YAKIMBIE MAFUNDISHO YA UONGO.

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.

Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.
Ujumbe leo unasema kwamba ''Yakimbie mafundisho ya uongo''
Mafundisho ya uongo ni mafundisho yote yaliyo kinyume na Wokovu wa YESU KRISTO Mwokozi.
Wakati mwingine uongo ulianzia hapa hadi watu sasa hawamhitaji YESU Kuwa Mwokozi wao.
Maneno ya uongo yanapozidi yanaweza yakamfanya mtu auishi uongo huku akidhani uongo huo ndio ukweli.
Uongo unaweza kumjengea mtu imani na akafika hatua akadhani anaouamini ndio ukweli.
Uongo unaweza kumtumainishia mtu uongo na mtu huyo kuanza kuamini kwamba huo uongo ndio ukweli.
Kwa sababu hiyo ndio maana dini nyingi zipo na madhehebu mengi hapo, na hizo dini ziko kinyume na KRISTO YESU aliye pekee kweli ya MUNGU.
Kuongezeka madhehebu sio jambo baya Bali ni jambo jema sana kama madhehebu hayo yanaihubiri kweli ya MUNGU ambayo ni KRISTO. Shida ni kwamba Kuna madhehebu pia ni pando la shetani maana madhehebu hayo yako kinyume na injili ya KRISTO. Kwa jinsi hiyo fundisho la uongo linalotoka katika madhehebu hayo au dini hizo linaweza kumfanya mtu auamini uongo akidhani kwamba huo uongo ndio ukweli.
Ukiona dini au dhehebu hawamwamini YESU KRISTO kama Bwana na Mwokozi wao ujue hao wamefundishwa sasa uongo na wanauamini huo uongo wakidhani ndio ukweli.
Ndugu zangu, Biblia iko wazi sana kwamba kama humtaki YESU awe Mwokozi wako hakika wewe sio wa MUNGU.
Yohana 3:16-18 "Kwa maana jinsi hii MUNGU aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele. Maana MUNGU hakumtuma Mwana ulimwenguni ili auhukumu ulimwengu, bali ulimwengu uokolewe katika yeye. Amwaminiye yeye hahukumiwi; asiyeamini amekwisha kuhukumiwa; kwa sababu hakuliamini jina la Mwana pekee wa MUNGU."


Leo Kuna maelfu ya watu wameuamini uongo kwa kumuacha YESU au kumkataa ili asiwe Mwokozi wao.
Watu hawa kwa sasa wamefundishwa uongo na ikafika hatua wakadhani huo uongo ndio ukweli.
Kuna madhehebu wanajiita kanisa wakati wako kinyume na YESU KRISTO, hao wamefundishwa uongo na mawakala wa shetani na wameuamini uongo huo kiasi kwamba wanajua huo uongo waliouamini ndio ukweli.

Kuna makanisa wanasema YESU haokoi, ndio maana wanakataza watu kuokoka.
Kuna makanisa wanajua YESU ni nabii tu hivyo wana haki ya kumchagua nabii mwingine nje na YESU, kwa jinsi hiyo watu hao wamemchagua mwanzilishi wa dhehebu lao au dini yao kuwa ndio nabii wao, na YESU aliye kweli ya MUNGU ya milele wamemwacha, kiasi kwamba hata kama nabii wao aliwafundisha uongo, wao wameuamini huo uongo kiasi kwamba kwa sasa wanajua huo uongo ndio ukweli, ndio maana kuna mpaka wanadamu wanajiita Mungu na wafuasi wao hata hawashtuki kwamba wamefundishwa uongo na wameuamini huo.
Kuna watu wamechagua sanamu na sio YESU KRISTO.
Kuna watu wamechagua siku na sio YESU KRISTO.
Kuna watu wamechagua majira na sio YESU KRISTO.
kuna watu wamechagua vyakula na sio YESU KRISTO.
Kuna wamechagua mawe na sio YESU KRISTO.
Kuna watu wamechagua shetani na sio YESU KRISTO.
Ndugu nakuomba sana chunguza misingi ya imani yako, chunguza misingi ya dini yako, chunguza misingi ya dhehebu lako, kama misingi hiyo iko kinyume na Wokovu wa YESU KRISTO ondoka huko upesi.
Kumbuka uzima wako wa milele una YESU KRISTO pekee hivyo mkimbilie yeye kama unautaka uzima wa milele.
Wakatae waongo wote maana hao siku zote wako kinyume na KRISTO.

Kumbuka kuna YESU KRISTO na kuna WapingaKristo, hivyo kama hauko upande wa YESU KRISTO tambua kwamba uko upande wa mpingaKristo.
Kumbuka Biblia pia inasema kwamba mtu asiyedumu katika Mafundisho ya KRISTO huyo hana MUNGU.
2 Yohana 1:7-11 '' Kwa maana wadanganyifu wengi wametokea duniani, wasiokiri ya kuwa YESU KRISTO yuaja katika mwili. Huyo ndiye yule mdanganyifu na mpinga Kristo.  Jiangalieni nafsi zenu msiyapoteze mliyoyatenda, bali mpokee thawabu timilifu. Kila apitaye cheo, wala asidumu katika mafundisho ya KRISTO, yeye hana MUNGU. Yeye adumuye katika mafundisho hayo, huyo ana Baba na Mwana pia. Mtu akija kwenu, naye haleti mafundisho hayo, msimkaribishe nyumbani mwenu, wala msimpe salamu. Maana yeye ampaye salamu azishiriki kazi zake mbovu.''

Ndugu  nakuomba sana usikae katika madhabahu ya Baali.
Madhabahu ya Baali ni madhabahu ya shetani.

Wapo watu wengi tu wako katika madhabahu ya baali, hata wafalme na watu maarufu baadhi wako katika madhabahu ya baali, mfano hai ni huu.
2 Wafalme 21:1-3 '' Manase alikuwa na umri wa miaka kumi na miwili alipoanza kutawala; akatawala miaka hamsini na mitano katika Yerusalemu, na jina la mamaye aliitwa Hefziba. Akafanya yaliyo mabaya machoni pa BWANA, sawasawa na machukizo ya mataifa, aliowafukuza BWANA mbele ya wana wa Israeli.  Kwa maana akapajenga tena mahali pa juu alipopaharibu Hezekia baba yake; akamjengea Baali(shetani) madhabahu, akafanya Ashera kama alivyofanya Ahabu mfalme wa Israeli. Akajiinama mbele ya jeshi lote la mbinguni na kulitumikia.''

 Ndugu nakuomba sana usikae katika madhabahu ya Baali yaani madhabahu ya shetani. 
Madhabahu ya shetani ni kila madhabahu iliyo kinyume na KRISTO YESU Mwokozi.
Madhabahu ya Baali haitaki Wokovu wa KRISTO, Haimtaki YESU kama Mwokozi.
Ndugu usikubali kukaa katika madhabahu ya Baali.
Mtumishi wa MUNGU Eliya aliamua kuitengeneza Madhabahu ya MUNGU iliyokuwa imevunjika kwa sababu ya jamii kubwa ya watu kumfuata mungu Baali ambaye ni shetani mwenyewe. Wakati huo Baali alikuwa na nabii wake mwanamke Jezebel ambaye alitumia kila mbinu kuwawafanya watu wa MUNGU wamwabudu shetani na kumtumikia yeye.
Eliya nabii akamua kuitengeneza madhabahu ya MUNGU aliye hai.

1 Wafalme "18:30 Kisha Eliya akawaambia watu wote, Nikaribieni mimi. Watu wote wakamkaribia. Akaitengeneza madhabahu ya BWANA iliyovunjika."
Hata leo Baali angali ana watumishi wake.
Ndugu ndio maana nakuomba sana usikubali kukaa katika madhabahu ya Baali.
Hakikisha unakaa katika madhabahu ya MUNGU aliye hai.
Madhabahu ya MUNGU ina;
1. Jina la YESU KRISTO.

2. Damu ya YESU KRISTO ya agano la milele.
3. Nguvu za ROHO MTAKATIFU.
4. Neno la KRISTO.
Madhabahu ya MUNGU inaongozwa na ROHO MTAKATIFU.
Madhabahu ya MUNGU unahusika na utii kwa MUNGU Baba, YESU KRISTO na ROHO MTAKATIFU.
Ndugu kaa katika madhabahu ya MUNGU aliye hai.
Madhabahu ya MUNGU aliye hai inafundisha watu kuacha dhambi, uovu na makosa.
Ndugu, kaa katika madhabahu ya MUNGU aliye hai.
Neema ya KRISTO YESU iwe nawe daima.
Hakikisha unakuwa safi rohoni mwako siku zote maana hujui siku wala saa ambayo Bwana YESU atakuja kuhukumu ulimwengu wote na watu wote.
Luka 12:40 "Nanyi jiwekeni tayari, kwa kuwa saa msiyodhani ndipo ajapo Mwana wa Adamu."
Inawezekana wewe ni mmoja wa wale wanaodhani kwamba wala YESU haji wakati huu, ndugu nakuomba tu jambo muhimu sana kwamba unatakiwa kuwa safi mbele za MUNGU maana hata siku ya kufa kwako huijui.
Kumbuka ni tukio moja tu linalofuata baada ya kila mwanadamu kufariki. Tukio hili ni hukumu, hivyo baada ya kufa inafuata hukumu. Kama hujatengeneza njia zako kwa Bwana YESU hakika makazi yako yatakuwa katikati ya ziwa la moto, ndio maana Neno la MUNGU Leo linakujulisha kwamba hakikisha uko safi rohoni mwako.
Waebrania 9:27 "Na kama vile watu wanavyowekewa kufa mara moja, na baada ya kufa hukumu;"

Usafi wa rohoni unatengenezwa na mambo matatu tu.
1. Kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi.

2. Kuishi Maisha matakatifu baada ya kumpokea YESU.
3. Kuacha dhambi zote, makosa na uovu.
Ndugu, hakikisha unakuwa safi mbele za MUNGU maana hujui siku wala saa ya YESU kurudi na hujui siku wala saa ya kufa.
Ndio maana Biblia inakujulisha kwamba kama KRISTO alivyokuita alivyo mtakatifu hivyo inakupasa na wewe kuwa mtakatifu siku zote na popote ulipo.
1 Petro 1:15 "bali kama yeye aliyewaita alivyo mtakatifu, ninyi nanyi iweni watakatifu katika mwenendo wenu wote;"
Ndugu inakupasa kuwa na mahusiano mazuri na MUNGU Muumbaji wako siku zote.
Usipange kuokoka baadae wakati nafasi ya kuokoka unayo Leo.

Tito 2:11-14 '' Maana neema ya MUNGU iwaokoayo wanadamu wote imefunuliwa; nayo yatufundisha kukataa ubaya na tamaa za kidunia; tupate kuishi kwa kiasi, na haki, na utauwa, katika ulimwengu huu wa sasa; tukilitazamia tumaini lenye baraka na mafunuo ya utukufu wa KRISTO YESU, MUNGU mkuu na Mwokozi wetu; ambaye alijitoa nafsi yake kwa ajili yetu, ili atukomboe na maasi yote, na kujisafishia watu wawe milki yake mwenyewe, wale walio na juhudi katika matendo mema. ''


Pamoja na umoja kuwa ni jambo jema, lakini sio watu wote wana umoja sahihi.
Kuna watu wana umoja na mawakala wa shetani, hiyo ni hatari sana kwao.
Kuna watu wana umoja na majini, hiyo ni hasara kubwa sana kwao.
Kuna watu wana umoja na watu walio maajenti wa kuzimu, hiyo ni hatari sana.
Kuna watu wana umoja na wapingaKristo, hiyo ni jambo hatari sana.
Ndugu hakikisha umoja wako ni umoja na sheria ya MUNGU, sheria ya MUNGU ni Neno la MUNGU.

Zaburi 1:1-2 " Heri mtu yule asiyekwenda Katika shauri la wasio haki; Wala hakusimama katika njia ya wakosaji; Wala hakuketi barazani pa wenye mizaha. Bali sheria ya BWANA ndiyo impendezayo, Na sheria yake huitafakari mchana na usiku."
Ndugu, vunja umoja ulionao na wachawi.
Kataa umoja wa aina yeyote na waganga wa kienyeji.
Kataa umoja na majini.
Kataa umoja na wanadamu wanaotumika ki shetani.

Nakuomba weka umoja na Kanisa la MUNGU, weka umoja na Maombi, weka umoja na ushirika na ROHO MTAKATIFU.

1 Kor 6:9-11 '' Au hamjui ya kuwa wadhalimu hawataurithi ufalme wa MUNGU? Msidanganyike; waasherati hawataurithi ufalme wa MUNGU, wala waabudu sanamu, wala wazinzi, wala wafiraji, wala walawiti, wala wevi, wala watamanio, wala walevi, wala watukanaji, wala wanyang'anyi. Na baadhi yenu mlikuwa watu wa namna hii; lakini mlioshwa, lakini mlitakaswa, lakini mlihesabiwa haki katika jina la Bwana YESU KRISTO, na katika ROHO wa MUNGU wetu. ''
 
Ndugu, Nakuomba umoja wako wa kibinadamu hakikisha haukuondoi kwa YESU.
Hakikisha umoja wako na wanadamu haukuondoi katika utakatifu na ucha MUNGU.
Hakikisha umoja ulio nao na marafiki zako au ndugu zako haukuondoi katika kusudi la MUNGU.

Kumbuka duniani tunapita tu hivyo umoja wako na wanaotumika kipepo unaweza Kukufanya baada ya kufa ushindwe kwenda uzima wa milele, hivyo ujumbe huu umekujia Leo ukikutaka utengeneze njia zako, kataa umoja unamuondoa YESU maishani mwako.
Weka umoja na watu ambao mnajengana kiroho na sio kuharibiana kiroho.
Hakikisha umoja wako na Biblia ni wa kudumu.
Hakikisha umoja wako na Kanisa la MUNGU ni wa kudumu.

 Natamani niseme mengi mno lakini naamini mwenye kuelewa ameelewa.
MUNGU akubariki kwa kujifunza somo hili muhimu pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane nitakujulisha jinsi ya kukipata.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.
0714252292(Hadi whatsapp).
0786719090
mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu.

Comments