UKIMPENDA MTU NA UKATAMANI UFUNGE NAYE NDOA JIULIZE YAFUATAYO.

 Peter na Scholar Mabula.
Watenda kazi katika shamba la Bwana YESU
UKIMPENDA MTU NA UKATAMANI UFUNGE NAYE NDOA JIULIZE YAFUATAYO.

  Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu yangu.
Karibu sana tujifunze Neno la MUNGU.
Najua kabisa kila mtu anatamani kumpata mwenzi sahihi wa ndoa.
Najua kabisa mawazo na malengo ya kila Mwanamke ni kumpata Mwanaume sahihi wa maisha yake.
Najua kabisa kila Mwanaume mipango yake ni kumpata mke sahihi wa kufunga naye ndoa takatifu.
Katika kundi la vijana wengi  au binti  wengi yuko mmoja miongoni mwao utampenda kuliko wengine na utataka mfunge ndoa.
Ni jambo jema na ni mpango wa MUNGU kabisa kwamba kila Mwanaume aoe mwanamke ampendaye  na kila mwanamke aolewe  na Mwanaume ampendaye.
Mfano hai ni huu ambapo Ahasuero alimpenda Esta kuliko mabinti wote hivyo akamuoa.
 Esta 2:27 ''Mfalme akampenda Esta kuliko wanawake wote, naye akapata neema na kibali machoni pake kuliko mabikira wote; basi akamtia taji ya kifalme kichwani pake, akamfanya awe malkia badala ya Vashti.''

 Sasa nisikilize kwa makini sana katika haya yafuatayo kabla ya ndoa ili yakiwa sahihi yaifanye ndoa yako ambayo utafunga kuwa ni paradiso ndogo.
 Mambo haya jiulize wakati wa uchumba na ujiridhishe katika  wakati huo huo wa uchumba maana katika ndoa hakuna kuachana wala kuchunguzana kama huyu ni mke sahihi au huyu ni mume sahihi, hata ukigundua kwamba umeoa mke asiye sahihi au umeolewa na mume asiye sahihi haitakusaidia lolote kama uko katika ndoa tayari, hivyo kwa ambaye unatarajia kufunga ndoa nifuatilie kwa makini katika somo hili.

Mambo matatu ya kujiuliza kwako uliyepata mchumba na mnatarajia kufunga ndoa takatifu.

1. Umempendea nini?

Wimbo 8:6 ''Nitie kama muhuri moyoni mwako, Kama muhuri juu ya mkono wako; Kwa maana upendo una nguvu kama mauti, Na wivu ni mkali kama ahera. Mwako wake ni mwako wa moto, Na miali yake ni miali ya Yahu.''
 Chunguza kwanza sababu ya upendo wako kwake, maana bila sababu huwezi kumpenda mtu.
Na Biblia inasema kwamba upendo una nguvu kama mauti, ukimpenda mtu hata kama kuna watu wanakushauri jambo sahihi wewe utawaona wao ndio hawana akili kwa sababu tu umemezwa katika upendo.
Upendo ni upofu, hivyo kabla upendo haujawa upofu kwako hakikisha unajiuliza na kujiridhisha kwamba umempenda mtu sahihi na umempendea sababu sahihi. Chunguza sana sababu za wewe kumpenda mtu huyo maana kama ni sababu zisizo sahihi hakika siku sababu hizo zitaondoka na upendo wake kwake utakoma, kama hatua hiyo itafika ukiwa katika ndoa hakika ndoa yako utaiona kama utumwa na sio paradiso ndogo.
Je umempendea mali Mchumba wako?
Je umempendea Elimu nzuri aliyonayo au umempendea  umbo?
 Je umempendea familia maarufu anayotoka? Je umempendea ucheshi wake?
Chunguza chanzo  cha upendo wako kwake  ili upime kama chanzo hicho ni sahihi kwa mtu ambaye utatakiwa kuishi naye maisha yako yote.
Hakikisha chanzo cha upendo wako kwake ni chanzo sahihi kitakachofanya  upendo wako kwake udumu hata wakati mkifunga ndoa.
Kumbuka Biblia inasema  ''Mdomo wa kweli utathibitishwa milele; Bali ulimi wa uongo ni wa kitambo tu.-Mithali  12:19''

 Mimi Peter  Mabula kama Mwalimu wa Neno la MUNGU nakushauri kwa uchache angalia mambo mawili yafuatayo  kama sehemu ya kwanza ya kupima upendo wako kwake.

A. Msimamo thabiti na wa kweli wa kiroho katika maisha ya wokovu.
Heri chanzo chako cha upendo kwake kiwe umempendea msimamo wake tahabiti kwa YESU.
Zaburi 128:1-4 ''Heri kila mtu amchaye BWANA, Aendaye katika njia yake. Taabu ya mikono yako hakika utaila; Utakuwa heri, na kwako kwema.  Mkeo atakuwa kama mzabibu uzaao, Vyumbani mwa nyumba yako. Wanao kama miche ya mizeituni Wakiizunguka meza yako. Tazama, atabarikiwa hivyo, yule amchaye BWANA.''

 B. Hofu ya MUNGU
 Waefeso 4:27 ''wala msimpe Ibilisi nafasi.''
 Hofu ya MUNGU itamfanya asimpe shetani nafasi katika maisha yake, huyo ni mtu bora hakika.

Ndugu nakuomba sana usimpende mtu kwa sababu huna wa kumpenda wakati huo.
Ndugu, Usimpende mtu kwa sababu umri wako umeenda sana.
Katika kumpata mke mwema au mume mwema hakikisha unaangalia sababu za kiroho na sio sababu za kimwili tu.
Mithali 31:10a ''Mke mwema, ni nani awezaye kumwona? ''

Kwanini uchunguze chanzo cha upendo wako kwake?
Majibu sahihi ni kwamba  Ni kwa sababu upendo una nguvu kama mauti(Wimbo 8:6)
Upendo unaweza ukakufanya usimsikilize mtu mwingine yeyote yule, hata kama anakuambia jambo la maana.
Dada  mmoja wa kanisani alijikuta ameolewa na kijana Mchawi na mganga wa kienyeji, ni hatari sana.
Dada huyu kabla hajaolewa kuna watumishi waliona katika maono juu ya mchumba wa huyo dada, dada yule aliwatukana watumishi na kuwaona kama hawana akili hadi akahama na kanisa lakini baada ya ndoa hata miaka miwili haikupita Dada yule alirudi kanisani akilia sana na kuja kuelezea uchawi na uganga wa mumewe. 
Upendo ni kama upofu, unaweza kukufanya usione mengine yote yaliyo nje na upendo wako kwa mchumba wako.
Hata kama watu watamuona anakusaliti, wakikuambia wewe utawaona wao ndio wasaliti na sio Mchumba wako.
Hata kama utaambiwa kwamba Mchumba wako huyo ni Mchawi au malaya hutaona kama ni kweli.
Kumbuka kama chanzo cha upendo wako kwake sio cha kudumu hakika hata upendo wako kwake hautadumu.
Kama chanzo chako cha upendo kitapata shida baadae hakika na upendo wako kwake utapata shida.
Ili yasiwe hayo basi chunguza mapema chanzo cha upendo wako kwake,  Mfano Kama unampendea kazi yake kumbuka siku akifukuzwa kazi na upendo wako kwake unakoma.
Kama umempendea unene basi kuna kukonda hivyo na upendo wako kuisha. Kama umempendea wembamba basi akinenepa huna hamu naye tena.

2. Je atalibeba kusudi la MUNGU kwa ajili yako?

Warumi 8:28 ''  Nasi twajua ya kuwa katika mambo yote MUNGU hufanya kazi pamoja na wale wampendao katika kuwapatia mema, yaani, wale walioitwa kwa kusudi lake.''
Hili la kusudi la MUNGU ni jambo la muhimu sana sana.
Chunguza na ujiridhishe kwamba Mchumba wako atalibeba kusudi la MUNGU kwa ajili yako.
Kuna watu wengi sana walikuwa watumishi wazuri Kanisani lakini baada tu ya kufunga ndoa waliacha huduma, lwa sababu wamewapata wenzi ambao ni kikwazo cha huduma zao.
Kuna watu wana maono mengi sana  mfano kurekodi nyimbo za injili, kufungua kituo cha kulea watoto yatima, kushuhudia n.k lakini mwenzi asiyelibeba kusudi la MUNGU ni kikwazo kikubwa sana cha kukamilika maono yako, hivyo kabla ya ndoa chunguza kama huyo Mchumba wako atakusaidia katika huduma yako na sio kuiua.
Je, Mchumba wako atakufaa kulingana na huduma ya kumtumikia Bwana YESU iliyoko ndani yako?
 Je ataifanya huduma yako kanisani iende mbele au ataizimisha? Chunguza.
Kuna watu wana nadhiri kabisa ya kufanya jambo fulani la ki MUNGU katika maisha yao, lakini kumpata mwenzi asiyelibeba kusudi la MUNGU hupelekea kushindwa kutimiza nadhiri zao na kupata hata mapigo wakati mwingine.
Mama mmoja siku moja alinipigia simu akiniambia kwamba rohoni kwake alisikia sauti ya ROHO MTAKATIFU ikimuambia kwamba atoe Mshahara wake wote wa Mwezi Jamuary kama sadaka kwa MUNGU. Mama yule alipomshirikisha mumewe alikutana na matusi makali sana na jambo hilo lilimsumbua sana rohoni mwake. aliponiomba ushauri nikamwambia kwamba inabidi atoe nusu mwezi huu na mwezi unaofuata atoe nusu. Kuna watu wameagizwa kabisa na MUNGU kutoa sadaka kwa ajili ya jambo fulani la ki MUNGU lakini mwenzi wa ndoa ndio anakuwa kikwazo. Kuna Mama mmoja aliniambia kwamba akiahidi kitu Kanisani katika michango ya ujenzi nyumbani anakutana na kipigo kikali kutoka kwa mumewe, kuna mama mwingine yeye hutoa fungu la kumi kwa kujificha kwa sababu ya kumuogopa mumewe. Ndugu ni hatari sana kama utampata mwenzi ambaye hajabeba kusudi la MUNGU kwa ajili yako.
Kila mtu na agano lake na MUNGU.
 Mimi zamani sana wakati nikiwa mdogo kuna wakati nilikuwa katika wakati mgumu sana sana, lakini siku moja nikaota ndoto Bwana YESU amenishika mkono kuelekea mbinguni, baadae nikaamua kuweka nadhiri kwa Bwana YESU kwamba kama atanipa baraka tatu ambazo nilimtajia hakika nitamtumikia hadi kila mwanadamu atanishangaa. Namshukuru MUNGU mambo hayo matatu mawili yameshakamilika na moja ndilo liko nusu ili litimie. Sasa kama ningeoa mke ambaye halibebi kusudi la MUNGU la mimi kumtumikia Bwana YESU ingekuwaje?
Hakika nadhiri yangu ingegeuka laana kwangu na kunitesa. Namshukuru MUNGU kwa neema yake maana katika ndoa yangu mke wangu ndiye mhimizaji wangu mkubwa wa kuambia nifanye kazi ya MUNGU, yeye huniombea kila siku na namshukuru MUNGU kwa ajili yake. Sasa ndugu wewe uliye na agano na MUNGU chunguza sana kwa Mcumba wako ili asiwe chanzo cha kulifuta agano lako na MUNGU hata agano hilo likageuka laana kwako.
Kuna wachumba wengine ukimpata tu kusudi la MUNGU anakuondolea mapema kabisa wakati mkiwa tu wachumba, ndugu usikubali mtu akuondolee kusudi jema la MUNGU katika maisha yako.

Labda ngoja nikuonyeshe makusudi 7 ya MUNGU ambayo hutakiwi Mchumba wako akuondolee.

A. Kuishi maisha matakatifu.
1 Peto 1:15-16 '' bali kama yeye(YESU) aliyewaita alivyo mtakatifu, ninyi nanyi iweni watakatifu katika mwenendo wenu wote; kwa maana imeandikwa, Mtakuwa watakatifu kwa kuwa mimi ni mtakatifu.''
Uisikubali mtu akufanye uache kuishi maisha matakatifu katika KRISTO YESU.

 B. Uchukie mabaya na upende mema.
Zaburi 34:14 ''Uache mabaya ukatende mema, Utafute amani ukaifuatie.''
Usikubali mtu akufanye upende mabaya na uyachukie mema.

C. Umtumikie Bwana YESU.
1 Kor 15:58 ''Basi, ndugu zangu wapendwa, mwimarike, msitikisike, mkazidi sana kutenda kazi ya Bwana sikuzote, kwa kuwa mwajua ya kwamba taabu yenu siyo bure katika Bwana. ''
 Usikubali mtu akufanye uache kumtumikia Bwana YESU.

D. Uenende kwa ROHO MTAKATIFU.
Wagalatia 5:25 '' Tukiishi kwa Roho, na tuenende kwa Roho.   ''
Usikubali mtu akufanye usienende kwa ROHO MTAKATIFU.

E. Utimize kusudi la MUNGU katika kila atakachokuagiza MUNGU.
Wafilipi 2:13 '' Kwa maana ndiye MUNGU atendaye kazi ndani yenu, kutaka kwenu na kutenda kwenu, kwa kulitimiza kusudi lake jema.''
Usikubali mtu akufanye usimtii MUNGU.

 F.  Umwabudu MUNGU Baba katika Roho na kweli.
Yohana 4:24 '' MUNGU ni ROHO, nao wamwabuduo yeye imewapasa kumwabudu katika roho na kweli. ''
Usikubali mtu akufanye umwache YAHWEH MUNGU pekee kwa kukulazimisha uigeukie miungu na majini.
 
G. Uwe ni mtu wa ibada Kanisani.
Waerania 10:25 '' wala tusiache kukusanyika pamoja, kama ilivyo desturi ya wengine; bali tuonyane; na kuzidi kufanya hivyo, kwa kadiri mwonavyo siku ile kuwa inakaribia.''
 Usikubali mtu akufanye uache ibada kanisani.

 3. Je anakupenda?

 Warumi 12:9 ''Pendo na lisiwe na unafiki lichukieni lililo ovu, mkiambatana na lililo jema.''
Katika maswali matatu ya kujiuliza na kuyapatia majibu kabla ya ndoa ni je wewe unampenda? Je atalibeba kusudi la MUNGU kwako? Na swali la tatu ni hili Je yeye anakupenda wewe?
 Ni muhimu sana kuhakikisha kwamba na yeye huyo Mchumba anakupenda.
Nimewahi kuwasiliana na watu wengi sana walio katika uchumba, baadhi yao niligundua kwamba huyo aliyewasiliana na mimi hapendwi na mchumba wake ila ni yeye analazimisha upendo.
Haiwezekana mtu anakusaliti na umemkuta mara mbili akifanya dhambi ya ngono harafu unadai kwamba anakupenda sana ila amepitiwa tu, mimi sijawahi kuona upendo wa hivyo. Kama anakupenda lazima akuheshimu, anayekusaliti wakati wa uchumba hakika huyo hakupendi ila ni wewe unalazimisha upendo. Kwanini ulazimishe upendo wakati na wewe ukimuomba MUNGU utampata atakayekupenda.
Watu wengi sana katika uchumba hawapendwi ila wanalazimisha tu upendo wao.
Mimi nakushauru ndugu, uwe na maamuzi magumu, usikubali kufunga ndoa na mtu ambaye hakupendi.
Kwa sababu hakupendi anaweza hata akakudhuru wakati wa ndoa, kwanini ulazimishe upendo kwa mtu asiyekupenda?
Hata kama unamuona anafaa kuliko watu wote duniani, kama hakupendi ni heri kuachana naye.
Ninachokuomba leo chunguza sana ili ujiridhishe kwamba Mchumba wako anakupenda sana ndipo mfunge ndoa?
Jiamini na jikubali kwamba hata wewe ipo siku uatapata umpendaye na yeye atakuwa anakupenda.
Mtu mmoja alinipigia simu na kuniambia kwamba Mwenzi wake wa ndoa kamwambia neno hili ''Mimi nilikuwa sikupendi tangu mwanzo ila nilikukubalia tu tuoane ili kukusaidia tu maana umri wako umeenda sana'' Ndugu huyu kidogo achanganyikiwe baada ya kuambiwa kwamba hakupendwa tangu mwanzo ila alisaidiwa tu kwa sababu ya umri wake kuwa mkubwa.
Ndugu ambaye bado hujafunga ndoa nakuomba hakikisha mchumba wako anakupenda, kama hakupendi achana naye.
Na inawezekana Mchumba wako anakupenda kweli lakini muulize anakupendea nini?
Ukijua kwamba anakupendea kitu cha ki MUNGU huyo anakufaa.
Kitunze pia sana kitu cha ki MUNGU alichokupendea.
Kama amekupenda kwa sababu umeokoka na unaishi maisha matakatifu hakikisha unaendelea kuishi maisha ya wokovu matakatifu.
Kama ukigundua kwamba amekupendea vitu vinavyopita basi muulize kwamba siku hivyo vitu vikiwa havipo atakupendea nini?
Kama vitu hivyo vikikoma atakupendea nini/
Kama haeleweki muulize MUNGUB kwa maombi na utajulishwa kama mtu huyo ni mtu sahihi kwako.

 Natamani niseme mengi mno lakini naamini mwenye kuelewa ameelewa.
MUNGU akubariki kwa kujifunza somo hili muhimu pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane nitakujulisha jinsi ya kukipata.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.
0714252292(Hadi whatsapp).
0786719090
mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu.

Comments