USIKATE TAMAA MTEULE WA KRISTO.

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.
Bwana YESU atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.
Kuwa Mteule wa MUNGU ni kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi kisha unaanza kuishi maisha matakatifu yanayoagizwa na Neno la MUNGU.
Uhai tulionao sasa sisi wateule , tunao katika Mwokozi wetu YESU KRISTO, aliyetupenda akatuokoa na kutupa uzima.
Wagalatia 2:20 " Nimesulibiwa pamoja na KRISTO; lakini ni hai; wala si mimi tena, bali KRISTO yu hai ndani yangu; na uhai nilio nao sasa katika mwili, ninao katika imani ya Mwana wa MUNGU, ambaye alinipenda, akajitoa nafsi yake kwa ajili yangu."
Mteule tembea kwa kujiamini.
Kataa tu dhambi na mambo ya dunia yaliyo Machukizo kwa MUNGU.
Uhai wako umetunzwa na MUNGU katika KRISTO.
Wewe ni mshindi na maisha yako yanatakiwa kudhibitisha ushindi shidi ya kila nfuvu za giza.


Mambo 2 muhimu sana kuzingatia baada ya kumpokea YESU ni haya.

 1. Bila utakatifu huwezi kumwona MUNGU
Mathayo 5:8 ''Heri wenye moyo safi; Maana hao watamwona Mungu.''   

2. Bila imani huwezi kumpendeza MUNGU.
Waebrania  11:6 '' Lakini pasipo imani haiwezekani kumpendeza; kwa maana mtu amwendeaye MUNGU lazima aamini kwamba yeye yuko, na kwamba huwapa thawabu wale wamtafutao.''

Katika maisha yako inawezekana ukakutana na changamoto za muda mfupi lakini  kukata tamaa ni marufuku kwa mteule wa KRISTO aliyeshiba Neno la MUNGU.
Ukiona unakataa tamaa tambua kwamba unaathiriwa na yafuatayo.
1. Unafanya dhambi kwa siri.
Zaburi 34:14 ''Uache mabaya ukatende mema, Utafute amani ukaifuatie. '' 
 
2. Umepungukiwa maombi.
1 Thesalonike 5:17 '' ombeni bila kukoma; ''
 
3. Husomi Neno la MUNGU wala kulitafakari.
Yoshua 1:8 ''Kitabu hiki cha torati kisiondoke kinywani mwako, bali yatafakari maneno yake mchana na usiku, upate kuangalia kutenda sawasawa na maneno yote yaliyoandikwa humo; maana ndipo utakapoifanikisha njia yako, kisha ndipo utakapositawi sana.'' 
 
4. Unategemea wanadamu sasa na sio kumtegemea MUNGU.
Yeremia 17:5-6 '' BWANA asema hivi, Amelaaniwa mtu yule amtegemeaye mwanadamu, Amfanyaye mwanadamu kuwa kinga yake Na moyoni mwake amemwacha BWANA.  Maana atakuwa kama fukara nyikani, Hataona yatakapotokea mema; Bali atakaa jangwani palipo ukame, Katika nchi ya chumvi isiyokaliwa na watu.'' 
 
5. Huhudhulii ibada kwa wingi kanisani.
Waebrania 10:25 ''wala tusiache kukusanyika pamoja, kama ilivyo desturi ya wengine; bali tuonyane; na kuzidi kufanya hivyo, kwa kadiri mwonavyo siku ile kuwa inakaribia.'' 
 
6. Huenendi kwa ROHO MTAKATIFU.
Wagalatia 5:16 '' Basi nasema, Enendeni kwa ROHO, wala hamtazitimiza kamwe tamaa za mwili.''
 
7. Humjui MUNGU na mpango wake kwako.
Yeremia 29:11-13 '' Maana nayajua mawazo ninayowawazia ninyi, asema BWANA, ni mawazo ya amani wala si ya mabaya, kuwapa ninyi tumaini siku zenu za mwisho. Nanyi mtaniita, mtakwenda na kuniomba, nami nitawasikiliza. Nanyi mtanitafuta na kuniona, mtakaponitafuta kwa moyo wenu wote. ''


Ukiwa kama Mteule wa MUNGU inahitajika bidii katika maisha yako.
1. Bidii ya kumtumikia MUNGU.
 Bidii yako katika kumtumikia Bwana YESU itakufanya ulindwe na MUNGU siku zote.

2. Bidii ya maombi na kumtafuta MUNGU.
 Kitu kimoja muhimu katika kukufanya ufaulu ni Bidii ya maombi.
Bidii ya maombi itakufanya ushinde kila jambo katika ulimwengu wa roho na kisha kudhihilika katika ulimwengu wa mwili.


3. Bidii ya kufanya kazi zako.
Bidii yako katika kazi yako njema aliyokubariki MUNGU itakuwa mlango wa MUNGU kukubariki katika maisha yako.
 

4. Bidii ya kusoma Neno la MUNGU na kulitafakari.
Bidii yako katika kusoma Neno la MUNGU na kulitafakari itakupa nguvu za kiroho na maarifa sahihi ya kiroho na kwa maarifa hayo shetani ataogopa hata kukusogelea.
5. Bidii katika ibada.
Bidii yako katika ibada na utakatifu itakupa kushinda dunia yote.


2 Petro 3:13-14 '' Lakini, kama ilivyo ahadi yake, mnatazamia mbingu mpya na nchi mpya, ambayo haki yakaa ndani yake.
Kwa hiyo, wapenzi, kwa kuwa mnatazamia mambo hayo, FANYENI BIDII ili mwonekane katika amani kuwa hamna mawaa wala aibu mbele yake.''

Tunahitaji kuwa na bidii hata ya kuwasaidia wengine ili wamche MUNGU.
 ''Ndugu zangu, ikiwa mtu wa kwenu amepotelea mbali na kweli, na mtu mwingine akamrejeza; jueni ya kuwa yeye amrejezaye mwenye dhambi hata atoke katika njia ya upotevu, ataokoa roho na mauti, na kufunika wingi wa dhambi.-Yakobo 5:19-20

 Ndugu, Kaa katika kambi ya Waebrania siku zote, na sio kukaa katika kambi ya wafilisti.
 Kaa katika kambi ya wateule wa KRISTO.

Jambo lingine muhimu sana  nataka Mteule ujue ni hili.
Usije ukafanikiwa kiuchumi ukamsahau MUNGU.
Usije ukafanikiwa kikazi ukamsahau MUNGU.
Usije ukafanikiwa kibiashara ukamsahau Bwana YESU.
Kumb 8:12-14 '' Angalia, utakapokuwa umekula na kushiba, na kujenga nyumba nzuri na kukaa ndani yake; na makundi yako ya ng'ombe na kondoo yatakapoongezeka, na fedha yako na dhahabu yako itakapoongezeka, na kila kitu ulicho nacho kitakapoongezeka; basi hapo moyo wako usiinuke, ukamsahau BWANA, Mungu wako, aliyekutoa katika nchi ya Misri, katika nyumba ya utumwa;'' 
Misri ni kwa shetani, ni kipindi hujaokoka, ni kipindi unateswa na nguvu za giza na laana.
Usije ukafanikiwa kielimu ukamsahau Bwana YESU.
Usikiache kitu cha thamani sana ambacho MUNGU alikupa.
Ndugu, Wokovu wa KRISTO ndio kitu cha thamani sana ambacho MUNGU alikupa.
Usikubali hadhi yako kwa wanadamu ikakufanya ukaacha Wokovu.

Inawezekana wewe bado uko katika vifungo kwa sababu hujasimama imara kwa YESU, ndugu, Kumbuka kwamba utafunguliwa kulingana na unavyomwamini Bwana YESU.
Utapona kulingana na unavyomwamini Bwana YESU.
Utapokea ushindi kulingana na kiwango chako cha kuamini.

Kiwango chako cha kuamini ndio pia kipimo chako cha kupokea.
Kaa kwenye neema ya KRISTO, Kumbuka neema ya MUNGU haitegemei ufahamu wako.
Neema ya MUNGU haitegemei akili zako.
Neema ya MUNGU haitegemei elimu yako.
Neema ya MUNGU inategemea moyo wenye utayari, utii kwa MUNGU na kumtafuta MUNGU.
Mathayo 6:33 " Bali utafuteni kwanza ufalme wake, na haki yake; na hayo yote mtazidishiwa."
Neema ya MUNGU ina YESU KRISTO.
Utafute kwanza ufalme wa MUNGU.
Neema ni kustahilishwa na kusaidiwa kupata ushindi ambao haukuustahili.


Natamani niseme mengi mno lakini naamini mwenye kuelewa ameelewa.
MUNGU akubariki kwa kujifunza somo hili muhimu pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane nitakujulisha jinsi ya kukipata.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.
0714252292.
0786719090
mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu
.

Comments