UKO KATIKA KIZAZI GANI?

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.

Bwana YESU atukuzwe sana.
  Tuko katika nyakati za hatari sana sana kwa sababu ya mafundisho ya uongo.
Kuna watumishi walio mawakala wa shetani walikuja na uongo wao kuhusu vizazi, wakijipachika kizazi wakitakacho.
Ndugu mmoja siku moja aliniambia kwamba mwanzilishi wa dhehebu lao ni nabii kizazi cha nne maana ametumwa na MUNGU kuifanya kazi ambayo YESU ilimshinda, hata nilipomwambia ukweli ndugu yule alikakamaa sana sana akiwa hana hata andiko linalosema kwamba ''Mwanzilishi wa dhehebu lake ni nabii kizazi cha nne''
Ndugu Mwingine akasema kwamba Adamu ni kizazi cha kwanza, YESU ni kizazi cha pili na Mwanzilishi wa dhehebu lako ndio Mtume kizazi cha tatu ili aifanye kazi ambayo kizazi cha kwanza na kizazi cha pili walishindwa.
Kumekuwa na utitili wa watumishi wa uongo wakiingia katika utumishi kwa gia ya kujiiita kizazi fulani.
Ndugu zangu Biblia iko wazi kwanza YESU ndiye Mzaliwa wa kwanza na huyo tu ndio Mwokozi na MUNGU husema na sisi kupitia YESU KRISTO na sio zaidi ya hapo, na YESU ni mkuu sana maana hata Malaika wote Mbinguni humsujudia.
YESU ndiye chapa ya nafsi ya MUNGU, Ni alama ya nafsi ya MUNGU, Biblia iko wazi mno ikisema katika
Waebrania 1:1-6 kwamba ''MUNGU, ambaye alisema zamani na baba zetu katika manabii kwa sehemu nyingi na kwa njia nyingi, mwisho wa siku hizi amesema na sisi katika Mwana, aliyemweka kuwa mrithi wa yote, tena kwa yeye aliufanya ulimwengu. Yeye kwa kuwa ni mng'ao wa utukufu wake na chapa ya nafsi yake, akivichukua vyote kwa amri ya uweza wake, akiisha kufanya utakaso wa dhambi, aliketi mkono wa kuume wa Ukuu huko juu; amefanyika bora kupita malaika, kwa kadiri jina alilolirithi lilivyo tukufu kuliko lao. Kwa maana alimwambia malaika yupi wakati wo wote, Ndiwe mwanangu, Mimi leo nimekuzaa? Na tena, Mimi nitakuwa kwake baba, Na yeye atakuwa kwangu mwana? Hata tena, amletapo mzaliwa wa kwanza ulimwenguni, asema, Na wamsujudu malaika wote wa MUNGU.''
Mawakala wa shetani waliovaa kofia ya kikanisa leo au kidini wanadanganya watu kwamba wao ni kizazi cha tatu mara cha nne mara cha tano ili tu kuwapata wasiomjua MUNGU wa kweli.

Nimejikuta naangalia Biblia katika maandiko yanayozungumzia kizazi ili hata nipate kitu cha kumsaidia mtu mmoja ili aiepuke jehanamu kwa kuujua ukweli wa MUNGU ambao ni KRISTO tu kwa ajili ya uzima wa milele.

Kwanza kizazi ni nini?
Kizazi ni watu waliotokana na uzao mmoja.
Kizazi ni jumla ya watu walioishi katika muda mmoja wa wakati katika Historia.
Ni sawa kabisa kuwa katika kizazi fulani lakini sio kama watumishi feki hao wanavyojiita.
Ni sawa kabisa hata sasa tuko katika kizazi fulani lakini sio kama mafundisho ya manabii hao wa uongo yanavyofundisha.
Huu ni wakati wa Neema au wakati wa Kanisa, wakati huu ulianzia Kalvari/Golgotha na utaishia kipindi YESU atarudi.
Kwa kupitia Biblia nilikutana na vizazi vingi vikizungumzwa.
Labda wewe ndugu uko kizazi gani?
Baadhi ya vizazi ni hivi.


1. Kizazi cha wasio taka kutubu.
 
Mithali 30:12-14 '' Kuna kizazi cha watu walio safi machoni pao wenyewe; Ambao hawakuoshwa uchafu wao. Kuna kizazi cha watu ambao macho yao yameinuka kama nini! Na kope zao zimeinuka sana. Kuna kizazi cha watu ambao meno yao ni panga; Na vigego vyao ni kama visu. Ili kuwala maskini waondolewe katika nchi, Na wahitaji katika wanadamu.''

 
Kizazi hiki hakimhusu kila mtu bali kinamhusu mtu mchafu ambaye hataki kutubu. Na njia ya kutubu ni moja tu yaani Kutubu kwa MUNGU katika KRISTO YESU.
1 Yohana 1:7-10 ''bali tukienenda nuruni, kama yeye alivyo katika nuru, twashirikiana sisi kwa sisi, na damu yake YESU, Mwana wake, yatusafisha dhambi yote. Tukisema kwamba hatuna dhambi, twajidanganya wenyewe, wala kweli haimo mwetu.Tukiziungama dhambi zetu, Yeye ni mwaminifu na wa haki hata atuondolee dhambi zetu, na kutusafisha na udhalimu wote. Tukisema kwamba hatukutenda dhambi, twamfanya Yeye kuwa mwongo wala neno lake halimo mwetu. '' 

 
Damu ya YESU ndio unatusafisha dhambi zote kupitia kumpokea yeye na kutubu, sasa wewe mkatae YESU harafu unataka dhambi zako zifutike, haitawezekana, wewe utajiita kizazi cha nne lakini cha wasiotaka kutubu.
Kizazi cha kukataa kutubu ni watu ambao ukiwaambia wampokee YESU kama Mwokozi wao na kuacha dhambi zao hawataki. Ndugu kwa dakika moja kabisa unaweza kuhama kizazi hicho leo kwa kumpokea YESU kama Mwokozi wako, kutubu na kuacha dhambi zako zote.


2. Kizazi cha na uasi kwa MUNGU.
 
Zaburi 78:8 '' Naam, wasiwe kama baba zao, Kizazi cha ukaidi na uasi. Kizazi kisichojitengeneza moyo, Wala roho yake haikuwa amini kwa MUNGU.''
Kizazi hiki hawamwamini MUNGU na ni watenda dhambi.
Kizazi hiki hawataki Wokovu wa Bwana YESU maana matendo yao ya gizani hawataki kuyaleta nuruni ili yakemewe na wayaache.
Yohana 3: 17-21 ''Maana MUNGU hakumtuma Mwana(YESU) ulimwenguni ili auhukumu ulimwengu, bali ulimwengu uokolewe katika yeye.Amwaminiye yeye hahukumiwi; asiyeamini amekwisha kuhukumiwa; kwa sababu hakuliamini jina la Mwana pekee wa MUNGU. Na hii ndiyo hukumu; ya kuwa nuru imekuja ulimwenguni, na watu wakapenda giza kuliko nuru; kwa maana matendo yao yalikuwa maovu. Maana kila mtu atendaye mabaya huichukia nuru, wala haji kwenye nuru, matendo yake yasije yakakemewa. Bali yeye aitendaye kweli huja kwenye nuru, ili matendo yake yaonekane wazi ya kuwa yametendwa katika MUNGU. ''
Ndugu unaweza kujiita kizazi cha pili au cha tatu au cha nne au cha tano na kumbe ni kizazi cha uasi.
Kumbuka ukimwasi KRISTO YESU umemwasi MUNGU aliyeumba mbingu na dunia.
Toka kwenye kizazi cha ukaidi na uasi.


3. Kizazi cha kutafuta ishara.
 
Marko 8:12 '' Akaugua rohoni mwake, akasema, Mbona kizazi hiki chatafuta ishara? Amin, nawaambieni, Hakitapewa ishara kizazi hiki.''
Bwana YESU alikiona kizazi hiki cha watafuta ishara tu na kukikemea.
Kizazi hiki imani yao iko katika miujiza tu, hata kama itakuwa miujiza ya uongo au ya kishetani. Hata kama watumishi husika ni maajenti wa kuzimu lakini kwa sababu ni kizazi cha kutafuta ishara tu basi wanaweza kumwacha YESU Mwokozi anayeokoa na kukimbilia kwa nabii wa kuzimu anayejiita kizazi cha nne au cha tano.
Ndugu, kumbuka MUNGU anatenda sana miujiza, Hakika YESU hakuna uogonjwa au tatizo ambalo hawezi kuliondoa.
Uthibitisho ni huu.
Mathayo 9:35 ''Naye YESU alikuwa akizunguka katika miji yote na vijiji, akifundisha katika masinagogi yao, na kuihubiri habari njema ya ufalme, na kuponya magonjwa yote na udhaifu wa kila aina. ''
Kumbe ni hakika kabisa kwamba Bwana YESU anaponya magonjwa yote na madhaifu yote, hata mimi kwa macho yangu nimeshuhudia watu wengi sana akiwaponya, lakini ndugu kumbuka sasa pia kwamba shetani naye anafanya miujiza.
Ufunuo 13:11-12 '' Kisha nikaona mnyama mwingine, akipanda juu kutoka katika nchi; naye alikuwa na pembe mbili mfano wa Mwana-Kondoo, akanena kama joka. Naye atumia uwezo wote wa mnyama yule wa kwanza mbele yake. Naye aifanya dunia na wote wakaao ndani yake wamsujudie mnyama wa kwanza, ambaye jeraha lake la mauti lilipona.''

Ndugu unaweza kukimbilia ishara na miujiza lakini kama hiyo miujiza haitokani na YESU KRISTO ujue umepotea sana.
Rafiki yangu mmoja aliniambia jambo la ajabu sana. Alisema kama ifuatavyo ''Kuna siku Kanisani kwetu watu 15 wageni walikuja kuabudu na Mchungaji wakati anawaombea wote wakadondoka, baada ya kufunguliwa wote wakashuhudia jambo moja kwamba katika mkoa wao alikuja mtumishi mmoja akitumia mafuta ya upako na wote aliwapaka mafuta hayo ya upako na mengine waliyakanyaga na tangu sio hiyo nguvu za giza ndipo zikaanza kuwatesa''
Nilishangaa sana jambo hilo yaani watu 15 waliopakwa mafuta ya upako na mtumishi wote wanadondoka chini kwa mapepo yaliyosababishwa na mafuta ya upako, yaani ni kama mafuta ya upako yalikuwa ni mapepo na vifungo.
Ndugu Usikubali kuwa kizazi cha kutafuta ishara na miujiza tu bali tafuta Neno la KRISTO la kweli.
Tafuta kuenenda katika ROHO MTAKATIFU.
Tafuta utakatifu.


4. Kizazi cha ukaidi.
 
Matendo 2:40 ''Akawashuhudia kwa maneno mengine mengi sana na kuwaonya, akisema, Jiokoeni na kizazi hiki chenye ukaidi.''
Kizazi chenye ukaidi ni watu wanaomkataa YESU KRISTO kuwa Mwokozi wao.
Kizazi cha ukaidi ni wapinga Wokovu wa KRISTO.
Biblia inakushauri kwamba jiokoe na kizazi chenye ukaidi, jitenge mbali na kizazi chenye ukaidi.
Wanaomkataa YESU kuwa ni Mwokozi wao hao achana nao maana ni kizazi chenye ukaidi.
Wewe mkubali YESU kisha mpokee kama Mwokozi wako na anza kuishi maisha matakatifu katika yeye.
Marko 16:16 '' Aaminiye na kubatizwa ataokoka; asiyeamini, atahukumiwa.''



Ndugu nakushauri hakikisha uko katika vizazi hivi.

1. Kizazi cha haki.
 
Zaburi 14:5 '' Hapo ndipo walipoingiwa na hofu nyingi, Maana MUNGU yupo pamoja na kizazi cha haki.''
Kizazi cha haki ni watu waliompokea YESU KRISTO kama Bwana na Mwokozi wao na wanaishi maisha matakatifu ya haki.
Kumb 10:12 '' Na sasa, Israeli, BWANA, Mungu wako, anataka nini kwako, ila umche BWANA, Mungu wako, na kwenda katika njia zake zote, na kumpenda, na kumtumikia BWANA, Mungu wako, kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote; ''


2. Kizazi cha wamtafutao BWANA.
 
Zaburi 24:6 '' Hiki ndicho kizazi cha wamtafutao, Wakutafutao uso wako, Ee MUNGU wa Yakobo. ''
Kizazi hiki ni wateule wa KRISTO waombaji na watoaji.
Hiki ni kizazi cha watu ambao wanajua kumtafuta MUNGU kwa maombi na matoleo sahihi yote.


3. Kizazi kinachodumu.
 
Yoeli 3:20 '' Bali Yuda atadumu milele, na Yerusalemu tangu kizazi hata kizazi.''
Wateule wa KRISTO watadumu milele yaani baada ya kuondoka duniani ni uzima wa milele.
1 Yohana 2:15-17 '' Msiipende dunia, wala mambo yaliyomo katika dunia. Mtu akiipenda dunia, kumpenda Baba(MUNGU) hakumo ndani yake. Maana kila kilichomo duniani, yaani, tamaa ya mwili, na tamaa ya macho, na kiburi cha uzima, havitokani na Baba, bali vyatokana na dunia.Na dunia inapita, pamoja na tamaa zake, bali yeye afanyaye mapenzi ya MUNGU adumu hata milele. ''
Afanyaye mapenzi ya MUNGU atadumu milele.
Mapenzi ya MUNGU yaanzia na kumpokea YESU kama Mwokozi, kuishi maisha matakatifu, kuwa na ROHO MTAKATIFU na kuliishi Neno la MUNGU la injili ya KRISTO ya Wokovu ulio wa thamani sana.

Ndugu nakuomba usiwe miongozi mwa waliodanganywa na watumishi feki wanaojiita kizazi cha
Ukiona Mtumishi yuko kinyume na Wokovu wa YESU KRISTO huyo mkatae.
Ukiona mtumishi anajiita Mungu ujue huyo ni mkuu wa giza kutoka kuzimu.
Ndugu usidanganywe na vizazi maana ukisoma Biblia utakutana na vizazi vingi mno hivyo wanajipangia vizazi mara cha nne mara cha tatu mara cha tano na wako kinyume na YESU KRISTO tambua leo kwamba hao ni matapeli tu.
Ukiona Mtumishi hatumii jina la YESU ujue huyo ni mwongo.
Siku hizi hadi kuna watumishi hawataji jina la YESU KRISTO bali husema ''Kwa jina la esu'' Ndugu hakika mtumishi wako anataja jina la YESU KRISTO na sio kuishia tu kusema ''jina la esu'' Esu hatumjui bali tunamjua YESU KRISTO.
Wako watu mpaka wanasujudia mawe kwa kudanganywa na mkuu wa giza mmoja aliyepagawa na majini.
Wako watu hadi wanaabudu ng'ombe kwa kudanganywa na shetani mwenyewe.
Ndugu yangu Biblia inasema hivi
2 Yohana 1:7-11 '' Kwa maana wadanganyifu wengi wametokea duniani, wasiokiri ya kuwa YESU KRISTO yuaja katika mwili. Huyo ndiye yule mdanganyifu na mpinga Kristo. Jiangalieni nafsi zenu msiyapoteze mliyoyatenda, bali mpokee thawabu timilifu. Kila apitaye cheo, wala asidumu katika mafundisho ya KRISTO, yeye hana MUNGU. Yeye adumuye katika mafundisho hayo, huyo ana Baba na Mwana pia. Mtu akija kwenu, naye haleti mafundisho hayo, msimkaribishe nyumbani mwenu, wala msimpe salamu. Maana yeye ampaye salamu azishiriki kazi zake mbovu.''
Natamani niseme mengi mno lakini naamini mwenye kuelewa ameelewa.
MUNGU akubariki kwa kujifunza somo hili muhimu pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane nitakujulisha jinsi ya kukipata.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.
0714252292(Hadi whatsapp).
0786719090
mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu.

Comments