KUMJUA MUNGU NA KUUFUATA MPANGO WAKE WA UZIMA WA MILELE.

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU
Bwana YESU atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.
Ujumbe huu nataka nikushauri mambo kadhaa wewe uliyempokea YESU KRISTO kama Mwokozi wako na unaliishi kusudi la MUNGU.
Kuna tofauti kati ya kumfahamu MUNGU, Kumjua MUNGU na kumpenda MUNGU.
Yote Biblia inatuagiza tuyafuate, yaani tumjue MUNGU, tumpende MUNGU  na tumfahamu MUNGU, lakini jambo kubwa na muhimu zaidi ni kumjua MUNGU.

Ndugu hakikisha maisha yako yote unayaishi katika MUNGU aliye hai. Zamani Waisraeli walimuita MUNGU Baba kwa jina la JEHOVAH ADONAI yaani  MUNGU Mwenye Enzi Yote (Mwanzo 15:2-8 ), hakikisha ndugu unaishi katika MUNGU mwenye enzi yote.
Mjue MUNGU wako na ujue mpango wake wa wokovu kwako
 Usiwe kama watu wanaompenda tu MUNGU lakini hawamjui,   maana  mtu wa aina hiyo anaweza akampenda MUNGU au YESU kwa sababu alimbariki alichokuwa anahitaji lakini ikija dhoruba kidogo anaweza akamwacha MUNGU.
Unaweza ukamfahamu YESU na ukawa unamtaja kila wakati lakini matendo yako na tabia zako haziwafanani  wanaomjua MUNGU wa kweli.
Ndugu, nakuomba usiishie tu kumpenda MUNGU na kumfahamu Bali hakikisha unamjua pia MUNGU.
Ayubu 22:21-22 "Mjue sana MUNGU, ili uwe na amani; Ndivyo mema yatakavyokujia. Uyapokee, tafadhali, mafunzo yatokayo kinywani mwake, Na maneno yake yaweke moyoni mwako."

 
Kumjua MUNGU ni kujua Neno lake, mpango wake, kusudi lake na kanuni zake.
Kumpenda MUNGU ni kupenda kile akifanyacho MUNGU.
Kumjua YESU ni kutumikia mpango wake na njia zake.
Inawezekana wewe humjui MUNGU wala kumfahamu ila unampenda.
Inawezekana unampenda YESU kwa sababu umezaliwa katika familia ya Wakristo, lakini humjui ndio maana humtii tena hutaki kuungama dhambi zako na kuziacha.

Biblia inasema


Mithali 28:13 ''Afichaye dhambi zake hatafanikiwa; Bali yeye aziungamaye na kuziacha atapata rehema.''  

 Inawezekana unampenda YESU KRISTO kwa sababu amekuponya.
Kumjua YESU au MUNGU ni zaidi ya kumpenda.
Tunatakuwa kumpenda MUNGU, kumfahamu na Kumjua.
Kuna maelfu ya watu wa kanisa hata jina la MUNGU hawalijui.
Kuna watu kwa sababu hawamjui MUNGU basi hutekwa na elimu za uongo na kumwacha YESU KRISTO Mwokozi wao.


Warumi 6:23 ''3 Kwa maana mshahara wa dhambi ni mauti; bali karama ya MUNGU ni uzima wa milele katika KRISTO YESU  Bwana wetu.'' 

 Kuna watu kwa sababu hawajui mpango wa MUNGU wa Wokovu, hujikuta wanaenda kwa waganga, wanashirikiana na mizimu na majini.
Ndugu hakikisha unamjua MUNGU na Neno lake na mpango wake wa wakati huu kwako.
Usipomjua MUNGU unaweza kukata tamaa kipindi ambacho baraka yako iko dakika chache kukufikia.
Ndugu, usiishie tu kumpenda MUNGU Bali mjue MUNGU na fahamu mpango wake wa wokovu kwako.


Yohana 3:17-18 '' Maana MUNGU hakumtuma Mwana ulimwenguni ili auhukumu ulimwengu, bali ulimwengu uokolewe katika yeye. Amwaminiye yeye hahukumiwi; asiyeamini amekwisha kuhukumiwa; kwa sababu hakuliamini jina la Mwana pekee wa MUNGU.'' 
 
Uzima wa mtu hauko katika wingi wa vitu alivyonavyo.
Uzima wa milele hauko katika wingi wa vitu ulivyonavyo.
Uzima wa duniani hauko katika wingi wa vitu ulivyonavyo.
Kuwa na afya njema au kutokuteswa na magonjwa haiko katika wingi wa vitu ulivyonavyo.
Watu wengi baada ya kufanikiwa kidogo kiuchumi hujiona hawahitaji tena msaada wa MUNGU, ndio maana huacha ibada na maombi.
Ndugu, Uzima wako hauko katika wingi wa vitu ulivyonavyo bali Uzima wako uko kwa MUNGU Baba.
Hivyo mtegemee MUNGU hata wakati ukiwa na uchumi mzuri, kumbuka kwamba Uzima wa mtu hauko katika wingi wa vitu alivyonavyo.

Luka 12:15" Akawaambia, Angalieni, jilindeni na choyo, maana uzima wa mtu haumo katika wingi wa vitu vyake alivyo navyo."

 Ndugu, kama umempokea YESU kama Mwokozi wako hakikisha sasa unaishi maisha matakatifu katika yeye.
Usiiangalie tena dunia na wala usikubali watu wa dunia kukurudisha nyuma.
 Mtu mmoja alinidharau akisema napoteza muda wangu mwingi kumtumikia MUNGU na hata sipati sapoti.
Ndugu mwingine ambaye ni rafiki Yangu sana siku moja aliniambia kwamba "Wewe kalia kuandika vitabu tu huku wenzako tunakula raha za duniani"
Wakati naambiwa maneno hayo rohoni nilisikia sauti ikisema "Unayemtumikia ni YESU KRISTO, ndiye atakayewahukumu watu wote unaowaona, uliowahi kuwaona na hata ambao hujawahi kuwaona. Uzuri ni kwamba kila mtu ipo siku atagundua kwamba ni hasara kama alijifurahisha kwa shetani, na kwa aliyeokoka, mkamilifu na mwaminifu hakika atafurahia uzima na milele na milele yote"

 1 Yohana 5:11-13 ''Na huu ndio ushuhuda, ya kwamba MUNGU alitupa uzima wa milele; na uzima huu umo katika Mwanawe. Yeye aliye naye Mwana, anao huo uzima; asiye naye Mwana wa MUNGU hana huo uzima. Nimewaandikia ninyi mambo hayo, ili mjue ya kuwa mna uzima wa milele, ninyi mnaoliamini Jina la Mwana wa MUNGU.''
Ndugu unayedharau kazi ya MUNGU Mimi nakuonea huruma sana hata kama wewe ndio unajiona mjanja sasa na mwenye akili sasa.
Wewe mtumishi wa KRISTO nakuomba songa mbele hata kama wanaokupinga ni wengi kuliko wanaokukubali.
Tafuta kukubaliwa na MUNGU na sio kukubaliwa na wanadamu.

Hata kama unadharauliwa wewe songa mbele maadamu unamjua MUNGU na mpango wake wa wokovu ambao ni KRISTO.
Ipo siku wanaoipinga kweli ya MUNGU watatahayalika, ipo siku wanaodharau kuokoka watatafuta msaada na wasiuone, ndugu uliyeokoka hakikisha unamtumikia KRISTO kwa uaminifu.
Malaki 3:14-18 '' Mmesema, Kumtumikia MUNGU hakuna faida; na, Tumepata faida gani kwa kuyashika maagizo yake, na kwa kwenda kwa huzuni mbele za BWANA wa majeshi? Na sasa twasema ya kwamba wenye kiburi ndio walio heri; naam, watendao uovu ndio wajengwao; naam, wamjaribuo MUNGU ndio waponywao. Ndipo wale waliomcha BWANA waliposemezana wao kwa wao. Naye BWANA akasikiliza, akasikia; na kitabu cha ukumbusho kikaandikwa mbele zake, kwa ajili ya hao waliomcha BWANA, na kulitafakari jina lake. Nao watakuwa wangu, asemaBWANA  wa majeshi, katika siku ile niifanyayo; naam, watakuwa hazina yangu hasa; nami nitawaachilia, kama vile mtu amwachiliavyo mwanawe mwenyewe amtumikiaye. Ndipo mtakaporudi, nanyi mtapambanua kati ya wenye haki na waovu, na kati ya yeye amtumikiaye MUNGU na yeye asiyemtumikia. ''

Napenda pia kukueleza jambo hili ndugu, Sifa mojawapo ya nafsi ni kuwa na akili ,utashi , Kujua na ufahamu.
MUNGU BABA anajua yote, anafahamu yote na anaweza akatenda lolote kwa utukufu wake.

BWANA YESU anajua yote , anaweza yote na kupitia yeye peke yake tunapata uzima wa milele.
ROHO MTAKATIFU anajua yote na ana nguvu zote .
Ni nafsi za MUNGU mmoja kwa sababu katika lolote maamuzi ya BABA ndio hayo hayo maamuzi ya YESU KRISTO na hayo hayo ndio maamuzi ya ROHO MTAKATIFU.
Popote aliposema ROHO hayo ya ROHO ndio hayo ya MUNGU.
Kumdharau ROHO ni kumdharau MUNGU.
Kumdharau YESU ni kujitenda na MUNGU.

Hakikisha sasa utumishi wako unaambatana na MUNGU, YESU KRISTO na ROHO MTAKATIFU.
1 Yohana 5:7 ''Kwa maana wako watatu washuhudiao [mbinguni, Baba(MUNGU), na Neno(YESU KRISTO), na ROHO MTAKATIFU, na watatu hawa ni umoja.''
Zingatia sana jambo hili kaytika maisha yako ya kiroho. 
  Kuwa Na ROHO MTAKATIFU Ni Ulinzi Kwako.
Kuwa Na YESU KRISTO Ni Uzima Kwako
Na Kuwa MUNGU BABA Ni Furaha Ya Milele.
Alipo BABA Na MWANA Yuko Hapo Hapo, Alipo YESU Na ROHO MTAKATIFU Yuko Hapo Hapo.

Tuna Furaha Sana Tulikombolewa Kwa Damu Ya KRISTO. 

Ukiwa pia katika safari ya maisha ya wokovu napenda kukujulisha jambo hili muhimu sana ambalo baadhi hawalioni.
 Usiamini kila maono wanayokuambia watu kukuhusu wewe.
Inawezekana mengine ni Maono sahihi kabisa lakini hata maono ya uongo yapo, hivyo uwe makini.

Na pia napenda kukushauri katika jambo hili; Ni kwamba kwa kila Mtumishi wa MUNGU, matendo huongea zaidi kuliko maneno.
Hivyo jitahidi sana katika matendo mema kuliko maneno tu maana matendo huongea zaidi kuliko maneno.
Kila mtu atalipwa kulingana na matendo yake, mtu atahukumiwa kutokana na matendo yake.

Mbele ya jamii vitu vingi vinaweza vikaongea lakini matendo yako ndio huongea zaidi ya vyote.
Elimu inaweza ikaongea, sura na umbo vinaweza vikaongea, msimamo wako unaweza ukaongea, kujiamini kunaweza kukaongea, mavazi yanaweza yakaongea, lakini vyote ni bure kama matendo yako yataongea mabaya mbele za jamii.
MUNGU akubariki na Fanya juhudi katika matendo na sio maneno tu.
1 Wakorintho 15:58 " Basi, ndugu zangu wapendwa, mwimarike, msitikisike, mkazidi sana kutenda kazi ya BWANA sikuzote, kwa kuwa mwajua ya kwamba taabu yenu siyo bure katika BWANA."

Nampenda YESU Maana Ameniponya, Ameponya roho Yangu Na Mwili Wangu.
Kumbuka sana pia hii; Kama mtu hajaweka rehani maisha yake kwa YESU, ujue mtu huyo kaweka maisha yake rehani kwa shetani.
Walioweka maisha yao rehani kwa YESU KRISTO ni wale waliompokea kama Mwokozi na wanaishi maisha matakatifu katika yeye. Watu waliomkataa YESU hao wameweka maisha yao rehani kwa shetani.
Wazinzi na walevi wameweka maisha yao rehani kwa shetani.
Waongo na wachawi wameweka maisha yao rehani kwa shetani.
Wanajimu na wezi wameweka rehani maisha yako kwa shetani.
Watenda dhambi wote wameweka rehani maisha yao kwa shetani.
Kufanya dhambi ni kuweka maisha yako kwa shetani.
Kuokoka na kuenenda kwa ROHO MTAKATIFU huko ndiko kuweka rehani maisha yako kwa MUNGU.
Ndugu hakikisha unaweka rehani maisha yako kwa YESU na sio kwa shetani.
Biblia inasema juu yetu wateule wa MUNGU kwamba

"Yeye(YESU) mwenyewe alizichukua dhambi zetu katika mwili wake juu ya mti, tukiwa wafu kwa mambo ya dhambi, tuwe hai kwa mambo ya haki; na kwa kupigwa kwake mliponywa. Kwa maana mlikuwa mnapotea kama kondoo; lakini sasa mmemrudia Mchungaji na Mwangalizi wa roho zenu.-1 Petro 2:24-25

Naipenda sana Biblia maana ni msema kweli pekee wa milele.Sisi hupokea Wokovu Kwa kuokoka(Yohana 1:12-13)
Lakini ili majina yetu ili yabaki kwenye kitabu cha Uzima inabidi tuishi maisha matakatifu siku zote(Waebrania 12:14)
Ndio maana aliyetuokoa ambaye ni BWANA wetu YESU KRISTO anasema tukivumilia hadi mwisho ndio tutaokoka yaani ndio tutafika Uzima Wa milele.
Tunapoisikia sauti ya Neno la MUNGU kwenye Neno la MUNGU, tukafanyia kazi utu wetu wa ndani unabadilika na kumpendeza MUNGU.
Changamoto kwa baadhi ya watu ni kwamba wao husikiliza Neno la MUNGU lakini mioyo yao hawairuhusu isikie sauti ya Neno la MUNGU kutoka ndani ya Neno la MUNGU.
Kumbuka kuna tofauti kati ya kulisikia Neno la MUNGU na kuisikia sauti ya Neno la MUNGU.
Katika ibada ukiona mtu anafanyia kazi Neno la MUNGU alilofundishwa Ibadani ujue kwamba ndugu huyo hakusikia Tu Neno la MUNGU Bali aliisikia pia sauti ya Neno la MUNGU ndani ya Neno la MUNGU alilofundishwa.
Kanisa zima wakiwa ibadani husikia Neno la MUNGU lakini waliosikia sauti ya MUNGU ndani ya Neno la MUNGU ndio hufanyia kazi walichojifunza.
Kila mmoja duniani anaweza kuisikia sauti ya Neno la MUNGU akipenda lakini utii kwa MUNGU wengi hawana.
Ndio maana hata wazinzi unaweza kuwakuta wanajifunza Neno la MUNGU lakini wakitoka ibadani wanaendelea na uzinzi.
Hata mchawi anaweza kujifunza Neno la MUNGU lakini hakuna mabadiliko kwenye maisha yake hata atubu na kuacha dhambi kwa sababu moyo wake huwa hataki kuruhusu kuisikia sauti ya Neno la MUNGU Bali yeye huishia tu kusikia Neno la MUNGU.

Ndugu, hakikisha unakuwa mtu unayelisikia Neno la MUNGU na kuisikia sauti ya Neno la MUNGU ndani ya Neno la MUNGU na kuitii na kuifanyia kazi.

 Natamani niseme mengi mno lakini naamini mwenye kuelewa ameelewa.
MUNGU akubariki kwa kujifunza somo hili muhimu pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane nitakujulisha jinsi ya kukipata.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.
0714252292(Hadi whatsapp).
0786719090
mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu.

Comments