NENO BINAFSI UNALOTUMIWA NA MUNGU.

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
 Shalom mteule wa KRISTO upendwaye sana na MUNGU Baba.
Nakukaribisha katika somo hili liitwalo NENO BINAFSI UNALOTUMIWA NA MUNGU.

Watu wengi hukosea sana maana wanapopewa ujumbe wa andiko huwa hawafanyii kazi andiko hilo.
Mara nyingi nimekutana na watu ambao walinipa maandiko ili niwasadie kuelewa ujumbe ule maana walipewa binafsi kama ufunuo, huo Ujumbe. 

Mfano mtu alikuwa kwenye maombi ya kufunga siku 3 na kabla hajamaliza maombi yake anapewa andiko na ROHO MTAKATIFU, mfano anapewa andiko la Isaya 41:10 linalosema '' usiogope, kwa maana mimi ni pamoja nawe; usifadhaike, kwa maana mimi ni Mungu wako; nitakutia nguvu, naam, nitakusaidia, naam, nitakushika kwa mkono wa kuume wa haki yangu.''
Hata Mimi binafsi ni Mara nyingi ROHO wa MUNGU amenipa andiko juu ya mahitaji yangu, mahitaji ya wengine au juu ya maombi ninayoomba.
Jambo la kwanza kabisa naomba ndugu ujue kwamba MUNGU hulituma Neno kwako na neno hilo lina kazi kubwa sana kwa aliyepewa, Na neno hilo hutoa ripoti kwa MUNGU maana linatakiwa litimize kile MUNGU alilituma.
Isaya 55:11 "ndivyo litakavyokuwa neno langu, litokalo katika kinywa changu; halitanirudia bure, bali litatimiza mapenzi yangu, nalo litafanikiwa katika mambo yale niliyolituma."


Ngoja nikupe mifano michache yangu mwenyewe.

Mfano wa kwanza.

Baada ya kuokoka nilikuwa mgumu sana kuomba maombi ya kufunga. 
Nilikuwa ninakaa na marafiki zangu na siku moja nilitakiwa kwenda kanisani. 
Kabla ya kuondoka kwenda kanisani nilimtaarifu rafiki yangu mmoja kwamba anitunzie chakula maana ndio ulikuwa utaratibu wetu. Nikaondoka kwenda kanisani na kufanya ibada kama kawaida. Baada ya ibada nikampigia simu rafiki yangu na akanijulisha kwamba chakula kipo. Kwa sababu nilikuwa na njaa sana basi niliwahi nyumbani ili Nile chakula. Nilipokaribia nilisikia sauti ya andiko hili la Mathayo 4:4 ambapo Biblia inasema ''Imeandikwa, Mtu hataishi kwa mkate tu, ila kwa kila neno litokalo katika kinywa cha Mungu. '', moja kwa moja ROHO wa MUNGU akanielekeza kufanya maombi ya kufunga. Na usiku huo sikula chakula baada tu ya kujulishwa kwa andiko kwamba nifunge.
Leo nazungumzia Neno binafsi unalotumiwa na MUNGU binafsi.

Mfano wa pili ni huu.
Siku moja niliposoma Yohana 1:12-13 inayosema ''
Bali wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa MUNGU, ndio wale waliaminio jina lake; waliozaliwa, si kwa damu, wala si kwa mapenzi ya mwili, wala si kwa mapenzi ya mtu, bali kwa MUNGU.''  nilijihisi utofauti sana na Mwanzo. Niliona neema kubwa sana ya MUNGU juu ya wanadamu. Niliwahurumia sana ghafla wanadamu wanaomkataa Bwana YESU kama Mwokozi wao. Nilipata mzigo mzito sana wa kuwaeleza injili ya Wokovu wale watakaotii. Hadi Leo nikisoma andiko hilo najihisi nguvu na utofauti sana. Niligundua kwamba bila YESU KRISTO hakuna uzima wa milele kwa mwanadamu yeyote.
Ndugu naomba utambue kwamba MUNGU anaweza kukutumia wewe Neno Binafsi ili likusaidie.


Mfano wa tatu ni huu.
Siku moja Niliposoma Yohana 14:17 ambapo Biblia inasema ''
ndiye ROHO wa kweli; ambaye ulimwengu hauwezi kumpokea, kwa kuwa haumwoni wala haumtambui; bali ninyi mnamtambua, maana anakaa kwenu, naye atakuwa ndani yenu. ''   nilisononeka sana rohoni mwangu kwa ajili ya watu wanaomkataa ROHO MTAKATIFU.
Baada ya hapo kuna wakati nilipokuwa nasoma andiko hilo nilikuwa naona maono kabisa ya kuona umuhimu mkubwa sana wa ROHO MTAKATIFU katika maisha yetu sisi tuliookolewa na Bwana YESU, jambo hili la kusoma andiko hilo na kujiona tofauti liliendelea kwa muda mrefu sana.
Hali ambayo huwa naiona nikisoma Yohana 14:17  hata kuielezea vizuri nashindwa. Tangu wakati huo natambua kwamba bila ROHO MTAKATIFU katika kanisa, hilo sio kanisa la MUNGU.
Mkristo bila ROHO MTAKATIFU hawezi kushinda ulimwengu na mambo yaliyomo.
Kanisa bila ROHO MTAKATIFU huhama kutoka kanisa la MUNGU na kuwa kanisa la dunia au la dini tu.


MUNGU hutoa neno binafsi kwa mteule wa KRISTO ili kumuongoza, kwa ajili ya huduma n.k

Nimewahi Mara kadhaa kuhudhuria semina za Neno la MUNGU za Mwalimu mwakasege na Mara zote nimeona tangazo la huduma likisema "Lisha kondoo zangu-Yohana 21:17"
Nilihudhuria Mara mbili kanisani kwa Askofu Silvester Gamanywa na kukuta madhabahuni tangazo kubwa likisema "Mtapokea nguvu akisha kuwajilia juu yenu ROHO MTAKATIFU-Matendo 1:8.
Nilienda siku moja Eagt Bugando alikokuwa Askofu Moses Kulola na kukuta maandiko matatu yameandikwa ndani ya kanisa.
Na maeneo mengi tena kwenye makanisa mengi tu ya kiroho nilikuta kuna tangazo la huduma likiwa na andiko.
Wakati mwingine nilijiuliza " Je ni neno binafsi ambalo MUNGU aliwapa watumishi wake?" Maana kile walichopewa kinaonekana na ushahidi ukiwa ni maandiko ambayo MUNGU amewapa.
Mimi binafsi sijawahi kupewa andiko la huduma Bali ROHO wa MUNGU hunipa andiko la mwaka, mfano mwaka huu 2017 Nilipewa Yeremia 10:6 inayosema ''
Hapana hata mmoja aliye kama wewe, Ee BWANA; wewe ndiwe uliye mkuu, na jina lako ni kuu katika uweza.''  na Mwaka 2016 Nilipewa Mathayo 3:2 inayosema  ''Tubuni; kwa maana ufalme wa mbinguni umekaribia.''  na hata mwaka  2015 na 2014 nilipewa kila mwaka andiko,  lakini naamini kuna watumishi MUNGU anapowaita katika wito huwapa na maandiko kama mihuri ya kazi yao.
Tarehe 2 April mwaka fulani ROHO wa MUNGU aliniambia kwamba ameniita kuwa Mwalimu wa Neno la MUNGU, hicho ndicho hukifanya Mimi kwa neema yake na kwa msaada Wake.
Sasa nisikilize kwa makini.


KWANINI MUNGU AKUPE NENO BINAFSI?

1. Ili kukuonyesha nini cha kufanya.
Yona 1:1-2 ''
Basi NENO la BWANA Likamjia Yona, mwana wa Amitai, KUSEMA, ONDOKA, UENDE Ninawi, mji ule mkubwa, UKAPIGE KELELE JUU YAKE; kwa maana uovu wao umepanda juu mbele zangu.''
 Neno lilitoa maelekezo ya nini cha kufanya, hata wewe unaweza ukapewa Neno na ROHO MTAKATIFU ili ujue nini cha kufanya.

2. Ili likuongoze kuendelea mbele katika hatua uliyonayo, ili ufanikiwe
1 Wafalme 17:8-9 ''
NENO la BWANA Likamjia, kusema, Ondoka, uende Sarepta, ulio mji wa Sidoni, ukae huko. Tazama, nimemwagiza mwanamke mjane wa huko akulishe.''
 Hatua ya Eliya ilikuwa ni nguvu na alikuwa anahitaji chakula, Neno la MUNGU lilimwelekeza sehemu atakayopata chakula maana kulikuwa wakati wa ukame katika nchi miaka mitatu na nusu, hata wewe MUNGU anaweza akakupa Neno ili likuonyeshe jinsi utakavyofanikiwa katika hitaji lako uliloliomba kwa MUNGU.

3. Ili nikufanye uone njia ya kufanikiwa kwako.
Zaburi 119:105 ''
Neno lako ni taa ya miguu yangu, Na mwanga wa njia yangu.''
Hakuna njia sahihi kama unayoelekezwa na ROHO MTAKATIFU kwa njia ya Neno la MUNGU.

4. Ili ujue wazo la MUNGU katika wakati huo.
Yetemia 29:11''
Maana nayajua mawazo ninayowawazia ninyi, asema BWANA, ni mawazo ya amani wala si ya mabaya, kuwapa ninyi tumaini siku zenu za mwisho.''
Unaweza ukang'ang'ania jambo fulani ulitakalo kwa wakati huu lakini kumbe sio wakati wake hivyo hata uking'ang'ania hutalipata, lakini unaweza ukashangaa ROHO wa MUNGU anakupa andiko ambalo linaonyesha wazo au mpango wa MUNGU wa wakati huu, hivyo unatakiwa kufuata wazo hilo la MUNGU la wakati huu.
Siku moja mimi Peter Niliamua kufunga siku tatu maombi, katika maombi hayo niliamua kujiombea mimi binafsi bila kumuombea mtu mwingine yeyote na nikaandika maombi yangu kwenye daftari ili nizingatie, lakini ajabu nilipoanza tu kuomba nilikuwa naletewa watu na kanisa kuombea na katika siku tatu zote nilijikuta nimeombewa wengine tu na mimi sikujiombea. Lakini ajabu hata mimi, MUNGU alinitendea mahitaji yangu huku pia niliowaombea akiwatendea, ningeng'ang'ana na mahitaji yangu sijui ingekuwaje.
Unaweza ukang'ang'ana katika maombi kuombea mahitaji yako fulani na ghafla MUNGU akakufunulia kwa andiko jambo lingine ambalo ukisoma unaona kabisa unakatazwa kuhusu unayoombea na hivyo unapewa mapya ambayo ndio muhimu kwako zaidi kuliko mengine. Kumbuka MUNGU hukupa unachostahili sio kila unachoomba.
Unaweza ukafanya jambo fulani au huduma fulani kumbe sio mpango wa MUNGU kwako kwa wakati huo, hivyo ukipewa Neno la ufunuo fanyia kazi ndipo utaliendea kusudi la MUNGU.

5. Ili kukupa utulivu wa rohoni utakaokusaidia kuamua vyema.
2 Nyakati 20:3,14,15 ''
Yehoshafati akaogopa, akauelekeza uso wake amtafute BWANA; akatangaza mbiu ya watu kufunga katika Yuda yote.  ..... Ndipo Yahazieli mwana wa Zekaria, mwana wa Benaya, mwana wa Yeieli, mwana wa Matania, Mlawi, wa wana wa Asafu, akajiliwa na roho ya BWANA, katikati ya kusanyiko; akasema, Sikieni, Yuda wote, nanyi mkaao Yerusalemu, na wewe mfalme Yehoshafati; BWANA awaambia hivi, Msiogope, wala msifadhaike kwa ajili ya jeshi kubwa hili; kwani vita si yenu bali ni ya MUNGU.''
Mfalme, wakuu wa jeshi na wanachi hawakuwa na utulivu maana walijua muda wowote watashambuliwa maana aliyekuwa anakuja kuwashambulia ni taifa lenye nguvu sana kivita. Mfano nchi ndogo mojawapo iliyo kisiwa katika Bahari ya hindi ijue inakuja kushambuliwa na taifa kubwa la Ulaya au America au Asia na taifa hilo kubwa linakuja na silaha za nyuklia na makombora, hakika hofu itakuwa kubwa sana na hakutakuwa na utulivu, ni mfano kama huo uliowakuta Israeli, hofu ilikuwa kubwa sana na walikuwa wameamua kufunga lakini MUNGU alipowapa Neno hakika utulivu ulirudi na jambo la ajabu MUNGU ni Mwaminifu anapolituma Neno lake walishinda vita bila kupigana vita.

 6. Ili kukupa majibu ya ulichouliza kwa MUNGU.


2 Samweli 5:18-19 '' Basi Wafilisti walikuwa wamekuja na kujitawanya bondeni mwa Warefai. Basi Daudi akauliza kwa BWANA, akisema, Je! Nipande juu ya Wafilisti? Utawatia mkononi mwangu? Naye BWANA akamwambia Daudi, Panda; kwa kuwa hakika nitawatia Wafilisti mikononi mwako.''
Daudi aliuliza kwa MUNGU akajibiwa kama ambavyo wewe unaweza ukauliza kwa MUNGU na kujibiwa kwa Neno la MUNGU.
 
7. Ili ujue siri iliyokuwa imejificha.
Amosi 3:7 ''Hakika Bwana MUNGU hatafanya neno lo lote, bila kuwafunulia watumishi wake manabii siri yake.''
Mambo mengi sana na karibia yote yanayotokea MUNGU huwajulisha watumishi wake.
MUNGU anaweza kukupa andiko la Biblia likiwa linajulisha jambo la siri lililopo katika ulimwengu wa roho kukuhusu wewe na kupewa njia za kushinda, kufanikiwa au kutenda.

UFANYEJE BAADA YA KUPEWA NENO BINAFSI NA ROHO MTAKATIFU?


1. Tengeneza kwa MUNGU kulingana na Neno hilo Binafsi alilokupa, kama kunahitajika matengenezo
Isaya 38:1-2 ''
Siku hizo Hezekia aliugua, akawa katika hatari ya kufa; na Isaya nabii, mwana wa Amozi, akaenda kwa mfalme, akamwambia, BWANA asema hivi, Tengeneza mambo ya nyumba yako; maana utakufa, wala hutapona. Basi Hezekia akajigeuza, akaelekeza uso wake ukutani, akamwomba BWANA,''
Hezekia alipotengeneza kwa MUNGU baada ya kupewa Neno Binafsi aliongezewa miaka kumi na tano ya kuishi, hata wewe unaweza kufaidika sana kama utatengeneza kwa MUNGU baada ya kupewa Neno binafsi linalokuhitaji utengeneze.

2. Fanyia kazi kilicho ndani ya Neno hilo binafsi alilokupa MUNGU.
Zaburi 107:20 ''
Hulituma neno lake, huwaponya, Huwatoa katika maangamizo yao.''
 Neno la MUNGU lina kazi nyingi sana hivyo lifanyie kazi Neno Binafsi unalopewa.
 
3. Omba ROHO MTAKATIFU akuongoze katika hicho alichokusemesha.
Zaburi 32:8 ''
Nitakufundisha na kukuonyesha njia utakayoiendea; Nitakushauri, jicho langu likikutazama.''
Maongozi ya ROHO MTAKATIFU kwako ni muhimu sana ili ufanikiwe na utembee kwenye kusudi la MUNGU.
 
4. Mshukuru MUNGU kwa kukupa Neno binafsi.
Wakolosai 4:2 ''
Dumuni sana katika kuomba, mkikesha katika kuomba huku na shukrani;''
Wateule wa KRISTO huishi maisha ya shukrani mbele za MUNGU hivyo kumshukuru MUNGU ni muhimu sana hata wakati akikusemesha mshukuru.

NENO BINAFSI ANALOKUPA ROHO MTAKATIFU LINABEBA NINI?

1. Ushindi wako.
Ufunuo 12:11''
Nao wakamshinda kwa damu ya Mwana-Kondoo, na kwa neno la ushuhuda wao; ambao hawakupenda maisha yao hata kufa. ''
Kumshinda shetani na mawakala zake kunahitaji Damu ya YESU KRISTO na Neno la MUNGU, Hivyo Neno binafsi analokupa MUNGU linaweza kubeba ushindi wako.

2. Kazi unayotakiwa uifanye.
Amosi 7:14-15 ''
Ndipo Amosii akajibu akamwambia Amazia, Mimi sikuwa nabii, wala sikuwa mwana wa nabii; bali nalikuwa mchungaji, na mtunza mikuyu; naye BWANA akanitwaa, katika kufuatana na kundi; BWANA akaniambia, Enenda uwatabirie watu wangu Israeli.''
Amos Hakujua kama anatakiwa kuwa mtumishi wa MUNGU hadi pale ambapo MUNGU alimpa Neno kwa kumwambia kwamba aende kuwatabiria watu wa MUNGU, Neno lilimpa kujua kazi yake aliyopangiwa na MUNGU.

3. Mtazamo sahihi unatakiwa kuwa nao au kuufuata.
2 Timotheo 3:16 ''
Kila andiko, lenye pumzi ya MUNGU, lafaa kwa mafundisho, na kwa kuwaonya watu makosa yao, na kwa kuwaongoza, na kwa kuwaadibisha katika haki;''
Neno la MUNGU limejaa mtazamo sahihi, ukipewa Neno na ROHO MTAKATIFU ujue hilo ndilo linakuelekeza mtazamo sahihi unaotakiwa kuwa nao.
 Waefeso 6:17 ''Tena ipokeeni chapeo ya wokovu, na upanga wa ROHO ambao ni neno la MUNGU;''

4. Nguvu za MUNGU za kukusaidia.
Yohana 15:3 ''
Ninyi mmekwisha kuwa safi kwa sababu ya lile neno nililowaambia.''
Neno linaweza kukufanya uwe safi kama ukilitii.
Neno la MUNGU pia linaumba ushindi wako.
 Zaburi 33:9 ''Maana Yeye alisema, ikawa; Na Yeye aliamuru, ikasimama.'' 
 
5. Kanuni za MUNGU unazotakiwa kuzifuata ili ufanikiwe.
1. Petro 2:2 ''
Kama watoto wachanga waliozaliwa sasa yatamanini maziwa ya akili yasiyoghoshiwa, ili kwa hayo mpate kuukulia wokovu; ''
Ziko kanuni nyingi sana unazotakiwa uzifuate na hizo utazipata kwenye Neno la MUNGU, Hata Neno binafsi unalopewa na MUNGU linaweza kubeba kanuni za kukusaidia kushinda. Mimi Neno la MUNGU lilinijulisha kufanya maombi ya kufunga.
 
6. Imani ya ushindi wako.
Warumi 10:17 ''
Basi imani, chanzo chake ni kusikia; na kusikia huja kwa neno la KRISTO.''
Kama imani chanzo chake ni kusikia basi hakika ukilisikia Neno la KRISTO la ufunuo unalopewa Binafsi na ROHO wa MUNGU hakika imani yako lazima iwe kubwa. Neno litakufanya uwe na imani kuu. 
Neno Binafsi unalopewa linaweza kubeba Julisho la wewe kupokea kutoka kwa MUNGU.

7. Msimamo ulio kwenye ulimwengu wa roho kuhusu wewe.
Sefania 1:1-2 ''
Neno la BWANA lililomjia Sefania, mwana wa Kushi, mwana wa Gedalia, mwana wa Amaria, mwana wa Hezekia; katika siku za Yosia, mwana wa Amoni, mfalme wa Yuda. Nitavikomesha kabisa vitu vyote, visionekane juu ya uso wa nchi, asema BWANA.''
Msimamo uliokuwepo kwenye ulimwengu wa roho ni kukomeshwa kwa vitu vyote, katika maombi yako unaweza kung'ang'nia jambo fulani kumbe jambo hilo liko kwenye adhabu ya MUNGU. Unaweza ukakesha bure, unaweza ukaomba sana kumbe inayohitajika ni toba na sio kinginecho.
 Yeremia 15:1 ''Ndipo BWANA akaniambia, Hata wangesimama mbele zangu Musa na Samweli, moyo wangu usingewaelekea watu hawa; watupe, watoke mbele za macho yangu, wakaende zao.''
Yeremia alikuwa anawaombea watu ambao MUNGU ameshawakataa hivyo Neno la MUNGU linamjia likionyesha msimamo uliopo katika ulimwengu wa roho, unaweza ukang'ang'ania vitu visivyo kwa sababu unapewa Neno lakini hufanyii kazi.
 1 Samweli 16:1 '' BWANA akamwambia Samweli, Hata lini utamlilia Sauli, ikiwa mimi nimemkataa asiwamiliki Israeli? Ijaze pembe yako mafuta, uende, nami nitakupeleka kwa Yese, Mbethlehemi; maana nimejipatia mfalme katika wanawe.''
Samweli alikuwa anamlilia Sauli na Neno la MUNGU likamjia likionyesha msimamo ulioko katika ulimwengu wa roho kwamba Sauli alishakataliwa siku nyingi ili asiwe Mfalme. Ingekuwaje Samweli angeendelea kufunga na kuomba kwa ajili ya Sauli ambaye alishakataliwa?
Angejichosha bure. Hivyo Neno binafsi linaweza kuonyesha msimamo ulioko katika ulimwengu wa roho wa nuru ambao wewe hutakiwi kwenda kinyume.

8. Ufahamu wa ki MUNGU wa kukusadia.
Mathayo 7:24-25 ''
Basi kila asikiaye hayo maneno yangu, na kuyafanya, atafananishwa na mtu mwenye akili, aliyejenga nyumba yake juu ya mwamba; mvua ikanyesha, mafuriko yakaja, pepo zikavuma, zikaipiga nyumba ile, isianguke; kwa maana misingi yake imewekwa juu ya mwamba.''
MUNGU akubariki sana kwa kunifuatilia tangu Mwanzo.

Natamani niseme mengi mno lakini naamini mwenye kuelewa ameelewa.
MUNGU akubariki kwa kujifunza somo hili muhimu pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane nitakujulisha jinsi ya kukipata.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.
0714252292.
0786719090
mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu.

Comments