UNAVYOHITAJI KWA MCHUMBA WAKO ILI AENDELEE KUKUPENDA HATA MFIKIE HATUA YA NDOA

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.

Bwana YESU atukuzwe ndugu!
Ni siku moja ghafla tu nilifunuliwa ujumbe huu ili nikujulishe wewe kijana au binti unayetarajia kufunga ndoa na mchumba wako uliyenaye au yule ambaye MUNGU Baba atakupa.
Esta 2:17 " Mfalme akampenda Esta kuliko wanawake wote, naye akapata neema na kibali machoni pake kuliko mabikira wote; basi akamtia taji ya kifalme kichwani pake, akamfanya awe malkia badala ya Vashti."

Mfalme Ahausuero alitaka mke kutoka miongoni mwa wanawake wengi sana katika taifa, akampenda Esta mkimbizi miongoni mwa maelfu ya mabinti.
Esta wala hakuwa mzuri kuliko wengine, wapo waliomzidi mbali sana kwa uzuri wa sura, shepu au umbo kwa ujumla.
Esta alikuwa  mkimbizi katika taifa lile, lakini huyo ndio akapendwa na Ahausuero.


Kwanini Esta alipendwa pekee yake wakati wenye sifa kuliko yeye walikuwa ni wengi sana?
Kuna sababu na sababu hii ifanyie kazi hata wewe imvae mchumba wako, ili akupende hadi mfunge ndoa na kuendelea siku zote.
Kumbuka upendo huwa hauji hivi hivi Bali kuna vyanzo vya upendo ambavyo ndivyo vilileta upendo husika, hata Mimi Peter kuhusu Mrembo wangu ambaye ndiye mke wangu mpenzi Scholar kuna vyanzo vilivyosababisha nimpende au yeye anipende.
(Nakuona unasoma huku unatabasamu)
Ngoja niendelee na somo hili fupi.


Sababu 2 za Esta kupendwa na Ahausiero kuliko warembo wengine wote Biblia inasema ni hizi.

1. Neema .

 Esta 2:17 " Mfalme akampenda Esta kuliko wanawake wote, naye akapata neema na kibali machoni pake kuliko mabikira wote;
Neema ni kustahilishwa hata kama kiuhalisia hustahili.
Esta alipata neema machoni mwa Ahausuero ndio maana akafunga naye ndoa.
Hata wewe unahitaji kupata neema machoni mwa huyo binti/kijana umpendaye sana ili iwezekane kuja kufunga ndoa.
Hata kama wewe kwa sura ni mbaya(kwa mtazamo wa watu) lakini neema inaweza ikakufanya ukaonekana ni mzuri sana mbele ya kijana/binti fulani kuliko hao wote wanaojiona ni wazuri.
Binti/kijana ambaye wengine humuona kama wa kawaida sana, yupo mtu ambaye halali usingizi akimuwaza kwamba wachumbiane na kufunga ndoa.
kwa sababu gani iwe hivi?
Ni kwa sababu huyo binti/kijana amepata neema mbele ya huyo kijana au binti.
Hata wewe kijana hakikisha unapata neema machoni mwa Binti unayetaka umuoe, ikiondoka neema uchumba wenu unaweza ukaishia njiani.
Wewe Binti au mama unahitaji neema machoni pa mchumba wako ili mfikie hatua njema ya ndoa, ikiondoka hiyo neema ujue neema hiyo imehamia kwa mtu mwingine.
Jinsi ya kuipata neema ni wewe kuishi maisha matakatifu katika KRISTO huku ukiomba kwa MUNGU kwamba upate neema ya kudumu machoni pa mchumba wako.


2. Kibali.

 Esta 2:17 " Mfalme akampenda Esta kuliko wanawake wote, naye akapata neema na kibali machoni pake kuliko mabikira wote;
Biblia inasema Esta alipata kibali machoni mwa Ahusuero.
Nimeshafafanua sana kuhusu neema au kibali na mpaka kuna somo la maombi niliwahi kuandika juu ya kuombea kibali, hapa nadonoa donoa tu kulingana na ufunuo wa Leo.
Kibali ndio nini?
Kibali ni idhini anayopata mtu ili kupata vitu fulani avitakavyo.
Kibali ni kukubaliwa kufanya jambo jema unalolitaka kulifanya.
Kibali ni ruhusa inayovisukuma nje vizuizi vyote.
Kibali ni ridhaa ya kutenda unachotaka kutenda.
Kama huna kibali kwa mchumba wako utakuwa wewe unalazimisha uchumba huo na hamtafikia ndoa.
Kama huna kibali moyoni mwa mchumba wako ujue hakupendi na hamtafunga ndoa.
Ndugu hakikisha kwa maombi katika jina la YESU KRISTO unatafuta kibali ndani ya mchumba wako ndipo mtafanikiwa.
Kama unadhani mchumba wako anakupenda kwa sababu ya uzuri wako, ndugu wako wazuri kuliko wewe na wanaachwa kirahisi kabisa.
Kama unadhani mchumba wako anakupenda kwa sababu ya makalio makubwa au mkorogo, ndugu wapo wenye makalio kuliko wewe lakini waliachwa kwa sababu tu neema na kibali hawana.
Wapo waliotenda dhambi ya mkorogo na bado waliachwa kwenye mataa.
Kama unadhani mchumba wako anakupenda kwa sababu ya elimu au umaarufu, ndugu wapo maarufu na wapo wasomi sana lakini waliachwa na kubaki tu wakisema wamesamehe ila hawatasahau.
Ndugu yangu yakumbuke haya na omba kwa Bwana YESU ndipo utapata neema na kibali machoni mwa upendaye.
 Natamani niseme mengi mno lakini naamini mwenye kuelewa ameelewa.
MUNGU akubariki kwa kujifunza somo hili muhimu pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane nitakujulisha jinsi ya kukipata.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.
0714252292(Hadi whatsapp).
0786719090
mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu.

Comments