JINSI YA KUTOKA KWENYE VIFUNGO VYA GIZA

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.

JINSI YA KUTOKA KWENYE VIFUNGO VYA GIZA


Bwana YESU atukuzwe ndugu yangu.

Karibu tujifunze Neno la MUNGU.

Leo tunajifunza jinsi ya kutoka katika vifungo vya kishetani.

Kifungo cha kipepo ni nini?

Kifungo cha kipepo ni adhabu ya mtu kuwekwa jela kipepo na mawakala wa shetani.

Jela ni mahali wanapowekwa waharifu ili watumikie adhabu.

Wako watu wengi tu wanateswa na vifungo vya giza katika maisha yao, wengine wanatamani watoke katika vifungo hivyo lakini imeshindikana maana hawaijui njia sahihi ya kuwatoa katika vifungo..

Jambo la kwanza kabisa nataka kukuambia ni kwamba Bwana YESU alikuja ili kuzivunja na kuziharibu kazi zote za shetani vikiwemo vifungo vya kipepo.

1 Yohana 3:8b ''Kwa kusudi hili Mwana wa MUNGU alidhihirishwa, ili azivunje kazi za Ibilisi. ''

Kuna mambo mengi yanaweza yakahitajika ili hadi mtu husika afunguliwe kutoka vifungo vya giza.

Kufunguliwa vifungo kunahitaji maombi sahihi, kujitambua, kujielewa, kutii Neno  la MUNGU na kuenenda katika ROHO MTAKATIFU.

Kuna vifungo vingi vya giza ambavyo watu wengi wamefungwa kichawi.

Baadhi ya vifungo hivyo  vimetajwa katika Isaya 42:22 ''Lakini watu hawa ni watu walioibiwa na kutekwa; wote wamenaswa katika mashimo, wamefichwa katika magereza; wamekuwa mawindo, wala hapana aokoaye; wamekuwa mateka, wala hapana asemaye, Rudisha. '' acha nikifafanulie.  

Vifungo hivyo vya giza ni hivi.

    1. Kuibiwa ufahamu kipepo ili ulitumikie kusudi la shetani na sio la MUNGU.

''Lakini watu hawa ni watu walioibiwa ''
Kuna watu wengi fahamu zao zimefunga kipepo kiasi kwamba wanalitumikia kusudi la shetani na sio la MUNGU, Leo kwa njia ya maombi yako katika jina la YESU KRISTO hakikisha unakiharibu kifungo hicho cha giza kilichokufunga ufahamu.

Fikra zako zinatakiwa zimtii KRISTO na sio kutii majini na mizimu.

2 Kor 10:3-5 '' Maana ingawa tunaenenda katika mwili, hatufanyi vita kwa jinsi ya mwili;  (maana silaha za vita vyetu si za mwili, bali zina uwezo katika MUNGU hata kuangusha ngome;)  tukiangusha mawazo na kila kitu kilichoinuka, kijiinuacho juu ya elimu ya MUNGU; na tukiteka nyara kila fikira ipate kumtii KRISTO; ''



   2. Kutekwa na nguvu za giza.

 ''Lakini watu hawa ni watu waliotekwa''

Baadhi ya dalili ya mtu aliye katika kifungo cha kutekwa na nguvu za giza ni kuonewa sana na majini au wachawi kwa sababu tu wamekuteka katika ulimwengu wa roho.

Somo linaitwa jinsi ya kutoka kwenye vifungo vya giza, ni muhimu kujua kwamba kila kifungo kina kanuni zake hadi utoke katika kifungo hicho, kuna vifungo vingine huhitaji hata maombi bali unahitaji tu kubadilika tabia na kifungo hicho kinaondoka.

   3.Kunaswa katika mashimo ya giza.

''Lakini watu hawa ni watu  walionaswa katika mashimo''
Inawezekana wewe uko katika kifungo cha mashimo ya giza.

Inawezekana uko katika shimo la dhambi.
Inawezekana wewe uko katika shimo la madeni au kufilisika.

Inawezekana umenaswa katika shimo la magonjwa na hadi kwa sasa unadhani hutapona kabisa kulingana na jinsi unavyouona ugonjwa wako.

Inawezekana uko katika shimo la kifo ili siku chache zijazo upate ajali mbaya waliyoipanga wachawi na wakuu wa giza ili ikupate.

Wakati mwingine kupitia ndoto ambazo unaota unakuwa unajulishwa aina ya kifungo ambacho umefungwa ili ujue jinsi ya kutoka katika kifungo hicho.

Inawezekana wewe huota ndoto kabisa ukiwa ndani ya shimo refu sana na huoni pa kutokea, hapo unaonyeshwa aina ya kifungo kinachokutesa.

Ndugu, leo katika jina la YESU KRISTO nakuomba kimbilia maombezi makanisani na utaombewa na kifungo hicho kukuacha.

   4. Kufichwa katika magereza.

''Lakini watu hawa ni watu waliofichwa katika magereza ''
Kuna kifungo cha giza kinaitwa gereza.

Inawezekana wewe uko katika gereza la magaonjwa, kukataliwa,kudhalauliwa bila sababu, kutengwa n.k

Inawezekana ndoa yako iko gerezani, inawezekana uchumba wako uko gerezani, iinawezekana biashara yako au wito wako viko gerezani

Ndugu leo hakikisha unandoka katika gereza la kipepo ulimofungwa kipepo.

    5. Kuwa Mawindo ya nguvu za giza.

''Lakini watu hawa ni watu ambaob  wamekuwa mawindo, ''
Kuna kifungo kinaitwa mawindo, inawezekana wewe siku zote uko katika mawindo ya majini au wachawi.

Kuna watu huwa hawalali usiku kwa sababu wako katika mawindo ya wachawi na majini.

Mama mmoja kutoka nchi jirani siku moja alinipigia simu ili nimuombee, nilipomuombea kesho yake alituma sadaka kisha akasema hivi ’ Mtumishi Mabula huwezi kuamini mimi na mtoto wangu tuna zaidi ya miezi miwili bila kulala usiku, jana uliponiombea ndio nilishangaa maana nilipojaribu kulala nikashtuka nikidhani wachawi sasa wanakuja kumbe ili asubuhi saa mbili yaani nililala salama kwa mara ya kwanza’’

Mama Yule aliniambia kwamba alikosana na Baba mmoja mfuga majini ambaye alimwambia kwamba hatalala usiku hata siku moja, kifungo kile kilimtesa sana lakini baada ya maombi kifungo kiliondoka.

Ndugu  uko katika mawindo gani?

Kuna watu kila siku ni kukabwa tu na majinamizi.

Kuna mtu kila ugonjwa ukitokea na yeye lazima aumwe.

Kuna watu huchapwa viboko usingizini.

Ndugu, uko kwenye mawindo gani ya kipepo?

Leo katika jina la YESU KRISTO kataa kuwa mawindo.

Kwa maombi yako, wachawi au majini wanaweza kukuogopa na wasikufuatilie tena maisha yako yote, kama ukiomba inavyotakiwa.

Maombi ya vita ni ya muhimu sana ili utoke katika vifungo vya giza, watu wengi hawaelewi jambo hilo wakidhani kwamba shetani unaweza ukambeleleza kutoka, ndugu yangu, mashetani huwa hayabembelezwi kutoka bali toa amri kwa jina la YESU kwamba watoke na watatoka hakika, usiombe kistaarabu sana kila maombi yako.

Nguvu za giza zinaondolewa kwa nguvu na sio vinginevyo.

Mathayo 18:18 '' Amin, nawaambieni, yo yote mtakayoyafunga duniani yatakuwa yamefungwa mbinguni; na yo yote mtakayoyafungua duniani yatakuwa yamefunguliwa mbinguni. ''

Ndugu kumbuka kwamba YESU alikuwa anaziamuru nguvu za giza ziwatoke watu na zinatoka.

Mitume walikuwa wanaziamuru nguvu za giza ziwatoke watu na zinawatoka, mbona wewe unazibembeleza nguvu za giza kutoka?

Kama kuna jambo muhimu sana ukitaka kutoka katika vifungo vya giza ni muhimu sana ukaenda kuombewa

ROHO MTAKATIFU ni muhimu sana ili ajulishe jinsi ya kutoka katika vifungo vya giza, ndio maana unapaswa pia kuwashirikisha watumishi wa MUNGU.

Mwanamke mmoja aliota ndoto  amefungwa kipepo ili asizae, lakini hakuwa amefungwa kifungo kimoja tu bali alikuwa amefungwa vifungo saba vyote kwa ajili ya kumzuia kuzaa. Ndugu, Bila ROHO MTAKATIFU unaweza kuwa unapambana na kifungo kimoja kila mwaka hivyo baada ya miaka 7 ndipo vitaisha hivyo vifungo, na kama ulianza kuomba ndoa yako ikiwa na miaka 2 maana yake unaweza kupata uzao ndoa ikiwa na miaka 9.

Je kama ndoa yako ulianza kuomba ikiwa na miaka 7, utakuja kuzaa ndoa ikiwa na umri gani?

Ndugu, leo fungua kila kifungo kwa damu ya YESU KRISTO ya agano.

Nyunyuzia damu ya YESU ili ikapeleleze katika ardhi ulikofungwa au katika bahari ulikofungwa au popote  ili hicho kifungo kiondoke.

Kuna binti yeye alivalishwa pete za kichawi kila kidole cha mkono wake, aliona kwenye ndoto lakini hakujali.

Pete zile ni maagano ya kishetani kati yake na majini mahaba ili kumzuilia kuolewa.

Ndugu kwa YESU ni sehemu pekee salama ambapo unaweza kufunguliwa vifungo vya giza vyote.
Ukimwamini na maombi katika jina lake hakika utafunguliwa.

Marko 9:23 ''YESU akamwambia, Ukiweza! Yote yawezekana kwake aaminiye.''

Jambo la kujua ni kwamba kila kifungo kina njia zake za kutoka katika kifungo hicho, kama unajua kifungo ulichofungwa basi tafuta kujua jinsi ya kutoka katika kifungo hicho.

Kuna vifungo unahitaji tu kubadilika tabia baada ya kutubu ndipo vinaondoka.

Kuna vifungo unahitaji kujulishwa na Neno la MUNGU  jinsi ya kutoka.

Kuna vifungo vinahitaji sadaka na maombi ili kutoka katika vifungo hivyo.

Ngoja nikupe namna ya kutoka katika baadhi ya vifungo vya kipepo maana kila kifungo kina kanuni zake za kutoka katika vifungo hivyo.
Hivi ni baadhi tu lakini wewe ndio unajua kifungo kinachokutesa hivyo tafuta kujua jinsi ya kutoka katika kifungo hicho na hakika katika jina la YESU KRISTO utatoka katika kifungo hicho.



A.    Jinsi ya kutoka kwenye kifungo cha magonjwa.

1.  Tubu kwa kilichosababisha ufungwe kifungo cha magonjwa. 
Matendo 3:19 '' Tubuni basi, mrejee, ili dhambi zenu zifutwe, zipate kuja nyakati za kuburudishwa kwa kuwako kwake BWANA; ''
 

2.  Amuru ugonjwa utoke ndani yako.
 Mathayo 18:18 '' Amin, nawaambieni, yo yote mtakayoyafunga duniani yatakuwa yamefungwa mbinguni; na yo yote mtakayoyafungua duniani yatakuwa yamefunguliwa mbinguni. ''

3.  Omba MUNGU akuponye. 
Mathayo 7:8 '' kwa maana kila aombaye hupokea; naye atafutaye huona; naye abishaye atafunguliwa. ''
 

4.  Isemeshe nafsi yako kwamba unapona.
Zaburi 116:7 '' Ee nafsi yangu, urudi rahani mwako, Kwa kuwa BWANA amekutendea ukarimu.''
 

5.  Ita afya itokayo kwa MUNGU.
 Yeremia 33:6 ''Tazama, nitauletea afya na kupona, nami nitawaponya; nami nitawafunulia wingi wa amani na kweli.''



B. Jinsi  ya kutoka katika vifungo vya dhambi.

1.  Tubu na kuziacha dhambi zote. 
Zaburi 34:14 ''Uache mabaya ukatende mema, Utafute amani ukaifuatie.''
 

2.   Vunja uhusiano  na watu  ulioshirikiana nao kwenye dhambi.
Zaburi 1:1 '' Heri mtu yule asiyekwenda Katika shauri la wasio haki; Wala hakusimama katika njia ya wakosaji; Wala hakuketi barazani pa wenye mizaha.''
 

3.  Amua kuwa mtu wa ibada na maombi. 
Yohana 4:24 ''MUNGU ni ROHO, nao wamwabuduo yeye imewapasa kumwabudu katika roho na kweli. ''
 

4.  Ishi maisha matakatifu ya wokovu wa KRISTO YESU. 
1 Petro 1:15 '' bali kama yeye aliyewaita alivyo mtakatifu, ninyi nanyi iweni watakatifu katika mwenendo wenu wote; ''
 

5.  Usikumbuke mambo ya kwanza yaani mambo ya  dhambi.
Isaya 43:18 ''Msiyakumbuke mambo ya kwanza, wala msiyatafakari mambo ya zamani.''

6.  Enenda kwa ROHO MTAKATIFU. 
Warumi 8:14 ''Kwa kuwa wote wanaoongozwa na ROHO wa MUNGU, hao ndio wana wa MUNGU.''
 

7.  Haribu kwa damu ya YESU kila madhabahu ya giza au nguvu za giza zilizokuwa zinakutumikisha kufanya dhambi. 
Kumb 7:5 '' Lakini watendeni hivi; zivunjeni madhabahu zao zibomosheni nguzo zao, yakateni maashera yao, ziteketezeni kwa moto sanamu zao za kuchonga.''
 

C.  Vifungo vya madeni.

1.  Omba MUNGU upate pesa ya kulipa kisha lipa deni hilo.

2.  Epuka kukopa 

3.  Omba MUNGU akubariki na  fanya kazi kwa bidii ili uwe na pesa zako mwenyewe.

4.  Haribu kila nguvu za giza zinazoleta uharibifu maishani mwako ili ukope pesa kushughulikia matatizo yako.

D.Vifungo vya ajali au balaa au mikosi.

1.  Haribu kwa maombi kila watenda kazi ya kishetani wanaotumika kuleta ajali, mikosi au balaa kwako.

2.  Haribu madhabahu za giza zinazoleta  mambo yao kwako.

3.  Mtegemee MUNGU na kumtumaini kisha omba  yeye akulinde. Isaya 26:3 ''Utamlinda yeye ambaye moyo wake umekutegemea Katika amani kamilifu, kwa kuwa anakutumaini. ''
Kila siku omba katika jina la YESU na kabla ya jambo lolote au safari yeyote omba kwa MUNGU.

4.  Msikilize ROHO MTAKATIFU ili kama kuna mahali hatakupa amani kwenda basi uusiende.

E.  Kifungo cha utasa.

1.  Omba Bwana YESU akufungue kifungo hicho huku ukitumia damu ya YESU maana hujui ni wapi ulifungwa.
 Yohana 14:14 ''Mkiniomba neno lo lote kwa jina langu, nitalifanya. ''
 

2.  Haribu kila nguvu za giza zilizoitumika kukuzuilia uzao.
 Luka 10:19 '' Tazama, nimewapa amri ya kukanyaga nyoka na nge, na nguvu zote za yule adui, wala hakuna kitu kitakachowadhuru. ''
 

3.  Futa kila maneno ya watu mabaya waliyokutamkia ili kukuzuia uzao.
Yakobo 3:5 ''Vivyo hivyo ulimi nao ni kiungo kidogo, nao hujivuna majivuno makuu. Angalieni jinsi moto mdogo uwashavyo msitu mkubwa sana. ''

4.  Fungua tumbo lako la uzazi kwa maombi na takasa kila sehemu ya mwili wako na ya mume/mke wako inayohusika na uzao.
 Waamuzi 13:3 '' Malaika wa BWANA akamtokea yule mwanamke, akamwambia, Tazama, WEWE SASA U TASA, HUZAI; LAKINI UTACHUKUA MIMBA, NAWE UTAPATA MTOTO mwanamume. ''

5.  Ita uzao wako kwa jina la YESU KRISTO.
 
Mathayo 12:37 '' KWA KUWA KWA MANENO YAKO UTAHESABIWA HAKI, na kwa maneno yako utahukumiwa.''


6.  Ukomboe uzao wako uliozuiliwa kipepo ili usije.
 Zaburi 91:10 '' Mabaya hayatakupata wewe, Wala tauni haitaikaribia hema yako. ''
 

7.  Mpinge shetani na kazi zake zote na uwe mtu wa maombi.
 Zaburi 91:13 '' Utawakanyaga simba na nyoka, Mwana-simba na joka utawaseta kwa miguu.''
 

8.  Omba kwa MUNGU kwamba majira yako ya kupata uzao yaje na asizuie yeyote.
Mhubiri 3:1 '' Kwa kila jambo kuna majira yake, Na wakati kwa kila kusudi chini ya mbingu.''

9.  Ishi maisha ya uaminifu katika ndoa yako huku ukifanyia kazi kimaombi kila unachoona kwenye ndoto au maono kinachohusika na uzao.
 Waebrania 13:4 '' Ndoa na iheshimiwe na watu wote, na malazi yawe safi; kwa maana waasherati na wazinzi MUNGU atawahukumia adhabu. ''

10.  Ita ahadi ya MUNGU ya uzao kwako ili itimie.
 Mwanzo 18:14 ''Kuna neno gani lililo gumu la kumshinda BWANA? Kwa muhula wake nitakurudia, wakati huu huu mwakani, na Sara atapata mwana wa kiume. ''

11.  Omba nguvu za MUNGU zikufunike siku zote.
 Isaya 40:29-31 ''Huwapa nguvu wazimiao, humwongezea nguvu yeye asiyekuwa na uwezo. Hata vijana watazimia na kuchoka, na wanaume vijana wataanguka; bali wao wamngojeao BWANA watapata nguvu mpya; watapanda juu kwa mbawa kama tai; watapiga mbio, wala hawatachoka; watakwenda kwa miguu, wala hawatazimia.''
 

12.  Omba kujua  mapenzi/Matakwa ya MUNGU juu ya uzao wako. 
Isaya 14:27 ''Maana BWANA wa majeshi amekusudia, naye ni nani atakayelibatili? Na mkono wake ulionyoshwa, ni nani atakayeugeuza nyuma?''
Somo lina ufafanuzi mwingi sana hivyo siku moja nitalifafanua zaidi katika kitabu ambacho nitachapisha na kitakufikia.
 
Natamani niseme mengi mno lakini naamini mwenye kuelewa ameelewa.
MUNGU akubariki kwa kujifunza somo hili muhimu pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane nitakujulisha jinsi ya kukipata.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.
0714252292(Hadi whatsapp).
0786719090
mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu.

Comments