IKATAE HOFU MAANA INACHELEWESHA USHINDI WAKO.

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.

Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.
Ninajua kabisa wewe umeokoka na kwa sababu hiyo wewe ni askari wa kiroho unayepigana katika vita ya kiroho zidi ya kila kazi ya giza.
Kama askari wa kiroho inakupasa sana kuwa jasiri na hodari zidi ya kila wakala wa shetani anayejaribu kushindana na wewe.
MUNGU tangu zamani anawaambia wateule wake kuwa hodari na wenye moyo wa ushujaa, mfano hai ni hapa ambapo MUNGU Mwenyezi anamwambia Yoshua.
Yoshua 1: 5-7 ''Hapatakuwa mtu ye yote atakayeweza kusimama mbele yako siku zote za maisha yako; kama nilivyokuwa pamoja na Musa, ndivyo nitakavyokuwa pamoja na wewe; sitakupungukia wala sitakuacha. Uwe hodari na moyo wa ushujaa, maana ni wewe utakayewarithisha watu hawa nchi hii niliyowaapia baba zao ya kwamba nitawapa. Uwe hodari tu na ushujaa mwingi, uangalie kutenda sawasawa na sheria yote aliyokuamuru Musa mtumishi wangu; usiiache, kwenda mkono wa kuume, au wa kushoto, upate kufanikiwa sana kila uendako''
Ukisoma maandiko hayo kiuchunguzi utagundua mambo mengi lakini jambo mojawapo ambalo lingemfanya Joshua kuwa hodari na shujaa dhidi ya adui ni yeye kuhakikisha Neno la MUNGU haliondoki kwake na Neno hilo hulitafakari usiku na mchana, hata wewe ndio Yoshua wa leo, kanuni hiyo unaweza kuitumia kwamba hakikisha Neno la KRISTO haliondoki kinywani mwako bali ulitafakari usiku na mchana ndipo utakuwa shujaa katika vita ya kiroho unayopitia. Kwanini nakuambia hivyo hivyo?
Ni kwa sababu jambo moja kubwa sana linaweza kuathiri ushindi wako ni Hofu. 
Hofu ni nini?
Hofu ina maana zifuatazo;
1. Hofu ni uoga unaokufanya kushindwa kukabili jambo au ni jambo linalokufanya uogope kitisho.
2. Hofu ni hali ya kuogopa.
3. Hofu ni hali ya kujawa mashaka na wasiwasi.
4. Hofu  ni hali ya kutokuwa shujaa.
Hofu ndilo jambo la kwanza ambalo humzuia Mteule wa KRISTO kushinda vita ya kiroho dhidi ya mawakala wa shetani.
Ndugu, kama unamwamini MUNGU katika KRISTO YESU na unaishi maisha matakatifu na ya haki,kwanini uwe na hofu?
Wewe kama ni muombaji na unapambana kiroho dhidi ya nguvu za Giza inakupasa sana kuikataa hofu.
Kumbu 20:1-4 " Utokapo kwenda vitani kupigana na adui zako, na kuona farasi, na magari, na watu wengi kuliko wewe, usiwaogope; kwa kuwa BWANA Mungu wako, yu pamoja nawe, aliyekukweza kutoka nchi ya Misri. Na iwe, msongeapo mapiganoni, kuhani na akaribie na kusema na watu, awaambie, Sikizeni, enyi Israeli, hivi leo mwasongea mapiganoni juu ya adui zenu mioyo yenu na isizime; msiche, wala msiteteme, wala msiingiwe na hofu kwa ajili ya wao;
kwa maana BWANA, Mungu wenu, ndiye awaandamaye kwenda kuwapigania juu ya adui zenu, ili kuwaokoa ninyi."


 Hofu ni silaha kuu ya shetani ili kumshinda Mteule wa MUNGU.
Mteule hakikisha unaishinda hofu wakati wa kuhitaji MUNGU kukujibu na kukushindia dhidi ya mawakala wa shetani.

Wakati mwingine mawakala wa shetani wamejaa vitisho sana, lakini mwisho wao huwa vitisho tu na sio ushindi kama kweli wewe ni muombaji unayeishi maisha matakatifu.
Wakati mwingine MUNGU anaweza kuwaacha mawakala wa shetani washindane na wewe lakini ushindi kwako ni lazima maana una YESU KRISTO Mwokozi aliye hai.
Yeremia 1:9 '' Nao watapigana nawe; lakini hawatakushinda; maana mimi nipo pamoja nawe, asema BWANA, ili nikuokoe.''

Usipoishinda hofu ujue hofu ina kazi nyingi na hizo kazi zina madhara kwako muombaji.


Hofu hukufanya;
1. Hofu hukufanya Uwe muoga, Hivyo ikatae hofu inayokufanya uwe muoga.

2 Timotheo 1:7 '' Maana MUNGU hakutupa roho ya woga, bali ya nguvu na ya upendo na ya moyo wa kiasi.''
 
2. Hofu hukufanya ulegee, hivyo ikate hofu inayokufanya ulegee.

Warumi 12:11-12 '' kwa bidii, si walegevu; mkiwa na juhudi katika roho zenu; mkimtumikia BWANA; kwa tumaini, mkifurahi; katika dhiki, mkisubiri; katika kusali, mkidumu;''
 
3. Hofu hukufanya usijiamini, hivyo ikate hiyo hofu maana MUNGU yuko pamoja na wewe.

Isaya 41:10 '' usiogope, kwa maana mimi ni pamoja nawe; usifadhaike, kwa maana mimi ni MUNGU wako; nitakutia nguvu, naam, nitakusaidia, naam, nitakushika kwa mkono wa kuume wa haki yangu.''

4. Hofu hukufanya usimwamini MUNGU, Biblia inakushauri kwamba Mwamini MUNGU ndipo utathibitika, waamini watumishi wake ndipo utafanikiwa, hivyo ikatae hofu.

Usikubali kufanya dhambi ya kutokumwamini MUNGU.
 2 Nyakati 20:20b ''mwaminini BWANA, Mungu wenu, ndivyo mtakavyothibitika; waaminini manabii wake, ndivyo mtakavyofanikiwa.''


5. Hofu hukufanya Usipambane vyema kiroho, Biblia inakukataza kuwa na hofu.

Isaya 35:4 '' Waambieni walio na moyo wa hofu, Jipeni moyo, msiogope; tazama, MUNGU wenu atakuja na kisasi, na malipo ya MUNGU; atakuja na kuwaokoa ninyi. ''

6. Hofu hukufanya utetemeke na kushindwa kumkiri YESU KRISTO, hilo nin jambo baya sana.

Mathayo 10:32-33 ''Basi, kila mtu atakayenikiri mbele ya watu, nami nitamkiri mbele za Baba yangu aliye mbinguni. Bali mtu ye yote atakayenikana mbele ya watu, nami nitamkana mbele za Baba yangu aliye mbinguni.''
Haiwezekani wewe unaogopa kumkiri YESU KRISTO mbele za watu kwamba ndiye Mwokozi wako, harafu unataka YESU akushindie.

7. Hofu hukufanya ukose malengo yako ya ushindi, hivyo uwe na akili na dumu katika maombi.

1 Petro 4:7 '' Lakini mwisho wa mambo yote umekaribia; basi, iweni na akili, mkeshe katika sala.''

hofu usiiruhusu kabisa katika maombi yako na mapambano yako ya kiroho, unaweza kujikuta unalia tu badala ya kuomba na kukemea nguvu za Giza kwa sababu tu umetawaliwa na hofu.
MUNGU anakuhakikishia ushindi Kama ukimwamini na kuomba.
Isaya 43:26 " Unikumbushe, na tuhojiane; eleza mambo yako, upate kupewa haki yako."
Ndugu kataa hofu kwa jina la YESU na kisha endelea na maombi maana adui zako watapigwa tu mbele yako.
Kataa hofu maana hofu ni adui wa ushindi wako.

Mimi Peter nimejifunza mambo mengi sana mabyo yanaweza kunifanya nisiwe na hofu yeyote katika maombi. Moja ya mambo hayo ni kumsikiliza ROHO MTAKATIFU katika maombi pamoja na kutembea kwenye Neno la MUNGU bila kuangalia kingine chochote.
Ndugu hakikisha Neno la MUNGU limejaa kwa wingi ndani yako.
Hakikisha unamwamini MUNGU na amini nguvu zake za kukushindia.
Ongeza upendo kwa MUNGU maana upendo huo utaitupa nje hofu na wewe sasa kubaki huna hofu wala mashaka yeyote.
1 Yohana 4:18 ''Katika pendo hamna hofu; lakini pendo lililo kamili huitupa nje hofu, kwa maana hofu ina adhabu; na mwenye hofu hakukamilishwa katika pendo. ''
Natamani niseme mengi mno lakini naamini mwenye kuelewa ameelewa.
MUNGU akubariki kwa kujifunza somo hili muhimu pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane nitakujulisha jinsi ya kukipata.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.
0714252292(Hadi whatsapp).
0786719090
mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu.

Comments