SHETANI ANAWEZA KUTUMIA KAZI YA MTU KUMLETEA MTU HUYO UHARIBIFU.

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.

Bwana YESU atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.
Leo tunajifunza jinsi ambavyo wakati mwingine shetani anaweza kuitumia kazi ya mtu ili kumletea uharibifu mtu husika.
Biblia inasema sisi wateule wa MUNGU hatukosi kuzijua fikra zake shetani hivyo tukijua fikra zake shetani tutamshinda kirahisi sana.
2 Kor 2:11 '' Shetani asije akapata kutushinda; kwa maana hatukosi kuzijua fikira zake. ''
Shetani huwa hafanyi kazi akiwa katika hali yake aliyonayo Bali ili afanye kazi ni lazima aingie ndani ya mtu.
shetani alimwingia Yuda Iskarioti sawasawa na cheo chake  au kazi yake Yuda. Yuda alikuwa mtunza fedha na shetani alimwingia Yuda kupitia mambo yanayohusu fedha na kwa njia hiyo Yuda akamsaliti YESU KRISTO.
Yuda kwa tamaa ya pesa akamsaliti YESU, na huyo Yuda ndio alikuwa anatunza fedha.
Nini tunajifunza?
Shetani anaweza kumwingia mtu na mtu huyo kupitia cheo chake, karama yake, Huduma yake, kazi yake au madaraka yake akifanya uovu.
Wewe mwenye cheo, wewe mwenye kazi, na wewe mwenye madaraka nakuomba usikubali shetani akakutumia kupitia cheo chako au madaraka yako au kazi yako.
Kumbuka Yuda mtunza fedha alimsaliti Bwana wake kwa kutamani fedha.

Luka 22:36 "Shetani akamwingia Yuda, aitwaye Iskariote, naye ni mmoja wa wale Thenashara. Akaondoka, akaenda akasema na wakuu wa makuhani na majemadari, jinsi atakavyoweza kumtia mikononi mwao. Wakafurahi, wakapatana naye kumpa fedha. Akakubali, akatafuta nafasi ya kumsaliti kwao pasipokuwapo mkutano."
Leo kwa mfano wewe unaweza kuwa ni Mwalimu shuleni na ukimruhusu shetani akuingie hakika anaweza kukufanya uwe mzinzi kwa kufanya uzinifu na wanafunzi wako na ukakosa mbingu, hapo shetani ametumia kazi yako na tamaa yako kukunasa.
Unaweza kuwa Mkurugenzi au Meneja na ukimruhusu shetani atakitumia cheo chako na kazi yako kukufanya kuwa mtu wa kupokea rushwa tu siku zote, hapo shetani amekitumia cheo chako kukuangamiza.
Kumbuka Yuda alipomruhusu shetani amtumie, shetani alimtumia Yuda kupitia kazi yake ya mambo ya fedha.

Unaweza ukawa diwani au mwenyekiti katika eneo lako na ukamruhusu shetani kukutumia, atakachokifanya shetani ni kukufanya wewe uwe mtu wa kutenda dhambi kila Leo kwa wewe kuahidi uongo wananchi unaowaongoza.
Unaweza ukawa askari na ukimruhusu shetani akutumie yeye atakitumia cheo chako, kazi yako na madaraka yako kukufanya utende maovu mengi na kumkosea MUNGU.
Kila Kazi isiyo machukizo kwa MUNGU ni njema tu, lakini ukimruhusu shetani akutumie basi atakufanya utumie kazi yako kutenda dhambi na ukose mbingu.
Ndugu mkumbuke Yuda ambaye alikuwa bwana fedha lakini shetani akamtumia Yuda kumsaliti Mwokozi kwa kutumia pesa vupande 30.

Naamini umejifunza kitu kupitia kazi yako, madaraka yako au cheo chako na hautamfungulia mlango shetani ili aingie kwako na kukutumia kupitia nafasi yako kutenda dhambi.
Ndugu nakuomba usimpe nafasi shetani katika maisha yako kwa kupitia kazi yako au chochote.
Waefeso 4:27-29 '' wala msimpe Ibilisi nafasi. Mwibaji asiibe tena; bali afadhali afanye juhudi, akitenda kazi iliyo nzuri kwa mikono yake mwenyewe, apate kuwa na kitu cha kumgawia mhitaji. Neno lo lote lililo ovu lisitoke vinywani mwenu, bali lililo jema la kumfaa mwenye kuhitaji, ili liwape neema wanaosikia. ''

Jambo jingine muhimu sana ni hili kwamba Watu wengi hawajui kwamba kazi zao za kuajiriwa au kujiajiri haziwaongezei kitu katika ufalme wa MUNGU.
Unaweza ukawa na juhudi kubwa kazini kwako, ukafanya kazi jumatatu hadi jumapili, ukasifiwa sana na ukapata heshima kubwa sana kwa wanadamu. Ni sawa na ni haki yako kabisa lakini hiyo kazi haikuongezei kitu katika ufalme wa MUNGU. 

Ndugu usiangamie kwa kukosa maarifa sahihi.
Hosea 4:6a '' Watu wangu wanaangamizwa kwa kukosa maarifa; kwa kuwa wewe umeyakataa maarifa,''
 
Nakujulisha kuwa kazi yako ni muhimu sana lakini kumbuka pia kwamba mambo yanayoweza kukuongezea kitu kwenye ufalme wa MUNGU ni masuala ya kiroho tu.
Ukimshuhudia mtu kuokoka, ukiwasaidia watu kiroho, ukiwafanya watu ili wampokee YESU na kuokoka, ukiwa unamtolea MUNGU sadaka na zaka kwa uaminifu hayo ndio mambo ya kiroho na yanayoweza kukuongezea kitu kwenye ufalme wa MUNGU.
Ukimshauri mtu aache dhambi dhambi hapo utakuwa na faida katika ufalme wa MUNGU.
Ukiishi maisha matakatifu na ukawa ni Mkristo mwenye hofu ya MUNGU, hiyo ni faida yako kuu katika ufalme wa MUNGU.
Katika jamii ya Leo watu wengi wako busy sana na kutafuta pesa, ni sawa kabisa lakini usisahau mambo ya kiroho na usiisahau kazi ya MUNGU.
Ndugu, katika maisha yako fanya kazi yako kwa juhudi kubwa sana na kwa uaminifu lakini hakikisha kazi yako inamzalia MUNGU matunda.
Kama kazi yako haimletei KRISTO matunda hakika hiyo kazi haitakusaidia wewe chochote katika ufalme wa MUNGU.
Uwe makini pia maana kuna kazi zingine ni Kukufanya utende dhambi, hiyo ni hatari ya maisha yako unatotakiwa kuiepuka haraka Sana.
Ndugu, hata kama umeshachukua tuzo ya mfanya kazi bora Mara saba lakini kama kazi yako hiyo haina faida katika KRISTO basi kazi hiyo haitakusaidia chochote tena haina kuongezea chochote katika ufalme wa MUNGU.
Ndugu nakuomba mpe kaisari yaliyo yake lakini hakikisha mambo hayo ya kaisari unafanyayo sio mambo ya dhambi.
Usikubali pia katika maisha yako kila kitu ukampa Kaisari na MUNGU Muumbaji wako ukamsahau.
Marko 12:17 "YESU akajibu, akawaambia, Mpeni Kaisari yaliyo ya Kaisari, na yaliyo ya MUNGU mpeni Mungu. Wakamstaajabia sana."

Usikubali muda wako wote ukampa kaisari tu huku MUNGU umemsahau.
Usikubali Mali zako zote ukampa Kaisari huku huna habari na MUNGU.
Kumbuka kazi yako ya kidunia haina msaada katika wewe kuupata ufalme wa MUNGU.
Hakikisha humsahau MUNGU katika maisha yako yote na kokote uliko.
Hakikisha huendi kinyume na YESU KRISTO katika kazi yako.
Usikubali kumhuzunisha ROHO MTAKATIFU kwa sababu ya kazi yako ya kuajiriwa au kujiajiri.
Usikubali kazi yako ndio ikawa jaribu lako la kukuzuia kumcha MUNGU na kuokoka.

Kumbuka shetani anaweza kuitumia kazi yako hiyo hiyo kukumaliza kiroho, uwe makini na hakikisha unamcha MUNGU daima hata kupitia kazi yako.
Tangu zamani MUNGU anataka tumche yeye na kuishi maisha ya haki.
Yoshua 24:14 '' Basi sasa mcheni BWANA, mkamtumikie kwa unyofu wa moyo na kwa kweli; na kuiweka mbali miungu ambayo baba zenu waliitumikia ng'ambo ya Mto, na huko Misri; mkamtumikie yeye BWANA.' 


 Kuwa makini ni muhimu sana.
Kuwa makini kwenye Huduma yako mteule ni jambo la muhimu sana.
Usipokuwa makini shetani anaweza kuitumia huduma yako hiyo maana umemfungulia mlango kwa sababu tu ya kukosa kwako umakini.

Kumbuka pia kila mmoja ana uwezo wa kukwazwa na kila mmoja ana uwezo wa kujizuia kuwakwaza wengine.
Kila mmoja na uwezo wa kukasirika, na kila mmoja ana uwezo wa kujizuia kuwakarisilsha wengine.

Mimi nakushauri kwamba usikubali kuwa mtu wa makwazo kazini kwako maana hayo yanaweza kukufanya ukamkosea MUNGU kupitia hiyo hiyo kazi.
Kumbuka pia kwamba dhambi ina tabia ya kutafuna baraka zako.
Iache dhambi maana usipoiacha ujue itakufungulia vifungo vya Giza kukuandama.

Mithali 28:13 "Afichaye dhambi zake hatafanikiwa; Bali yeye aziungamaye na kuziacha atapata rehema."
Dhambi ina uwezo wa kutafuna kibali chako.
Dhambi zako za Mara kwa Mara zinaweza kutafuna nafasi na fursa zako.
Hakuna mafanikio ya ki MUNGU katika dhambi.

Yuda dhambi ilimtafuna akaishia kujingonga.
Dhambi ni mlango mkuu wa shetani kukushambulia.
Unaweza ukafanya dhambi ya uzinzi na uasherati na dhambi hiyo ikafungulia mlango wa magonjwa kwako.
Unaweza ukafanya dhambi ya wizi na dhambi hiyo ikafungua mlango wa wewe kuwa gerezani miaka mingi.
Ndugu nakuomba kataa dhambi, ogopa dhambi, iache dhambi na ikimbie dhambi maana hakuna mafanikio katika dhambi.
Kwenye dhambi kuna vifungo tu na maagano ya Giza.

Yeremia 5:25 "Maovu yenu yameyageuza haya, na dhambi zenu zimewazuilia mema msiyapate."
  Ndugu hakikisha unaishi maisha matakatifu ya Wokovu wa thamani sana wa YESU KRISTO hata ukiwa kazini kwako, ili kazi yako isifanyike daraja la shetani kukufunga vifungo vya giza.
1 Petro 1:13-15 ''Kwa hiyo vifungeni viuno vya nia zenu, na kuwa na kiasi; mkiitumainia kwa utimilifu ile neema mtakayoletewa katika ufunuo wake YESU KRISTO. Kama watoto wa kutii msijifananishe na tamaa zenu za kwanza za ujinga wenu; bali kama yeye aliyewaita alivyo mtakatifu, ninyi nanyi iweni watakatifu katika mwenendo wenu wote; ''

Wakati mwingine nimeulizwa na watu wengi juu ya kuwatambua hata watumishi ambao shetani huwashika kupitia huduma zao au karama zao za kiutumishi na hivyo wao kujikuta ni watumishi wa shetani na sio wa KRISTO YESU Mwokozi.
Nimeulizwa na watu  mara nyingi juu ya kuwatambua watumishi wanaotumika kipepo.
Nimejibu nilivyoweza lakini naomba niseme machache Leo.
Kwanza kumtambua Mtumishi anayetumika kipepo ni rahisi sana ukiwa na ROHO MTAKATIFU.
Biblia inasema ROHO MTAKATIFU hutujulisha sisi wateule wa KRISTO.

1 Kor 2:10 '' Lakini MUNGU ametufunulia sisi kwa ROHO. Maana ROHO huchunguza yote, hata mafumbo ya MUNGU''
Lakini kwa mambo ya nje yanayoweza kumtambulisha mtu kuwa anatumika kipepo ni pamoja na haya yafuatayo:
1. Anafanya mambo ya kishetani.

2. Anashirikiana na mawakala wa shetani.
3. Anafanya dhambi na wakati mwingine anazitetea hizo dhambi.
4. Yuko Kinyume na YESU KRISTO.
5. Hakemei dhambi wala hafundishi utakatifu.
6. Anajaribu kwa njia za kipepo kuwahamisha watu kwenye Wokovu wa KRISTO.
7. Ni mtu wa vitisho na hujionyesha kwamba yeye ndiye Mtumishi wa kweli na wengine sio watumishi.
8. Anatumia nguvu za Giza.
9. Anafundisha uongo yaani kinyume na Injili ya YESU KRISTO.
10. Anamtii shetani na sio YESU KRISTO.
Ndugu, usikubali kutumika kipepo.
Usikubali kazi yako ya utumishi shetani akaitumia kukuletea uharibifu.
Usikubali kushirikiana na wanaotumika kipepo.
Usifanyie kazi neno na Mtumishi anayetumika kipepo, Bali likemee.
Usikubali kwa vyovyote kwenda kwa anayetumika kipepo.

 Natamani niseme mengi mno lakini naamini mwenye kuelewa ameelewa.
MUNGU akubariki kwa kujifunza somo hili muhimu pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane nitakujulisha jinsi ya kukipata.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.
0714252292(Hadi whatsapp).
0786719090
mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu.

Comments