MAMBO YANAYOWEZA KUMFANYA BINTI ACHELEWE KUOLEWA.

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU


Bwana YESU atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.
Mimi naamini kila mmoja anatamani siku moja awe kwenye ndoa yake.
Ndoa ni moja ya baraka tano za MUNGU.
Ndoa ni baraka njema ambayo kila mtu anaihitaji.
Mwanzo 2:24 '' Kwa hiyo mwanamume atamwacha baba yake na mama yake naye ataambatana na mkewe, nao watakuwa mwili mmoja. '' 
Ndoa huwa haiji tu kama muujiza bali ni baraka ambayo inahitaji mambo mengi ili kuifikia.
Mambo hayo yanaweza kuwa ni uchumba(Mahusiano ya awali), Wazazi pande zote mbili kukubali, posa, mahari, Kanisa la MUNGU kubariki na kisha ndoa kufungwa Kanisani.
Mambo mengine yanaweza kuwa rahisi lakini kikwazo kikubwa ni mahusiano ya awali au uchumba kwa jina lingine.
Nimewahi kuwasiliana kwa simu na watu wengi sana lakini baadhi yao waliniacha nikiwa nawaza sana. Mama mmoja kwa ujasiri siku moja alinipigia simu na kuniambia kwamba nimuombee apate Mchumba na afunge ndoa maana amekuwa kwenye uchumba zaidi ya mara 7 lakini hakufanikiwa kuolewa, rohoni mwangu nikasukumwa nimuulize juu ya kufanya mapenzi na wachumba hao akasema kwamba alitembea nao wote. Nilijisemea moyoni kwamba ''Hakika tuko nyakati za mwisho'' . Mama yule nikamuongoza sala ya toba na kisha nikamuombea ili apate Mchumba kama hitaji lake lilivyo. Baada ya maombi akaniambia neno gumu sana akisema kwamba ''Mtumishi Peter naamini sasa nitapata Mume mwema lakini endelea Mtumishi kuombea ili mchumba nitakayempata asiishie tu na yeye kutembea na mimi na kuniacha''. Baada ya maneno yale hadi nywele zangu zilisisimka na nikagundua ndugu yule alikuwa anahitaji msaada mkubwa wa kiroho, nikajikuta namuuliza tu dhehebu lake(Alikuwa hajaokoka) na niligundua kwamba kwake kufanya mapenzi na Mchumba anayempata ni jambo la kawaida kabisa. Nikamwambia kwa uchungu kwamba uasherati huo ndio uliosababisha asiolewe, tofauti na anavyodhani kwamba kuna Mchawi anamroga.
Ndugu zangu, dhambi ya ngono katika uchumba ndio umekuwa chanzo kikuu cha watu wengi kushindwa kufikia ndoa, na hata wakifikia ndoa basi ndoa zao zinakuwa katika migogoro, kusalitiana na vita kila siku.
Najua kabisa haiwezekani ukafunga ndoa na bila kupitia uchumba, lakini sana nisikilize itakusaidia.
Tunapaswa kuwa na uhusiano au ushirikiano ambao unamleta KRISTO ndani yetu.
Watu wengi wako katika mahusiano yanayomuondoa YESU KRISTO ndani yao.

Natambua kabisa kwamba sio mahusiano ua uchumba tu yanayoweza kumuondoa YESU ndani yako kama ukiruhusu dhambi, lakini pia
 

 unaweza kuwa na uhusiano wa karibu na marafiki zako au wafanyakazi wenzako kazini lakini mahusiano hayo yakawa yanamuondoa YESU KRISTO maishani mwako.
Unaweza kuwa na ukaribu na watu ambao story zao, matendo yao na vyote hata ambavyo wanakushirikisha wewe, vyote vina lengo la kumuondoa KRISTO ndani yako.
Ndugu hakikisha hukai katika uhusiano au urafiki na watu ambao uwepo wao katika maisha yako utakufanya umwache YESU, uache utakatifu , au uache ibada.
Ndio maana Biblia inakushauri kwamba usikae kimaongezi au kimatendo na watu wabaya katika mabaya yao.
Zaburi 1:1-2 "Heri mtu yule asiyekwenda Katika shauri la wasio haki; Wala hakusimama katika njia ya wakosaji; Wala hakuketi barazani pa wenye mizaha.Bali sheria ya BWANA ndiyo impendezayo, Na sheria yake huitafakari mchana na usiku."

Dhambi ya uasherati katika wachumba huwa inaondoa mambo mengi sana, mojawapo ya mambo hayo ni kibali.
Unaweza ukakosa kibali kwa Mchumba wako mara tu baada ya kufanya dhambi ya uasherati, shetani anakuwa ameshaingilia kati.
Inawezekana mwanzo ulipata kibali kwake ndio maana mkawa wachumba lakini dhambi inaweza kufuta kibali hicho. 
Ninachoweza kukushauri ndugu ni kwamba ukipata kibali cha MUNGU kitunze sana, usiruhusu dhambi hata kibali hicho kiondoke.
 Ukipata kibali kwa MUNGU umepata jambo kubwa sana.
Ndugu usitafute tu kibali kwa wanadamu Bali tafuta kibali kwa MUNGU, maana kibali cha MUNGU kina mamlaka ya kuwalazimisha wanadamu kukukubali au kukupa kibali hata kama hawataki.
Kibali cha MUNGU ni muhimu sana katika kila eneo la maisha yako.
Vipo vibali vingi vya MUNGU kwenye maisha yako kama ukiliishi kusudi la MUNGU ila ngoja nikujulishe kibali cha kwanza kabisa unachotakiwa kuwa nacho.
Kibali cha kwanza kabisa cha kila mteule wa MUNGU ni kuwa na ROHO MTAKATIFU.
Kama huna ROHO MTAKATIFU huna kibali cha MUNGU sahihi.
ROHO MTAKATIFU ndiye hutupa kibali hivyo mhitaji sana ROHO MTAKATIFU katika maisha yako ili kupata mambo mengi ya ki MUNGU ikiwemo kibali.
Wateule wa kweli wa KRISTO huwezi kuwatenganisha na ROHO MTAKATIFU.


Baada ya utangulizi huo sasa kiini cha somo langu ni hiki.

 MAMBO YANAYOWEZA KUMFANYA BINTI ACHELEWE KUOLEWA.

1. Ubinafsi.

Uninafsi ni nini?
Ubinafsi ni hali ya mtu kujifikiria na kujipenda yeye mwenyewe tu.
Binti anaweza akaonekana ni mbinafsi pale ambapo atajifikiria yeye tu au kujipenda yeye tu. Mfano akipata Mchumba ataonekana kwa kuwasema vibaya watu wengine wote mbele ya Mchumba wake, kutaka afanyiwe kila anachokitaka yeye tu. 
Kwake watu wengine wote hawana thamani hata moja. 
Kijana wa kiume akikutana na Binti ya namna hiyo ni vigumu sana kumuoa maana atafikiri sana juu ya ubinafsi wa Mchumba wake huyo, Mchumba wa hivyo anaweza kukukataza kumtumia Pesa mama yako anayeumwa ili umpe yeye aende saloon.
Yuko tayari wengine walale na njaa ila yeye achezee pesa au vyakula na vingine atupe.
Wabinafsi wengi pia ni waasherati hivyo asipotimiziwa anaweza akalalamika kwamba hapendwi, sasa Kama Mchumba wake naye hana akili basi wataanguka dhambini na shetani kupanda magugu ambayo hawawezi kuyang'oa na hivyo kuishia kuachana kabla ya ndoa.
 Biblia inatoa kanuni muhimu ambayo inaweza ikaondoa mabaya mengi ukiwemo ubinafsi.
Wafilipi 2:3 '' Msitende neno lo lote kwa kushindana wala kwa majivuno; bali kwa unyenyekevu, kila mtu na amhesabu mwenziwe kuwa bora kuliko nafsi yake.  Kila mtu asiangalie mambo yake mwenyewe, bali kila mtu aangalie mambo ya wengine.''
Binti au Mwanamke jichunge sana ili usimfanye Mchumba wako akachukia ndugu zake au hata wazazi wake kwa sababu ya ubinfsi wako.
Biblia inakushauri kwamba usiangalie mambo yako tu bali angalia mambo ya wengine.
Unaweza ukamteka kweli kijana kwa sababu ya ubinafsi wako lakini anaweza kushtuka mapema kabla ya ndoa na kukuacha hivyo hasara kubwa inakuwa kwako.
Lakini pia kama kijana anakuita mbinafsi kwa sababu tu umemkatalia kukutana kimwili kabla ya ndoa, hapo napenda kukujulisha kwamba huo sio ubinafsi bali ni Ucha MUNGU sahihi.
Kataa ubinafsi lakini pia usikubali kuingia kwenye mitego ya shetani kwa sababu ya kuitwa mbinafsi.


2. Kujiweka viwango ambavyo sio vyao.

Nimekutana na vijana wengi waliokataliwa na mabinti wakilalamika kwamba waliambiwa kwamba ''wao sio type ya mabinti hao''
Nilipouliza hiyo type ni ipi niliambiwa kwamba Elimu ndogo, kukosa pesa, hawana uwezo wa kuwahudumia mabinti hao, hawana kazi nzuri, ukoo wao masikini, sio watu maarufu n.k
Hizo sio sababu za kiroho hata kidogo.
Wakati mwingine kijana anaweza kuonekana masikini leo na kesho huyo ndio akawa tajiri mkubwa, na inawezekana kabisa tajiri wa leo akawa pia ndio masikini mkubwa wa kesho.
Kwenye masuala ya mtu wa kufunga naye ndoa hakikisha unafuata sababu za kiroho na sio za kimwili tu. 
Kujiweka kwako viwango vya juu kunaweza kukufanya ukose wa kukuoa na hivyo  kuchelewa sana kuolewa.
Kujiweka viwango vya juu kunaweza kuwaleta waume za watu wasio na hofu ya MUNGU, na hao kazi yao ni kukuchezea tu.
Ukijiweka viwango vya juu maana yake wengine wote utawadharau na kuwaona hawana thamani kama yako. 
Mtu wa kundi huli huangalia tu vitu na sio mtu husika.
  Ni mtu aliyejaa Dharau.
 Biblia inakutaka kuwa na unyenyekevu wa Ki MUNGU na wahesabu wengine kuwa ni bora kuliko wewe.
Wafilipi 2:3'' Msitende neno lo lote kwa kushindana wala kwa majivuno; bali kwa unyenyekevu, kila mtu na amhesabu mwenziwe kuwa bora kuliko nafsi yake.


3. Kutokumuuliza MUNGU ili awape alama na ishara ya mtu sahihi

Kuna mabinti ni wacha MUNGU wazuri, wametulia na hakika wametimia katika viwango vizuri vya kuwafanya wawe wake wema popote, lakini tatizo lao ni wao kutokumuuliza MUNGU juu ya mtu sahihi katika kundi kubwa la vijana wanaowaendea ili kutaka wawamchumbie.
Binti anaweza kuwa anamkataa kila kijana anayekuja mbele yake akitaka hadi MUNGU amjulishe.
Binti anaweza kumkataa kila kijana akisubiri hadi aote ndoto.
Ndugu, ni nani alikuambia kwamba MUNGU husema na wewe kwa ndoto tu?
Ni nani alikuambia kwamba MUNGU atasema na wewe hata kama hujaomba kuuliza kwake?
Biblia inasema 
 Habakuki 2:1 ''Mimi nitasimama katika zamu yangu, nitajiweka juu ya mnara, nitaangalia ili nione atakaloniambia, na jinsi nitakavyojibu katika habari ya kulalamika kwangu.''
Hata wewe inakupasa kusimama katika zamu yako ya maombi ili kumuuliza MUNGU juu ya kila kijana anayetaka kukuoa.
Simama katika zamu yako ya utakatifu, utumishi na maombi ukiuliza kwa MUNGU juu ya kijana anayetaka kukuoa?
Ukienda kwa akili zako tu unaweza  kumkataa mtu sahihi na ukamchagua mtu asiye sahihi.
Inawezekana sio wote uliowakataa hawakufai.
MUNGU ana njia zaidi ya nane anaweza akasema na wewe hivyo usitegemee tu ndoto na maono ndipo ujue ni MUNGU amekuhakikisha. Kumbuka pia ndoa zina vyanzo vitatu  hivyo unaweza ukasubiri ndoto na ukaota ndoto ambayo haitoki kwa MUNGU hivyo ukajichanganya zaidi.
Ngoja nikupe mfano mmoja. Rebeka alipofuatwa juu ya suala la kuolewa na Isaka, ROHO wa MUNGU alimpa amani juu ya isaka hivyo akamkubalia.
Mwanzo 24:58 ''Wakamwita Rebeka wakamwuliza, Je! Utakwenda na mtu huyu? Akasema, Nitakwenda.'' 
Yaani amani ya KRISTO tu inaweza kuamua moyoni mwako juu ya kijana anayekujia akitaka mfunge ndoa.



4. Washauri wabaya.

Kila mtu ana washauri wake katika mambo kadhaa yanayohitaji ushauri.
Sio watu wote ni washauri wazuri kwako.
Sio ndugu zako wote ni washauri wazuri kwako kuhusu suala la wewe kumkubalia Mchumba.
Hata watumishi wengine pahali pengine wamewafanya watu kushindwa kulifuata kusudi la MUNGU la ndoa.
Mtumishi anaweza kukuwekea masharti zaidi ya kumi wakati yeye alipokuwa anataka kufunga ndoa hakuwekewa hata robo ya hayo mashariti.
Unaweza ukamuomba ushauri rafiki yako na yeye akawa anamtaka mtu huyo hivyo akakushauri vibaya kabisa hata kama ni kusudi la MUNGU huyo awe mwenzi wako.
Washauri wabaya wanaweza kukufanya uwe katika njia ya wakosaji.
Biblia inakushauri
Zaburi 1:1-2 ''Heri mtu yule asiyekwenda Katika shauri la wasio haki; Wala hakusimama katika njia ya wakosaji; Wala hakuketi barazani pa wenye mizaha. Bali sheria ya Bwana ndiyo impendezayo, Na sheria yake huitafakari mchana na usiku. ''
Sheria  ya BWANA ni Neno la MUNGU hivyo ni heri Neno la MUNGU ndilo likawa kiongozi wako katika kumkubalia Mchumba.
Kama akili yako inadhani kwamba bila ushauri wa mjomba au rafiki huwezi kumkubalia mtu anayeishi maisha matakatifu ili akuchumbie basi kumbuka kwamba huyo Mjomba au rafiki au ndugu au mtumishi naye ni mwanadamu hivyo hata yeye anaweza kukushauri vibaya.
Hivyo hakikisha katika maisha yako una ROHO MTAKATIFU maana ni huyo tu ndiye mshauri wa kweli na ambaye hajawahi kukosea kushauri popote, akikukataza acha, akikupa amani endelea, akikuondolea amani acha au omba kwanza, akikupa huzuni acha maana kunaweza kutokea hatari mbele yako kuhusu uhusiano huo unaotaka kuuendea.
Washauri wabaya ni wengi sana, filamu inaweza kuwa mshauri wako mbaya, riwaya au mkufunzi wako popote anaweza pia kuwa mshauri mbaya kwako.


5. Kukubali kuchezewa.

 Kuruhusu kuchezewa ni kumruhusu shetani ili akutumie vile atakavyo.
Mabinti wengi sana au wanawake wengi sana wamechelewa au kushindwa kabisa kuolewa kwa sababu tu wamekubali kuchezewa na wanaume.
Mwanaume anaweza akakushawishi sana mkutane kingono na bada tu ya kukutana anakuacha.
Heshima ya binti huondoa na kupotea ghafla ya mbele ya Mchumba kwa sababu tu ya kuruhusu dhambi ya uasherati.
Ni zama za magonjwa hatari hizi hivyo hakuna kijana anayejielewa anaweza kumuoa mwanamke ambaye ametembea na kila mtu.
Kitu kimoja baadhi ya wanawake hawajui ni kwamba vijana wengi sana husimuliana kuhusu mabinti ambao wameshatembea nao kiasi kwamba ni rahisi sana kila mtu kujua kwamba wewe ulitembea na fulani na hivyo kukosa wa kukuoa.
Vijana wengi wa kiume ambao hawamchi MUNGU huona ufahari sana kutangaza wanawake waliotembea nao.
Nilipohamia Dar es salaam kabla sijaoa nilikuwa mtulivu sana na sikutaka mawasiliano na watu wengi. Lakini hata miezi miwili haikuisha nilikuwa nimeshajulisha juu ya mabinti wengi ambao tulikuwa tunashirikiana mambo mbalimbali pamoja, yaani ukikaa na kijana wa kiume dakika kadhaa tu utashangaa ushaambiwa juu ya anayetembea na fulani, juu list ya wanaume ambao fulani alikuwa nao n.k
Hiyo ilinifanya mapema kabisa baadhi ya watu kuwaondoa katika kundi la mwanamke wa kuoa, maana nilikuwa sina Mchumba.
Sasa moja ya hasara mbaya sana kwa mwanamke ambaye hajaolewa ni kuruhusu uasherati.
Biblia kwa maonyo makali ya kukusaidia inasema kwako kwamba
 '' Ikimbieni zinaa. Kila dhambi aitendayo mwanadamu ni nje ya mwili wake; ila yeye afanyaye zinaa hutenda dhambi juu ya mwili wake mwenyewe.-1 Kor 6:16''

6. Vifungo vya giza alivyofungwa


Zaburi 116:3 '' Kamba za mauti zilinizunguka, Shida za kuzimu zilinipata. Naliona taabu na huzuni; '' 
 Kwenye suala la vifungo hapo ni kasheshe kubwa kwa wengi sana.
Wako watu wana roho za kukataliwa.
Wako watu wako katika ndoa za kipepo na majini mahaba kiasi kwamba mtu kama huyu hawezi kupata mchumba, hata akipata hadumu naye maana agano la kipepo katika yake na majini linawafukuza wachumba.
Wako watu walivalishwa peter za kipepo.
Wako watu wala laana za wazazi au watumishi au watu tu wengine.
Wako watu wamerogwa na wako watu wako katika vifungo mbalimbali vya kipepo.
Wako watu wana mapepo ambayo hayo huwazuia.
Wako watu wameingia maagano ya kipepo , wako watu waliwaendea kwa waganga, wako watu kwa sababu ya mahusiano ya zamani wamewafungwa kipepo mabinti hawa.
Wako watu kwa kutembea na waume za watu waliambulia laana, wako watu kwa kutoa mimba  walitengeneza laana na vifungo, wako watu wanafanya dhambi za siri hata sasa na dhambi hizo ndizo zinawazuia kuolewa siku zote.
Kuna watu wana maroho ya urithi ya ukoo au familia.
Kuna watu wanateswa na mizimu.
Kuna watu wamefungwa kwa maneno ya vinywa vyao wenyewe(Mitahli 6:2,Basi umetegwa kwa maneno ya kinywa chako, Umekamatwa kwa maneno ya kinywa chako, )
Kuna watu walikubaliana na waliokuwa na mahusiano nao zamani kwamba ''Hwataachana milele'' wakaandikiana, wakala viapo vingi lakini baadae wakaachana na viapo hivyo vipo na ndivyo vinawazuia kuolewa.
Ndio maana Biblia inakataza kuwa na mahusiano ya kimapenzi na mtu yeyote maana vifungo vinavyotoka huko ni vingi.
Kuna watu walilikataa kusudi la MUNGU ndio maana imekuwa vigumu kwao kufanikiwa.
Viko vifungo vya namna nyingi sana na vimewafunga watu wengi.
Ndugu, dawa ya vifungo kwanza okoka, mpokee Bwana YESU kama Mwokozi wako, ishi maisha matakatifu katika yeye, acha dhambi zote na omba na kuombewa juu ya kuharibu vifungo vya giza vyote ulivyofungwa vinavyokuzuia kuolewa.
Kuna watu wana nguvu za giza ndani yao kiasi kwamba akipata mchumba tu ni yeye ndiye anamkataa mchumba wake, hata kama ameshamtolea mahari na wameshatambulishana kila sehemu.
Kuna mtu ana kifungo cha kipepo kiasi kwamba akitaka kuolewa anajikuta anadharau kuolewa na kuona hamna faida kuolewa, hicho ni kifungo kibaya na kinawatesa wengi.
Wengine vifungo vyao wamefungwa wazazi wao au wote wanaowahusu kiasi kwamba akipata mchumba ukoo mzima wanamkatalia n.k
Ndugu, kubali kufunguliwa vifungo vya giza vyote.
Natamani niendelea lakini tengeneza katika hayo itakusaidia sana.
La mwisho zingatia usafi wa roho hata kabla ya usafi wa mwili.


Kwa wewe uliyeokoka.
Ukiwa bado mwanzoni mwa mwaka huu unahitaji kuomba MUNGU juu ya mwaka huu.
Leo omba maombi yafuatayo.
1. Omba MUNGU auvike mwaka kwako taji ya wema(Zaburi 65:11)
2. Utabirie mwaka wako ili uwe ni mwaka uliojaa mema kwako(Mithali 18:21)
3. Futa kila nguvu za Giza zinazopanga kupindisha mwaka wako.
Futa mipango mibaya dhidi ya afya yako, uchumi wako, uzao wako, ndoa yako na kibali chako(Yohana 14:13)

4. Hakikisha kwa maombi na utakatifu maadui zako wanaabika, wanafedheheka na wanarudishwa nyuma hali ya ukiwa wote wanaokuwazia mabaya (Zaburi 40:14-15)
5. Mshukuru MUNGU kwa ajili ya mwaka uliopita na mshukuru tena BWANA kwa ajili ya mwaka huu mpya(Isaya 12:3-4)

  Natamani niseme mengi mno lakini naamini mwenye kuelewa ameelewa.
MUNGU akubariki kwa kujifunza somo hili muhimu pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane nitakujulisha jinsi ya kukipata.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.
0714252292(Hadi whatsapp).

mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu.

Comments