USIYACHOCHEE MAPENZI WALA KUYAAMSHA HADI MUDA WA NDOA UFIKE.

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU

 Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.
Wimbo 8:4 ''Nawasihi, enyi binti za Yerusalemu, Kwani kuyachochea mapenzi, au kuyaamsha, Hata yatakapoona vema?''
 Biblia inawaagiza watu kutokuyachochea mapenzi hadi yatakapoona vema yaani hadi ukiingia katika ndoa.
Neno la MUNGU linamkataza kila mmoja ambaye hajaolewa au kuoa kwamba asiyachochee mapenzi.
Muda wa kuyachochea mapenzi ni kipindi uko kwenye ndoa yako na utayachochea kwa mwenzi wako tu wa ndoa, na sio vinginevyo.
Kuchochea mapenzi ni kugusagusana kimapenzi na mtu wa jinsia tofauti na yako.
Kuyachochea mapenzi ni kufanya mambo yanayokufanya utake kufanya ngono.
Kuyachochea mapenzi ni kufanya vitu vya kukufanya uwake tamaa ya ngono.
Kuyachochea mapenzi ni kuchipua hamu ya ngono.
Biblia inakutaka usiyachochee mapenzi.
Ukiyachochea mapenzi utajikuta unafanya dhambi mbaya ya uasherati. Na Biblia iko wazi sana kwamba hakuna mbingu ya waasherati. 
Waefeso 5:3-5 '' Lakini uasherati usitajwe kwenu kamwe, wala uchafu wo wote wa kutamani, kama iwastahilivyo watakatifu;  wala aibu wala maneno ya upuzi wala ubishi; hayo hayapendezi; bali afadhali kushukuru.  Maana neno hili mnalijua hakika, ya kwamba hakuna mwasherati wala mchafu wala mwenye tamaa, ndiye mwabudu sanamu, aliye na urithi katika ufalme wa KRISTO na MUNGU. ''
Kwanini uitwe mzinzi?
Kwanini uitwe mwasherati?
Hata huoni kuwa ni jambo baya sana kuwa mzinifu?

 Biblia inamuasa kila aliye Kanisa hai la MUNGU kwamba '' Maana Haya Ndiyo Mapenzi Ya MUNGU, Kutakaswa Kwenu, Mwepukane Na Uasherati- 1 Thesalonike 4:3.'' 

 MAMBO MABAYA YANAYOCHOCHEA MAPENZI KABLA YA NDOA.

1.Uvaaji mbaya.

Mithali 11:16 ''Mwanamke wa adabu huheshimiwa daima; .........'
Adabu ikiondoka lazima uvaaji wa kikahaba huingia.
Wengi sana huvaa vizuri misibani na ukweni tu, ni hatari.
Adabu maana yake ni tabia njema, hivyo mtu akikosa tabia njema kuna mambo mengi yataonekana kwake. Suala hili na kukosa maadili liko zaidi kwa wanawake maana kwa maumbile yao tu haiwapasi kuvaa kikahaba, lakini mabinti wengi leo hata wamekosa wachumba sahihi kwa sababu ya uvaaji wa kikahaba.
Uvaaji mbaya ni kichocheo kikubwa zaidi cha mapenzi.
Biblia inawapa kielelezo wanawake.
1 Timotheo 2:9-10 ''Vivyo hivyo wanawake na wajipambe kwa mavazi ya kujisitiri, pamoja na adabu nzuri, na moyo wa kiasi; si kwa kusuka nywele, wala kwa dhahabu na lulu, wala kwa nguo za thamani; bali kwa matendo mema, kama iwapasavyo wanawake wanaoukiri uchaji wa MUNGU.''
 Wengi sana huvaa mavazi isivyotakiwa kabisa.
Nguo za kulalia wengine huzivaa mitaani.
Wengi wanavaa sketi fupi mno au vimini.
Wengi huvaa nguo nyepesi sana na zinawaonyesha maungo yao kabisa.
Wengi huacha matiti nje, hiyo ni kazi ya makahaba na sio mteule wa MUNGU.
Wengine kwa mavazi yao ya uchi  uchi huonekana mitaani kwamba wanajiuza au wanatafuta wanaume, mabinti wa hivyo hawapati mwanaume wa kuoa ila wanapata mwanaume aliyepagawa na pepo la ngono na kuishia kuchezewa na kuachwa.
Biblia inakukataza kuyachochea mapenzi hata kwa kupitia uvaaji wako.
Kama unavyovaa kiheshima msibani au kanisani basi kokote unakoenda hakikisha unavaa kiheshima.

2. Filamu na picha za ngono.

Hili nalo ni tatizo kubwa sana kwa vijana wengi.
Watu kuangalia  video za ngono huona kawaida kabisa.
Kuna vijana hadi wana majarida ya x, hiyo ni mbaya sana.
Wapo watu kila siku internet lakini kwa lengo la kuangalia filamu za ngono tu.
Filamu na picha za ngono ni kichocheo kikubwa sana cha ngono.

Biblia inasema Yakobo 1:21 '' Kwa hiyo wekeeni mbali uchafu wote na ubaya uzidio, ................... ''
 Picha za ngono ni uchafu, filamu za ngono ni uchafu ambao hautakiwi kukaa kwa vijana wanaomcha MUNGU.
Warumi 6:12 '' Basi, dhambi isitawale ndani ya miili yenu ipatikanayo na mauti, hata mkazitii tamaa zake; ''
Kama kuna vichocheo vikubwa vya ngono ni pamoja na filamu za ngono au picha za ngono.
Achana na tabia hiyo chafu.

3. Boyfriend na Girlfriend

Hili ni janga kubwa sana linalochochea mapenzi na ni janga linalosababisha vijana wengi kufeli hadi maisha au masomo.
Boyfriend na Girlfriend ni mpango wa shetani kuwateka wanadamu ili wakose mbingu. Watu walio katika u-boyfriend na u-girlfriend inatupasa kuwaokoa kutoka katika moto ''na wengine waokoeni kwa kuwanyakua katika moto; na wengine wahurumieni kwa hofu, mkilichukia hata vazi lililotiwa uchafu na mwili.-Yuda 1:23''
 Jambo hili limekuwa fashion lakini ni fashion ya kishetani.
Leo mashuleni karibia kila binti ana boyfriend hata watatu au zaidi.
Leo karibia kila kijana ana girlfriend, ni hatari sana.
Lengo la boyfriend na girlfiend ni ngono na kuwa mbali na MUNGU. Biblia hairuhusu mtu yeyote kuwa na boyfriend wake au girlfriend wake.
Yakobo 4:4 '' Enyi wazinzi, hamjui ya kwamba kuwa rafiki wa dunia ni kuwa adui wa MUNGU? Basi kila atakaye kuwa rafiki wa dunia hujifanya kuwa adui wa MUNGU.''
Watu wengi sana wanayachochea mapenzi ni kwa sababu ya uhusiano huu wa kipepo.
Binti mmoja ameshazalishwa watoto 3 na wanaume watatu tofauti na chanzo aliniambia ni mahusiano hayo.
Ndugu, vunja uhusiano huu kama uko nao.
Mika 7:5 '' Msimwamini rafiki, msimwekee kiongozi tumaini; ilinde milango ya midomo ya kinywa chako .......... ''

Biblia ina maonyo mengi sana juu ya dhambi au juu ya vitu vinavyopelekea dhambi.
Mhubiri 8:8 ''Hakuna mwenye uwezo juu ya roho aizuie roho; Wala hana mamlaka juu ya siku ya kufa; Wala hakuna kuruhusiwa katika vita vile; Wala uovu hautamwokoa yule aliyeuzoea. ''
  4. Mazoea mabaya kati ya watu wa jinsia mbili tofauti.

Hii nayo ni kichocheo kikubwa sana cha mapenzi.
Unakuta binti na kijana wawili tu wako chumbani kwa kijana, kitakachofuata hapo ni uharibifu.
Binti kukubali kushikwa shikwa na vijana, ni hatari inayoyachochea mapenzi.
Kwenda disko ni sehemu ya kishetani inayoamsha mapenzi.
Kuzikiliza nyimbo za kidunia ambazo nyingi katika hizo ni za kusifia ngono tu.
Ushauri mbaya kutoka kwa watu wasiomcha MUNGU.
Shetani ana mbinu nyingi sana na wengine wamejikuta katika mazoelea mabaya na kupelekea uharibifu.
Biblia inasema 
Warumi 13:14 ''Bali mvaeni Bwana Yesu Kristo, wala msiuangalie mwili, hata kuwasha tamaa zake. ''

Natamani niseme mengi mno lakini naamini mwenye kuelewa ameelewa.
MUNGU akubariki kwa kujifunza somo hili muhimu pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane nitakujulisha jinsi ya kukipata.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.
0714252292.
0786719090
mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu.

Comments