NI SIKU ZA MWISHO, HERI KUTENGENEZA NA YESU KRISTO MWOKOZI..

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.

Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.
Zipo dalili nyingi za siku za mwisho.
Dalili mojawapo ya siku za mwisho ni watu kufundisha mafundisho ya kuwakataza watu kula baadhi ya vyakula eti kwamba vyakula hivyo ni najisi.
Biblia inasema
" Basi ROHO anena waziwazi ya kwamba nyakati za mwisho wengine watajitenga na imani, wakisikiliza roho zidanganyazo, na mafundisho ya mashetani; kwa unafiki wa watu wasemao uongo, wakichomwa moto dhamiri zao wenyewe;
wakiwazuia watu wasioe, na KUWAAMURU WAJIEPUSHE NA VYAKULA, ambavyo MUNGU aliviumba vipokewe kwa shukrani na walio na imani wenye kuijua hiyo kweli. Kwa maana kila kiumbe cha MUNGU ni kizuri, wala hakuna cha kukataliwa, kama kikipokewa kwa shukrani; kwa kuwa kimetakaswa kwa Neno la MUNGU na kwa kuomba.-1Timotheo 4:1-5"

Lengo langu ni nini katika Ujumbe huu?
Lengo langu ni kukujulisha ndugu kwamba hizi ni siku za mwisho?
Ukiona watu wanafundisha kutokula baadhi ya vyakula tambua kwamba mwisho u karibu.
Wanaokataza waumini wao kula baadhi ya vyakula wanakuwa wanatimiza tu unabii bila kujua.
Siku ya mwisho I karibu sana.
Ndugu huu sio wakati wa kujisahau, huu sio wakati wa kuacha Wokovu ili upate mwenzi au kazi.
Huu ni wakati wa kutubu na kujisalimisha kwa YESU KRISTO Mwokozi.


Tito 2:11-14 '' Maana neema ya MUNGU iwaokoayo wanadamu wote imefunuliwa; nayo yatufundisha kukataa ubaya na tamaa za kidunia; tupate kuishi kwa kiasi, na haki, na utauwa, katika ulimwengu huu wa sasa; tukilitazamia tumaini lenye baraka na mafunuo ya utukufu wa KRISTO YESU, MUNGU mkuu na Mwokozi wetu; ambaye alijitoa nafsi yake kwa ajili yetu, ili atukomboe na maasi yote, na kujisafishia watu wawe milki yake mwenyewe, wale walio na juhudi katika matendo mema. '' 

  Ndugu, Dini tu haitoshi kumpeleka mtu uzima wa milele, Bali ni Utakatifu katika KRISTO tu.
Dhehebu tu haliwezi kumpeleka mtu uzima ni, Bali ni Wokovu na Utauwa katika kweli.


Zaburi 37:28 '' Kwa kuwa BWANA hupenda haki, Wala hawaachi watauwa wake. Wao hulindwa milele, Bali mzao wa wasio haki ataharibiwa.''

Mengi ya yanayotokea duniani ni julisho tu kwetu kwamba mwisho u karibu.

Ndugu, kuna watakaonyakuliwa na Bwana YESU ili kupelekwa uzima wa milele na kuna watakaoachwa ili ziwa la moto liwapate.
Kitu muhimu kwa wakati wetu huu ni kuokoka na kuishi maisha matakatifu katika Wokovu wa Bwana YESU.

 1 Yohana 5:11-13 ''Na huu ndio ushuhuda, ya kwamba MUNGU alitupa uzima wa milele; na uzima huu umo katika Mwanawe. Yeye aliye naye Mwana, anao huo uzima; asiye naye Mwana wa MUNGU hana huo uzima. Nimewaandikia ninyi mambo hayo, ili mjue ya kuwa mna uzima wa milele, ninyi mnaoliamini Jina la Mwana wa MUNGU.''

 Ndugu, kumbuka kuna kuondoka duniani.
Ndugu, Hata kama utajiwekea pesa ya matibabu.
Hata kama umejiwekea bajeti kubwa ya kutibu magonjwa yatakayotokea kwako(Kwa mtazamo wako), MUNGU akitaka kukuchukua anakuchukua tu hata kama na bajeti ya matibabu unayo. Ni heri sana kunyenyekea kwa MUNGU, kumcha yeye na kulitii Neno lake la injili ya KRISTO iliyo ya thamani sana.
Ndugu mmoja akasema "Mimi hata nikiumwa Leo Nina pesa benki za kunitibu" mtu huyo hataki kitu kinachoitwa maombi wala kunyenyekea kwa MUNGU. Kwake huyo pesa ndio kila kitu lakini anasahau kwamba pesa haiwezi kukunua uhai.
Ni vyema sana kwenda Hospitalini lakini tambua kwamba MUNGU ndiye mponyaji ndio maana anaitwa JEHOVAH RAPHA.
Kuna watu walikuwa wanaumwa ugonjwa kama wako na wakanywa dawa kama ulizokunywa wewe lakini hawakupona. Wewe umepona lakini hata shukrani kwa MUNGU huna.
Hivyo ndugu nakushauri mche MUNGU katika hali zote, sio kweli kwamba wanaokufa ni maskini tu, hapo ndipo unagundua kwamba mponyaji ni MUNGU.
Madaktari ni watumishi wa MUNGU kama watakaa kwenye kusudi la MUNGU lakini ukweli mmoja ni kwamba mponyaji ni MUNGU pekee.
Yeye YESU KRISTO akisema uishi hakika utaishi haijalishi watu duniani wanasema hatapona.
Niliwahi kufikia hatua hiyo Mwishoni mwa 2010 lakini Bwana YESU alinitokea na kuniponya, nilikaa masaa 15 sijitambui, na nilipozinduka tu kwa masikio Yangu nilimsikia Daktari akisema sitapona lakini YESU akasema nimepona na hakika nikapona.
Ndugu usiwekee tumaini kwenye dawa Bali weka tumaini kwa MUNGU na MUNGU anaweza akatumia dawa kukuponya na anaweza pia akakuponya bila kutumia dawa.
Usiende kwa waganga wa kienyeji wa aina yeyote, maana kuenda huko ni kupishana na kusudi la MUNGU na kwenda huko ni kujiangamiza nafsi yako huku unajiona.
Mche MUNGU katika hali zote, mpokee YESU kama Mwokozi wako na anza kuishi maisha matakatifu.
Na mwisho kumbuka kwamba muda wako wa kuondoka ukifika hakika utaondoka tu hata kama una bajeti ya mamilioni kwa ajili ya matibabu yako binafsi, heri kumaliza na YESU KRISTO kuliko kumaliza na shetani kisha uende jehanamu.

Kumbuka Waebrania 9:27 Biblia inasema '' Na kama vile watu wanavyowekewa kufa mara moja, na baada ya kufa hukumu; ''
Nimejulishwa nikuambie hivyo na waliokusudiwa naamini watatengeneza na Bwana YESU na watamtegemea MUNGU kwanza kuwaponya.


Imani ya kumkiri YESU KRISTO kuwa Bwana na Mwokozi ndio sifa ya kwanza ya wateule wa MUNGU.
Warumi 10:9-11 '' Kwa sababu, ukimkiri Yesu kwa kinywa chako ya kuwa ni Bwana, na kuamini moyoni mwako ya kuwa Mungu alimfufua katika wafu, utaokoka. Kwa maana kwa moyo mtu huamini hata kupata haki, na kwa kinywa hukiri hata kupata wokovu. Kwa maana andiko lanena, Kila amwaminiye hatatahayarika. ''
Hakuna kuwa mteule wa MUNGU bila kumkiri YESU KRISTO kama Mwokozi.
Ndugu, mkiri YESU katika maisha yako, matendo yako.
Mkiri YESU kwa kinywa chako kama Bwana na Mwokozi wa maisha yako.

Mathayo 10:32-33 '' Basi, kila mtu atakayenikiri mbele ya watu, nami nitamkiri mbele za Baba yangu aliye mbinguni. Bali mtu ye yote atakayenikana mbele ya watu, nami nitamkana mbele za Baba yangu aliye mbinguni. ''
 
Kumpokea YESU kama Mwokozi kisha ukaanza kuishi maisha matakatifu katika yeye huko ndio kuwekea muhuri ukiri wako kwa YESU.

1 Petro 1:15 '' bali kama yeye(YESU KRISTO) aliyewaita alivyo mtakatifu, ninyi nanyi iweni watakatifu katika mwenendo wenu wote; ''
 
Kutenda dhambi ni kumkana YESU hata kama ulishawahi kumkiri zamani kisha ukamwacha nankuifuata dunia.
Ndugu, mkiri YESU kwa kinywa chako ya kwamba ndiye Mwokozi wako, acha dhambi na kataa machukizo ya dunia maana hayo yanafuta ukiri wako kwa YESU.
Wanaomkiri YESU inawapasa kutembea katika utakatifu.

2Timotheo 2:19 '' Lakini msingi wa MUNGU ulio imara umesimama, wenye muhuri hii, Bwana awajua walio wake. Na tena, Kila alitajaye jina la Bwana na auache uovu. ''
 Ndugu tunza maisha yako.
Utunze utu wako, Itunze afya yako ya kiroho.
Usimwazime shetani maisha yako.
Tunza maisha yako ukiwa ndani ya Mwokozi YESU KRISTO.
Tii Neno la MUNGU na enenda kwa ROHO MTAKATIFU.


Leo mpaka kuna watumishi wa ajabu sana.
Mtu atawapelekaje watu kwa MUNGU ikiwa yeye mwenyewe hamjui MUNGU?
Huwezi kuwapeleka watu kwa MUNGU wakati wewe mwenyewe unamkana YESU na humjui MUNGU.
Tito 1:16 "Wanakiri ya kwamba wanamjua MUNGU, bali kwa matendo yao wanamkana; ni wenye machukizo, waasi, wala kwa kila tendo jema hawafai."

Kuna watu mizimu ndio mungu wake, huyo hawezi kuwapeleka watu kwa MUNGU wa mbinguni.
Majini ndio mungu wake, huyo lazima awe kinyume na KRISTO na kwa vyovyote mtu wa aina hiyo hawezi kuwapeleka watu kwa MUNGU.
Ndugu zangu KRISTO YESU ndio njia ya kwenda kwa MUNGU.
Kumjua Bwana YESU ndio kuijua njia ya kwenda kwa MUNGU.
Kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi ndio kumtii MUNGU aliyeumba mbingu na dunia.
Kuna watu wang'ang'ania dini na dini hizo chanzo chake sio MUNGU, Bali chanzo chake ni shetani.
Ndugu, kumbuka Neno hili kwamba mtu hawezi kuwapeleka watu kwa MUNGU ikiwa yeye mwenyewe hamjua MUNGU.
Je unamhitaji MUNGU?
1 Yohana 4:2-3 " Katika hili mwamjua ROHO wa MUNGU; kila roho ikiriyo kwamba YESU KRISTO amekuja katika mwili yatokana na MUNGU. Na kila roho isiyomkiri YESU haitokani na MUNGU. Na hii ndiyo roho ya mpinga Kristo ambayo mmesikia kwamba yaja; na sasa imekwisha kuwako duniani."


Natamani niseme mengi mno lakini naamini mwenye kuelewa ameelewa.
MUNGU akubariki kwa kujifunza somo hili muhimu pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane nitakujulisha jinsi ya kukipata.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.
0714252292(Hadi whatsapp).
0786719090
mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu.

Comments