HAKIKISHA KUANZIA SASA UNAISHI MAISHA MATAKATIFU KATIKA KRISTO.

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU

Bwana YESU KRISTO atukuzwe.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.
Ndugu zangu wote nawaombeni sana, tena sana kwamba tujitahidi sana kuishi maisha matakatifu katika KRISTO YESU. 
Mwisho wa kila mwenye mwili mtenda dhambi upo na siku ya mwisho ipo. 
Zamani za Nuru MUNGU alisema   '' Mwisho wa kila mwenye mwili umekuja mbele zangu; kwa sababu wameijaza dunia dhuluma, basi nitawaharibu pamoja na dunia.-Mwanzo 6:13''
Na hakika MUNGU akawaangamiza waovu wote, na hata sasa upo mwisho mbaya sana kwa watenda dhambi.
  ''Kwa maana mshahara wa dhambi ni mauti; bali karama ya MUNGU ni uzima wa milele katika KRISTO YESU BWANA  wetu.-Warumi 6:23''
Upo mwisho wa kutisha kwa wanaomkataa YESU KRISTO kama Mwokozi wao.
Na hadi naandika huu ujumbe najua nisemalo na nimeona kwa macho kwamba ni hatari kama wewe unaendekeza dhambi na uovu.
Inawezekana unajitahidi sana kutengeneza maisha yako ya duniani, ni sawa kabisa lakini ni muhimu kujua kwamba hata maisha yako ya milele wa kuyatengeneza ni wewe na muda wa kuyatengeneza ni sasa, ninajua nilisemalo ndugu zangu.
Nisipokuambia maumivu yangu rohoni hayatatoka, ila nikikuambia ndipo nakuwa nimetua mzigo mzigo, na mzigo huo nimekupatia wewe kwamba okoka kwa upya na mche MUNGU. Ukipenda kuutupa mzigo huo niliokubebesha kupitia ujumbe huu, unaweza, na ukiubeba na ukachukua hatua ya kumpokea YESU KRISTO kwa upya na ukaacha dhambi hata upate uzima wa milele, unaweza pia.
Nimesema katika ROHO wa MUNGU hivyo uamuzi ni wako. YESU anakungoja Leo ili usiende jehanamu, maamuzi unayo wewe na moyo wako, najua nilisemalo.

1 Petro 4:7 "Lakini mwisho wa mambo yote umekaribia; basi, iweni na akili, mkeshe katika sala."

Ndugu yangu mpendwa, hakika mbingu zitafurahi ukifanyia kazi ujumbe huu kwa kuokoka kisawasawa.
Kumbuka ndugu yangu hii.
Waebrania 9:27 " Na kama vile watu wanavyowekewa kufa mara moja, na baada ya kufa hukumu;"


Kifo kipo, je wewe ukifa utaenda wapi?
Baada ya kifo ni hukumu.
Je ukifa utaenda mbinguni au wewe utaenda kuzimu ukingoja ziwa la moto?, najua nilisemalo ndio maana nakushauri muda huu kwamba mpokee YESU KRISTO kwa upya na anza sasa kuishi maisha matakatifu.


Mathayo 13:49-51 ''Ndivyo itakavyokuwa katika mwisho wa dunia; malaika watatokea, watawatenga waovu mbali na wenye haki, na kuwatupa katika tanuru ya moto; ndiko kutakuwako kilio na kusaga meno. YESU aliwauliza, Mmeyafahamu hayo yote? Wakamwambia, Naam.''
  Inawezekana mwaka huu unaishi kwa sababu umepewa offer na MUNGU ili utengeneze njia zako.
Mtii MUNGU Leo kupitia Neno hili.
Dunia isikupoteze ndugu.
Kumbuka uzima wa milele sio wa ukoo na wala sio wa familia Bali ni wa mtu binafsi.
Uzima wa milele sio wa dhehebu Bali ni wa mtu binafsi, najua nilisemalo.


Warumi 6:23 '' Kwa maana mshahara wa dhambi ni mauti; bali karama ya MUNGU ni uzima wa milele katika KRISTO YESU  Bwana wetu.''

Namshukuru MUNGU maana nimesema alichoniambia.


Kama wewe umeokoka na unaishi maisha matakatifu nakuomba nisikilize katika haya.
Mteule jipe moyo maana Mwokozi wetu YESU KRISTO yu Karibu kuja kutuchukia.
Jipe moyo ndugu yangu unayeishi maisha matakatifu ya wokovu maana MUNGU wetu yu karibu kuja kutuchukua.
Wakati huo mateso yatakoma, kujeruhiwa moyo kutaisha, magonjwa yatakoma na misiba itakoma.
Ng'ang'ana na YESU ndugu.
Tusonge mbele na KRISTO ili tumalize safari yetu salama.
Usikubali kufia jangwani wala usikubali kutekwa na dunia

Isaya 35:8 "Na hapo patakuwa na njia kuu, na njia, nayo itaitwa, Njia ya utakatifu; wasio safi hawatapita juu yake; bali itakuwa kwa ajili ya watu hao; wasafirio, wajapokuwa wajinga, hawatapotea katika njia hiyo."

Wewe u heri wewe uliyeokolewa na YESU KRISTO.
Kumbu 33:29 "U heri, Israeli. Ni nani aliye kama wewe, taifa lililookolewa na BWANA! Ndiye ngao ya msaada wako, Na upanga wa utukufu wako; Na adui zako watajitiisha chini yako, Nawe utapakanyaga mahali pao pa juu."


Siku za karibuni nilifundisha mfululizo masomo kuhusu uchumba kuelekea ndoa. Jambo la ajabu nilipigiwa simu na watu zaidi ya kumi wenye changamoto ya aina moja.
Walionipigia simu juu ya changamoto hiyo wote ni wanawake isipokuwa mtu mmoja tu ambaye yeye ni mwanaume. Watu wale wanawake wote walikuwa mimba wakati huo wakiwa katika uchumba. Baadhi yao baada ya kupata mimba wachumba zao waliwaacha, wengine walikuwa kwenye shinikizo la kutoa mimba. Wengine baada ya kupata mimba wazazi wa wachumba zao waliwakataa. Ni hatari sana zama hizi.  Niliwashauri hao na kuwaombea na naamini aliyetubu kutokea ndani na kuacha uasherati, MUNGU alimsamehe na sasa anampa nafasi mpya. Lakini unaweza kujiuliza Kama katika wachumba kumi basi 9 wanafanya dhambi ya uasherati basi hakika tuko mwisho wa dunia, Ndugu zangu ni wakati wa kutubu.
Wizi katika jamii ya leo imekuwa jambo la kawaida.
Rushwa imekuwa jambo la kawaida, kutoa mimba imekuwa jambo la kawaida, ni hatari hakika.
Mimi ninachojua kwako wewe ndugu unayejifunza somo hili ni kwamba inawezekana umepewa mwaka huu ili utengeneze maisha yako na sio uendelee na dhambi.
MUNGU yeye yuko tayari kukusamehe kama utatubu toba ya kweli.
Toba ya kweli inahusika kutubu na kisha kuachana na dhambi hizo.
Hatuna kipimo tu cha kupima watu lakini kama unaongea na watu wengi kila mara kuhusu mahusiano unaweza ukagundua kabisa kwamba inawezekana watoto wanaozaliwa ni wachache kuliko mimba zinazotolewa, hakika ni siku za mwisho.
Biblia  inasema ''Au waudharau wingi wa wema wake na ustahimili wake na uvumilivu wake, usijue ya kuwa wema wa MUNGU wakuvuta upate kutubu?  Bali kwa kadiri ya ugumu wako, na kwa moyo wako usio na toba, wajiwekea akiba ya hasira kwa siku ile ya hasira na ufunuo wa hukumu ya haki ya MUNGU, atakayemlipa kila mtu kwa kadiri ya matendo yake; wale ambao kwa saburi katika kutenda mema wanatafuta utukufu na heshima na kutokuharibika, watapewa uzima wa milele; na wale wenye fitina, wasioitii kweli, bali wakubalio dhuluma, watapata hasira na ghadhabu;- Warumi 2:4-8 ''
 Uonevu na kuoneana umekuwa mwingi sana wakati huu.
Utapeli na uchawi umekuwa mwingi.
Uongo umekuwa mwingi.
Ndugu, ipo siku ya mambo peupe na hiyo inakuja, ole wako usipotubu na kuacha dhambi zako sasa.
Inawezekana unaisaliti ndoa yako na kujiona salama tu, ipo siku kila mtu atajua kwamba wewe ulikuwa msaliti na wakati huo kwa sababu hukutubu basi utakuwa unaelekea jehanamu.
Inawezekana unaua ndugu zako kwa siri ili uwe tajiri kwa uongo wa wakala wa shetani mganga.
Inawezekana watu wanakuita mtakatifu lakini katika uhalisia wewe ni mtenda maovu mkubwa.
 Biblia inasema  ''Nawaambia, Sivyo; lakini msipotubu, ninyi nyote mtaangamia vivyo hivyo.-Luka 13:3''

Inawezekana umegeuza Kanisa kama kichaka chako cha kuficha maovu, ndugu iko hatari kwa watakaokosa uzima wa milele.
Mama mmoja alinipigia simu akinimbia kwamba ana watoto zaidi ya wanne lakini ana uhakika hao watoto sio wa mume wake wa ndoa maana amekuwa akiisaliti ndoa yake kwa miaka mingi, nilimuonya  na kumwambia aache dhambi hiyo.
Vijana fulani walimuua baba yao mzazai ili wagawane mali zote alizokuwa nazo, ni kweli walimuua lakini hata mali hizo walizogawana hazikudumu popote, ndugu zangu ni saa ya kutubu na kuacha maovu, ipo siku kila kitu kitakuwa wazi kabisa.
 Ndugu usikubali kuiga dunia inavyokwenda, nakuomba mpokee Bwana YESU kama Mwokozi wako na anza kuishi maisha matakatifu katika yeye.

Warumi 12:2 ''  Wala msiifuatishe namna ya dunia hii; bali mgeuzwe kwa kufanywa upya nia zenu, mpate kujua hakika mapenzi ya MUNGU yaliyo mema, ya kumpendeza, na ukamilifu. ''

 KAMA UNATAKA KUTUBU RUDIA MANENO HAYA  KWA KUMAANISHA, KISHA TAFUTA KANISA LA KIROHO UKAJIUNGE NA KUANZA KUISHI MAISHA MATAKATIFU.
 
''BABA katika jina la YESU KRISTO Niko mbele zako mimi mwenye dhambi, lakini leo nimetambua kosa langu na naomba unisamehe dhambi zangu zote, makosa yangu yote na uovu wangu wote, nisamehe dhambi ninazozikumbuka na pia zile ambazo sizikumbuki. futa jina langu katika kitabu cha hukumu na uliandike jina langu katika kitabu cha uzima. Neno lako katika Warumi sura ya 10 Mstari wa 9 na wa 10 Neno lako linasema ''Kwa sababu, ukimkiri YESU kwa kinywa chako ya kuwa ni BWANA, na kuamini moyoni mwako ya kuwa MUNGU alimfufua katika wafu, utaokoka. Kwa maana kwa moyo mtu huamini hata kupata haki, na kwa kinywa hukiri hata kupata wokovu '' . Bwana YESU mimi nimekuamini leo na hivyo naamini sasa napokea wokovu wako na hakika nimeokoka. Kuanzia leo Naufunga ukurasa wa dhambi na ninaufungua ukurasa wa matendo mema na matakatifu. BWANA nipe ROHO wako Mtakatifu ili aniwezeshe kushinda dhambi na anasa zote za dunia. Kuanzia leo mimi nimeokoka na ni mtoto wa MUNGU mwenye haki zote. ninafuta laana zote na kila roho ya shetani inayonifuatilia naiharibu kwa jina la YESU KRISTO kama neno la MUNGU linavyosema katika Yeremia sura ya kwanza mstari wa 10. BWANA YESU nakushukuru sana kwa kuniokoa. Yote haya kwa imani nimepokea na niko tayari sasa kwa ROHO MTAKATIFU kunitumia.  Kuanzia leo mimi nimeacha dhambi na zitahusika nazo tena.

Katika jina la YESU KRISTO nimeomba na kupokea Amen.

  Natamani niseme mengi mno lakini naamini mwenye kuelewa ameelewa.
MUNGU akubariki kwa kujifunza somo hili muhimu pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane nitakujulisha jinsi ya kukipata.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.
0714252292(Hadi whatsapp).
0786719090
mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu.

Comments