MAOMBI YA KUIOMBEA THAMANI YAKO ILI IONEKANE.

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.

 Bwana YESU atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU na kisha tuombe maombi ya ushindi katika jina la YESU KRISTO.
Kwanza namshukuru MUNGU Baba kwa neema yake maana katika Miaka 7 tangu nimeanza kuhubiri Mtandaoni hili ni somo la 802, ni Kazi ngumu mno lakini atukuzwe MUNGU wa Israeli anayetupa nguvu za kumtumikia katika KRISTO YESU Mwokozi wetu, na sasa injili itasonga mbele sana sana hadi mwisho wa Kusudi la MUNGU.
Napokea shuhuda za ajabu sana kutoka kwa watu waliobarikiwa na waliofunguliwa kutokana na masomo haya, namtukuza sana MUNGU kwa ajili yao. Kipekee pia namshukuru sana MUNGU Baba kwa watu ambao huniombea na wale ambao huniunga mkono kwa sadaka zao  ili kupanua wigo wa kuhubiri injili kwa watu wengi zaidi.
Leo tunajifunza soma la kuiombea thamani yako ili ionekane.
Thamani ni nini?
Thamani  ni ubora wa kitu  kutokana na hali ya kuhitajika kwake katika jamii.
Ayubu 28:13 ''Mwanadamu hajui thamani yake, Wala haionekani katika nchi ya walio hai.''
Kulingana na somo langu hili, Thamani ya mtu  ni ubora wake  kutokana na kuhitajika kwake  katika jamii, kundi, ofisi, taasisi n.k
Thamani ya mtu inaweza kuwa kubwa kiasi kwamba kila mtu atatamani kumwajiri n.k lakini pia thamani ya mtu inaweza kuwa chini kiasi kwamba  kuna watu wengine watatamani hata asiwepo au afukuzwe tu.
Maombolezo 4:2 ''Wana wa Sayuni wenye thamani, Walinganao na dhahabu safi, Jinsi wanavyodhaniwa kuwa vyombo vya udongo, Kazi ya mikono ya mfinyanzi! '' 
Huu ni Mfano hai kwamba Wana wa Sayuni walikuwa na thamani  kama dhahabu lakini lakini baadae kwa sababu ya mambo fulani kupita wakawa  hawana thamani, wakawa kama vyombo vya udongo na sio dhahabu.
 Kwa maana nyingine ni kwamba thamani ya mtu ni bei yake.
Je wewe ni wa bei gani kulingana na thamani yako?
Je thamani yako iko juu au iko chini?
Kama umeokoka na unaishi maisha matakatifu inakupasa thamani yako iwe juu kama ulivyookolewa kwa damu ya thamani sana ya YESU KRISTO.
1 Petro 1:18-19 ''Nanyi mfahamu kwamba mlikombolewa si kwa vitu viharibikavyo, kwa fedha au dhahabu; mpate kutoka katika mwenendo wenu usiofaa mlioupokea kwa baba zenu;
19 bali kwa damu ya thamani, kama ya mwana-kondoo asiye na ila, asiye na waa, yaani, ya KRISTO.'
'


Kuna watu thamani yao huonekana kipindi tu wamekufa, ni ajabu sana maana wakati huo ndipo utasikia kila mtu akizungumzia thamani yake njema, ndugu tafuta katika KRISTO thamani yako ionekane ukiwa hai na sio ukiwa umekufa.
Kuna watu akiwa hayupo tu ndio anaonekana wa thamani lakini akiwiwepo anaonekana kama takataka tu mbele za watu.
Kuna ndoa zingine mke au mume akiwa mbali safarini au mkoani mbali ndio anaonekana wa thamani, anapigiwa simu na kusifiwa sana kwamba hakuna kama yeye lakini akitokea tu thamani yote inaondoka na hapo vita vinaanza huku akionekana hana thamani hata moja.
Ndugu, Kuna mambo mengi tu yanayoweza kuiondoa thamani ya mtu, kama ni mambo mabaya ndio yameifuta thamani yako hata isionekane basi tengeneza haraka sana.
Mteule wa MUNGU inakupasa kuwa wa thamani siku zote.
1 Kor 6:20 ''maana mlinunuliwa kwa thamani. Sasa basi, mtukuzeni MUNGU katika miili yenu. ''
 Sasa ni ajabu kwamba kuna watu huonekana wa thamani kipindi tu hawapo, wamesafiri au wamehama.
Inawezekana Mume wako hajawahi kuiona thamani yako hata siku moja kwa sababu ya  kutekwa kipepo na mawakala wa shetani, ndio maana anakusaliti na kukudharau.
 Inawezekana kwenye familia yenu au ukoo wenu wewe hujulikani na ndio maana huwa wanakaa kikao cha familia au ukoo bila kukuhusisha wewe kwa sababu huna thamani, lakini kuna mtu mmoja tu akikosekana na kikao kinaailishwa hata kama yeye ni mtoto mdogo kwenye familia kuliko hata wewe.
Inawezekana wewe kila ukipata mchumba baada ya muda mfupi anakuacha maana thamani yako inakuwa haionekani tena.
Inawezekana wewe una elimu nzuri lakini kila ukiomba kazi hupati maana unaonekana huna thamani mbele ya unaowaomba kazi, wengine wasio na elimu kama yako pale pale wanapata kazi kwa sababu wao thamani zao zinaonekana.
Ndugu, sio kila jambo ni kawaida tu bali kumbuka pia shetani na mawakala zake wako kazini hivyo inawezekana kabisa unateswa na kifungo cha giza cha kuifanya thamani yako isiwepo.
Inawezekana wewe ndio mfanyakazi   bora kazini kwako na mwenye juhudi kubwa  sana na mwaminifu sana lakini thamani yako  kwa bosi wako haijawahi kuonekana, labda kwa sababu wenzako wanaitafuta thamani kwa njia za kipepo.
Nisikilize itakusaidia sana. Somo la leo ni ufunuo ili uhusike na maombi ya kuiombea thamani yako ili ionekane.
Wewe ni wa thamani sana mbele za MUNGU.
Isaya 43:4 ''Kwa kuwa ulikuwa wa thamani machoni pangu, na mwenye kuheshimiwa, nami nimekupenda; kwa sababu hiyo nitatoa watu kwa ajili yako; na kabila za watu kwa ajili ya maisha yako. ''

 MAMBO YANAYOWEZA KUONDOA THAMANI YAKO.

 1.Dhambi na makosa.
Zaburi 34:14 '' Uache mabaya ukatende mema, Utafute amani ukaifuatie.''
 Dhambi ndio adui namba moja anayeipunguza thamani yako.
Unaweza ukaonekana huna thamani kazini, nyumbani ua hata kwa watumishi wa MUNGU kwa sababu ya dhambi zako kila mara.
Ukitaka thamani yako ionekane hakikisha unaishi maisha matakatifu na ya haki katika KRISTO YESU.

2. Kutokujitambua na kutokutambua  haki yako na wajibu wako.
 Isaya 42:22  '' Lakini watu hawa ni watu walioibiwa na kutekwa; wote wamenaswa katika mashimo, wamefichwa katika magereza; wamekuwa mawindo, wala hapana aokoaye; wamekuwa mateka, wala hapana asemaye, Rudisha. ''
Usipojitambua utajikuta katika gereza la kiroho au vifungo vingine vya kiroho na hivyo thamani yako kuondoka. Huwezi kuwa na thamani wakati uko katika gereza la kutumia madawa ya mganga, vifungo vya ulevi, bangi, wengine wana nguvu za giza kabisa  n.k
Wasiojitambua wengi wako katika vifungo mbalimbali na hawataki kufunguliwa ndio maana wana haribu kila leo na thamani zao kuondoka. Ndugu jitambue na tambua haki zako kwamba unamhitaji YESU akufungue na kukuweka huru ndipo thamani yako itaonekana.

3. Kuwa na tabia zisizofaa.
Ziko tabia zisizofaa nyingi sana ambazo zinaweza kuishusha thamani ya mtu husika, Mfano wa tabia zisizofaa ni Kutoa siri usizotakiwa kutoa, uzembe, ulegevu, kukosa msimamo, kuwavuruga wengine kwa  kwa maneno yako au kauli zako sisizo na maana n.k
Biblia inakushauri katika hilo ikisema '' mkihakiki ni nini impendezayo BWANA. Wala msishirikiane na matendo yasiyozaa ya giza, bali myakemee;-Waefeso 5:10-11 ''
Hakiki kila ukifanyacho kama unampendeza MUNGU. 
Ndugu, kama ni tabia zisizofaa ndio zimeondoa thamani yako basi anza kuliishi Neno la MUNGU ili uwe na tabia njema.

4. Kutokutenda mema.
1 Petro 3:13 ''Naye ni nani atakayewadhuru, mkiwa wenye juhudi katika mema?   '' 
Maana yake ukiwa na juhudi katika kutenda mema hata thamani yako haitakuwa chini.
Inawezekana wewe thamani yako haionekani kazini kwako, kwenye ndoa yako, kwenye huduma yako, au kwenye jamii yako kwa sababu hutendi mema, ndugu mema yanaweza kuifanya thamani yako ionekane.

5. Kurogwa, kuteswa na nguvu za giza au kutumika kipepo.
Isaya 28:15 '' Kwa sababu mmesema, Tumefanya agano na mauti, tumepatana na kuzimu; pigo lifurikalo litakapopita, halitatufikia sisi; kwa maana tumefanya maneno ya uongo kuwa kimbilio letu, tumejificha chini ya maneno yasiyo kweli; ''
Hapa ndipo watu wengi pia hunaswa na hivyo thamani zao kutokuonekana.
Kama wewe unatumika kipepo hakikisha leo unafunguliwa maana ukiendelea kutumika kipepo thamani yako haitaonekana kamwe, utakuwa huna kibali cha MUNGU na wanadamu.

6. Kushirikiana na watu wabaya.
Zaburi 1:1 ''Heri mtu yule asiyekwenda Katika shauri la wasio haki; Wala hakusimama katika njia ya wakosaji; Wala hakuketi barazani pa wenye mizaha.''
Marafiki zako wanaotumika kipepo unaoshirikiana nao kila siku wanaweza kukufanya thamani yako isionekane.
Watu wabaya watakudanganya na kukufanya ukubali kufanyia kazi uongo. Mojawapo wa watu wabaya ni wale walio na tabia chafu, waabudu shetani, waenda kwa waganga n.k
Kushirikiana na watu wabaya wa namna yeyote kutakufanya thamani yako isionekane.
Hivyo ili thamani yako ionekane hakikisha hushirikiani na watu wabaya, watu husema ukitembea na mwizi/mlevi na wewe utakuwa mwizi/mlevi, huko ni kushushwa thamani yako sana, hivyo usikubali kushirikiana na watu wabaya maana wataishusha thamani yako.
Biblia inasema usikae barazani pa wenye mizaha yaani walio kinyume na utakatifu, usiende katika njia ya wakosaji yaani watenda mabaya.

7. Kunenewa uongo na kuzingiziwa.
 Kutoka 20:16 '' Usimshuhudie jirani yako uongo. ''
Neno la MUNGU aliye hai linakataza mtu yeyote kumsemea uongo mtu mwingine, lakini wako watu wanawazushia uongo watu wengine. 
Hapa napo ni watu wengi sana thamani zao hazionekani kwa sababu tu walisingiziwa au kunenewa uongo.
Binti anaweza akakosa wa kumuoa kwa sababu kila mtu mtaani kwake anajua kwamba binti yule ni malaya hata kama sio kweli bali kuna mtu mmoja kwa hila alieneza uongo juu ya binti huyo, leo tunaomba katika jina la YESU KRISTO na kuna mtu anaenda kupona.
Wako watu kila mtu anamuogopa kwa sababu tu alisingiziwa na kunenewa uongo juu ya jambo fulani, Kuna watu wanaitwa mtaani kwao kwamba ni wachawi lakini katika uhalisia sio kweli kabisa.
Kuna watu wamevikwa tabia mbalimbali kwa kunenewa uongo kiasi kwamba kila mtu anadhani kwamba ni kweli wako hivyo.
Ndugu kusingiziwa au kunenewa uongo hupolomosha ghafla sana thamani ya mtu husika hivyo leo tunaomba na MUNGU anaenda kufuta kila maneno ya uongo uliyonenewa yaliyoifuta kabisa thamani yako kwa ndugu zako, kwa mwenzi wako wa ndoa au mchumba wako, kwa jamii yako na kila sehemu ya maisha yako.
Mimi kama Peter nayajua madhara  ya kunenewa uongo, zamani sana utotoni kuna mtu aliwahi kuninenea uongo kwa watu wengi, mimi sikuwepo na nipokukuja kila mtu alikuwa ananicheka tu, nilidharaulika mno na kadri siku zilivyosonga ndipo walioambiwa uongo kuhusu mimi waligundua kwamba haukuwa ukweli ndipo wakaniambia na kumgeukia yule aliyenizushia uongo.

8. Kutokumtegemea MUNGU .
2 Nyakati 20:20 '' ..............  mwaminini BWANA, Mungu wenu, ndivyo mtakavyothibitika; waaminini manabii wake, ndivyo mtakavyofanikiwa.''
Siri mojawapo ya mtu ili afanikiwe katika jambo lolote ni kumwamini MUNGU na kuwaamini watumishi wa MUNGU walio wa kweli  maana hao watakufundisha Neno la KRISTO na kukujulisha ujumbe wa MUNGU kwako ili ufanikiwe katika jambo lolote.
Thamani yako inaweza isikue hata siku moja kwa sababu tu humtegemei MUNGU na hauwaamini watumishi wa KRISTO wenye ROHO MTAKATIFU wanaoweza kukusaidia katika maisha yako.
Moja ya makosa makubwa sana ambayo mwanadamu anaweza kuyafanya katika maisha yake ni kutokumwamini MUNGU katika KRISTO YESU.

Inawezekana Biashara yako haijawahi kuvutia watu kwa sababu majirani zako wanaiziba kipepo na wao kijipandisha.
Inawezekana una elimu kubwa na nzuri sana lakini thamani yako iko chini sana kwa sababu ta tabia zako, ndugu tengeneza kwa Bwana YESU Mwokozi.

ILI THAMANI YAKO IONEKANE FANYIA KAZI MAMBO HAYA.

1. Acha dhambi. uovu na makosa
Zaburi 34:14 '' Uache mabaya ukatende mema, Utafute amani ukaifuatie. ''

2. Mtii  YESU KRISTO aliyekununua kwa damu yake  ili sasa MUNGU akuinue na sio kutegemea wanadamu ili wakuinue.
1 Kor 7:23 ''Mlinunuliwa kwa thamani; msiwe watumwa wa wanadamu.''

3. Uwe na juhudi katika MUNGU , Kumwabudu, kumtumikia KRISTO na kutii yaliyo ya MUNGU.
1 Kor 15:58 ''Basi, ndugu zangu wapendwa, mwimarike, msitikisike, mkazidi sana kutenda kazi ya BWANA sikuzote, kwa kuwa mwajua ya kwamba taabu yenu siyo bure katika BWANA.''

4. Haribu nguvu za giza  zilizotumika kukushusha na kuondoa thamani yako.
Yeremia 1:10 ''angalia, nimekuweka leo juu ya mataifa na juu ya falme, ili kung'oa, na kubomoa, na kuharibu, na kuangamiza; ili kujenga na kupanda.''
Haribu nguvu za giza zote, na kisha ujenge ufalme wa MUNGU  na kupanda katika ufalme wa MUNGU.

5. Haribu nguvu za giza zinazowainua watu watu kipepo katika eneo lako.
Mathayo 15:13 '' ......   Kila pando asilolipanda Baba yangu wa mbinguni litang'olewa. ''

6. Washushe wote wanaotumika kipepo.
 Zaburi 2:9 ''Utawaponda kwa fimbo ya chuma, Na kuwavunja kama chombo cha mfinyanzi. ''
Maana hao wanaotumika kipepo kazi yao ni kukuonea na kuishusha thamani yako, washushe na futa nguvu ya giza inayowatumia.
Unaweza ukadhaulika kazini kwako kumbe kuna mfanyakazi mwenzako anatumika kipepo, ameeenda kwa mganga ili kukufanya usiwe na thamani.
Unaweza ukawa mtu wa kuachwa tu kumbe kuna mtu anatumika kipepo kukufunga kichawi n.k. 

7. Omba MUNGU akupe kibali na omba thamani yako ionekane.
1 Thesalonike 5:17 '' ombeni bila kukoma;''
Maombi ni ufunguo Special sana ambao unaweza kuutumikia ufunguo huo kufungua kila jambo katika maisha yako.

Ndugu, najua kabisa unataka sana thamani yako ionekane.
Ndugu, kama ni makosa yako kulingana na ulivyojifunza somo hili basi tengeneza kwa Bwana YESU.
Kama wewe umeokoka na unaishi maisha matakatifu ya wokovu wa Bwana YESU endelea kuomba maana utamuona MUNGU hakika, wewe unayetakiwa kutengeneza  basi husika na kila kipengele unachohusika nacho ili utengeneze na thamani yako itaonekana.

Maombi ya leo.
1. Tubu kwa mambo yote uliyoyafanya yaliyosababisha  thamani yako kushuka au kuondoka.

2. Omba MUNGU akufungue ili ujitambue katika eneo unalotakiwa kujitambua.

3. Futa maneno ya uongo ya wanadamu waliyokuzushia au kukutangaza ili kuishusha thamani yako.

4. Haribu nguvu za giza zinazotumika kuishusha thamani yako.

5. Haribu nguvu za giza zinazowapandisha watu kipepo kwa lengo la wewe kuwa chini ya watu hao.

6. Omba MUNGU akupe kibali  katika kila eneo la maisha yako.

7. Omba MUNGU akupe kubaini kila kinachokushusha thamani yako na omba ujue watu wanaotumika kipepo ili kushusha thamani yako ili sasa  ujitenge nao.
 Natamani niseme mengi mno lakini naamini mwenye kuelewa ameelewa.
MUNGU akubariki kwa kujifunza somo hili muhimu pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane na nitakujulisha jinsi ya kukipata na  Naamini kitakusaidia sana.
Hapa chini ni
MAOMBI YA KUIOMBEA THAMANI YAKO ILI IONEKANE.
  Maombi haya naomba yamsaidie mtu yule ambaye hajui kuomba ili katika kuomba kwa kutumia hayo basi atakumbuka mahitaji yake na kuyataja katika maombi yake. Haya hapa chini ni maombi ya kuanzia tu katika maombi yako ili uendelee zaidi kuomba
Kwa waombaji wazoefu naamini baada tu ya kulisoma somo na kulielewa basi anajua aombee nini maana alikuwa anaandika points za kuombea. Kumbuka pia fundisho ni muhimu kuliko maombi hivyo wewe ambaye huwa unahusika na maombi tu hakikisha unajifunza kwanza somo lote ndipo utapata nguvu za kuomba na kushinda. 


 MAOMBI YA KUIOMBEA THAMANI YAKO ILI IONEKANE.

MUNGU Baba wa mbinguni inanipasa kukushukuru maana isingekuwa ni wewe mimi nisingepata Wokovu popote.
Niko JEHOVAH mahali hapa naomba unisamehe dhambi zako zote, makosa yangu yote na uovu wangu wote na naomba Eee MUNGU wangu unisafisha uovu huo, dhambi hizo na makosa hayo kama ahadi yako ilivyo kwa wanaotubu kati 1 Yohana 1:7.
Nisamehe BWANA kwa jambo lolote nililolifanya lililosababisha thamani yangu kuondoka, natubu MUNGU Muumbaji wangu naomba unisamehe.
Eee MUNGU wangu naomba unifungue sasa ili nijitambue katika kila eneo ninalotakiwa kujitambua. Nisaidie ROHO wa MUNGU ili nisifanye makosa ambayo yatanishusha thamani yangu.
 Eee MUNGU wangu niko mbele zako nikifuta kila maneno ya uongo ambayo watu walinizushia ili kuondoa thamani yangu.
Nayafuta maneno hayo ya uongo katika jina la YESU KRISTO aliye hai.
Mahali popote niliposhindwa kufanikiwa kwa sababu watu waliondoa thamani yangu kwa maneno yao ya uongo kunihusu, leo, katika jina la YESU KRISTO nafuta maneno hayo ya uongo niliyozushiwa.
Damu ya YESU KRISTO Mwokozi wangu na ifute sasa kila Neno la uongo nililozushiwa ili kuondoa thamani yangu.
Sasa naharibu kila nguvu za giza zilizotumika kunishusha, naziharibu kwa damu ya YESU KRISTO na katika jina la YESU KRISTO Mwokozi aliye hai.
Kila mchawi na mganga waliotumika kuondoa thamani yangu, naharibu kazi zao na nguvu zao za giza nazifuta kwa damu ya YESU KRISTO na katika jina la YESU KRISTO.
Kila jini au nguvu za giza zilizowekwa ndani yangu na wakuu wa giza sasa kwa damu ya YESU KRISTO na katika jina la YESU KRISTO naziharibu hizo nguvu za giza.
Kila mtu kazini kwangu anayetumia nguvu za giza ili kuwa juu, leo hizo nguvu za giza naziamuru zimtoke katika jina la YESU KRISTO.
Kila wafanya biashara wenzangu ambao wanatumia nguvu za giza ili kuwa juu na mimi niwe chini yao, leo, kwa damu ya YESU KRISTO ninaziharibu hizo nguvu za giza na kuzifuta na sasa hazitafanya kazi kamwe.
Kila mwanadamu anayetumika kipepo ili mimi nisiwe na thamani kwa Mchumba wangu au mwenzi wangu wa ndoa, sasa naukataa mpango huo wa kipepo, na naufuta katika jina la YESU KRISTO Mwokozi aliye hai.
Kila mtu anayefanya mipango ili mimi nisiwe na thamani kazini kwangu, kwa ndugu zangu au kwa jamii yangu, sasa naukataa mpango huo wa kipepo,  na naufuta katika jina la YESU KRISTO Mwokozi aliye hai.
Kila nguvu za giza zinazotumika kupandisha watu ili mimi niwe chini, sasa katika jina la YESU KRISTO naziharibu hizo nguvu za giza na kuzitowesha, kwa moto wa jina la YESU KRISTO.
Imeandikwa katika Kumb 28:13 kwamba  '' BWANA atakufanya kuwa kichwa, wala si mkia; nawe utakuwa juu tu, wala huwi chini; utakapoyasikiza maagizo ya BWANA, Mungu wako, nikuagizayo hivi leo, kuyaangalia na kufanya; '' Hivyo kuanzia leo nakataa kuwa chini ya anayetumika kipepo, naharibu nguvu zake za giza, katika jina la YESU KRISTO aliye hai.
Kila mtumishi wa shetani anayeshindana na mimi ili niwe chini kwenye maisha yangu, namtangazia huyo mpambe wa shetani kwamba Mwokozi wangu YESU KRISTO anataka niwe juu katika kila Eneo la maisha yangu kama Neno lake linavyosema katika Kumbu 28:13 hivyo sitakuwa chini kamwe katika maisha yangu, kazi yangu, biashara yangu na katika kila jambo langu lolote.
Namkataa shetani na kazi zake zote tena kuanzia sasa shetani achia maisha yangu, ndoa yangu, kazi yangu, kipato changu, uchumba wako, familia yangu, uzao wangu, biashara yangu na kila baraka yangu, kwa jina la YESU KRISTO aliye hai na iwe hivyo sasa.
Baba MUNGU ninakushuru sana maana katika KRISTO YESU ninashinda na zaidi ya kushinda.
Sasa Eee ROHO MTAKATIFU ninakuomba BWANA unipe kujua kila kilichosababisha thamani yangu kushuka ili kunzia leo nikiepuke kitu hicho.
Nakuomba BWANA unipe kuwajua watu wanaotumika kipepo ili kushusha thamani yangu, nipe kuwajua ili nijiepushe nao.
Eee MUNGU Baba nakuomba unipe kibali katika maisha yangu ili thamani yangu iwe juu daima.
Nipe kibali katika ndoa yangu ili thamani yangu ionekane.
Nipe Kibali katika kazi yangu ili thamani yangu ionekane, na nipate haki zangu stahiki zote.
 Nipe kibali katika  Biashara yangu yangu ili thamani yangu ionekane na nipate faida timilifu.
Nipe Kibali katika huduma yangu  yangu ili thamani yangu ionekane na ili nitende kazi ya huduma katika KRISTO vyema.
Bila kibali chako MUNGU Baba siwezi kufika popote, hivyo Ninaomba kibali chako Eee MUNGU wangu.
Nipe kibali kwa ndugu zangu  ili thamani yangu ionekane kisha wasinichukie bila kosa lolote..
Nipe Kibali kwa Mchumba wangu ili thamani yangu ionekane kisha tufunge ndoa takatifu mbele zako Eee YAHWEH MUNGU wangu.Nipe kibali katika masomo yangu, safari yangu, utumishi wangu   ili thamani yangu ionekane.
Nipe Kibali katika mipango yangu ya kihuduma na kimaendeleo  ili thamani yangu ionekane.
Naamini imekuwa katika wewe MUNGU Muumbaji wangu.
Katika jina la YESU KRISTO nimeomba na sasa thamani yangu itaonekana.
Amen Amen Ameeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeen.
Hakika umeshinda.
Ukiweza kufunga unaweza kufunga hata siku 1 au 3 au 3 au hata 5 au zile ambazo wewe utaona unaweza ukihusika kila siku na kipengele kimoja kuombea na kumbuka baada ya maombi ya kufunga au hata maombi ya bila kufunga fanya tendo la imani kwa MUNGU kwa kutoa sadaka nzuri itakayoambatana na maombi  juu ya ukomo wa kuteswa na maadui zako katika ulimwengu wa roho
Nawaonya pia wanaotumia masomo yangu vibaya na kwa manufaa yao waache tabia hiyo.
 Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa BWANA YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
0714252292.
0786719090
mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu.

Comments