MAOMBI YA KUFUTA AGANO LA KIPEPO LILILOFANYWA KWA DAMU YAKO MWENYEWE.

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU

 Bwana YESU atukuzwe mtu wa MUNGU.
Namshukuru MUNGU kwa Neema yake na na hili ni somo la 796 kukuletea tangu nimeanza kufundisha Mtandaoni mwishoni mwa mwaka 2012.  Nachukizwa sana na wanaochukua masomo yangu na kufuta jina langu na baadhi ya maneno yangu na kujibandika wao kwa tamaa zao, nimeyaona sana masomo hayo katika blogs na website mbalimbali, kuna wengine wanatafuta kipato kupitia masomo yangu, nachukizwa na hata wakati mwingine natamani kuacha kuandika masomo maana tabia hiyo imezidi sana, kuna watu wameunda groups za whatsap za maombi wakitumia maombi ya masomo yangu huku wakiwa na malengo ya tamaa mbaya. Nimekuwa nikiomba ROHO wa MUNGU anisaidie nini cha kufanya katika hili, hakika sifurahii hata kidogo, ndugu kama unahusika nakuonya kwa jina la YESU KRISTO,acha.
Baada ya maelezo hayo sasa tuendelee.
Nimeshawahi kuandika masomo mengi  ya maombi   yanayoelekeza  kufuta maagano mbalimbali ya kipepo, leo tunajifunza maombi ya kufuta agano la kipepo lililofanywa kwa damu yako mwenyewe.
Siku moja nikiwa katika maombi nilifunuliwa  ujumbe huu nikiambiwa  kwamba '''wapo watu wamefungwa maagano ya kipepo kwa damu zao wenyewe na hawajawahi kufuta agano hilo la giza.'' Wakati nafunuliwa ujumbe huu nilimuona kijana fulani wa kiume  akichanjwa chale  na mganga wa kienyeji na damu iliyotoka katika mwili wake  palipochanjwa mganga alipaka pale dawa na kuichanganya na damu iliyotoka baada ya kuchanjwa huku akisugua eneo hilo la chale kwa damu na dawa yake. Nilimshangaa kijana yule maana alikuwa anachanjwa bila kushtuka maumivu. Nilishangaa sana pia kwa maono hayo na nikakumbuka kabisa hata mimi sijawahi kuomba maombi ya kufuta agano la kipepo  lililofanyika kwa kutumia damu yangu mwenyewe.
Najua kwa watu wengi ni rahisi sana kuomba maombi ya kufuta maagano ya giza yaliyofanyika kwa damu za wanyama au kwa kafara mbalimbali lakini ni vigumu mno kukumbuka kufuta agano la kipepo lililofanyika kwa damu yako mwenyewe.
Biblia inasema ROHO MTAKATIFU hutufunulia mafumbo yote katika ulimwengu wa roho.
1 Kor 2:10 '' Lakini MUNGU ametufunulia sisi kwa ROHO. Maana ROHO huchunguza yote, hata mafumbo ya MUNGU.''

 Ndugu nisikilize kwa makini sana itakusaidia sana kujinasua katika mateso unayoyapata kutokana na maagano ya giza yaliyofanyika kwa damu yako mwenyewe.
Unajisikiaje unateswa na magonjwa na matatizo ambayo yanakuwa ukiomba yanaondoka kisha ukipunguza maombi matatizo yanarudi. Huku hujui chanzo cha magonjwa hayo au matatizo hayo, ndugu kumbuka kufuta kila agano la kipepo lililofanyika kwa damu yako mwenyewe.
Unaweza ukashindwa kuolewa au kuoa kwa sababu tu ulifungwa kipepo kwa agano la damu yako mwenyewe.
Unaweza uakachanganyikiwa au kuwa kichaa kabisa kwa sababu tu ulifungwa kishetani kwa agano la damu yako mwenyewe.
Unaweza ukawa mtu wa kukataliwa kuteswa, kukosa kibali au kuumwa kila amara kwa sababu tu kuna agano la kipepo lililofanyika kwa damu yako mwenyewe.
Hata watumishi wa MUNGU pia ufunuo wa ROHO MTAKATIFU kama huu ni vigumu sana kukumbuka kumuombea mtu kufuta agano lab kipepo kupitia damu yake mwenyewe.
Kumbuka damu ni uhai hivyo mtu akifunga kifungo katika damu yake mwenyewe ni jambo baya sana na la hatari sana.

Kumbuka agano ni patano na MUNGU anakuonya kwamba usikubali kufanya agano la kishetani.
Kutoka 23:32  ''Usifanye maagano pamoja nao, wala pamoja na miungu yao.''

 Mawakala wa shetani wanaweza kukaa kikao kisha kumpa dawa mmoja katika wao ili afanyike mganga kwa lengo la kuchanja watu chale, chale zile ni agano la damu la kishetani kwa kutumia damu yako mwenyewe.
Ndugu, ni damu ya YESU KRISTO pekee inayoweza kufuta kila agano la damu la kipepo lililofanyika kwa damu yako mwenyewe.

Kwa  jinsi gani damu mwenyewe inaweza ikatumika kutengeneza agano la kipepo ambalo litakutesa?

Ndugu jipime na kutafakari katika haya ili kama unahusika basib maombi ya leo yanakuhusu sana.

1. Kwa kuchanjwa chale na waganga au wewe kuota umechanjwa chale na kisha ukiamka unakuta ni kweli umechanjwa chale.
Walawi 19:28 '' Msichanje chale yo yote katika nyama ya miili yenu kwa ajili ya wafu, wala msiandike alama miilini mwenu; mimi ndimi BWANA.''
Watu wengi sana wamechanjwa chale, ndugu hilo ni agano la kipepo kupitia damu yako mwenyewe.

2.  Damu yako inapomwagika wakati wa ajali  yenye mtego wa shetani.
Zaburi 106:37 '' Naam, walitoa wana wao na binti zao Kuwa dhabihu kwa mashetani. ''
Kuna ajali zingine ni majini  yanakusanya damu inayoweza kuwa dhabihu kwa mashetani.

3. Damu ya Hedhi kwa wanawake, kama kuna mtego wa shetani.
Watu wengi pa wamefungwa maagano ya kipepo kwa damu zao wenyewe.
Unaweza ukateswa na vifungo vya kishetani mbalimbali na kumbe chanzo ni agano la kipepo lililofanyika kwa damu yako mwenyewe.
Uwe makini maana wengine ni mawakala wa kuzimu na wanakufuatilia tu ili wakipata done kidogo tu ya damu yako wakufunge vifungo ambavyo kukumbuka kuombea ni vigumu mno.

4. Kuchomwa sindano za kichawi ndotoni.
Mimi Peter  ni mara kadhaa nimewasiliana na watu kwa simu wakinieleza jinsi ambavyo waliona wachawi na majini wakiwachoma kwa sindano ndotoni na kutoa damu ili damu zao wenyewe  zitumike kuwafunga vifungo vibaya.
Dada mmoja yeye siku moja aliota ndoto hiyo na alipoamka hakika mwili wake ulikuwa unauma katika eneo ambalo alichomwa sindano za kichawi ndotoni.
Ndugu mmoja yeye aliona kabisa majini yakimuambia kwamba yamechukua damu yake hivyo ili afunguliwe ajiunge nao kupitia waganga. Ndugu huyo aliponieleza tuliomba kufuta hilo hizo za kishetani.
Ndugu utaonewa na nguvu za giza hata lini?
Nakuomba leo okoka, mkimbilie Bwana YESU na anza kuwa mtu wa ibada huku ukiomba ili kufuta mipango hiyo ya giza inayokutesa.

5. Tendo la ndoa kwa mara ya kwanza, kama kuna mtego wa kishetani, pia tendo la ndoa na mawakala wa shetani wanadamu waliojipata madawa na wanaotumika kipepo au  kufanya mapenzi na majini.
Ni watu wachache sana ambayo hawajawahi kufanya mapenzi katika maisha yao, kufanya mapenzi isipokuwa katika ndoa hufungua milango ya shetani kukuvamia na kukufanya atakavyo, wengi sana damu ya kwanza siku wanafanya mapenzi kwa mara ya kwanza ilitumika na mawakala wa shetani kuwafunga maagano ya giza.
Ndugu, MUNGU anapokukataza uasherati ni kwa faida yako mwenyewe.
Kuna watu wamefanya mapenzi na mawakala wa kuzimu waliokuwa wamejipaka madawa hivyo kuwafunga vifungo vya giza  na madhara wanayaona katika maisha yao, unaweza ukashindwa kuzaa, ukashindwa kufunga ndoa na ukapata kila aina ya mateso kwa sababu tu umefungwa kipepo kwa agano la damu yako mwenyewe.
Kuna watu kila leo wanafanya mapenzi na majini, ndugu ufunge huo mlango kwa kuokoka na kuombewa maombi ya kufunga milango ya majini mahaba kukutesa. Unaweza usizae maisha yako yote kwa sababu tu ya ndoa na majini mahaba, unaweza kuwa kila ukipata mchumba baada ya muda anakufa, unaweza kila ukifunga ndoa mwenzi wako anafariki mwaka wa kwanza wa ndoa kwa sababu tu wewe una mikataba na majini mahaba na wamekufunga kwa damu yako mwenyewe. Ndugu, kuna kupona katika jina la YESU KRISTO, Fanya hima sana kuokoka na kuombewa.
 
 
6. Mtoto wa dawa, yaani mtoto anayepatikana kwa nguvu za kishetani za uganga kufanya kazi.
Mtoto wa dawa ni mtoto aliyepatikana kwa wazazi wake kutumia nguvu za giza kumpata, huyo moja kwa moja yuko katika agano la kishetani.
Ndugu wakati kama unateswa sana na vifungo vya giza nakuomba hata uliza wazazi wako ulipatikanaje maana wako watu baada ya kuona wanachelewa kuzaa waliamua kwenda kwa waganga. Ndugu shetani ni shetani tu na hakuna shetani mweupe hivyo haribu mikataba ya kishetani katika maisha yako.

7. Maagano ya kurithi yaliyohusisha damu ya wazazi wako au Babu zako.
Baba yako au babu zako kama waliingia maagano ya damu ya namna yeyote  iwe kupitia mila za kikabila au tohara fulani au kukeketwa ujue na wewe ni mzao wao hivyo agano la kipepo la damu linaweza kukuvamia na kukutesa kwa sababu wewe ni damu yao hao walioingia agano la kishetani la damu.
Leo Yupo YESU KRISTO Mwokozi asiyeshindwa na jambo lolote. nakushauri kimbilia maombezi utafunguliwa.

8. Kuna watu katika uchumba wao au mahusiano kipindi wakiwa na furaha walichanjana miili yao na damu  iliyotoka wakaichanganya kama ishara ya kupendana au kutokuachana, hilo ni agano la kishetani la damu yako mwenyewe, ni hatari sana kwako.
Mimi Peter Nimewahi kuwasiliana na vijana wengi ambao waliniambia mambo ya ajabu sana. Kuna watu walipokuwa katika furaha ya mahusiano waliapiana viapo wakichanganya damu zao, hilo ni agano la kishetani ambalo linaweza kukutesa sana.
Unaweza ukashindwa kutulia katika ndoa yako au uchumba wako kwa sababu tu zamani ulipokuwa uko katika mahusiano uliiingia agano la kishetani, ndugu hata mahusiano yeyote ya kimapenzi nje na ndoa takatifu iliyofungwa Kanisani ni dhambi.
 

9. Kutoa damu kama ni katika mtego wa shetani.

10.  Siku ya kuzaliwa, kama kulikuwa na mtego wa shetani na kama ulizaliwa katika mazingira ya kimila na jadi.
Kuna watu walizawaliwa vijijini katika nyumba za waganga wa kienyeji au kwa ndugu lakini wanatumia uganga au ushirikina au uchawi au madawa ya kiganga n.k
Jinsi ya kufuta agano la kipepo lililofanyika kwa damu yako mwenyewe..

1. Mpokee YESU KRISTO kama Mwokozi wako ili ufanye agano  na yeye ili kupata kibali cha MUNGU cha maombi ya ushindi.
1 Yohana 1:9 ''Tukiziungama dhambi zetu, Yeye ni mwaminifu na wa haki hata atuondolee dhambi zetu, na kutusafisha na udhalimu wote. ''
MUNGU anakusafidha udhalimu wote kwa damu ya YESU KRISTO pekee baada ya wewe kumpokea YESU kama Mwokozi.

2. Omba maombi ya kufuta maagano ya giza yaliyofanyika  damu yako mwenyewe, tumia damu ya YESU na Neno la MUNGU kuomba.
Ufunuo 12:11 '' Nao wakamshinda kwa damu ya Mwana-Kondoo, na kwa neno la ushuhuda wao;  ..........  ''

3. Haribu madhabahu za giza zilizotengeneza  maagano hayo ya giza.
Kumb 7:5 '' Lakini watendeni hivi; zivunjeni madhabahu zao zibomosheni nguzo zao, yakateni maashera yao, ziteketezeni kwa moto sanamu zao za kuchonga.   ''

Mawakala wa shetani wakati mwingine hufanya kazi kwa usiri mkubwa sana, ndugu ROHO MTAKATIFU amekufunulia haya ili upone.
Unaweza kuwa kila ukipata mtajai unapotea, unaweza kuwa wewe ni mtu wa kuibiwa tu kila siku, unaweza kuwa ni mtu wa chini tu kila siku katika maisha yako, unaweza kuwa ni mtu usiye na kibali siku zote.
Ndugu, wakati mwingine shida yako au vifungo vyako umefungwa kwa agano la kipepo la damu yako mwenyewe.

Maombi ya leo.

1. Tubu na fanya agano na damu ya YESU KRISTO.

2. Futa kwa damu ya YESU KRISTO kila agano la giza lililofanyika katika damu yako mwenyewe.

3. Haribu madhabahu za giza zilizotengeneza agano la kipepo kupitia damu yako mwenyewe.
Takasa damu yako na mwili wako kwa damu ya YESU KRISTO.

  Natamani niseme mengi mno lakini naamini mwenye kuelewa ameelewa.
MUNGU akubariki kwa kujifunza somo hili muhimu pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane na nitakujulisha jinsi ya kukipata na  Naamini kitakusaidia sana.
Hapa chini ni
MAOMBI YA KUFUTA AGANO LA KIPEPO LILILOFANYWA  KWA DAMU YAKO MWENYEWE.

  Maombi haya naomba yamsaidie mtu yule ambaye hajui kuomba ili katika kuomba kwa kutumia hayo basi atakumbuka mahitaji yake na kuyataja katika maombi yake. Haya hapa chini ni maombi ya kuanzia tu katika maombi yako ili uendelee zaidi kuomba
Kwa waombaji wazoefu naamini baada tu ya kulisoma somo na kulielewa basi anajua aombee nini maana alikuwa anaandika points za kuombea. Kumbuka pia fundisho ni muhimu kuliko maombi hivyo wewe ambaye huwa unahusika na maombi tu hakikisha unajifunza kwanza somo lote ndipo utapata nguvu za kuomba na kushinda. 


MAOMBI YA KUFUTA AGANO LA KIPEPO LILILOFANYWA  KWA DAMU YAKO MWENYEWE.

 MUNGU Baba ninakushukuru katika jina la YESU KRISTO.
Asante BWANA kwa ajili ya Damu ya YESU KRISTO  ya Pasaka.
Niko mahali hapa Ee YAHWEH nikiomba unisamehe dhambi zangu na unisamehe ni kila kitu  nilichosababisha mimi mwenyewe hata nikafungwa kipepo kwa agano la damu yangu mwenyewe.
Nisamehe Eee MUNGU Baba kwa makosa ya wazazi wangu na mababu zangu katika kuingia agano baya la damu, ninatubu kwa ajili yao na naomba niachiliwe leo kutoka katika kila adhabu ya kipepo ililokuwa imekusudiwa kwa ajili yangu.
Nisamehe MUNGU Muumbaji wangu kila dhambi na kila kosa na kila uovu, nitakase kwa damu ya thamani ya YESU KRISTO.
Eeee Bwana YESU niko mahali hapa nikitumia jina lako la thamani sana  kuzishinda kazi zote za shetani zilizonifunga kwa maagano ya giza yote.
Kwa damu ya YESU KRISTO na katika jina la YESU KRISTO ninafuta kila agano la kipepo lililofanyika katika damu yangu mwenyewe.
Kila agano la kipepo la damu yangu mwenyewe kupitia chale nilizochanjwa kwa mganga au ndotoni, ninalifuta agano hilo la giza kwa damu ya YESU KRISTO na katika jina la YESU KRISTO.
 Kila agano la kipepo kupitia damu yako katika ajali au katika utoaji damu wa aina yeyote, ninalifuta agano hilo la giza kwa damu ya YESU KRISTO na katika jina la YESU KRISTO.
Kila agano la damu la kipepo kupitia damu yangu mwenyewe siku ninazaliwa, ninalifuta agano hilo la giza kwa damu ya YESU KRISTO na katika jina la YESU KRISTO.
 Kila agano la kipepo la damu yangu mwenyewe siku nilipofanya dhambi ya uasherati, ninalifuta agano hilo la giza kwa damu ya YESU KRISTO na katika jina la YESU KRISTO.
Kila agano la kipepo la damu yangu mwenyewe kupitia Hedhi, 
Kila agano la damu yangu mwenyewe kupitia maagano ya kipepo ya mahusiano niliyowahi kuingia, ninalifuta agano hilo la giza kwa damu ya YESU KRISTO na katika jina la YESU KRISTO.
Kila agano la kipepo la damu yangu mwenyewe kupitia ajali au sindano za kichawi ndotoni, ninalifuta agano hilo la giza kwa damu ya YESU KRISTO na katika jina la YESU KRISTO.
Kila agano la kipepo la damu yangu mwenyewe kupitia kuzini na majini mahaba, ninalifuta agano hilo la giza kwa damu ya YESU KRISTO na katika jina la YESU KRISTO.
Kila agano la kipepo la damu yangu mwenyewe, kokote lilikofanyika likihusisha damu yangu mwenyewe, ninalifuta agano hilo la giza kwa damu ya YESU KRISTO na katika jina la YESU KRISTO.
 Sasa naingia agano na damu ya YESU KRISTO ili damu yangu ilindwe na nguvu za MUNGU.
Sasa naitakasa damu yangu iliyoharibiwa na magonjwa na laana na vifungo vya giza vilivyotokana na maagano ya kipepo kupitia damu yangu mwenyewe, naitakasa damau yangu katika damu ya YESU KRISTO na kwa jina la YESU KRISTO Mwokozi aliye hai.
Eee JEHOVAH MUNGU uliye hai ssa niko mbele zako BWANA MUNGU wangu nikiharibu na kuangusha kila madhabahu ya kishetani iliyohusika kufanya agano la damu yangu mwenyewe.
Naharibu madhabahu hizo za giza leo, naziharibu madhabahu hizo kwa Damu ya YESU KRISTO na katika jina la YESU KRISTO.
Kila madhabahu ya laana, magonjwa na kuteseka, naziharibu madhabahu hizo kwa Damu ya YESU KRISTO na katika jina la YESU KRISTO.
Kila madhabahu ya uharibifu na madeni, naziharibu madhabahu hizo kwa Damu ya YESU KRISTO na katika jina la YESU KRISTO.
Kila madhabahu ya umasikini na kuniondolea baraka zangu, naziharibu madhabahu hizo kwa Damu ya YESU KRISTO na katika jina la YESU KRISTO.
Kila madhabahu ya kiganga au kichawi,  naziharibu madhabahu hizo kwa Damu ya YESU KRISTO na katika jina la YESU KRISTO.
Kila madhabahu ya majini na mizimu, naziharibu madhabahu hizo kwa Damu ya YESU KRISTO na katika jina la YESU KRISTO.
Kila madhabahu za giza kokote ziliko, naziharibu madhabahu hizo kwa Damu ya YESU KRISTO na katika jina la YESU KRISTO.
Katika jina la YESU KRISTO leo nimeshinda na zaidi ya Kushinde.
Nakushukuru MUNGU Baba maana katika wewe Muumbaji wangu imekuwa.
Katika jina la MUNGU Baba, MUNGU Mwana, na MUNGU ROHO MTAKATIFU ninaomba na kushukuru.
 Amen Amen Ameeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeen.
Hakika umeshinda.
Ukiweza kufunga unaweza kufunga hata siku 1 au 3 au 3 au hata 5 au zile ambazo wewe utaona unaweza ukihusika kila siku na kipengele kimoja kuombea na kumbuka baada ya maombi ya kufunga au hata maombi ya bila kufunga fanya tendo la imani kwa MUNGU kwa kutoa sadaka nzuri itakayoambatana na maombi  juu ya ukomo wa kuteswa na maadui zako katika ulimwengu wa roho
Nawaonya pia wanaotumia masomo yangu vibaya na kwa manufaa yao waache tabia hiyo.
 Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa BWANA YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
0714252292.
0786719090
mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu.



Comments