UFANYEJE JUU YA MTU ANAYETAKA KUKUSHUSHA?

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU

  Bwana YESU atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.
Kuna watu kazi yao ni kuwashusha wengine.
Yeremia 18:18 '' Hapo ndipo waliposema, Njoni na tufanye mashauri juu ya Yeremia; maana sheria haitampotea kuhani, wala shauri halitampotea mwenye hekima, wala neno halitampotea nabii. Njoni, na tumpige kwa ndimi zetu, wala tusiyaangalie maneno yake yo yote.''
Ndugu uwe makini na mtu anayetaka kukushusha.
Katika andiko hili ni watu waliokaa kikao ili tu wampige Mtumishi wa MUNGU kwa maneno ya vinywa vyao.
Kumpiga kwa ndimi inaweza ikahusisha kuzusha uongo, huko ni kumshusha.
Kumlaani au kumtamkia mabaya, huko ni kumshusha.
Hata wewe unaweza ukakutana na changamoto ya watu wanaotaka kukushusha.
Una mchumba na kuna mtu anataka uachane na mchumba wako, huko ni kukushusha.
Una kazi nzuri  na kuna mtu kazini anataka ufukuzwe kazi, huko ni kukushusha.
Una Biashara nzuri na kuna mtu ankwendea kwa mganga ili ufilisike, huko ni kutaka kukushusha.
Mtu kuisema vibaya huduma yako, huko ni kutaka kukushusha.
Mtu anakufanyia mipango ili ufeli usaili, huko ni kukushusha.
Mtu anaeneza uongo au kufanya mipango ya siri ili ndoa yako ife, huko ni kukushusha.
Mtu anafanya mipango ili ukosane na ndugu zako,  au mwenzi  wako wa ndoa, huko ni kukushusha.
Ngoja nikupe mfano. Dada mmoja alipata mchumba na huyo dada alikuwa na rafiki yake ambaye naye alikuwa anamtamani huyo mchumba wa dada huyo. Yule rafiki siku moja akapanga mpango wa rafiki yake kuachwa na Mchumba ili ampate yeye. Yule rafiki  alimwambia yule kijana kwamba huyo dada ana mtu mwingine hivyo aachane naye. Yule kaka hakuamini na huyu rafiki akasema kwamba siku moja atamuonyesha kila kitu kuhusu mchumba wake. Siku moja yule Rafiki akammwambia rafiki yake mwenye mchumba kwamba waende beach na huko beach alikuwa ameshaandaa vijana wa kufanya yule binti aachwe tena kipindi muda wa kufunga ndoa umekaribia sana, na yule rafiki akamwandikia meseji yule kaka mwenye mchumba kwamba aje beach aone usaliti wa mchumba wake. Yule Rafiki na yule Binti aliyechumbiwa wakaenda beach na walipofika wakaanza kupiga picha na vijana fulani huku yule kaka akiona. na katika picha zile kuna kijana alikuwa anamshika kimahaba kwa hila yule binti aliyechumbiwa huku mchumba wake akiona kwa mbali. Uchumba ulikufa tangu siku hiyo na baada ya muda yule rafiki aliyetengeneza hila ili rafiki yake aachwe hakika akachumbiwa yeye na kuolewa. Yule Binti bila kosa aliachwa kwa sababu ya rafiki mnafiki aliyetaka kumshusha na akamshusha kweli.
Ndugu uwe makini na mtu anayetaka kukushusha.
Nasema tena  uwe makini sana na mtu anayetaka kukushusha.

 JINSI YA KUMSJHINDA MTU ANAYETAKA KUKUSHUSHA.

1. Mtegemee MUNGU kwa maombi.
Mithali 18:10 ''Jina la BWANA ni ngome imara; Mwenye haki huikimbilia, akawa salama.''
Maombi ndio mkono mrefu zaidi wa kuushika ushindi wako na kuuleta kwako. Hata kama unaumia kwa kitendo unachofanyiwa lakini hakikisha kwanza unamuomba MUNGU juu ya hayo yaliyopo, ya watu kutaka kukushusha.
Hakikisha kwa maombi yako MUNGU anajua na msihi akusaidie.
Wafilipi 4;6 '' Msijisumbue kwa neno lo lote; bali katika kila neno kwa kusali na kuomba, pamoja na kushukuru, haja zenu na zijulikane na MUNGU.''

 2. Usimpe nafasi mtu huyo kukuchunguza na kutafuta nafasi ya kukushusha.
Zaburi 1:1 ''Heri mtu yule asiyekwenda Katika shauri la wasio haki; Wala hakusimama katika njia ya wakosaji; Wala hakuketi barazani pa wenye mizaha.''
 Usimpe siri zako na wala usimjulishe mipango yako uliyoipanga kwa ajili ya maendeleo yako.
Jitahidi hata akikuchunguza lakini hafanikiwi kujua unapanga nini na unataka MUNGU akutendee nini.
Usikae kikao naye chochote na hata kuna ulazima basi usiongee mambo yako ili asipate kujua kitu kukuhusu na akakitumia hicho kukushusha.

 3. Ujue wakati wa yeye kukushusha ili ujue ufanyeje  ili kufuta hila yake ya kukushusha.
1 Yohana 4:1 '' Wapenzi, msiiamini kila roho, bali zijaribuni hizo roho, kwamba zimetokana na MUNGU; kwa sababu manabii wa uongo wengi wametokea duniani.''
 Chunguza na ukigundua ni nani anayetaka kukushusha kazini, kwenye ndoa, uchumba, biashara au popote basi wakati yeye akifanya hila zake uwepo ili asifanikiwe. Mfano kama huwa anatabia ya kukusemea uongo kwa bosi wako kila asubuhi basi hakikisha muda ule ule wa yeye kufanya hila yake unatokea ili asiendelea na ajue kwamba unafahamu hila yake.

 4.  Ongeza juhudi katika kile chema anachotaka kukushusha.
 Wafilipi 4:8 '' Hatimaye, ndugu zangu, mambo yo yote yaliyo ya kweli, yo yote yaliyo ya staha, yo yote yaliyo ya haki, yo yote yaliyo safi, yo yote yenye kupendeza, yo yote yenye sifa njema; ukiwapo wema wo wote, ikiwapo sifa nzuri yo yote, yatafakarini hayo. ''
 Mfano kwa sababu ya wewe kumtegemeza mchungaji kila mara basi watu wanakusema vibaya ili uache kumtegemeza Mtumishi, basi wewe ungeza juhudi katkia kumtegemeza.
Kama kwa sababu ya kuimba nyimbo za kumtukuza MUNGU, watu wanakuongea na kutaka uache kumsifu MUNGU, Wewe ongeza juhudi katika kumtukuza MUNGU.
Kama unashuhudia injili na watu wanasema una kihelehele, wewe ongeza juhudi ya kushuhudia.
Kama umenunua gitaa ya kanisa na watu wanakusema vibaya, basi nunua na Speaker kabisa kama unao uwezo.
Kama wanakuzushia kwa mchumba wako wewe ongea na mchumba wako huku ukimpenda na kumwombea.

 5. Uwe na upendo wa MUNGU na furaha.
Wafilipi 4:4'' Furahini katika BWANA sikuzote; tena nasema, Furahini.''
Hata wakati wa watu kutaka kukushusha wewe furahi kwa MUNGU huku ukimtegemea kwa maombi.
Adui yako alitarajia utalia sana na kukonda, wewe tunza furaha ya MUNGU ndani yako na songa mbele kwa ujasiri.

6. Itafute amani ya MUNGU.
Wafilipi 4:7 '' Na amani ya MUNGU, ipitayo akili zote, itawahifadhi mioyo yenu na nia zenu katika KRISTO YESU.''
Amani ya KRISTO ndio amani ya MUNGU.
Amani ya MUNGU ni silaha kubwa sana ya kumshinda adui anayetaka kukushusha.
Akina Paulo na Sila walikamatwa bila kosa lakini wakiwa gerezani walikuwa wakimsifu MUNGU na kumwabudu na kuomba hakika MUNGU aliwaokoa. Hawakuwa na majuto ndani yao wala manung'uniko wala lawama bali amani ya MUNGU iliwahifadhi wakabaki wakimtukuza MUNGU hata katika wakati wao mgumu.
Tunza amani ya MUNGU moyoni mwako, usiruhusu uchungu na maumivu, usilipe kisasi bali hakikisha una amani ya MUNGU. Soma Neno la MUNGU huku ukiomba, imba nyimbo za kusifu na kuabudu na kaa katika uwepo wa MUNGU ili hila ya shetani isikufanye unajisike kwa hasira na kutaka kulipa kisasi, adui atakimbia hakika ukifanya hivyo.

7. Usishindane na anayetaka kukushusha.
Warumi 12:21 ''Usishindwe na ubaya, bali uushinde ubaya kwa wema.''
Tenda Mema na sio mabaya. Kumbuka Bwana YESU anakuambia kwamba   '' Lakini mimi nawaambia, Msishindane na mtu mwovu;-Mathayo 5:39a  ''
Ukishindana naye utakuwa unatafuta heshima za kibinadamu, wewe mtegemee MUNGU na utashinda.
Wafilipi 2:14-15 ''Yatendeni mambo yote pasipo manung'uniko wala mashindano, mpate kuwa wana wa MUNGU wasio na lawama, wala udanganyifu, wasio na ila kati ya kizazi chenye ukaidi, kilichopotoka; ambao kati ya hao mnaonekana kuwa kama mianga katika ulimwengu, '

8. Mwache MUNGU akulipizie kisasi kwa watu wabaya wanaotaka kukushusha. 
 Warumi 12:19'' Wapenzi, msijilipize kisasi, bali ipisheni ghadhabu ya MUNGU; maana imeandikwa, Kisasi ni juu yangu mimi; mimi nitalipa, anena BWANA.''
Kumbuka kisasi cha MUNGU ni kibaya sana. Wewe usilipe kisasi maana ukitaka kulipa kisasi wewe utatenda dhambi, utafungua mlango wa shetani kukuonea zaidi na ukitaka kulipa kisasi ujue MUNGU hatakusaidia kwa lolote katika vita hiyo, hivyo Mwache MUNGU akulipizie kisasi kwa watesi wako hao wanaotaka kukushusha.

Natamani niseme mengi mno lakini naamini mwenye kuelewa ameelewa.
MUNGU akubariki kwa kujifunza somo hili muhimu pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane nitakujulisha jinsi ya kukipata.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.
0714252292.

mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu.

Comments