UCHUMBA SUGU WA NINI?

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU

Bwana YESU atukuzwe ndugu yangu.
Nakuomba ndugu soma somo hili hadi mwisho.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.
Uchumba ni nini?
Uchumba ni mahusiano ya awali baina mwanamume na mwanamke ambao bado hawajaingia katika ndoa, wanakubaliana kuoana, na hivyo wanaanzisha mahusiano ya karibu yasiyohusisha Vitendo ya ndani ya ndoa.

Shetani amewavuruga wengi wanaojita wachumba, hata kama sifa za uchumba hawana, kwa sababu tu ya dhambi.

Yeremia 23:10 ''Maana nchi imejaa wazinzi; kwa sababu ya kuapa nchi inaomboleza; malisho ya nyikani yamekauka; mwenendo wao ni mbaya, na nguvu zao si za haki.''
Ni ukweli kwamba Uchumba ni hatua ya kuelekea katika ndoa lakini lakini sio kila wachumba wote wana mipango ya kuingia katika ndoa.
Mmoja anaweza kupanga kuingia katika ndoa lakini mchumba wake akawa hana mpango wa kuingia katika ndoa.
Kuna watu wana wachumba wa matazamio tu na sio kuoa/kuolewa.
Uchumba mwingine umeharibika kwa sababu ya uasherati na machukizo mengine.

 Kwa sababu hiyo uchumba sugu umeongezeka sana nyakati hizi.
Unakuta watu ni wachumba mwaka wa kwanza, mwaka wa pili, mwaka wa tano, mwaka wa saba mara mwaka wa kumi. Shetani anawajaribu wachumba hao na wanajikuta wanafanya dhambi ya uasherati, lakini uasherati huo wakati mwingine  unazaa mimba kisha mtoto
Kwa sababu bado ni wachumba basi mara mtoto wa pili mara mtoto wa tatu bado wakiwa wachumba tu.
Mara utasikia wachumba wale wameozesha mara wamepata wajukuu wakiwa bado ni wachumba tu. Mara wanakuwa wazee wakiwa bado ni wachumba. Huo ni uchumba sugu, maana watu hao hawakufunga ndoa takatifu Kanisani.

Nisamehe kama naumiza roho yako ila nataka upone katika jina la YESU KRISTO.
Ndugu zangu, Binafsi nimegundua kwamba uchumba wenye afya njema ya kiroho ni uchumba wa miezi 6 hadi mwaka mmoja kisha mnafunga ndoa, lakini uchumba wa miaka 7 au mitano sio uchumba mzuri.
Hayo yamezaa chumba sugu hadi watu wanajikuta wameozesha huku wakiwa bado wachumba.
Kumbuka ni heri kufunga ndoa kuliko kubaki wachumba harafu shetani akawanasa kwenye uzinifu.
Biblia inasema washerati na wazinzi sehemu yao ni katika ziwa la moto na sio mbinguni.
1 Kor 6:9 ''Au hamjui ya kuwa wadhalimu hawataurithi ufalme wa MUNGU? Msidanganyike; waasherati hawataurithi ufalme wa Mungu, wala waabudu sanamu, wala wazinzi, wala wafiraji, wala walawiti,''
Tuwe makini sana katika hilo ndugu zangu.

Ndugu mmoja mwanaumue alinusulika kuuawa baada ya kumchumbia binti mmoja na uchumba wao ukaa miaka mingi lakini baadae akavunja uchumba. Binti akabaki akihangika na kaka zake wakajaribu kumsaidia kwa kutaka kumuadabisha yule mwanaume. Chanzo kikuu cha uchumba kufa ni ngono na kuishi kama mke na mume kiasi kwamba kijana akawa hana mzigo tena roho wa kufunga ndoa, maana aliyotakiwa kuyapata akiwa kwenye ndoa anayapata sasa akiwa hayuko kwenye ndoa. Hata kwa leo ukichunguza sana katika wachumba ambao wamewahi kukutana kimwili utagundua kwamba wanawake walio kwenye uchumba wanataka sana wafunge ndoa lakini wanaume walio wengi walio katika uchumba hawako tayari kufunga ndoa, unadhani kwa nini?
1. Ni kwa sababu yale ambayo wangeyapata katika ndoa tu sasa wanayapata katika uchumba.
2. Hawana mzigo wala hamu ya  kufunga ndoa kwa sababu wameshajuana na wachumba wao kwa kila kitu, kiasi kwamba hata shetani kaingilia kati wanaona udhaifu mwingi kwa mabinti.
Waebrania 13:4 ''Ndoa na iheshimiwe na watu wote, na malazi yawe safi; kwa maana waasherati na wazinzi Mungu atawahukumia adhabu. ''
 
Ndugu zangu, Wakati mwingine kumjua mtu muongo katika uchumba ni rahisi sana.
Unakuta kijana au binti anatafuta mchumba kisha anasema ameshafunuliwa kwa ndoto zaidi ya Mara moja.
Baada ya kuwa wachumba utakuta watakaa katika uchumba miaka miwili au zaidi na ukiwauliza wanasema wanachunguzana.
Ndugu, kama ni MUNGU kweli amekupa na umethibitisha, je kuna kuchunguza nini tena? Unadhani MUNGU anaweza akakosea?
Kuna watu wako katika uchumba miaka 7 na wao ukiwauliza watakuambia walifunuliwa kuwapata wachumba hao ila bado wanawachunguza, kwa jambo la kuchunguza na unadai MUNGU amekupa huo ni uongo.

Yohana 8:44 ''Ninyi ni wa baba yenu, Ibilisi, na tamaa za baba yenu ndizo mpendazo kuzitenda. Yeye alikuwa mwuaji tangu mwanzo; wala hakusimama katika kweli, kwa kuwa hamna hiyo kweli ndani yake. Asemapo uongo, husema yaliyo yake mwenyewe; kwa sababu yeye ni mwongo, na baba wa huo.'' 
 
Wakati mwingine uchumba wa muda mrefu sana umekuwa kama silaha ya shetani kuwafanya watu watende dhambi ya uasherati na kujikuta hata wanapishana na kusudi la MUNGU.
Katika Biblia sijawahi kuona watu wa MUNGU wakikaa uchumba miaka mitano.
Isaka na Rebeka hawakukaa kwenye uchumba miaka 5, Musa na Sporah hawakukaa uchumba miaka 4.
Hata Elkana na Hana hatuoni wakikaa uchumba miaka 3
Daudi na Abigaili hawakukaa uchumba miaka 2.

Tukio la uchumba wa muda mrefu limetengeneza wakati mwingine kitu knachoitwa Boyfriend na Girlfriend huku wakiwa wanandoa wasio rasmi. Uchumba wa muda mrefu umegeuka hawara na buzi.
Kitaalamu wachumba wanatakiwa wakae kuanzia miezi 6 hadi mwaka wawe wamefunga ndoa, na muda huo wa uchumba wanaishi maisha matakatifu huku wakifanya maandalizi ya kufunga ndoa.
Nimewahi kuwasiliana na watu waliojeruhiwa moyo kwa sababu ya uchumba wa muda mrefu uliovunjika ukingoni.
Unakuta binti amekuwa kwenye uchumba miaka mitano, amawakataa wengi lakini mwaka wa tano wa uchumba wanaaachana maana ameruhusu ngono muda mrefu na kijana hana tena mzigo moyoni wa kumuoa.
Mbele ya kijana binti amekuwa kama gari lililochoka sana baada ya kulitumia miaka mingi.
Kijana mmoja alinipigia Simu akilia sana baada ya mchumba wake wa muda mrefu sana ametolewa mahali na kijana mwingine tajiri ambaye chanzo ni shinikizo la ndugu.
Ndugu Yangu, kuruhusu uasherati kunaweza kumfanya shetani hata akaamsha wazazi au ndugu kukukataa wewe ili usiolewe na kijana wao au usioe binti yao na ukaendelea kuteseka kumbe ni wewe uliyemfungulia hiyo shetani mlango.
Mko wachumba miaka 5, je mnasubiri nini kufunga ndoa?
Umeruhusu uzinifu ukitarajia kuingia katika ndoa?
Inawezekana uko katika kundi la aonywaye Mara nyingi
Mithali 29:1 " Aonywaye mara nyingi akishupaza shingo, Atavunjika ghafula, wala hapati dawa."



Ndugu, Mwenda pole hajikwai watu husema.
 Inawezekana ni kweli lakini kuna watu japo wapo kundi la mwenda pole wao hujikwaa.
Binti au kijana anaenda pole pole tena kwa pozi kabisa katika kuchagua mchumba lakini kwa sababu ameenda kimwili anapata mtu asiye sahihi.
Ndugu unahitaji kuenenda kwa ROHO MTAKATIFU na sio kwa akili na mitazamo yako binafsi.

Wagalatia 5:25 '' Tukiishi kwa ROHO, na tuenende kwa ROHO. ''
Shetani ni mjanja mjanja kama walio upande wake walivyo wajanja wajanja.
Binti mmoja aliwakataa vijana wacha MUNGU wengi waliotaka kumchumbia akisema hao sio type yake, baadae alikuja kutoka mbali aliyemuona kwamba huyo ndiye lakini ajabu kumbe ni tapeli maana ana mke wa watoto wawili.
Ndugu, unaweza kuwa mwenda pole na bado ukajikwaa kwa sababu tu unajitegemea pasipo MUNGU.
Dada mmoja aliahidiwa na kijana mmoja ambaye alikuwa Ulaya kwamba akirudi wataoana. Dada yule baada ya kuahidiwa hivyo akawa mkali na mtukanaji kwa kila kijana anayetaka kumchumbia. Dada yule alisema hataki mwanaume kutokea Tanzania Bali anamngoja Mtanzania safi anayetokea Ulaya.
Kijana mmoja aliona maono kwamba yule Dada ndiye anafaa kumchumbia, yule kijana alipojaribu kumwambia akakutana na mvua ya matusi, maono yake yakayeyuka. Baada ya miaka 4 baadae yule Dada akashtuka lakini akajipa moyo. Cha ajabu baada ya miaka 5 yule wa Ulaya akaja Tanzania akiwa na mke na mtoto, hapo ndipo mwenda pole akajikwaa.
Ndugu hakikisha unaishi maisha matakatifu na hakikisha unaenenda katika ROHO MTAKATIFU huku ukisikiliza watumishi wa MUNGU wanaoongozwa na ROHO MTAKATIFU.

2 Nyakati 20:20 ''.........  mwaminini BWANA, Mungu wenu, ndivyo mtakavyothibitika; waaminini manabii wake, ndivyo mtakavyofanikiwa.''

 Ndugu yangu, unayetarajia kuingia katika ndoa naomba ujue kwamba Watakatifu wapo sana lakini pia tukumbuke kwamba watakavitu wapo pia. Tuwaepuke watakavitu maana hao ni mapando ya giza.
Sio dhambi uchumba kukaa miaka yeyote ile ila dhambi ni kuruhusu dhambi wakati wa uchumba huo. Kwa uzoefu wangu ni kwamba uchumba wa muda mrefu ndio chanzo cha uasherati au dhambi ya kutamaniana kingono. Wengi wa walio katika uchumba wa muda mrefu sana kama hawajazini basi wametamaniana kingono au wamesalitiana. Kama hakuna hayo matatu katika uchumba wenu basi mko sahihi lakini usije ukamfundisha Mtu kukaa kwenye uchumba wa muda mrefu sana maana wengi hudanganyana na kusalitiana. unakuta binti anajua ana mchumba kumbe jamaa kashahamia kwingine muda sana. Biblia inasema "Usiyachochee mapenzi, hadi yatakapoona yenyewe" yaani hadi muda wa kufunga ndoa ufike.
Wimbo 3:5 ''Nawasihi, enyi binti za Yerusalemu, Kwa paa na kwa ayala wa porini, Msiyachochee mapenzi, wala kuyaamsha, Hata yatakapoona vema yenyewe. ''

Sasa jiulize Mfano vijana  wanachumbiana wakiwa na miaka 18 kisha wanapanga kufunga ndoa wakiwa na miaka 30. Baada ya hapo binti anafanikiwa kuendelea na masomo huku kijana akifeli, huko chuoni binti atakutana na wasomi wenzake huku kijana akiendelea kujipa moyo kwamba ana mchumba, ni mara chache sana watu wa aina hiyo kuoana. Vijana wanajaribiwa na mengi sana. Hakuna anayetaka kuoa asiye na kazi, hakuna anayetaka kuolewa na asiye na kazi nk. sasa kwa vigezo hivyo tu havitoshi kumfanya mmoja adhani alikosea kuchagua mwanzo? kwa kigezo hicho kijana hayatamwijia mawazo ya kwamba mwanzo alikurupuka kuchumbia?
Ni nadhani kila mwanaume au mwanamke asome au afanye aliyokusudia maishani mwake kisha muda wake wa kuolewa au wa kuoa ukifika basi ndipo achumbiwe au achumbiwe na baada ya mwaka mmoja afunge ndoa, hiyo nadhani ingepunguza matatizo katika baadhi ya mahusiano. Na tukumbuke kwamba Kibiblia hakuna Boyfriend wala girlfriend maana hayo yote ni mapando ya shetani kuwaharibia watu wa MUNGU.

1 Kor 6:18 '' Ikimbieni zinaa. Kila dhambi aitendayo mwanadamu ni nje ya mwili wake; ila yeye afanyaye zinaa hutenda dhambi juu ya mwili wake mwenyewe. ''
 
 Kinacho wafanya wachumba wengi kuanguka ni kuyachochea mapenzi kabla ya wakati wake, utakuta wanatumiana sms na za kuamsha hisia alafu kesho yake wakikutana wanaoneana hadi aibu na kusema BWANA asifiwe ila tayari ni wazinzi kwa mawazo. Bwana YESU anasema ''Mmesikia kwamba imenenwa, Usizini;
 lakini mimi nawaambia, Kila mtu atazamaye mwanamke kwa kumtamani, amekwisha kuzini naye moyoni mwake.-Mathayo 5:27-28''

Sasa kuna watu wamezini moyoni na wachumba wao kwa miaka mingi sana.
Kuna wadada wamezini moyoni mwao kwa sababu ya kutamani ngono na wachumba wao, kuna wakaka wamezini sana moyoni mwao wakitamani kufanya ngono na wachumba wao.
Ndugu, Biblia inasema kwako leo  '' Lakini ikiwa hawawezi kujizuia, na waoe; maana ni afadhali kuoa kuliko kuwaka tamaa.-1 Kor 7:9

 Achana na habari za wanaotumiana sms za kuamsha hisia za mapenzi , huo ni  uasherati tu

 Wakati mwingine tatizo ninaloliona  sasa hivi watu wengi wanashindwa kufunga ndoa kwa sababu ya kuangalia gharama za harusi na mashindano ya harusi na makomplication ya harusi. 
Watu wanatumia muda mrefu kuandaa harusi badala ya kauandaa ndoa takatifu. Yaani natamani kila vijana wanaotaka kuoana wakishafuata ataratibu zote za kiroho na kijamii wafunge ndoa na harusi simple tu. 
Hapo kanisani unanunua soda au juice mambo yanaendelea. Badala ya kukaa muda mrefu na kuwakwa na tamaa na baadae kuanguka kwenye dhambi.  Ndugu, angalia  upya nini bora harusi au ndoa. kuondoa uchumba sugu, kumbuka kuna jehanamu ya moto kwa waasherati.

Yakobo 4:4 '' Enyi wazinzi, hamjui ya kwamba kuwa rafiki wa dunia ni kuwa adui wa MUNGU? Basi kila atakaye kuwa rafiki wa dunia hujifanya kuwa adui wa MUNGU. ''


Kwa wewe uliyeokoka na unateswa na uchumba sugu nakuomba soma Neno la MUNGU hili, 1 Petro 2:20 ambapo Biblia inasema  '' Kwa maana wale waliokwisha kuyakimbia machafu ya dunia kwa kumjua Bwana na Mwokozi YESU KRISTO, kama wakinaswa tena na kushindwa, hali yao ya mwisho imekuwa mbaya kuliko ile ya kwanza.'
Ndugu, usikubali kunaswa.
Kumbuka ndoa itapita, mwenzi atapita lakini uzima wa Milele katika KRISTO haupiti, hivyo usikubali kujichafua.
Usikubali kuingia katika kundi la wazinzi na waasherati.

Natamani niseme mengi mno lakini naamini mwenye kuelewa ameelewa.
MUNGU akubariki kwa kujifunza somo hili muhimu pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane nitakujulisha jinsi ya kukipata.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.
0714252292.
0786719090
mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu.

Comments