MAOMBI YA KULIVUA VAZI LA KIPEPO ULILOVIKWA NA MAWAKALA WA SHETANI.

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.





Bwana YESU atukuzwe ndugu yangu.

Karibu tujifunze Neno la MUNGU kisha tuombe maombi ya ushindi.

Neno vazi lina maana ya kitu chenye kuvaliwa.

Kibiblia kuna aina mbili za Neno vazi

   1.  Vazi linaloonekana mfano Mwanzo 3:21 '' BWANA Mungu akawafanyia Adamu na mkewe mavazi ya ngozi, akawavika. ''

    2. Vazi la kiroho ambalo halionekani kwa macho ya kawaida ila matokeo ya vazi hilo huonekana, mfano Warumi 13:14 '' Bali mvaeni Bwana YESU KRISTO, wala msiuangalie mwili, hata kuwasha tamaa zake. ''

Ukiangalia tafasiri ya BHN juu ya andiko hilo Biblia inasema kwamba ‘’Bwana YESU awe vazi lenu’’

Kwa jinsi gani tumvae KRISTO?

Wagalatia 3:27 inajibu kwa kusema ‘’Maana ninyi nyote mliobatizwa katika KRISTO mmemvaa KRISTO.‘’


Tena 1 Petro 1 :15 inajibu kwa kusema ‘’ bali kama yeye(YESU) aliyewaita alivyo mtakatifu, ninyi nanyi iweni watakatifu katika mwenendo wenu wote;‘’

Vazi la KRISTO ni vazi jema sana.


Lakini pia kuna vazi baya kiroho ambalo mtu anaweza akavikwa kutoka ulimwengu wa roho wa giza, vazi hilo ndilo tunataka tupambane nalo leo kwa jina la YESU ili litoke katika miili ya watu ambao MUNGU amewakusudia ukiwemo wewe kama ulivalishwa vazi hilo la giza ili likutese.

Ni damu YESU KRISTO pekee inayoweza kuliondoa vazi hilo la giza kwa maombi kupitia jina la YESU KRISTO.

Tutashinda leo kwa jina la YESU KRISTO kama ambavyo ROHO MTAKATIFU ametupa ufunuo huu muhimu wa maombi.

Inawezekana bado hujaelewa, ngoja nikupe ushuhuda huu.

Mchungaji mmoja ambaye mimi Peter huwasiliana naye mara kwa mara  alikaa miaka mingi sana bila kuumwa, hakuwahi kulazwa na ana miaka mingi sana sana bila kunywa dawa yeyote.

Kuna wakati mwaka jana  aliumwa sana hali iliyopelekea kwenda Hospitali, alikutwa anaumwa magonjwa ya ajabu ajabu, mara kisukari, mara tatizo kwenye damu n.k. Kanisa likaingia katika maombi. Siku hiyo hiyo mmoja wa wana Kanisa akaota ndoto kuona Mchungaji wao amevikwa kipepo koti jeusi na akafunuliwa kwamba ili apone Kanisa liombe kumvua hilo vazi la magonjwa alilovikwa. Kanisa lilipoomba maombi ya kulivua vazi la kipepo hilo yule Mtumishi wa KRISTO alipona hakika na akaanza kuhubiri injili kama kawaida maana alikuwa hana hata uwezo wa kusimama madhabahuni tena.

Kwa hiyo kipepo wachawi au majini wanaweza kumvika mtu vazi la kipepo ili limtese, unaweza kuvikwa vazi la kukataliwa, kuumwa umwa kila mara, kudharauliwa, kuwa mtu wa hofu tu , kufuatiliwa na majini kila siku, umasikini, mateso n.k

Ndio maana leo niko hapa kukuomba uombe maombi ya kufuta kwa damu ya YESU kila vazi la kipepo ulilovikwa na mawakala za shetani.


Lakini kabla sijaendelea naomba kukupanua ufahamu juu ya vazi kiroho.


1.  Wenye dhambi wasiotubu kwa Bwana YESU watakwenda jehanamu kwa sababu kiroho watu hao wamevaa vazi la kigeni yaani vazi wasilotakiwa kulivaa wanadamu walioumbwa na MUNGU.

Vazi hilo la kigeni ni dhambi. 
Sefania 1:8 '' Na itakuwa, katika siku ile ya dhabihu ya Bwana, nitawaadhibu wakuu, na wana wa mfalme, na watu wote waliovaa mavazi ya kigeni.''

Vazi hilo hakuna anayemvalisha mtu yeyote ila ni mtu mwenyewe kwa matendo yake ya dhambi anajivalisha, kumpokea YESU na kutubu tu ndio njia pekee ya kulivua vazi hilo la kigeni liitwalo dhambi ambalo halitakiwi kuwako katika wanadamu wanaoutaka uzima wa milele. Ndugu livue vazi liitwalo dhambi ili lisiwe kamwe kwenye maisha yako maana hilo ni vazi la kigeni yaani ni vazi baya kwako.



2.  Wokovu wa YESU KRISTO ni vazi wanalotakiwa kulivaa watu wote duniani. 
 Isaya 61:10 '' Nitafurahi sana katika BWANA, nafsi yangu itashangilia katika MUNGU wangu; maana amenivika mavazi ya wokovu, amenifunika vazi la haki, kama bwana arusi ajipambavyo kwa kilemba cha maua, na kama bibi arusi ajipambavyo kwa vyombo vya dhahabu.''.
 Ndugu hakikisha unalivaa vazi hili muhimu sana. 
Zaburi 132:16 '' Na makuhani wake nitawavika wokovu, Na watauwa wake watashangilia.''

3.  Maisha ya haki katika KRISTO YESU ni vazi analotakiwa kulivaa kila mtu.
 Ayubu 29:14 '' Nalijivika haki, ikanifunika, Adili yangu ilikuwa kama joho na kilemba.''

4.  Utakatifu katika KRISTO ni vazi la wateule wa MUNGU. 
Ufunuo 3:5-6 '' Yeye ashindaye atavikwa hivyo mavazi meupe, wala sitalifuta kamwe jina lake katika kitabu cha uzima, nami nitalikiri jina lake mbele za Baba yangu, na mbele ya malaika zake. Yeye aliye na sikio, na alisikie neno hili ambalo ROHO ayaambia makanisa. ''. Ndugu hakikisha unalivaa vazi hilo bila kulivua hata siku moja. Wakolosai 3:10 ''mkivaa utu mpya, unaofanywa upya upate ufahamu sawasawa na mfano wake yeye aliyeuumba. ''

5.  Wito/Huduma ni vazi kwenye ulimwengu wa kiroho.
  2 Wafalme 2:9-15 ''......   Kisha akaliokota lile vazi la Eliya lililomwangukia, akarudi, akasimama katika ukingo wa Yordani.
14 Akalitwaa lile vazi la Eliya lililomwangukia, akayapiga maji, akasema, Yuko wapi Bwana, Mungu wa Eliya? Naye alipoyapiga maji, yakagawanyika huku na huku, Elisha akavuka.   .......'''
 Kama MUNGU amekupa wito  au huduma kwa ajili ya kazi yake katika Kanisa la MUNGU hakikisha unatimiza wito wako na huduma yako. 
Usikatae kufanya kazi ya MUNGU. Usilivue vazi hilo wanalovaliswa na MUNGU wateule wake waliookoka.


6.  Nguvu za ROHO MTAKATIFU ni vazi la wateule wa KRISTO. 
Luka 24:49 ''Na tazama, nawaletea juu yenu ahadi ya Baba yangu; lakini kaeni humu mjini, hata mvikwe uwezo utokao juu. ''

7.  Vazi safi la utakaso wa damu ya YESU KRISTO.
 Zakaria 3:4 '' Naye huyo akajibu, akawaambia wale waliosimama mbele yake, akisema, Mvueni nguo hizi zenye uchafu. Kisha akamwambia yeye, Tazama, nimekuondolea uovu wako, nami nitakuvika mavazi ya thamani nyingi. ''.
  Ndugu hakikisha unamkimbilia Bwana YESU kwa ajili ya kutubu  na baada ya kutubu atakuvika vazi jipya la utakaso, hivyo utaanza kuwa mtoto wa MUNGU na vazi la kwanza la dhambi malaika wataliondoa kwako maana sasa utakuwa safi mbele za MUNGU.



Katika kitabu cha Ayubu tunafahamu kwamba kwa kibali cha MUNGU na kwa sababu Maalumu MUNGU alimpa kibali shetani amshambulie Ayubu(Hiyo ilikuwa kwa Ayubu tu hivyo usijenge Imani yako kwamba unateseka kwa sababu MUNGU ametaka uteseke) Katika Maandiko anayemshambulia Ayubu ni shetani na shetani alimshambulia Ayubu kwa magonjwa mabaya . Nataka ujifunze kitu kwamba Ugonjwa unaopigana nao kipepo ni vazi.
 Ayubu 7:5-6 ''Mwili wangu unavikwa mabuu na madongoa ya udongo; Ngozi yangu hufumba, kisha ikatumbuka tena.  Siku zangu hupita upesi kuliko chombo cha kufumia, Nazo zapita pasipokuwa na matumaini. ''. Ayubu anakiri kwamba amevikwa vazi la ugonjwa.

Hata wewe wakuu wa giza wanaweza kukuvika vazi baya hivyo maombi yako ya leo vua kila vazi la kipepo ulilovikwa na mawakala wa shetani.

Kuna watu wamevikwa mavazi machafu. 
Zakaria 3:3 ''Basi, Yoshua alikuwa amevaa nguo chafu sana, naye alikuwa akisimama mbele ya malaika.''

Kuna watu watu wamevikwa vazi la aibu,kudharauliwa, kuonewa, magonjwa, madeni, umasikini,ajali, matatizo na kila uonevu.

Kuna watu kila akijaribu kuomba kazi hapati lakini wengine wanajaribu  tu na kupata kazi, ndugu livue vazi la kipepo ulilovalishwa kwa kutamkiwa kichawi na mawakala wa shetani.

Kuna waliovikwa kichawi vazi la laana, kukataliwa, kuabishwa na kufeli katika maisha.

Kuna watu wamevikwa vazi la kipepo la kuwafanya wawe chini tu.

Leo vua mavazi hayo ya kipepo, yavue kwa damu ya YESU KRISTO kwa njia ya maombi.

Leo omba MUNGU ili awavike wao vazi  la aibu, kila mawakala wa shetani wanaokufuatilia.

Livue na kulitowesha kwa damu ya YESU KRISTO kila vazi la laana waliokuvika mawakala wa shetani.

Zaburi 109:18-29 ''Alijivika laana kana kwamba ni vazi lake. Ikamwingilia moyoni kama maji, Na kama mafuta mifupani mwake. Na iwe kwake kama vazi ajivikalo, Na kama mshipi ajifungao daima.''

Vua mavazi ya kipepo, yavue kwa damu ya YESU KRISTO.

Mtu  mmoja aliota ndoto akimuona mtu mwingine akiwa kavalishwa kipepo makoti 7, yeye  hakujua lakini alipoona yule aliyemuona akiteseka katika mambo mengi ndipo akamwambia na mimi wakanihusisha tukaomba ili kuyaondoa mavazi hayo ya giza, ndipo  matatizo yakaisha.

Kuna mtu kila usingiziwaji na yeye yumo.

Kuna mtu kila balaa na yeye yumo.

Ndugu leo kwa maombi fuata kanuni hii.

1.  Yavue mavazi ya kipepo yote uliyovalishwa.

2.  Yachome moto kwa damu ya YESU KRISTO.



Pia katika maisha yako yote usikubali tena  usikubali haswaa vazi lako la Wokovu likachakaa, 
Ufunuo 7:14 ''Nikamwambia, Bwana wangu, wajua wewe. Akaniambia, Hao ndio wanatoka katika dhiki ile iliyo kuu, nao wamefua mavazi yao, na kuyafanya meupe katika damu ya Mwana-Kondoo.''

Hakikisha unalifua kila siku vazi lako la Wokovu wa KRISTO ulio wa thamani sana. Fua vazi lako la Wokovu kwa wewe kuishi maisha matakatifu kila siku, Kufanya maombi kila mara, kuenenda kwa ROHO MTAKATIFU na kulisoma na kulitafarakri Neno la MUNGU.

Omba MUNGU akuvike vazi la furaha 
Zaburi 30:11 '' Uligeuza matanga yangu kuwa machezo; Ulinivua gunia, ukanivika furaha.''

Omba MUNGU kwamba majira yako ya baraka yavikwe wema.
 Zaburi 65:11 '' Umeuvika mwaka taji ya wema wako; Mapito yako yadondoza unono.''

Omba MUNGU awavike fedheha wote waliokuonea kipepo.
 Zaburi 109:29  '' Washitaki wangu watavikwa fedheha, Watajivika aibu yao kama joho.''.

Nakuomba pia unaposoma somo hili andika points za kuombea, andika hata kama utapata points 20 za kuombea andika hizo pembeni ili ukianza kuomba ugusie kila eneo la maisha yako.

Endelea kuishi maisha matakatifu ya Wokovu wa  Bwana YESU ili siku ya mwisho uvikwe mwili mpya usioharibika wala kuzeeka.

1 Kor 15:53-54 '' Maana sharti huu uharibikao uvae kutokuharibika, nao huu wa kufa uvae kutokufa. Basi huu uharibikao utakapovaa kutokuharibika, na huu wa kufa utakapovaa kutokufa, hapo ndipo litakapokuwa lile neno lililoandikwa, Mauti imemezwa kwa kushinda. ''

Omba MUNGU vazi la haki alilokuvika lilete baraka kwako.



Maombi ya leo.

1.  Vua mavazi yote ya kipepo uliyovalishwa na mawakala wa shetani kwenye ulimwengu wa roho. Yataje mavazi hayo kupitia vifungo unavyoona umefungwa mfano magonjwa, kuteswa n.k

2.  Choma moto kwa damu ya YESU KRISTO kila vazi la kipepo ulilovalishwa na mawakala wa shetani.

3.  Omba MUNGU awavike fedheha maadui zako.

4.  Omba MUNGU ili majira yako ya baraka yavikwe wema

5.  Omba MUNGU kwamba vazi la haki alilokuvika likupe baraka

6.  Omba MUNGU akuvike vazi la furaha.

7.  Funika kwa damu ya YESU kila kitu chako ambacho kilikuwa kimevamiwa zamani na nguvu za giza.

 Natamani niseme mengi mno lakini naamini mwenye kuelewa ameelewa.
MUNGU akubariki kwa kujifunza somo hili muhimu pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane na nitakujulisha jinsi ya kukipata na  Naamini kitakusaidia sana.
Hapa chini ni MAOMBI YA KULIVUA VAZI LA KIPEPO ULILOVIKWA NA MAWAKALA WA SHETANI.  
Maombi haya naomba yamsaidie mtu yule ambaye hajui kuomba ili katika kuomba kwa kutumia hayo basi atakumbuka mahitaji yake na kuyataja katika maombi yake. Haya hapa chini ni maombi ya kuanzia tu katika maombi yako ili uendelee zaidi kuomba
Kwa waombaji wazoefu naamini baada tu ya kulisoma somo na kulielewa basi anajua aombee nini maana alikuwa anaandika points za kuombea. Kumbuka pia fundisho ni muhimu kuliko maombi hivyo wewe ambaye huwa unahusika na maombi tu hakikisha unajifunza kwanza somo lote ndipo utapata nguvu za kuomba na kushinda. 


MAOMBI YA KULIVUA VAZI LA KIPEPO ULILOVIKWA NA MAWAKALA WA SHETANI.  


Niko Mbele zako Eee YAHWEH MUNGU Muumbaji wangu, ninakushukuru sana kwa uzima ulionipa na ninakushukuru sana kwa nafasi hii njema ya kuomba mbele zako katika jina la YESU KRISTO Mwokozi aliye hai.
Niko pahali hapa BWANA naomba unisamehe dhambi zangu zote na uovu wangu wote na makosa yangu yote. Ninatubu kwako MUNGU Baba na  naomba unisamehe Ee BWANA.
Namkataa shetani na kazi zake zote na kuanzia sasa mimi nitamtii Bwana YESU Mwokozi aliye hai.
Eee MUNGU Baba naamini nimepokea Msamaha wako maana ulisema tutubu kwa maana ufalme wako umekaribia kama Neno lako linavyosema katika Mathayo 3:2.
Nisaidie MUNGU wangu ili niishinde dhambi, nishinde machukizo ya dunia na nishinde kila hila ya shetani katika maisha yangu.
Niko sasa muda huu mahali hapa nikiyavua mavazi ya kipepo yote niliyovalishwa na maajenti wa kuzimu wote.
Kila vazi la kipepo nilivalishwa ili linitese katika ndoa, katika afya, katika uchumi na katika uzao, hilo vazi la kipepo ninalivua sasa kwa damu ya YESU KRISTO na kwa jina la YESU KRISTO aliye hai.
Kila vazi la kukataliwa na kuonewa , hilo vazi la kipepo ninalivua sasa kwa damu ya YESU KRISTO na kwa jina la YESU KRISTO aliye hai.
Kila vazi la  kupata hasara kila mara katika biashara yangu hilo vazi la kipepo ninalivua sasa kwa damu ya YESU KRISTO na kwa jina la YESU KRISTO aliye hai.
Kila vazi la  kufuatiliwa na majini katika maisha yangu hilo vazi la kipepo ninalivua sasa kwa damu ya YESU KRISTO na kwa jina la YESU KRISTO aliye hai.
 Kila vazi la balaa na majanga  hilo vazi la kipepo ninalivua sasa kwa damu ya YESU KRISTO na kwa jina la YESU KRISTO aliye hai.
 Kila vazi la  kuteswa na magonjwa hilo vazi la kipepo ninalivua sasa kwa damu ya YESU KRISTO na kwa jina la YESU KRISTO aliye hai.
 Kila vazi la  vifungo vya giza vyote hilo vazi la kipepo ninalivua sasa kwa damu ya YESU KRISTO na kwa jina la YESU KRISTO aliye hai.
 Kila vazi la  kuondoa amani na furaha katika ndoa hilo vazi la kipepo ninalivua sasa kwa damu ya YESU KRISTO na kwa jina la YESU KRISTO aliye hai.
 Kila vazi la kukataliwa na wachumba  hilo vazi la kipepo ninalivua sasa kwa damu ya YESU KRISTO na kwa jina la YESU KRISTO aliye hai.
 Kila vazi la  kunizuia kupata kazi nzuri hilo vazi la kipepo ninalivua sasa kwa damu ya YESU KRISTO na kwa jina la YESU KRISTO aliye hai.
 Kila vazi la kuzuia uzao  hilo vazi la kipepo ninalivua sasa kwa damu ya YESU KRISTO na kwa jina la YESU KRISTO aliye hai.
Tena sasa ninachoma kwa moto wa jina la YESU KRISTO kila vazi la kipepo lolote nililokuwa nimevalishwa, vazi hilo nalichoma kwa moto wa jina la YESU KRISTO aliye hai.
Kila vazi la kiroho la kipepo ambalo nimelivua leo kwa maombi sasa vazi hilo kwenye ulimwengu wa roho ninalichoma moto kwa damu ya YESU KRISTO aliye hai, na halitanirudia kamwe.
Naweka mpaka kwa damu ya YESU KRISTO kati yangu na ulimwengub wa roho wa giza, ninavunja kila muunganiko uliokuwepo kati yangu na ulimwengu wa roho wa giza, ninavunja kila muunganiko uliokuwepo kati ya baraka zangu, uchumi wangu, ardhi yangu na kila fursa yangu, huo muunganiko uliokuwepo kati ya vitu vyangu hivyo na ulimwengu wa roho wa giza ninauvunja kwa damu ya YESU KRISTO na katika jina la YESU KRISTO aliye hai.
 Eee MUNGU Baba nakuomba uwavike fedheha maadui zangu wote katika ulimwengu wa roho, kama Neno lako BWANA linavyosema katika Zaburi 71:24 Kwamba  '' Ulimi wangu nao utasimulia Haki yako mchana kutwa. Kwa maana wameaibishwa, Wametahayarika, wanaonitakia mabaya.''
Kila wakala wa shetani ambaye aliwahi kunivika vazi la kipepo leo nimelivua vazi hilo, kwa jina la YESU KRISTO na nakuomba MUNGU Baba kwamba sasa uwapige kwa aibu na watahayarike sana maadui zangu wote katika ulimwengu wa roho.
Ninaomba wafedheheke na kuangamia wote waliokuwa wamenifunga katika afya yangu, uchumi wangu, ndoa yangu, uzao wangu na kibali changu.
Sasa Eee MUNGU Mwenyezi ninakuomba univike vazi la amani, furaha na baraka. Nivike Bwana YESU vazi lako la Wokovu na niishi maisha matakatifu siku zote katika wewe.
Kila baraka yangu popote iliko sasa naifunika kwa damu ya YESU KRISTO na mawakala wa kuzimu hawataigusa kamwe  hiyo baraka yangu.
Niseme nini Bwana YESU? Bali ninashukuru tu maana ni leo umenipa Ushindi kupitia jina lako na damu yako ya agano na ya thamani kupita vyote.
Ninakushukuru JEHOVAH MUNGU wangu maana hakuna aliye kama wewe MUNGU wa Israeli.
Ni katika jina la YESU KRISTO nimeomba na ninashukuru.
  Amen Amen Ameeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeen.
Hakika umeshinda.
Ukiweza kufunga unaweza kufunga hata siku 1 au 3 au 3 au hata 5 au zile ambazo wewe utaona unaweza ukihusika kila siku na kipengele kimoja kuombea na kumbuka baada ya maombi ya kufunga au hata maombi ya bila kufunga fanya tendo la imani kwa MUNGU kwa kutoa sadaka nzuri itakayoambatana na maombi  juu ya ukomo wa kuteswa na maadui zako katika ulimwengu wa roho
Nawaonya pia wanaotumia masomo yangu vibaya na kwa manufaa yao waache tabia hiyo.
 Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa BWANA YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
0714252292.
0786719090
mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu.

Comments