MAOMBI YA KUMUOMBEA MTU ALIYEBEBA KUSUDI LA MUNGU KWA AJILI YAKO.

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU

 Bwana YESU KRISTO atukuzwe sana ndugu zangu wote.
Karibu sana tujifunze Neno la MUNGU kisha tuombe maombi ya ushindi.
Kusudi la MUNGU ni sababu ya MUNGU kufanya jambo fulani kwa mtu fulani.
Kusudi la MUNGU ni malengo ya MUNGU yaliyobeba malengo ya MUNGU na azamio la MUNGU.
Jambo zuri kwako Mteule wa KRISTO ni kwamba Kusudi la MUNGU huwa halizuiliki labda tu wewe mhusika ulizuie kwa dhambi zako au  kutokujitambua kwako.
Ayubu 42:2 '' Najua ya kuwa waweza kufanya mambo yote, Na ya kuwa makusudi yako hayawezi kuzuilika.'' 
 
Neno ''kwa kusudi'' lina maana ya ''Kwa ajili ya'' au ''ili'' au ''Kwa nia ya''
Maneno hayo yana maana sawa na Neno ''Kwa kusudi''
 Jambo la kwanza kabisa kuhusu kusudi la MUNGU ni Kusudi la MUNGU la kumleta Bwana YESU duniani.
Kabla ya kusudi jingine lolote naomba utambue kusudi la MUNGU kumleta YESU KRISTO ili awe Mwokozi wetu.
Kusudi la MUNGU kumleta YESU KRISTO duniani limebeba kwa uchache tu mambo yafuatayo.
1. Ili watakaomwamini YESU kama Mwokozi wao waupate uzima wa milele.
Yohana 3:16 ''Kwa maana jinsi hii MUNGU aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele.   ''
Neno ''ili'' lina maana ya ''Kwa kusudi''
Kwa hiyo YESU alikuwa kwa kusudi kwamba atakayemwamini asipotee bali awe na uzima wa milele.
 
2. YESU alikuja ili kuziharibu kazi zote za shetani  kwenye maisha yako kama ukiamua kujihusika na yeye YESU Mwokozi.
1 Yohana 3:8b  ''Kwa kusudi hili Mwana wa MUNGU alidhihirishwa, ili azivunje kazi za Ibilisi.''

3. YESU alikuja kuwatafuta waliopotea ili sasa kwa kupitia yeye wasipotee.
Luka 19:10 ''Kwa kuwa Mwana wa Adamu alikuja kutafuta na kuokoa kile kilichopotea.''

4. YESU alikuja ili watakaotubu na kumpokea kama Mwokozi wapate ondoleo la dhambi.
Mathayo  1:21 '' Naye atazaa mwana, nawe utamwita jina lake YESU, maana, yeye ndiye atakayewaokoa watu wake na dhambi zao.''
 Kwa YESU hata kama ni dhambi nyingi kiasi gani ukitubu kwake  na kubadilika yaani kuziacha dhambi hizo hakika unasamehewa.
 
Hayo ni sehemu kidogo ya kusudi la MUNGU kumleta YESU KRISTO duniani, kusudi hilo la MUNGU ndilo la kwanza kabisa ambalo kila binadamu duniani anatakiwa kulifuata.
 Baada ya hilo kusudi kuu la MUNGU sasa yako pia makusudi ya MUNGU mengi kipindi ambacho wewe umeshaokoka na unaishi maisha matakatifu.
Unatakiwa kushirikiana na makusudi hayo ya MUNGU ili ufanikiwe.
Mithali 16:4 ''BWANA amefanya kila kitu kwa kusudi lake; Naam, hata wabaya kwa siku ya ubaya.''
 Kumbe MUNGU amefanya kila kitu kwa kusudi.
Hata wabaya wakati wa ubaya, mfano mnaweza mkawa na Baba wa familia mkali sana akiwachapa ili msome shule, kweli kwa sababu ya ukali wa baba mnasoma kisha baadae mnapata kazi nzuri, huyo ametimiza kusudi la MUNGU.
Watu wa MUNGU sana sana huombea  watu waliobeba kusudi la MUNGU kwao kuhusu ndoa tu na kujisahau kuhusu kuombea watu waliobeba makusudi ya MUNGU katika maeneo mengine.
 Binti anaweza akaomba sana juu ya atakayekuja kuwa mumewe, ni sawa kabisa maana huyo mume wake anatakiwa awe kwa  kusudi la MUNGU la ndoa.
Kijana anaweza akafunga na kuomba sana juu ya atakayekuja kuwa mkewe,  maana mke anatakiwa awe kusudi la MUNGU na alibebe kusudi la MUNGU.
Ni sawa kabisa kuombea mume au mke aliye kusudi la MUNGU na aliyelibeba kusudi la MUNGU, Lakini ni muhimu pia kukumbuka kuomba kila mtu aliyebeba kusudi la MUNGU kwa ajili yako katika kila eneo la Maisha yako, ikumbuke hiyo na izingatie sana hiyo katika maombi yako.
Muombee aliyebeba kusudi la MUNGU kwa ajili yako, muombee akae katika nafasi yake ya ki MUNGU kwa ajili yako.
Somo hili mimi Peter nilipata kama ufunuo wakati nikiomba katika  ibada ya jioni kanisani kwetu.
 Muhimu tu zingatia pia kwamba unapomuombea mtu aliyebeba kusudi la MUNGU kwa ajili yako hakikisha humtegemeo mtu huyo wala kumjaza moyoni mwako bali mtegemee MUNGU maana yeye MUNGU ndiye atamuweka mtu huyo katika nafasi ya kufanikisha kusudi la MUNGU kwa ajili yako.
Hebu ngoja nikuonyeshe mifano kadhaa katika Biblia ya watu waliokuwa wamebeba kusudi la MUNGU kwa ajili ya watu wengine.

1. Mama wa Sarepta aliandaliwa na MUNGU ili amrishe chakula Nabii Eliya.
1 Wafalme 17:9 '' Ondoka, uende Sarepta, ulio mji wa Sidoni, ukae huko. Tazama, nimemwagiza mwanamke mjane wa huko akulishe.''
 Mama huyu alikuwa amelibeba kusudi la MUNGU la kumlisha Eliya kwa muda mrefu, mama huyu alikaa katika nafasi yake ya ki MUNGU kwa ajili ya Eliya.
Hata wewe inawezekana unatafuta kuapata kazi. Maombi yako ya kumuombea mtu aliyelibeba kusudi la MUNGU la wewe kupata kazi yanaweza kumfanya mtu huyo awe katika nafasi husika ili kukupatia kazi wewe. Unaweza ukashangaa wakuu wa nchi wanamteua mtu fulani kushika madaraka fulani kumbe mtu huyo anawekwa kwenye nafasi hiyo ili akuajiri wewe maana atakuwa amepewa na madaraka ya kuajiri.
Hata wewe kuna watu wanaweza wakalibeba kusudi la MUNGU la kuajiriwa kwako, kufunguliwa kwako vifungo vya giza, wakikuombea watumishi hao hakika unafunguliwa na kuwa huru.
Kuna watu wanaweza wakalibeba kusudi la MUNGU la kupona kwako magonjwa, watumishi hao wa KRISTO wakikuombea hakika unapona maana wako katika kusudi la MUNGU na wamekaa katika nafasi zao za kusudi la MUNGU kwako.
Kuna watu wanaweza wakalibeba kusudi la MUNGU la kupandishwa kwako cheo au kupandishwa mshahara kwako, omba tu ili wakae kwenye nafasi zao za kulitimiza kusudi la MUNGU kwako la kupandishwa cheo.
Omba MUNGU ili watu hao wakae kwenye nafasi zao kwa ajili yako.

2. Waisraeli walikuwa kwenye vifungo, walipomuomba MUNGU yeye MUNGU aliwaletea mtu wa kuwaokoa.
Waamuzi 3:15 '' Lakini wana wa Israeli walipomlilia BWANA, BWANA akawainulia mwokozi, Ehudi, mwana wa Gera, Mbenyamini, mtu aliyekuwa mwenye shoto; nao wana wa Israeli walimpelekea Egloni mfalme wa Moabu tunu mkononi mwa huyo Ehudi.''

Waisraeli walimlilia MUNGU yaani walimuomba MUNGU msaada, jibu la MUNGU lilikuwa kuwainulia mtu miongoni mwao ili aweze kuwaokoa.
Hata wewe inawezekana umesingiziwa kesi na anayekushitaki anatumia nguvu yake ya pesa ili akukandamize, ndugu kwa maombi yako nakuambia MUNGU anaweza kukuinulia watu watakaoiona thamani yako, hao hawatapokea rushwa wala hawatapindisha sheria bali watamkamata na haki yako itakurudia, naamini sasa unaanza kuelewa juu ya kuombea mtu aliyebeba kusudi la MUNGU kwa ajili yako.
Inawezekana kabisa wewe ni mjane na ndugu za mumeo wanataka kukufukuza katika nyumba yako mliyojenga na mumeo, kwa maombi yako MUNGU anaweza akakuinuliwa watetezi ambao watakuwa upande wako na utashinda.
Yako mambo mengi sana unaweza ukaonewa na wanaotumika kishetani lakini ukiomba kwa MUNGU yeye ni mwaminifu na wa haki hakika atakuinuliwa watu kiasi kwamba hata mawakala wa shetani watakimbia na kuhama mji huku hata wewe hujui imekuaje.
Inawezekana kuna mtu anatumika kipepo ili akupore mchumba wako, kwa maombi yako na utakatifu  MUNGU anaweza akakuinulia waombaji kiasi kwamba hila za shetani zinavunjika dakika hiyo hiyo. Kumbuka tu kuwa unaombea kila aliyebeba kusudi la MUNGU kwa ajili yako.

 3. Yahazieli alisimama katika kusudi la MUNGU ili kuwapa mbinu za ushindi Waisraeli na kuwahakikishia ushindi.
2 Nyakati 20:14-17 '' Ndipo Yahazieli mwana wa Zekaria, mwana wa Benaya, mwana wa Yeieli, mwana wa Matania, Mlawi, wa wana wa Asafu, akajiliwa na roho ya BWANA, katikati ya kusanyiko; akasema, Sikieni, Yuda wote, nanyi mkaao Yerusalemu, na wewe mfalme Yehoshafati; BWANA awaambia hivi, Msiogope, wala msifadhaike kwa ajili ya jeshi kubwa hili; kwani vita si yenu bali ni ya MUNGU. Kesho shukeni juu yao; tazameni, wanakwea kwa kupandia Sisi; nanyi mtawapata penye mwisho wa bonde, mbele ya jangwa la Yerueli. Hamtahitaji kupigana vita, jipangeni, simameni, mkauone wokovu wa BWANA ulio pamoja nanyi, enyi Yuda na Yerusalemu; msiogope, wala msifadhaike; kesho tokeni juu yao; kwa kuwa BWANA yu pamoja nanyi.''
 Waisareli walikuwa katika wakati mgumu sana sana, walikuwa wamepanga vita dhidi ya maadui wenye nguvu kuliko wao na maadui zao walikuwa wengi tena wamewazunguka, ilikuwa mfano wake ni kama leo kwamba mataifa ya G7 yote kwa pamoja au mataifa ya NATO yote kwa pamoja yaandae wanajeshi na silaha kubwa za kijeshi zikiwemo silaha za nyuklia  kwenda kupigana na taifa mojawapo lililo katika kundi la mataifa matano masikini zaidi duniani, vita kama hiyo kujua mshindi ni rahisi sana sana lakini kwa Israeli haikuwa hivyo.
Neno la MUNGU likamjia Mtu mmoja katika kundi la waombaji kuonyesha mbinu za ushindi na kuwahakikishia ushindi. Ukiendelea kusoma maandiko katika hiyo 2 wafalme sura ya 20 utagundua kwamba njia za MUNGU hazichunguziki maana waliotarajiwa kushinda vita waliuana wao kwa wao na Israeli wala hakupigana vita maana kwa maombi yao yaliifanya vita yao iwe vita ya MUNGU na MUNGU ni mshindi milele.
Hata wewe inawezekana kabisa unapambana na maadui wakali sana lakini kwa maombi MUNGU anaweza akakuinuliwa watu wenye nguvu kuliko adui zako na ukashinda kirahisi sana.
Ndugu hakikisha unaombea watu waliobeba kusudi la MUNGU kwa ajili yako.

4. Elisha alibeba kusudi la MUNGU la kufunguliwa kwa mama mmoja kutoka katika vifungo vya madeni, hiyo iko 2 Wafalme 4:1-7 utasoma kwenye Biblia yako. Lakini Mstari wa 7 unasema kwamba   '' Ndipo akaja akamwambia yule mtu wa MUNGU. Naye akasema, Enenda ukayauze mafuta haya, uilipe deni yako; nayo yaliyosalia uyatumie wewe na watoto wako. ''
Hata wewe unaweza ukakutana na Mtumishi wa KRISTO akakuombea na ukafunguliwa.
Unaweza ukawa unateswa na madeni lakini MUNGU akamwinua mtu mmoja na kukupa mtaji utakaokufanya baada ya muda usiwe na deni, na wakati huo wewe ukawa mtu wa kukopesha na sio kukopa.
Ombea waliobeba kusudi al MUNGU kwa ajili yako.
Hata ninapoandika somo hili nauona muujiza wa MUNGU Baba.

MUNGU hutumia watu kwa kusudi lake kwa ajili ya yako.
Inawezekana kabisa wewe hujaokoka na MUNGU kila siku anakutumia watu kwa kusudi lake ili uokoke.
Inawezekana hata somo hili ni kusudi la MUNGU ili wewe uokoke na usiende jehanamu.
Inawezekana kabisa ni somo hili hili ni MUNGU amelituma kwako ili upate maarifa ya kukusaidia katika maombi ili sasa ufanikiwe na kustawi sana kimaisha na kiroho.
Ndugu, ombea watu wa MUNGU waliobeba kusudi la MUNGU kwa ajili yako.

Kwanini uombe juu ya mtu aliyelibeba kusudi la MUNGU  kwa ajili yako?

1. Maombi yatamfanya mtu huyo aliyebeba kusudi la MUNGU kwa ajili yako akae kwenye nafasi yake.
Wamuzi 6:7-10 '' Kisha ikawa, hapo wana wa Israeli walipomlilia BWANA kwa sababu ya Midiani,  BWANA akamtuma nabii aende kwa hao wana wa Israeli; naye akawaambia, BWANA, yeye MUNGU wa Israeli, asema hivi, Mimi niliwaleta ninyi mkwee kutoka Misri, nikawatoa katika nyumba ya utumwa; nami niliwaokoa na mikono ya Wamisri, na mikono ya wote waliokuwa wakiwaonea, nami niliwafukuza watoke mbele zenu, nami niliwapa ninyi nchi yao; kisha niliwaambia, Mimi ndimi BWANA, Mungu wenu; msiiche miungu ya Waamori, ambayo mwaketi katika nchi yao; lakini hamkuitii sauti yangu.   ''
Nabii alisimama kwenye nafasi yake kwa sababu ya maombi.
Hata kwako mtu aliyelibeba kusudi la MUNGU anaweza kukaa katika nafasi yake kwa ajili yako, kwa sababu ya maombi yako.

 2. Ili ROHO MTAKATIFU amjulishe kulitumikia kusudi la MUNGU kwa ajili yako.
Matendo 13:2 ''Basi hawa walipokuwa wakimfanyia BWANA ibada na kufunga, ROHO MTAKATIFU akasema, Nitengeeni Barnaba na Sauli kwa kazi ile niliyowaitia.''
 Maombi yao ndiyo yalimfanya ROHO MTAKATIFU ajulishe juu ya akina Mtume Paulo kuanza kazi ya MUNGU. Tunajua kazi mfano za mtume Paulo jinsi zilivokuwa na faida hata kwa walioomba siku hiyo. Mtume Paulo alilibeba kusudi la MUNGU kwa ajili ya Kanisa wakati ule na hata wakati wote wa Kanisa ikiwemo na leo.
Unaweza ukamuombea Mtu aliyebeba kusudi la MUNGU kwa ajili yako na ROHO MTAKATIFU anaksemesha mtu huyo ili achukue nafasi ya kukusaidia wewe.

3. Ili ujue kushirikiana na majira ya MUNGU ya wakati huu yaliyobeba kusudi la MUNGU kwa ajili yako.
Mhubiri 3:1 ''Kwa kila jambo kuna majira yake, Na wakati kwa kila kusudi chini ya mbingu.''
 Unapoombea mtu aliyebeba kusudi la MUNGU kwako hakika majira pia yatakujulisha kama jambo hilo ni wakati huu, ukijua hakika utashirikiana na majira yako ya wakati huu yaliyobeba kusudi la MUNGU.
Mfano unaomba kazi kisha ukasikia nafasi za kazi unayoitaka zinatangazwa, hapo majira yako unajua yamefika na kwa kuombea watu waliobeba kusudi la MUNGU la wewe kupata kazi basi ukiomba kazi hiyo utakuta watu husika wamekaa katika nafasi zao kiungozi na watakupatia kazi.

4. Ili walitimize kusudi la MUNGU kwa ajili yako waliloamuriwa na MUNGU.
Wafilipi 2:13 '' Kwa maana ndiye MUNGU atendaye kazi ndani yenu, kutaka kwenu na kutenda kwenu, kwa kulitimiza kusudi lake jema.''
 Ni MUNGU anayefanya kazi ndani ya watu ambao amekusudia walitimize kusudi lake kwa ajili yako.
ukiwaombea hakika wataanza kazi ya kulitimiza kusudi la MUNGU kwa ajili yako.
Kumbuka ''Nasi twajua ya kuwa katika mambo yote Mungu hufanya kazi pamoja na wale wampendao katika kuwapatia mema, yaani, wale walioitwa kwa kusudi lake.-Warumi 8:28 ''

 Katika maombi yako ya leo ufanyeje?

1. Omba kwa MUNGU kwa watu hao waliobeba kusudi la MUNGU kwa ajili yako wakae katika nafasi zao.

2. Omba MUNGU awalinde kama kusudi la MUNGU kwako sio la wakati huu.

3. Haribu kila mipango ya shetani ya kuzuia kusudi la MUNGU kwako kupitia watu hao.

4. Mwambie ROHO MTAKATIFU awakumbushe kutimiza kusudi la MUNGU kwako.

5. Ombea kusudi la MUNGU la mwaka huu kwako litimie.

Natamani niseme mengi mno lakini naamini mwenye kuelewa ameelewa.
MUNGU akubariki kwa kujifunza somo hili muhimu pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane na nitakujulisha jinsi ya kukipata
na  Naamini kitakusaidia sana.
Hapa chini ni 
MAOMBI YA KUMUOMBEA MTU ALIYEBEBA KUSUDI LA MUNGU KWA AJILI YAKO.
Maombi haya naomba yamsaidie mtu yule ambaye hajui kuomba ili katika kuomba kwa kutumia hayo basi atakumbuka mahitaji yake na kuyataja katika maombi yake. Haya hapa chini ni maombi ya kuanzia tu katika maombi yako ili uendelee zaidi kuomba
Kwa waombaji wazoefu naamini baada tu ya kulisoma somo na kulielewa basi anajua aombee nini maana alikuwa anaandika points za kuombea. Kumbuka pia fundisho ni muhimu kuliko maombi hivyo wewe ambaye huwa unahusika na maombi tu hakikisha unajifunza kwanza somo lote ndipo utapata nguvu za kuomba na kushinda.
 


MAOMBI YA KUMUOMBEA MTU ALIYEBEBA KUSUDI LA MUNGU KWA AJILI YAKO.

BABA wa mbinguni hakuna aliye kama wewe, ninakushukuru MUNGU Muumba wangu kwa ulinzi wako kwangu na uzima kwangu kupitia YESU KRISTO Mwanao wa pekee.
Jina lako litukuzwe milele yote na Nitasema kwamba '' BWANA ndiye kimbilio langu na ngome yangu, MUNGU wangu nitakayemtumaini.'' Kama isemavyo Zaburi 91:2
Na ukweli wa milele ni kwamba ''Wewe, BWANA, umekuwa makao yetu, Kizazi baada ya kizazi.  Kabla haijazaliwa milima, wala hujaiumba dunia, Na tangu milele hata milele ndiwe MUNGU.'' kama isemavyo Zaburi 90:1-2





Ninakushuru sana MUNGU wangu na pokea sifa na heshima milele yote.
Nakushukuru YESU KRISTO Mwokozi wangu kwa kunipenda na kunichagua ili nami niwe mtoto wa MUNGU.
Ninakushukuru ROHO MTAKATIFU Maana wewe ndiye mwangalizi wa Kanisa la KRISTO duniani, Ee BWANA hata mimi naomba nifanyike kanisa hai siku zote.
Nisamehe nilipokosea na nipe sasa kutembea kwenye kusudi lako la wokovu.
Niko sasa mahali hapa nikimuombea kila mtu aliyebeba kusudi lako MUNGU kwa ajili yangu.
Kila aliyebeba kusudi la MUNGU la mimi kupata kiwanja, kupata kazi au kupata baraka yangu namuombea kwa MUNGU mtu huyo ili akae katika nafasi yake na kutimiza kusudi la MUNGU juu yangu.
Kila aliyebeba kusudi la MUNGU la kushinda kwangu kesi au kupata haki zangu nilizodhulumiwa, namuombea kwa MUNGU mtu huyo ili akae katika nafasi yake na kutimiza kusudi la MUNGU kwangu.
Kila mtumishi wa KRISTO aliyebeba kusudi la MUNGU ili mimi nifunguliwe vifungo, nipone magonjwa na niwashinde mawakala wa shetani, namuombea kwa MUNGU mtu huyo ili akae katika nafasi yake na kutimiza kusudi la MUNGU kwangu , katika jina la YESU KRISTO na iwe kama nilivyoomba leo.
Kila mtu aliyebeba kusudi la MUNGU ili mimi nipate eneo la biashara na nipate haki za kufanya biashara,  namuombea kwa MUNGU mtu huyo ili akae katika nafasi yake na kutimiza kusudi la MUNGU juu yangu.
Kama kusudi la MUNGU sio la wakati huu namuombea mtu huyo ili muda ukifika akae kwenye nafasi yake kwa ajili ya kufanikiwa kwangu.
Najua kabisa wakati mwingine MUNGU hutumia watu ili mimi nifanikiwe, nawaombea watu hao kusimama katika nafasi yao ili kunisadia,katika jina la YESU KRISTO na iwe kama nilivyoomba.
Najua kabisa ili nisafiri kwenda nchi za nje inahitajika nauli, visa na kibali, Eee MUNGU Baba ninakuomba mtu uliyemkusudia anipe visa pale ubalozini, naomba awe katika zamu yake siku hiyo mimi nikifika katika ofisi hiyo, ninaomba yule anayetakiwa kunipa kibali awe kwenye nafasi yake kwa ajili yangu ili nifanikiwe.
Kama kuna mtumishi wa MUNGU anatakiwa kunisaidia katika huduma yangu, Eee Bwana YESU naomba mtu huyo akae katika katika nafasi yake,katika jina la YESU KRISTO na iwe kama nilivyoomba.
Kila ambaye amebeba kusudi la MUNGU kwa ajili yangu katika jambo lolote, ninaomba Eee ROHO MTAKATIFU umkumbushe mtu huyo kama amejisahau ili tu afanye kazi yake iliyo agizo lako MUNGU wa uzima.
Katika maamuzi ninaomba Eee MUNGU wangu uweke watu watakaonisaidia na wale waliojipanga  kunikandamiza uwatoe eneo hilo kwa uweza wako, katika kupata cheo au katika kuajiriwa au kuongezewa mshahara, Eee MUNGU Baba naomba katika hayo yote akae mtu sahihi aliyelibeba kusudi lako la kufanikiwa kwangu, katika jina la YESU KRISTO na iwe kama nilivyoomba.
Wewe MUNGU unaweza kumtuma mtu hata kutoka mbali ili tu aje awe msaada kwangu ili nifanikiwe kisha nikifanikiwa mtu huyo atarudi katika eneo lake la kwanza, Eee MUNGU Baba ni kwako tu nategemea na nawaombea wote waliobeba kusudi lako kwa ajili yangu wakae katika nafasi zao.
Katika kila ofisi ambako natakiwa kwenda ninaomba Eee MUNGU wangu akae mtu aliyelibeba kusudi lako kwa ajili ya kunisaidia mimi, nataka mtu yule ambaye nikifika tu atashughulikia suala langu dakika hiyo hiyo, nataka mtu ambaye atalishughulikia suala langu kama lake, Eee MUNGU Baba namwitaji mtu huyo akae katika kusudi lako kwa ajili yangu,
katika jina la YESU KRISTO na iwe kama nilivyoomba.
Ninamuombea daktari aliyebeba kusudi lako kule Hospitalini, Ninamuombea Polisi aliyelibeba kusudi lako MUNGU kule kituoni, Ninamuombea Waziri aliyebeba kusudi lako MUNGU kule Wizarani, Ninamuombea jaji au hakimu aliyebeba kusudi lako MUNGU kwa ajili yangu kule Mahakamani,
katika jina la YESU KRISTO na iwe kama nilivyoomba.
Ninaombea kila mtu kutoka katika kila idara ambayo mimi nitahusika kuhitaji msaada, Eee JEHOVAH MUNGU wa uzima ninaomba mbele zako BWANA kwamba katika eneo hilo akae mtu aliyelibeba kusudi lako kwa ajili ya kufanikiwa kwangu. Ninaomba akae mtu ambaye atanijali na kunithamini, ninaomba akae mtu atakayeiona thamani yangu, ninaomba akae mtu ambaye ana hofu ya MUNGU,  Wale wanaotaka rushwa au ngono naomba wafukuzwe kazi au watoke katika ofisi hiyo  kabla sijafika katika eneo hilo, katika jina la YESU KRISTO na iwe kama nilivyoomba.
Ninaomba kwa ajili ya mwenzi wa maisha aliye kusudi lako YAHWEH MUNGU wangu na naomba pia mtu huyo awe amelibeba kusudi lako MUNGU wangu, katika jina la YESU KRISTO namuombea mtu huyo ili atokee kwangu katika wakati sahihi wa MUNGU, Kama mtu huyo amefungwa na vifungo namfungua leo kwa damu ya YESU KRISTO na katika jina la YESU KRISTTO Mwokozi aliye hai..
Nakushuru MUNGU Baba maana ulisema kwamba kama kama ninamini hakika itakuwa kama nilivyoamini, kama Neno lako linavyosema katika Marko 9:23 Kwamba ''Ukiweza! Yote yawezekana kwake aaminiye.''
Mimi naamini  Bwana YESU na hakika najua imekuwa sawa sawa na nilivyoomba, katika jina la YESU KRISTO nimeomba na kupokea ushindi mkuu.
 Amen Amen Ameeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeen.
Hakika umeshinda.

Ukiweza kufunga unaweza kufunga hata siku 1 au 3 au 3 au hata 5 au zile ambazo wewe utaona unaweza ukihusika kila siku na kipengele kimoja kuombea na kumbuka baada ya maombi ya kufunga au hata maombi ya bila kufunga fanya tendo la imani kwa MUNGU kwa kutoa sadaka nzuri itakayoambatana na maombi  juu ya ukomo wa kuteswa na maadui zako katika ulimwengu wa roho 
Nawaonya pia wanaotumia masomo yangu vibaya na kwa manufaa yao waache tabia hiyo.
 Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa BWANA YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
0714252292.
0786719090
mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu.

Comments