MAMBO MATANO UNAYOPASWA KUJUA KIPINDI MUNGU ANAZUNGUMZA NA WEWE.

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.

Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu zangu wote.
Inawezekana wewe umeokoka na ni mtumishi mwaminifu wa MUNGU, nina neno kwa ajili yako kama sehemu ya utangulizi wa somo langu, ni kwamba Kubaliana na wito aliokupa MUNGU ili umtumikie.
Usiukatae wito wa utumishi aliokupa Bwana YESU, Bali fanyia kazi wito huo.
Umeitwa kushuhudia, hakikisha unashuhudia.
Umeitwa kuhubiri, hakikisha unahubiri.
Umeitwa kusifu na kuabudu kwa uimbaji, hakikisha unamwimbia MUNGU.
Umeitwa kuchangia injili au kuipeleka kwa pesa zako, Hakikisha unaipeleka injili.
Umeitwa kufundisha Neno la MUNGU, hakikisha unafundisha.
Umeitwa kuimba kwaya, hakikisha unaimba kwa upendo na uaminifu.
Umeitwa kuonya watu ili waache dhambi, hakikisha unawaonya.
Umeitwa kushauri watu ili wasifanye maamuzi mabaya, timiza wito wako.
Umeitwa kutengeneza palipobomoka, hakikisha unatengeneza.
Katika mambo mengi sana MUNGU anaweza kukuita ili umtumikie.
Ndugu, hakikisha unamtumikia kwa moyo na kwa uaminifu wote.
1 Wakorintho 15:58 "Basi, ndugu zangu wapendwa, mwimarike, msitikisike, mkazidi sana kutenda kazi ya BWANA sikuzote, kwa kuwa mwajua ya kwamba taabu yenu siyo bure katika BWANA."


Wewe uliyeokoka ni wakili wa KRISTO mbele ya ulimwengu.
Kazi ya wakili ni kuwakilisha na kuwasilisha.
Je wewe unawakilisha nini cha Injili ya KRISTO kwa jamii?
Je unawasilisha nini katika ufalme wa MUNGU kinachotokana na uwakili wako?
Dunia inataka useme yaliyo ya MUNGU, huo ndio uwakili.
Matendo yako mema yanatakiwa yawe uwakili mwema mbele ya jamii.
Kuwaombea watu ili wapate Neema ya wokovu, ni uwakili.
Kuwakataza watu wako wa karibu kufanya mabaya, ni uwakili.
Kuwaambia watu waokoke ndio kazi namba moja ya uwakili wako.
Kama kweli wewe ni wakili wa MUNGU basi ipeleke injili ya KRISTO.
1 Wakorintho 4:1-2" Mtu na atuhesabu hivi, kuwa tu watumishi wa KRISTO, na mawakili wa siri za MUNGU. Hapo tena inayohitajiwa katika mawakili, ndiyo mtu aonekane kuwa mwaminifu."


 Inawezekana wewe ni mtumishi au unatamani kumtumikia Bwana YESU lakini woga unakuzuilia kutumika mbele za watu.
Ngoja nikujulishe mambo haya.
Ukiwa mbele ya watu kwa ajili ya kuwashuhudia watu hao injili ya KRISTO inayookoa basi;
1. Jiamini na Uwe hodari
2. Ongea tu yakupasayo kuongea.
3. Enenda kwa ROHO MTAKATIFU.
4. Yajue mazingira uliyopo.
5. Wajue watu unaowafundisha.
Fanya kwa MUNGU kwanza ndipo MUNGU atafanya baraka kwako.
Watu wengi hupenda MUNGU afanye ya kwao, huku wao hawataki kufanya ya Ki MUNGU.
Kila baraka za Ki MUNGU zina kanuni zake, kuna baraka zingine unatakiwa ufanye yaliyo ya MUNGU ndipo MUNGU atakubariki.

Wakati wengine wakihubiri madhehebu yao au huduma zao, wewe hubiri Injili ya YESU KRISTO iokoayo.
Wakati wengine wakibishana tu kuhusu YESU ni MUNGU au sio MUNGU, Wewe hubiri Injili ya YESU KRISTO iokoayo.

Tito 2:11-13 ''Maana neema ya MUNGU iwaokoayo wanadamu wote imefunuliwa; nayo yatufundisha kukataa ubaya na tamaa za kidunia; tupate kuishi kwa kiasi, na haki, na utauwa, katika ulimwengu huu wa sasa; tukilitazamia tumaini lenye baraka na mafunuo ya utukufu wa KRISTO YESU, MUNGU mkuu na Mwokozi wetu; ''
 
Wakati wengine wakifundisha jinsi ya kuhesabiwa haki kwa torati, wewe Hubiri injili ya Uzima wa milele.
Waka.
Wakati wengine wakimkana aliyewaumba, wewe hubiri injili ya YESU KRISTO iokoayo.
Wakati wengine wakihubiri siasa kanisani, wewe hubiri Neno la MUNGU la uzima wa milele.
Nawapenda Mitume maana baada tu ya Bwana YESU kuondoka hawakuja na Neno jingine ila injili ya YESU KRISTO iokoayo.
Ndugu, acha kubishana tu maana ulimwengu unakusubiri uipeleke injili ili watu waokolewe.
Wakati wengine wanafundisha ujasiliamali ibadani wewe hubiri wokovu.
Wakati wengine wanahubiri tiba mbadala kanisani, wewe hubiri injili ya KRISTO iokoayo.
Ndugu acha kutafuta heshima mbele ya wateule wenzako bali hubiri Wokovu wa Bwana YESU.
Kazi ya MUNGU sio kumpinga MUNGU bali kumtii.
Usimpinge MUNGU Muumbaji wako kupitia mafundisho yako.


Kumbuka pia kwamba haiwezekani Mtu wa MUNGU ukajazwa nguvu za MUNGU bila kumtafuta MUNGU. 
MUNGU Baba anasema 
 '' Nanyi mtaniita, mtakwenda na kuniomba, nami nitawasikiliza. Nanyi mtanitafuta na kuniona, mtakaponitafuta kwa moyo wenu wote.-Yeremia 29:12-13''
Hivyo ni lazima sana kumtafuta MUNGU ndipo nguvu za MUNGU zitakuwa pamoja na wewe.
Bila maombi huwezi kujaa nguvu za MUNGU.
Bila utakatifu huwezi kujaa nguvu za MUNGU.
Bila kujifunza Neno la MUNGU na kulitafakari huwezi kujaa nguvu za MUNGU.
Bila kumtii ROHO MTAKATIFU sahau kuhusu kujaa nguvu za MUNGU.
Bila kuokolewa na Bwana YESU sahau kuhusu nguvu za MUNGU.
Bila kumtiii MUNGU sahau kuhusu nguvu za MUNGU.

Kama huliishi kusudi la MUNGU la kuitwa kwako katika Wokovu wa Bwana YESU hakika kujaa nguvu za MUNGU itakuwa vigumu sana kwako.

Tena likumbuke sana jambo hili kwamba  Mtumishi wa MUNGU haimpasi kuwa na kinyongo na mtu yeyote.
Heri Kuitwa Kafiri Kwa Sababu Umeyakataa Mafundisho Ya Mashetani Kuliko Kuitwa Mtakatifu Huku Unaabudu shetani.
Usipokuwa na Wokovu wa YESU KRISTO wewe umepotea na zaidi ya kupotea
Mtumishi wa MUNGU haikupasi kuwa na uchungu na mtu kwa sababu ya makosa yake ya zamani.
Kuwa na kinyongo na mtu wala sio mpango wa MUNGU.
Kuwa na uchungu na watu wakati mwingine ni dhambi mbaya sana.
Angalia sana maana wakati mwingine kinyongo chako na uchungu wako dhidi ya watu wengine, hayo ni mapando ya shetani kukuzuia.

 IIshi katika kweli.
Tembea katika hiyo kweli.
Fanyia kazi hiyo kweli.
Fanyika mtenda kazi wa hiyo kweli.
Mtii MUNGU aliyeileta hiyo kweli na umwabudu yeye peke yake.
Kweli ni moja tu ambayo ni injili ya Wokovu wa YESU KRISTO kwa wanadamu wote watakaotii.
Hakikisha unahusika na kweli hiyo maana ukienda kinyume na hiyo kweli hakika hutaupata Uzima wa milele.
Mimi nimekuambia kweli nikitumai utafanyia kazi hiyo kweli.

Yohana 3:16-18 " Kwa maana jinsi hii MUNGU aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele.
Maana MUNGU hakumtuma Mwana ulimwenguni ili auhukumu ulimwengu, bali ulimwengu uokolewe katika yeye. Amwaminiye yeye hahukumiwi; asiyeamini amekwisha kuhukumiwa; kwa sababu hakuliamini jina la Mwana pekee wa MUNGU."



Mambo matano unapaswa kujua na kuelewa kipindi MUNGU anapozungumza na wewe, ili sauti hiyo ya MUNGU ikusaidie kufanya maamuzi sahihi katika maisha yako.

1. Tambua kwamba sauti ya MUNGU inaendana na nyakati alizoziamuru juu yako.

Mhubiri 3:1 ''
Kwa kila jambo kuna majira yake, Na wakati kwa kila kusudi chini ya mbingu.''
Hakikisha unajua kile MUNGU amekuambia ni cha wakati gani.
Kuna watu MUNGU alisema nao mfano kuhusu huduma na siku hiyo hiyo wakaanza kufanya maagizo hayo ya kihuduma lakini wakashindwa. Kumbe walijulishwa ili wajue na wajiandae maana mambo waliyoona sio kwa wakati huo.
Hakikisha unajua kuhusu jambo uliloambiwa ni la wakati huo huo au ni la baadae au ni la zamani?
Ukijua  vyema sauti hiyo ya MUNGU itakusaidia kufanya maamuzi sahihi katika maisha yako.

2. Jifunze kuifuatilia na kuielewa sauti ya MUNGU.

Ayubu 33:14 ''
Kwa kuwa MUNGU hunena mara moja, Naam, hata mara ya pili, ajapokuwa mtu hajali.''
Inawezekana kwako MUNGU amezungumzia mara ya kwanza hukuelewa, akasema tena lakini hukuelewa. Ndugu unahitaji kufuatilia na kuielewa sauti ya MUNGU ili sauti hiyo ya MUNGU ikusaidie kufanya maamuzi sahihi katika maisha yako.
Hakikisha unakuwa muombaji sana ili kuielewa sauti ya MUNGU.
Hakikisha umejaa sana Neno la MUNGU moyoni mwako ili ujue kuielewa sauti ya Neno la MUNGU.
 Jiambatanishe na ROHO MTAKATIFU katika maisha yako yote ili akusaidie maana ni yeye tu ndio hufumbua mafumbo yote ya MUNGU.
1 Kor 2:10 '' Lakini MUNGU ametufunulia sisi kwa ROHO. Maana ROHO huchunguza yote, hata mafumbo ya Mungu.''
Tafuta sana kuelewa kile ambacho MUNGU amesema na wewe maana usipozingatia siku moja sauti hiyo ya MUNGU kwako inaweza kukoma.

3. Unahitaji utulivu na usikivu ili kuelewa kile ambacho MUNGU amekuambia.

Yeremia 23:18 ''
Maana, ni nani aliyesimama katika baraza la Bwana, hata akalifahamu neno lake na kulisikia? Ni nani aliyelitia moyoni neno langu, na kulisikia? ''
Unahitaji kuwa katika usikivu na utulivu mzuri ili uelewe kile ambacho MUNGU amekusemesha.
Kaa katika Baraza la MUNGU yaani kaa katika uwepo wa MUNGU, kaa katika ibada, kaa katika maombi, kaa katika tafakari ya Neno la MUNGU sana.
Ukiwa na usikivu na utulivu mzuri wa kuisikia sauti ya MUNGU hakika hiyo itakuwa faida kwako na  sauti hiyo ya MUNGU itakusaidia kufanya maamuzi sahihi katika maisha yako.

4. Jifunze kuandika Yale ambayo MUNGU amesema na wewe.

Habakuki 2:2 ''
BWANA akanijibu, akasema, Iandike njozi ukaifanye iwe wazi sana katika vibao, ili aisomaye apate kuisoma kama maji.''
MUNGU siku moja alimsemesha Habakuki kwa njia ya ndoto na kumwambia kwamba aindike ndoto ile maana itatimia baadae na sio wakati huo.
Hata wewe kuna jumbe zingine MUNGU anakusemesha iwe kwa ndoto, maono au kwa Neno la ufunuo, inakupasa sana ndugu kuandika hicho ambacho amekusemesha MUNGU.
Mimi Mabula nilipokuwa nataka kutengeneza blog ya kuhubiria injili nilijaribu mara kadhaa kuwapigia watu ambao nilijua watanisaidia maana wao ni wataalamu lakini watu hao hawakupokea simu yangu, ilikuwa inaita tu hadi nikakata tamaa. Siku moja usiku nikaota ndoto nikielekezwa jinsi ya kutengeneza Blog yangu ya Maisha ya ushindi, nilielekezwa vipengele vingi na bdoto ile ya muda mrefu ilipofika saa kumi usiku iliisha na baada tu ya kuisha nikajikuta niko macho. Nikaamua muda huo huo niandike maelekezo ya ndotoni juu ya kutengeneza blog, hakika MUNGU alitenda muujiza kwangu maana asubuhi nilichukua maelekezo yale ya ndotoni na kutengeneza blog ya Maisha ya Ushindi ambayo hadi sasa watu wameshaifungua zaidi ya mara milioni mbili na nusu, na shuhuda za watu kufunguliwa ni nyingi sana. Ningedharau ingekuwaje?
Ndugu uwe na tabia ya kuandika kile amacho umehakikisha ni MUNGU kasema na wewe.
Musa alimbiwa kuandika kile ambacho MUNGU alimsemesha, kwanini wewe usiandike?
 Kutoka 17:14 ''BWANA akamwambia Musa, Andika habari hii katika kitabu iwe ukumbusho, kisha ihubiri masikioni mwa Yoshua; ya kuwa nitaufuta ukumbusho wa Amaleki kabisa, usiwe tena chini ya mbingu.''
Mimi P Mabula  ni mara kadhaa nimewasiliana na watu ambao waliniambia juu ya maono au ndoto mbaya ambazo waliota na kupuuzia lakini baadae ilikuja kuwa kama walivyoona kwenye ndoto, na kubaki wakijuta maana hawakufanyia kazi.
Ndugu fanyia kazi ujumbe wa MUNGU anaosema na wewe baada ya kuuandika ili usisahau.

5. Jifunze kuzijua sauti zisizo za MUNGU ili ikusaidie kutofautisha sauti ya MUNGU na sauti isiyo ya MUNGU.

Yeremia 23:16 ''
BWANA wa majeshi asema hivi, Msisikilize maneno ya manabii wakiwatabiria; huwafundisha ubatili; hunena maono ya mioyo yao wenyewe; hayakutoka katika kinywa cha BWANA.''
Unapokuwa mtu wa kujifunza sana Neno la MUNGU itakusaidia sana kujua kila kilicho kinyume na Neno la MUNGU hivyo kutambua kirahisi kabisa sauti za kipepo au sauti za kibinadamu.
Ukiwa na ROHO MTAKATIFU itakuwa rahisi sana kujua kila jambo lililo kinyume na MUNGU.
Inawezekana wewe huwa unasikia sauti za majini na unadhani ni MUNGU anakusemesha.
Wako watu husikia mizimu au wachawi na kudhani ni Malaika wa MUNGU, Ndugu ukiwa na ROHO MTAKATIFU hakika atakujulisha juu ya hila hizo za giza ili usifanyie kazi.

Natamani niseme mengi mno lakini naamini mwenye kuelewa ameelewa.
MUNGU akubariki kwa kujifunza somo hili muhimu pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane nitakujulisha jinsi ya kukipata.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.
+255714252292(Hadi whatsapp).
+255786719090
mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu.

Comments