UFANYE NINI UKIPATA MCHUMBA ILI UCHUMBA WENU USIISHIE NJIANI

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU

Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu zangu.
Karibu sana tujifunze Neno la MUNGU.
Kwanza ni kusudi la MUNGU wewe kijana ufunge ndoa takatifu yaani uwe na mke wako mwenyewe, na ni kusudi la MUNGU wewe dada ufunge ndoa takatifu yaani uwe na mume wako mwenye.
1 Kor 7:2  '' Lakini kwa sababu ya zinaa kila mwanamume na awe na mke wake mwenyewe, na kila mwanamke na awe na mume wake mwenyewe.''
Ni mara nyingi sana nimewasiliana na watu ambao wameumizwa katika uchumba kwa sababu ya uchumba kuvunjika kabla ya ndoa kufika.
Kuna binti alishaachwa na wachumba zaidi ya watano, kuna kijana alishaachwa na wachumba watatu.
Kuna ndugu uchumba wake ulivunjika wiki moja kabla ya ndoa.
Ni mambo mengi sana yanayosababisha uchumba kuvunjika.
Kwa uzoefu wangu mimi Peter nimegundua kwamba uchumba mwingi huvunjika;
A.  Kwa sababu ya tabia mbaya zinazojitokeza wakati wa uchumba
B.  Kwa sababu ya Mtu kudhani hakuchagua mtu sahihi
C.  Kwa sababu ya Kuruhusu uasherati
D.  Kwa sababu ya Vifungo vya giza na maagano ya kipepo
E.  Kwa sababu ya Tamaa mbaya.
F.   Kwa sababu ya Kukosa hofu ya MUNGU.
G.  Kwa sababu ya Ushauri mbaya
Sasa kuna watu pia ambao wametulia na wana Mcha MUNGU kabisa tena wameokolewa kwa damu ya YESU KRISTO ya agano la milele. Lakini uchumba huvunjika na kuacha maumivu, nimeshafundisha masomo mengi kuhusu uchumba na kuhusu ndoa, leo napata msukumo wa kukufundisha mambo saba ya kufanya ili uchumba wako usivunjike tena bali ufikie katika ndoa takatifu ya amani na furaha.

Ufanye nini ukipata Mchumba ili uchumba wenu usiishie njiani?

1. Uwe na kiasi.

2 Petro 1:5-8 '' Naam, na kwa sababu iyo hiyo mkijitahidi sana kwa upande wenu, katika imani yenu tieni na wema, na katika wema wenu maarifa,  na katika maarifa yenu kiasi, na katika kiasi chenu saburi, na katika saburi yenu utauwa,  na katika utauwa wenu upendano wa ndugu, na katika upendano wa ndugu, upendo.  Maana mambo hayo yakiwa kwenu na kujaa tele, yawafanya ninyi kuwa si wavivu wala si watu wasio na matunda, kwa kumjua Bwana wetu YESU KRISTO.''

Biblia inasema kwamba ''
Naam, na kwa sababu iyo hiyo mkijitahidi sana kwa upande wenu ...  na katika maarifa yenu kiasi''
Ukikosa kiasi kwa mchumba wako unageuka mzigo hivyo kuachwa ni rahisi sana.
Kiasi kinachozungumzwa sio dhambi ya aina yeyote, dhambi ni dhambi tu na hiyo haiusiki na kiasi ila Biblia inakushauri kwamba katika maarifa yako uwe na kiasi. Kwanza kiasi ni tunda kabisa la ROHO MTAKATIFU.
Kaka mmoja aliniambia kwamba amwemwacha Mchumba wake kwa sababu hana kiasi, yaani uchumba una mwezi mmoja tu lakini amechatumia zaidi ya laki moja kumpa yule binti. Binti mara anataka pesa ya saluni mara kuna gauni mpya kaiona.
Kwanza kwa wachumba haifai  kuhudumiana kama kwamba ni mke na mume. Ulipokuwa hujampata huyo Mchumba ulikuwa unahudumiwa na nani? Hilo tu linaweza kumfanya mchumba wako akawa na mawazo tele na kukuacha, kumbe ni kwa sababu huna kiasi. Kumbuka pia kuna watu hawapendi sana kuongea na kuna watu hawapendi sana kuongea muda mrefu kwenye simu, sasa kwa kukosa kwako kiasi kijana au binti unaweza kuachwa kwa sababu huna kiasi. Mara saa tano usiku unapiga simu, mara saa nane usiku unapiga simu, mara saa tisa usiku unabip. Kwa jinsi hiyo na mambo mengine mengi yanayokuonyesha huna kiasi hakika unaweza ukaachwa na Mchumba wako hata kama ulifunga na kuomba sana ili kumpata.
Kuna wengine baada tu ya kumpata mchumba basi anabadilika, alikuwa havai wigi sasa anavaa wigi, ndugu unaweza ukaachwa kwa sababu ya mambo ya ajabu ambayo unazalisha baada ya kupata mchumba. Kama alikupenda kwa sababu ya ulivyokuwa, kwanini kuongeza asiyoyahitaji? na ambayo ni machukizo kwa MUNGU?
Kukosa kiasi kunaweza kukufanya uwe unaweka tu records za kuachwa na wachumba huku ukidhani una mkosi, kumbe huna kiasi.
2 Timotheo 4:5A '' Bali wewe, uwe na kiasi katika mambo yote,  ''

2.  Mpe Uhuru Mchumba wako, Usimgande kwenye maisha yake.

1 Kor 15:34 '' Tumieni akili kama ipasavyo, wala msitende dhambi; kwa maana wengine hawamjui MUNGU. Ninanena hayo niwafedheheshe. ''
Ninaposema umpe uhuru mchumba wako sina maana ya umpe uhuru kwenye mwili wako au kwenye maisha yako, hiyo ni dhambi, bali nina maana umpe uhuru katika maisha yake.
Kuna watu baada tu ya kuwa wachumba mmoja katika uchumba huo anaanza kuganda mwenzake na kugeuka kero kubwa sana inayoweza kuvunja uchumba.
Kila mra aunamuuliza uko wapi? uko na nani? na kwa nini
Akitumia pesa wazazi wake tu na wewe unataka ujue na unataka umlaumu kwanini hakukushirikisha.
Yuko Kanisani unamsumbua sana, akizima tu simu kwa sababu yuko ibadani wewe baadae unawaka na kumuondolea uhuru wake.
Kuna watu hugeuka kama Mfungwa aliyekamatwa na askari, kiasi kwamba kila jambo na kila sehemu anayotaka kwenda Mchumba wake basi lazima ajue na aamue yeye. Ndugu, ulimkuta na maisha yake na ukampenda kama alivyo kwanini sasa katika uchumba wa mwezi mmoja tu unamfanya aone unamnyima uhuru wake hata anataka kukuacha?
Uwe na akili na uwe makini. Mimi naamini kama ni mtu mzinifu na hakika usingetaka kuingia uchumba naye, sasa kama ni Mteule wa MUNGU na ni Mcha MUNGU mbona unamnyima uhuru wake katika maisha yake? Ndugu, unaweza ukaachwa dakika yeyote kwa sababu ya jambo hilo tu.
Hakikisha unampa uhuru Mchumba wako katika maisha yake, usijifanye mwalimu kwake wakati huu wakati amekutana na wewe akiwa na miaka 30. Usijifanye dereva wa maisha yake wakati hadi wewe unamuona alikuwa mtu mzima kabisa.
Ukipata Mchumba hakikisha unampa uhuru katika maisha yake ya siku zote. Mshauri tu kwa kiasi ili aendelee kumtumikia Bwana YESU na aendelee kumcha MUNGU.

3. Lengo la uchumba wenu liwe kufunga ndoa na sio vinginevyo.

Mwanzo 2:24 '' Kwa hiyo mwanamume atamwacha baba yake na mama yake naye ataambatana na mkewe, nao watakuwa mwili mmoja.'
 Lengo la MUNGU tangu zamani kwa wachumba ni kufunga ndoa na sio vinginevyo.
Kuna  watu wana wachumba kwa sababu marafiki zao wana wachumba.
Leo kuna wachumba wako hivyo kwa sababu za kupimana tu na sio kufunga ndoa.
Ndugu, mmoja ni Mwanafunzi wa Sekondari aliniambia nimuombee ili apate mchumba na watafunga ndoa akimaliza chuo kikuu, nilishtuka kwa sababu kutoka sekondari hadi chuo kikuu inaweza ikachukua miaka 7.
Ni heri mtu akasoma, akatafuta kazi au akafanya biashara yake na muda wake wa kuoa au kuolewa ukifika basi atafute Mchumba  ili ndani ya mwaka afunge ndoa.
Ndugu usiingine katika uchumba kwa lengo la dhambi ya uasherati, hapo utakosea sana na unaweza kupishana na kusudi la MUNGU.
Usiingie kwenye uchumba ili kuwafurahisha ndugu zako au marafiki zako, ingia katika uchumba kwa lengo la kufunga ndoa na fanyia kazi hilo.
Sasa jiulize umefunga na kuomba ili upate Mchumba na ukimpata anakuambia kwamba anampango wa kuingia katika ndoa miaka minne ijayo, hilo ni tatizo kubwa.
Wewe ndugu ukipata Mchumba hakikisha unamwelekeza na kumshauri kufunga ndoa na sio vinginevyo. 
Kuna wengine baada ya kuwa wachumba wanataka wajenge nyumba kwanza, shetani akijua hilo anashikilia uchumi kiasi kwamba baada ya muda watageuka wazinifu na sio wachumba.
Ndugu, ukipata Mchumba hatua ya kwanza kabisa ya mazungmzo yenu ni heri akuweke wazi kwamba ''ndoa ni lini''. Unaweza ukawakataa walio tayari kufunga ndoa na wewe mwaka mmoja ujao lakini wewe unang'ang'ania Mchumba ambaye hana hata mpango wa kufunga ndoa na wewe.
Kama kuna eneo la kuwa makini sana basi ni eneo la uchumba.
Unaweza ukafurahia kuwa na Mchumba na kumbe ndugu huyo ana mpango wa kuingia katika ndoa miaka mitano ijayo.
Kama Mchumba wako na mpango wa muda mrefu sana wa uchumba ni heri kuachana naye maana unaweza kuja kujikuta unasema ''Nimekusamehe lakini sitkusahau'' Muda unakuwa umeshapita sana.

 4. Uwe na msimamo thabiti wa wokovu.

Waefeso 6:14 '' Basi simameni, hali mmejifunga kweli viunoni, na kuvaa dirii ya haki kifuani,''
Kweli ya MUNGU ni Neno la KRISTO na Neno hilo litakuweka huru.
Kuna mtu akipata mchumba tu baada ya muda yule mchumba anaanza kujiuliza'' Huyu ndiye yule mtumishi? Huyu ndiye yule Mwimbaji? Huyu ndiye kiongozi wa idara kanisani?''
 Wengi sana wameachwa baada ya kuonekana hawajasimama vizuri kwa MUNGU.
Hakuna mtu anayetaka kuingia katika ndoa na mpagani.
Hakuna mtu anayetaka kuingia katika ndoa na mtu asiye Mcha MUNGU.
Inawezekana Mchumba wako alikufuata kwa sababu aliona wewe ni Mcha MUNGU mzuri, sasa akiona huna Msimano kwa YESU anaweza akakuacha mapema sana.
Dada mmoja wa kanisa   alipata Mchumba na baada ya muda Mchumba wake akamwambia kwamba 'Wafanye mapenzi kwanza ndipo waoane'' Yule dada akasema ''hakuna tatizo'' na uchumba ukafa siku hiyo hiyo. Yule kama alikuwa Mtumishi wa MUNGU na alikuwa anampima tu yule dada na akagundua kwamba yule dada hana hofu ya MUNGU maana yuko tayari kufanya uasherati ili aolewe.
Ndugu, sio vizuri kumwingiza mwenzako majaribuni lakini sio vizuri na ni haramu kabisaaaa kukubali kuukana Wokovu kwa sababu ya kutaka ndoa.
Wengi wanaachwa na wachumba wao maana huonekana kwamba hawana hofu ya MUNGU na wako tayari kuukana wokovu kwa sababu ya uchumba.
Ndugu, baki na msimamo wako kwa YESU haijalishi Mchumba anataka kukuacha kwa sababu umekataa dhambi.
Msimamo wako kwa YESU una thamani kuliko wanadamu wote akiwemo Mchumba wako. Kwenye masuala ya dhambi mkatalie live na muonye kabisa maana YESU ni bora kwako kuliko Mchumba.

5. Uwe na heshima na hekima katika kuvaa, kuongea na kuishi na watu.

Mithali 11:16a '' Mwanamke wa adabu huheshimiwa daima;''
Adabu ni tabia njema, tabia njema anatakiwa kuwa nayo mwanamke na mwanaume pia.
Hii nayo ni moja ya changamoto kubwa zaidi.
Unaweza ukawa unawasema vibaya wasichana wenzako mbele ya mchumba wako na akawapenda wao kuliko wewe mtoa siri.
Unaweza ukawa unawasema vibaya sana wavulana wenzako mbele ya Mchumba wako na yeye akawaona wao wanafaa zaidi kuliko wewe.
Ukipata Mchumba hakikisha unaendeleza heshima na hekima katika kuongea,  kuishi  na watu na katika mavazi.
Mchumba wako akigundua kwamba wewe ni muongo muongo anaweza kukuacha.
Mchumba wako akigundua kwamba wewe ni msingiziaji au wewe ni mtu wa matusi anaweza kukuacha.
Kumbuka Mchumba wako ataulizia habari zako kwa watu wako wa karibu au majirani, sasa kama unaishi vibaya na watu hakika unaweza kuachwa maana ukweli wako ukijulikana kwa Mchumba wako hakika ni hatari kwako.
Kumbuka pia alikupenda jinsi ulivyokuwa hivyo hakuna haja ya kuanza kuvaa vimini n.k ambavyo ni machukizo.
Uwe na heshima na hekima katika kuvaa, kuongea na kuishi na watu ili uchumba wako usiishie njiani, hiyo ni muhimu sana kwako.

 6. Usiruhusu kufanya mapenzi kabla ya ndoa.

Kumb 5:18 '' Wala usizini.''

Hili ndilo janga namba moja linalosababisha chumba nyingi kuvunjika kabla ya ndoa.
Kufanya uasherati ni kuzini, ni dhambi na ni machukizo kwa MUNGU.
Uasherati humvuta shetani kuwafunga vifungo, kuwaonea na kuua uchumba wetu.
Shetani anakuletea mawazo ya ngono ili akuharibie uchumba wako.
Wachumba Wengi baada tu ya kuruhusu ngono ndipo walipoonekana hawafai kwa wachumba wao.
Wachumba Wengi baada ya kuruhusu ngono ndipo mtu anasema '' Nilikosea kuchagua''
Wachumba Wengi baada tu ya kuruhusu dhambi ya uasherati  ndipo mtu anasema ''Sikuonyesha''
Wachumba Wengi baada tu ya kuruhusu dhambi ya uasherati  ndipo utasikia mmoja anasema ''Wewe sio type yangu''
Wachumba Wengi baada tu ya kuruhusu dhambi ya uasherati  ndipo utasikia anasema ''Heri nirudi kwa yule wa kwanza niliyemwacha''
 Wachumba Wengi baada tu ya kuruhusu dhambi ya uasherati  ndipo utasikia ''Mama na Baba wamenikataza nisifunge ndoa na wewe''
 Wachumba Wengi baada tu ya kuruhusu dhambi ya uasherati  ndipo utasikia ''Mimi sina mpango wa kuingia kwenye ndoa kwa sasa''
 Wachumba Wengi baada tu ya kuruhusu dhambi ya uasherati  ndipo utasikia mmoja anasema ''Ngoja nifikie kwanza kama kweli wewe ni kusudi la MUNGU''
Ndugu, hakuna kusudi la MUNGU kwenye dhambi.
Kwanini inakuwa hivyo baada ya kuruhusu dhambi?
Ni kwa sababu shetani anakuwa anawamiliki na kuanza kuwatesa na kuwataabisha maana ni ninyi mlimfungulia mlango kwa tendo la uasherati.
Hata walio katika ndoa zao wengi wanaishi kwa migogoro kwa sababu ya mapando ya dhambi aliyoyapanda shetani wakati wa uchumba.
Ndugu mmoja baada ya mimi Peter kufundisha somo la vyanzo vya migogoro katika ndoa alinitukana sana live mtandaoni akisema sina akili na sijui lolote kuhusu ndoa, nilichogundua ni kwamba ndugu yule yuko katika vita kubwa kwenye ndoa yake kwa sababu aliruhusu dhambi ya uasherati na hakuitubia dhambi hiyo maana kwa maneno yake ya hasira alikiri kwamba ni kweli katika uchumba alifanya uasherati na uchumba wake lakini katika ndoa Mke wake ndio kabadilika.
Ndugu zangu, kuruhusu uasherati katika uchumba ni jambo baya sana sana.

 7. Omba sana kwa MUNGU.

Mathayo 7:7 '' Ombeni, nanyi mtapewa; tafuteni, nanyi mtaona; bisheni, nanyi mtafunguliwa; ''
 Watu wengi sana akipata Mchumba huacha maombi akidhani kazi imeisha.
Kuna watu akipata mchumba  hata kwenye ibada za mikesha na maombi haendi tena.
Watu wengine akishathibitisha kwamba amepewa Mchumba na MUNGU hudhani vita haiwezib kuwepo.
Ndugu yangu, huko ni kujidanganya sana.
Hakikisha unakuwa mtu wa maombi.
Ngoja nikupe mbinu 5 za maombe za wewe Mteule wa KRISTO uliye katika uchumba na unatarajia kufunga ndoa.

Ombea mambo haya matano.

A. Ombea uchumba wako.
 Uchumba unaweza ukazikwa kipepo na mawakala wa shetani wanaoshirikiana na watu wabaya kwako au kwa mchumba wako, usipoomba uchumba unaweza kuvunjika kabla ya ndoa kwa sababu ya nguvu za kishetani. Watu wazushi na wasiokutakia mema wanaweza kusema mabaya kukuhusu wewe mbele ya Mchumba wako na ukaachwa.

B. Muombee Mchumba wako na maisha yake.
 Muombee Mchumba wako ili asitekwe kipepo na mtu mwingine au na fundisho lingine.

C. Jiombee wewe mwenyewe kama sehemu ya uchumba na ombea maisha yako.
 Jiombee wewe ili usivamiwe na nguvu za giza au mipango mingine, nimewahi kushuhudia mabinti watatu ndio wanavunja uchumba wiki moja kabla ya ndoa na wakiulizwa wanasema hawataki tu kuolewa, kumbe fahamu zao zimevamiwa kipepo na hawaoni tena thamani ya ndoa.

D. Ombea watumishi wa MUNGU Kanisani kwako na kanisani kwa Mchumba wako na ombea Mtumishi wa MUNGU atakayewafungisha ndoa.

Kuna Uchumba Mwingi umevunjika kwa sababu ya watumishi wa MUNGU. 
Kijana mmoja ambaye ni mtumishi kabisa wa MUNGU aliyeokoka alikataliwa kanisani kwa binti na kulazimishwa kwamba aanze kufundishwa ubatizo na abatizwe pale, wakati ameshabatizwa zaidi ya miaka 7 iliyopita na ni shemasi kanisani kwao.
Kuna watumishi hudhani kwamba ni wao tu ndio watumishi sahihi wa MUNGU hivyo anaweza akamkataa Mchumba wako na kuzuia ndoa hiyo. 
Hata Mchungaji wako anaweza kugeuka kikwazo cha wewe kufunga ndoa, ombea sana mambo hayo kabla ya ndoa.
Kuna Wachungaji wana mashariti magumu ambayo wala Biblia haiagizi popote, ombea sana jambo hilo.
Hata Mfungisha ndoa anaweza akapata dharula kila siku hadi ndoa isifungwe kwa muda sahihi.

E. Ombea wazazi pande zote mbili.
Wazazi pia wanaweza hata wakatumika vibaya ili kukuzuilia usifunge ndoa na Mchumba wako, wazazi wako wanaweza kumkataa Mchumba wako, wanaweza kutaja mahali kubwa ili asiweze kutoa. Ndugu zako wanaweza wakamkosoa Mchumba wako na kukulazimisha umwache maana sio type yako wakati wao wanaangalia umbo lakini MUNGU anaangalia roho iliyopondeka.
Hayo maeneo husika nayo sana katika maombi maana shetani anaweza akaona amekushindwa wewe lakini akawatumia wanaokuhusu hadi Mchumba wako akashindwa kuvumilia na kuvunja uchumba.
Omba sana wala usiache, Mche MUNGU na Mtumikie Bwana YESU utaitwa heri.

 Natamani niseme mengi mno lakini naamini mwenye kuelewa ameelewa.
MUNGU akubariki kwa kujifunza somo hili muhimu pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane nitakujulisha jinsi ya kukipata.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.
0714252292.
0786719090
mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu.


Comments