nitakupa wewe funguo za ufalme wa mbinguni; na lo lote utakalolifunga duniani, litakuwa limefungwa mbinguni; na lo lote utakalolifungua duniani, litakuwa limefunguliwa mbinguni. ''

7. Futa vifungo vya giza vyote vilivyokupata.
 Yohana 14:13 ''Nanyi mkiomba lo lote kwa jina langu(YESU KRISTO), hilo nitalifanya, ili Baba(MUNGU) atukuzwe ndani ya Mwana. ''
 Natamani niseme mengi mno lakini naamini mwenye kuelewa ameelewa.
MUNGU akubariki kwa kujifunza somo hili muhimu pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane na nitakujulisha jinsi ya kukipata
na  Naamini kitakusaidia sana.
Hapa chini ni 
MAOMBI YA KUBOMOA NA KUHARIBU MADHABAHU ZA UHARIBIFU.
Maombi haya naomba yamsaidie mtu yule ambaye hajui kuomba ili katika kuomba kwa kutumia hayo basi atakumbuka mahitaji yake na kuyataja katika maombi yake.Haya hapa chini ni maombi ya kuanzia tu katika maombi yako ili uendelee zaidi kuomba
Kwa waombaji wazoefu naamini baada tu ya kulisoma somo na kulielewa basi anajua aombee nini maana alikuwa anaandika points za kuombea.


 MAOMBI YA KUBOMOA NA KUHARIBU MADHABAHU ZA UHARIBIFU.

 MUNGU asante kwa neema yako ya uzima na upendeleo kwangu hata ninaishi.
Ninakushukuru MUNGU wangu na nalitukuza jina lako JEHOVAH ambalo lina maana njema sana kwangu yaani wewe ni MUNGU wa kuokoa kama Zaburi 68:20 inavyosema.
Niko mbele zako MUNGU wangu nikiomba katika jina la YESU KRISTO Malaika zako wanisaidie katika kuziharibu na kuzibomoa madhabahu zote za kichawi zilizonitesa miaka mingi.
Kwa mamlaka ya jina la YESU KRISTO ninampinga shetani na kazi zake zote nazipinga na kuziondoa katika maisha yangu.
Ninampinga shetani na na watoto wake wote anaowatuma ili kutesa maisha yangu, leo naikata kila connection kati yangu mimi na shetani, naivunja connection hiyo kwa damu ya YESU KRISTO na kwa jina la YESU KRISTO.
Kwa mamlaka ya jina la YESU KRISTO aliye hai, nakuamuru shetani toka katika maisha yangu. Shetani achia ndoa yangu, kwa jina la YESU KRISTO.  Achia afya yangu, kwa jina la YESU KRISTO.
Achia uchumi wangu na kipato changu, kwa jina la YESU KRISTO.
Achia kibali changu, kwa jina la YESU KRISTO.
Achia uzao wangu, kwa jina la YESU KRISTO.
 Kila kuhani wa madhabahu ya shetani anayefanya kazi kuharibu chochte kwangu ninampinga kuhani huyo na kuamuru mapigo mabaya yampate, kwa jina la YESU KRISTO.
Kuhani mganga wa kienyeji anayemiliki madhabahu ya uharibifu iliyonitesa, ninampiga kwa moto wa jina la YESU KRISTO na kuziharibu kazi zake zote.
 Kila kuhani mchawi au mkuu wa giza, ninampiga kwa moto wa jina la YESU KRISTO na kuziharibu kazi zake zote.
 Kila kuhani mwanadamu yeyote anayetumika kishetani dhidi yangu, ninampiga kwa moto wa jina la YESU KRISTO na kuziharibu kazi zake zote.
 Kila kuhani mshirikina anayefanya ushirikina juu ya kazi yangu, uchumba wangu, ndoa yangu au biashara yangu au kazi yangu, huyo kuhani wa giza ninampiga kwa moto wa jina la YESU KRISTO na kuziharibu kazi zake zote.
Kila msoma nyota, msihiri na msoma nyakati wa kipepo,  ninampiga kwa moto wa jina la YESU KRISTO na kuziharibu kazi zake zote.
 Kila kiongozi wa serikali kazini kwangu anayetumia madhabahu za giza ili kuniharibia, ninampiga kwa moto wa jina la YESU KRISTO na kuziharibu kazi zake zote.
 Kila mtendakazi wa kipepo anayetumwa kutoka madhabahu za giza, ninampiga kwa moto wa jina la YESU KRISTO na kuziharibu kazi zake zote.
 Kila mtenda kazi jini, mzimu au kila maroho ya kuzimu,  ninawapiga hao wote kwa moto wa jina la YESU KRISTO na kuziharibu kazi zao zote.
 Kila kafara ya damu au ya hela iliyofanyika katika madhabahu za giza ili inifunge, hiyo kafara naifuta kwa damu ya YESU KRISTO na kwa jina la YESU KRISTO.
Kafara ya nguo zangu za ndani iliyopelekwa kwenye madhabahu za giza, hiyo kafara naifuta kwa damu ya YESU KRISTO na kwa jina la YESU KRISTO.
Kafara ya nywele zangu au kucha zangu au nyayo zangu au chochote changu kilichopelekwa katika madhabahu za giza ,hiyo kafara naifuta kwa damu ya YESU KRISTO na kwa jina la YESU KRISTO.
 Kila agano ndani ya kafara iliyofanyika katika madhabahu za giza kunihusu, hiyo kafara  na agano lake nafuta kwa damu ya YESU KRISTO na kwa jina la YESU KRISTO.
 Kila kilichobebwa katika madhabahu za giza kunihusu mimi, kitu hicho nakifuta kwa damu ya YESU KRISTO na kwa jina la YESU KRISTO.
Iwe ni jina langu lilitajwa katika madhabahu hiyo ya giza, iwe ni kazi yangu ilitajwa katika madhabahu hiyo ya giza, iwe ni biashara yangu ilitajwa katika madhabahu hiyo ya giza, kwa mamlaka ya jina la YESU KRISTO ninafuta mipango hiyo kwa damu ya YESU KRISTO aliye hai.
Ninajua damu huwa haifi lakini damu ya YESU KRISTO inauwezo wa kufuta maagano yote na kafara zote za giza hata zisiwepo na zisitende kazi tena.
Sasa  kila madhabahu ya uharibifu naibomoa yote na kuiharibu yote hata isiwepo tena katika maisha yangu, naibomoa, kuivunja na kuiharibu kwa jina la YESU KRISTO aliye hai.
Kuanzia leo natangaza kwamba kwa jija la YESU KRISTO sitateswa tena na madhabahu za uharibifu.
Ndoa yangu, uchumba wangu, kazi yangu, masomo yangu, familia yangu, biashara yangu na kila kitu changu hakitakamatwa tena na madhabahu za uharibifu popote pale.
 Nakushukuru MUNGU wangu maana umenishindia na sasa nitatoa sadaka nzuri katika madhabahu yako MUNGU Baba iliyo hai ikiwa kama ishara ya ukomo wa madhabahu za giza kutesa maisha yangu.
Katika jina la YESU KRISTO nimeomba na kupokea ushindi mkuu kwa imani.
Amen Amen Ameeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeen.
Hakika umeshinda.
Ukiweza kufunga unaweza kufunga hata siku 1 au 3 au 3 au hata 5 au zile ambazo wewe utaona unaweza ukihusika kila siku na kipengele kimoja kuombea na kumbuka baada ya maombi ya kufunga au hata maombi ya bila kufunga fanya tendo la imani kwa MUNGU kwa kutoa sadaka nzuri ikiambatana na maombi kutoka kwako na kwa mtumishi hai wa Bwana YESU juu ya ukomo wa kuteswa na madhabahu za uharibifu.
 Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa BWANA YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
0714252292.
0786719090
mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu.


Comments